KUWA NA UHURU NA KUTOKUWA NAO

MWANDISHI: SAYYID MUJTABA MUSAWI LARI

KIMETAFSIRIWA KUTOKA KATIKA KIAJEMI NA : DR. HAMID ALGAR

MTAZAMO JUU YA TATIZO LENYEWE KWA UJUMLA:

Moja ya maswali yanayovutia watu wengi wakiwemo wanafalsafa ni juu ya asili ya mwanadamu na maisha yake kwa ujumla, tatizo lenyewe linaanzia katika kutaka kufahamu kama binadamu ana uhuru kamili katika matendo yake au anadhibitiwa? Je matamanio yake na mwelekeo wa maisha na uhuru alionao katika maamuzi ndio vitu pekee vinavyomfanya awe katika hali fulani? Au matemdo na tabia zake vyote hivyo vimedhibitiwa? (Yaani kuwa hali amri juu ya mwelekeo wake) je kuna vitu fulani katika mazingira anamoishi vinamlazimisha yeye kuwa katika hali fulani?

Il kufahamu umuhimu wa swali hili ni vyema ikumbukwe kwamba ufumbuzi/jibu lake linategemea faida/manufaa tunayoweza kuyapata yakiuchumi, sheria dini, saikolojia na matawi mengine mengi ya taaluma ambayo binadamu ndio mlengwa mkuu.

Suala la kuwa binadamu anao uhuru katika mambo yake au sio kwamba halihusu nyanja ya kielimu au falsafa bali yapaswa lihusishe kila nyanja. Lakini juu ya jambo kwamba huyu binadamu anao uhuru pia sio la kulipinga moja kwa moja kwa sababu kama hanao uhuru wowote vipi juu ya hukumu siku ya Mwisho? Kwa waliofanya mema watalipwa pepo na wale watakaofanya maovu kuwa watapewa adhabu ya Moto. Baada ya kuenea kwa Uislamu, Waislamu nao walikuwa wakijihusisha kwa kiasi kikubwa kupata majibu ya swali hilo kwamba binadamu yu ana uhuru au la?

Watu wa vipindi vyote viwili wakati uliopo au wakati uliopita wanaweza kugawanywa katika makundi mawili kuhusiana na suala hiko la kuwa binadmu anao uhuru au la? Kundi la kwanza lenyewe linapinga kuwa binadamu anao uhuru katika vitendo vyake na kama matendo yake yataonyesha aina fulani ya uhuru basi hiyo ni kwa sababu ya ufinyu wa ufahamu wa binadamu (yaani kwamba ni kutokana na makosa tu).

Kundi la pili ni lile linalo amini kwamba binadamu anao uhuru kamili katika mambo yake uwezo wake wa kufikiri na kuamua una athari kubwa katika matendo yake na wala hautegemei mazingira.

Kwa kweli binadmu anazungukwa/anakabiliwa na mambo fulani ambayo hana amri juu yake mfano kuzaliwa kufa na mambo mengine mengi tu yanayomzunguka. Kwa sababu hiyo ndio maana watu wengine wakalazimika kuamini kwamba binadamu hana uhuru kabisa katika matendo yake.

Wakati huohuo binadamu anatambua kwamba yeye yuko huru kabisa mfano anao uwezo wa kupambana na vikwazo vingi katika maisha yake pia katika harakati za kuyakabili mazingira yanamzunguka kwa kutumia elimu aliyo nayo, lakini kuna ukweli ambao kamwe hawezi kukanusha nao ni juu ya jinsi anavyoweza kuitumia mikono yake na miguu lakini wakati huo huo akashindwa kufanya hivyo kwa viungo kama vile moyo, ini na mapafu. Kwa kuwa na matakwa, uwezo wa kufahamu na uwezo wa kuchagua vitu ambavyo vinavyompa sifa ya ubinadamu na ndio chanzo cha majukumu na wajibu alionao, binadamu anatambua wazi kabisa kwamba kuna mambo ambayo yanauwezo wa kufanyika pasipo ridhaa ya mwanadamu huyo na mambo hayo yanachukua sehemu kubwa sana ya maisha ya mwanadamu.