8
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU
كَذَٰلِكَ أَرْسَلْنَاكَ فِي أُمَّةٍ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهَا أُمَمٌ لِّتَتْلُوَ عَلَيْهِمُ الَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَهُمْ يَكْفُرُونَ بِالرَّحْمَـٰنِ قُلْ هُوَ رَبِّي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ مَتَابِ ﴿٣٠﴾
30. Ndio kama hivi tumekutuma kwa umma ambao zimekwishapita kabla yao umma nyingine, ili uwasomee tunayokupa wahyi na wao wamemkufuru Mwingi wa rehema. Sema, Yeye ni Mola wangu hakuna Mola mwengine isipokuwa yeye. Juu yake nimetegemea na kwake Yeye ndio marejeo yangu.
وَلَوْ أَنَّ قُرْآنًا سُيِّرَتْ بِهِ الْجِبَالُ أَوْ قُطِّعَتْ بِهِ الْأَرْضُ أَوْ كُلِّمَ بِهِ الْمَوْتَىٰ بَل لِّلَّـهِ الْأَمْرُ جَمِيعًا أَفَلَمْ يَيْأَسِ الَّذِينَ آمَنُوا أَن لَّوْ يَشَاءُ اللَّـهُ لَهَدَى النَّاسَ جَمِيعًا وَلَا يَزَالُ الَّذِينَ كَفَرُوا تُصِيبُهُم بِمَا صَنَعُوا قَارِعَةٌ أَوْ تَحُلُّ قَرِيبًا مِّن دَارِهِمْ حَتَّىٰ يَأْتِيَ وَعْدُ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُخْلِفُ الْمِيعَادَ ﴿٣١﴾
31. Na lau kwamba Qura’n ndiyo inayoendeshewa milima au kupasuliwa ardhi au kusemeshewa wafu (wasingeliamini). Bali amri zote ni za Mwenyezi Mungu. Je, hawajajua wale ambao wameamini kwamba lau Mwenyezi Mungu angelipenda bila shaka angeliwaongoa watu wote,Wala wale ambao wamekufuru hawaachi kusibiwa na balaa kwa waliyoyatenda au ikawateremkia karibu na nyumbani kwao mpaka iwafikie ahadi ya Mwenyezi Mungu, Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi.
Aya 30-31
Ndio kama hivi tumekutuma kwa umma ambao zimekwishapita kabla yao umma nyingine, ili uwasomee tunayokupa wahyi na wao wamemkufuru Mwingi wa rehema.
Maneno yanelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w) . Mwenyezi Mungu amepeleka mitume kabla yao kwenye umma zilizopita kwa lengo hilo hilo, sasa basi kuna kioja gani? Wao si watu wa kwanza kupelekewa mtume na yeye si mtume wa kwanza kuwasomea watu wahyi wa Mwenyezi Mungu.
Sema: Yeye ni Mola wangu hakuna Mola mwengine isipokuwa yeye. Juu yake nimetegemea na kwake yeye ndio marejeo yangu.
Hii ndio imani ya Muhammad(s.a.w.w) na huu ndio mwito wake, Anamwamini Mwenyezi Mungu peke yake na anamwelekea Yeye kwenye mamabo yake wala haoni mwenye uwezo mwingine zaidi yake, Anawalingania watu kwenye imani hii, Ni mwito ambao unajifahamisha wenyewe.
Na lau kwamba Qur’an ndiyo inayoendeshewa milima au kupasuliwa ardhi au kusemeshewa wafu (wasingeliamini) Bali amri zote ni za Mwenyezi Mungu.
Umepita mafano wa Aya hii mwanzo wa Juz. 8, na tumefafanua huko kwa anuani ya ‘Aina ya watu.’ Pia utakuja mfano wake katika Juz. 15. (17:90).
Tukiunganisha tuliyoyatanguliza ni kwamba Aya hii inaleta picha ya njia wanayoifikiria mataghuti ambao maisha yao yanasimama kwa kuwany- onya wanyonge na kuwafanya watumwa wao. Si maumbile wala akili, hisia, yanayoshuhudiwa, miujiza au chochote kile kitakachoweza kubadilisha ukaidi wa mataghuti na ulafi wao. Dawa pekee ni kuwaondoa na kuondoa misingi yao ya uporaji na unyang’anyi. Pamoja na yote hayo Muhammad anawataka wamkubali yeye na Qura’n.
Lakini wapi? Ni mpaka majabali yaendeshwe na Qur’an? Au mpaka wasemeshwe wafu? Kisha ndio iweje! Watapata faida gani katika hayo? Au kumuona Mungu ana kwa ana kutaongeza faida kwenye mali zao?
Hii ndio fikra yao na hii ndiyo lugha wanayoifahamu na kuisikiliza; wala hawasikilizi lugha nyingine isiyokuwa hiyo – lugha ya uchumi na faida ya paundi na dola. Lakini haki, uadilifu, mantiki na akili ni mazungumzo ya kipumbavu, yanayosadikiwa na watoto na wajinga.
Je, baada ya hayo, mtu anaweza kuuliza kwanini mataghuti hawakumwamini Muhammad pamoja na wito wake wa uadilifu na wema?
Mwito huu unaotaka kung’oa mizizi ya dhulma na ufisadi wanauona ni kosa kubwa. Hii ndio fikra pekee wanyoifikiria wale wanaoishi kwa uny- onyaji na unyang’anyi. Alikuwa nayo fikra hii Abu Jahl na Abu Sufyan wakati wa Muhammad(s.a.w.w) , katika zama zetu wamekuwa nayo Hitler na Musolini na leo hii fikra hii iko kwenye dola za kiukandamizaji zikion- gozwa na Marekani.
Dalili wazi ya hilo ni Marekani. Leo inaushinikiza Umoja wa Mataifa, kwa nguvu zake zote, ijitie hamnazo kwa sula lolote la usawa na uadilifu, ikishindwa inajitokeza waziwazi kupiga vita kila taifa litakalotaka haki na uadilifu na kuisaida dhulma na utaghuti popote ulipo; ni sawa uje kwa njia ya Israil au Ureno au hata kwa serkali ya kibaguzi ya Rhodesia[3] na Afrika kusini au kwengineko.
Siri ya yote hayo ni kuifagilia Marekani, kama kiongozi wa ukoloni. Lakini mwisho wa ubabe huu utakuwa kama wa Hitler, Dalili zimejionyesha wazi katika Vietnam. Ama masononeko yanayosababishwa na siyasa ya ukoloni yameena mashariki na magharibi, na masononeko haya hayatapita bure bila ya kuacha athari.
Mwanzo nilikuwa nikistaajbu kutokana na baadhi ya watu jinsi wanavyowadharau watu wema wenye ikhlasi na wasiwaheshimu, tena wanawaona ni kama watu wa kawaida; hata kama wakifanya maajabu gani na wakajitolea mhanga kuithibitisha haki!
Niliendelea kushangaa hivyo mpaka nilipofikia kufasiri Aya hii tuliyo nayo nikagundua kuwa fikra hii haiko kwa mataghuti na wafisadi tu; isipokuwa watu wengi wameondoa akilini ubora na msimamo na kuupima kwa chumo na faida tu; sawa na wale waliompiga vita Muhammad na waliosimama upande wa Israil katika Umoja wa mataifa na Baraza la usalama; isipokuwa tofauti yao hawa ni kuwa waliifuata njia ya ufisadi na utaghuti, lakini waliposhindwa basi wakabakia kwenye upinzani.
Je, hawajajua wale ambao wameamini kwamba lau Mwenyezi Mungu angelipenda bila shaka angeliwaongoa watu wote.
Neno hawajajua limefasiriwa kutoka neno Yay’as, Tabari anasema: “wametofautiana wafasiri kuhusu neno ‘yay’as’ … Usawa hasa ni kubainikiwa na wamenukuu tafsiri hii wengi akiwemo Imam Ali(a.s) . Na sisi ni miongoni mwa wale wanaoamini kuwa watu wa nyumba ndio wanojua zaidi kilichomo humo nyumbani.”
Vyovyote iwavyo ni kuwa makusudio ya wale ambao wameamini ni maswahaba wa Mtume(s.a.w.w) pale walipotamaani kuwa washirikina wamuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ndipo Mwenyezi Mungu aliyetukuka akwaambia, mpaka lini mtakuwa na tamaa ya kuamini washirikina?
Je, hajajua na kubainikiwa kuwa wao kivyovyote hawataamini hata kama wafu watazungumza nao au majabali yatembee. Achaneni nao na utaghuti wao! Lau Mwenyezi Mungu angelitaka kuwaingiza kwenye imani angelifanya, lakini hekima yake Mtukufu imepitisha kumwachia mtu na hiyari yake ili kuweza kumpa uhuru na ubinadamu wake.
Lau angelimnyang’anya uhuru huu na hiyari, basi asingelikuwa ni chochote, na wala asingelistahiki kusifiwa au kushutumiwa wala thawabu au adhabu, Angalia tafsir yetu Juz. 12 (11: 118).
Wala wale ambao wamekufuru hawaachi kusibiwa na balaa kwa waliyoyatenda au ikawateremkia karibu na nyumbani kwao mpaka iwafikie ahadi ya Mwenyezi Mungu.
Makusudio ya wale ambao wamekufuru ni wale waliomkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) . Maana ni kuwa Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu hawachi duniani hawa waliokadhibisha bila ya kuwatia adabu; bali anawateremshia balaa kila baada ya muda.
Hayo ni kwa sababu ya msimamo wao kwa Muhammad(s.a.w.w) . Au anawateremshia balaa karibu yao iwatie hofu na fazaa nyoyoni mwao. Analifuatilia hilo Mwenyezi Mungu mpaka itimie ahadi yake ya ushindi kwa Mtume wake.
Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi.
Vipi avunje miadi naye ndie mkweli zaidi wa ahadi. Maswahaba na kila mumin ana imani kuwa Mwenyezi Mungu atatekeleza ahadi na atalinusuru jeshi lake tu.
وَلَقَدِ اسْتُهْزِئَ بِرُسُلٍ مِّن قَبْلِكَ فَأَمْلَيْتُ لِلَّذِينَ كَفَرُوا ثُمَّ أَخَذْتُهُمْ فَكَيْفَ كَانَ عِقَابِ ﴿٣٢﴾
32. Na hakika walifanyiwa stihizai Mitume waliokuwa kabla yako, lakini nikawapa muda wale ambao wamekufuru, kisha nikawashika! Basi ilikuwaje adhabu!
أَفَمَنْ هُوَ قَائِمٌ عَلَىٰ كُلِّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ وَجَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ قُلْ سَمُّوهُمْ أَمْ تُنَبِّئُونَهُ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي الْأَرْضِ أَم بِظَاهِرٍ مِّنَ الْقَوْلِ بَلْ زُيِّنَ لِلَّذِينَ كَفَرُوا مَكْرُهُمْ وَصُدُّوا عَنِ السَّبِيلِ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ ﴿٣٣﴾
33. Je anayesimamia kila nafsi kwa yale iliyoyachuma na wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika! Sema watajeni, Au ndio mnampa habari ya yale asiyoyajua katika ardhi? Au ni maneno matupu? Bali wale ambao wamekufuru wamepambiwa vitimbi vyao na wamezuiliwa njia. Na anayepotezwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumuongoza.
لَّهُمْ عَذَابٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَشَقُّ وَمَا لَهُم مِّنَ اللَّـهِ مِن وَاقٍ ﴿٣٤﴾
34. Wanayo adhabu katika maisha ya dunia. Na hakika adhabu ya Akhera ina mashaka zaidi. Na wala hawana wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu.
Aya 32-34
Na hakika walifanyiwa stihizai Mitume waliokuwa kabla yako, lakini nikawapa muda wale ambao wamekufuru, kisha nikawashika! Basi ilikuwaje adhabu!
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamwambia Mtume wake, vumilia na uendele na mwito wako na achana nao wale wanokukejeli na jiweke mbali na maoni yao kwako, Walikwishafanya waliokuwa kabla yako, nikawaacha kisha nikawaadhibu adhabu isiyowezekana. Huu kwa hakika ndio mwisho wa wakadhibishaji.
Mwenyezi Mungu hakumtuma mtume ila anampa mambo mawili: Ujuzi wa dalili za kilimwengu na za kiakili juu ya kuweko Muumba na umoja wake, Na muujiza unaojitokeza mikononi mwake utakaojulisha utume wake. Jambo hilo la kwanza ni kwa ajili ya kuwakinahisha watu na Tawhidi (umoja wa Mungu) na la pili ni kwa jili ya kuwakinaisha watu kuwa yeye ni mtume wa Mwenyezi Mungu.
Wale wasioamini isipokuwa manufaa yao na chumo lao tu walikuwa wakiwakejeli Mitume na kuwafanyia maskhara pamoja na dalili zao na miujiza yao. Mwenyezi Mungu naye huwapa muda ili warudi kwenye uongofu na awaonye kwa kuwapa muda, kama alivyowaonya kwa hoja.
Je anayesimamia kila nafsi kwa yale iliyoyachuma.
Anaichunga nafsi na kuilinda na kudhibiti kila kitu, kisha kuilipa thawabu ikifanya mema na adhabu ikifanya uovu. Mwenye sifa zote hizi anafanywa kuwa wenzake ni mawe?Na wawemfanyia Mwenyezi Mungu washirika! Mwenyezi Mungu anasema:
أَفَمَن يَخْلُقُ كَمَن لَّا يَخْلُقُ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿١٧﴾
Ati anayeumba ni kama asiyeumba? Basi hivi hamkumbuki? (16:17).
Sema watajeni.
Yaani enyi washirikina tajeni angalau sifa moja tu inayostahiki kuabudiwa masanamu yenu, Hii ni dharau na dhihaka, sawa na mwoga kusema: Mimi ni shujaa, kisha aambiwe: tutajie ushahidi mmoja wa ushujaa wako.
Au ndio mnampa habari ya yale asiyoyajua katika ardhi?
Mwenyezi Mungu anasema hana mshirika na nyinyi manasema ana washirika wengi. Maana yake ni kuwa wao wanajua zaidi na Mwenyezi Mungu hajui.
Ametakaka Mwenyezi Mungu na hayo kabisa; kama wase- mavyo watu wa mantiki: kikipatikana chenye kulazimiwa ndio umepatikana ulazima na kikikosekana chenye kulazimiwa ndio umekosekana ulazima – likipatikana jua ndio umeptikana mchana na likikosekana jua ndio umekosekana mchana na ukikosekana mchana ndio hakuna jua.
Kwa hiyo ikiwa kuna mshrika, kwa vyovyote Mwenyezi Mungu atamjua. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu hamjui mshirika huyo basi hayupo; vinginevyo Mungu atakuwa halijui hilo, jambo ambalo haliwezekani.
Mwenyezi Mungu amehusisha kutaja ardhi pamoja nakuwa Yeye hana mshirika ardhini na mbinguni, kwa vile mazungumzo yanahusiana na masanamu yaliyoko ardhini.
Au ni maneno matupu.
Hilo ni tamko la kufahamisha maana ya kupatikana. Maneno yoyote yasiyofahamisha kitu halisi basi ni maneno matupu. Na neno washirika hapa ni majina yasiyokuwa na wenyewe:
إِنْ هِيَ إِلَّا أَسْمَاءٌ سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ ﴿٢٣﴾
“Hayo hayakuwa ila ni majina mliyoyaita nyinyi na baba zenu ambayo Mwenyezi Mungu hakuyateremshia dalili yoyote” (53:23).
Umepita mfano wa Aya hii katika Juz. 8 (7:710) na katika Juz, 12 (12:40).
Bali wale ambao wamekufuru wamepambiwa vitimbi vyao.
Maana ya vitimbi ni hadaa. Washirikina walihadaliwa na masanamu, wakayadhania ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika viumbe vyake na wakajipambia wenyewe hadaa hii.
Na wamezuiliwa njia kwa kuchukulia lisilojulikana.
Yaani lile walilojipambia limewazuilia wao na haki na imani ya Mwenyezi Mungu na umoja wake.
Na anayepotezwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumuongoza. Tazama Juz. 5 (4:88).
Wanayo adhabu katika maisha ya dunia kwa kupata hizaya na utwevu.
Na hakika adhabu ya Akhera ina mashaka zaidi, kwa sababu kila kitu duniani kusikiwa kwake ni kukubwa kuliko kuonekana kwake na kila kitu katika Akhera kuonekana kwake ni kukubwa kuliko kusikiwa kwake; kama asemavyo Imam Ali(a.s) .
Na wala hawana wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu na adhabu yake.