11%

13

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU

اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ وَسَخَّرَ لَكُمُ الْفُلْكَ لِتَجْرِيَ فِي الْبَحْرِ بِأَمْرِهِ وَسَخَّرَ لَكُمُ الْأَنْهَارَ ﴿٣٢﴾

32. Mwenyezi Mungu ndiye ambaye ameziumba mbingu na ardhi na akateremsha maji kutoka mbinguni. Na kwayo akatoa matunda kuwa riziki kwa ajili yenu. Na akafanya yawatumikie majahazi yanayopita baharini kwa amri yake, na akaifanya mito iwatumikie.

وَسَخَّرَ لَكُمُ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ دَائِبَيْنِ وَسَخَّرَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ ﴿٣٣﴾

33. Na akalifanya liwatumikie Jua na Mwezi daima. Na akaufanya usiku na mchana uwatumikie.

وَآتَاكُم مِّن كُلِّ مَا سَأَلْتُمُوهُ وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَتَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا إِنَّ الْإِنسَانَ لَظَلُومٌ كَفَّارٌ ﴿٣٤﴾

34. Na akawapa kila mlichomuomba, Na mkihisabu neema za Mwenyezi Mungu hamuwezi kuzidhibiti. Hakika mtu ni dhalimu mkubwa mwingi wa kukufuru.

NA AKATEREMSHA MAJI KUTOKA MBINGUNI

Aya 32 -34

MAANA

Aya zote hizi tatu umepita mfano wake kama ifuatavyo:

Kuumbwa mbingu na ardhi: Juz. 7 (6:73).

Kutermshwa maji kutoka mbinguni: Juz. 1 (2:22) na Juz. hii tuliyo nayo (13:18).

Kupita majahazi: Juz. 2 (2:164).

Kunufaika na Jua na Mwezi: Juz. hii (13:2). Usiku na mchana Juz. 11(10: 67).

Mwenyezi Mungu ameweka idadi ya neema nyingi kwa waja wake katika Juz. hii na Juz. 8 (6:143144) na nyinginezo nyingi zilizokwisha tangulia pamoja na tafsiri yake na ufafanuzi wake. Mwenyezi Mungu amerudia hapa au kuzidokeza kwa mnasaba wa kubadilisha neema kwa kufuru.

Kwa ufupi Aya hizi tatu zinamaanisha kuwa neema za Mwenyezi Mungu hazihisabiki; kama vile kuumbwa mbingu na ardhi, kuteremshwa maji kuenda majahazi faida za jua, mwezi, usiku na mchana. Vile vile kuwafadhili watu kwa waliyoomba na wasiyoomba, lakini pamoja na neema zote hizo wengi wanamkufuru na kuzikufuru neema zake huku wakiabudu yasiyowanufaisha wala kuwadhuru.

JE MTU ANA MAUMBILE YA HATIA?

Kwa mnasaba wa kauli yake Mwenyezi Mungu:Hakika mtu ni dhalimu mkubwa mwingi wa kukufuru, tunadokeza kwamba wataalamu wa saikolojia wametofautiana kuhusu binadamu, kuwa je, ana maumbile ya kufanya hatia, kwamba yeye amezaliwa kumfanyia uadui ambaye hajamfanyia uadui na kukufuru neema za aliyemfanyia wema (hana shukrani)

Mnamo mwaka 1832 watalamu 528 walikutana huko Amerika wakilijadili suala hili, Wengi wakaonelea kuwa hakuna dalili kuwa mwanadamu anaweza kuepuka kufanya makosa, lakini kundi jingine likapinga.

Sisi tunaamini kuwa binadamu hakuzaliwa kuwa ni mwenye kufanya makosa; vinginevyo angelikuwa hana taklifa yoyote na kuhisabiwa kwake na kuadhibiwa ingelikuwa ni dhulma na uonevu. Vile vile dini na sharia ingelkiuwa ni upuzi na mchezo; kama vile unyoya kwenye mavumo ya upepo. Isipokuwa anakuwa ni mwenye hatia kwa sababu nyingine za nje; kama vile njaa inayofanya awe mwizi, hadaa zinazomfanya awe na hiyana na kuwa kibaraka n.k.

Hapa ndio unapata tofauti baina ya watu katika nafsi zao, Wengine wanakuwa dhaifu mbele ya hadaa na kushindwa na matamnio; kama vile mwenye chakula lakini bado anataka ziada tena kwa hali yoyote; au mwenye mke anayemtosheleza, lakini anazini; au anayeificha haki kwa kupupia cheo au manufaa yoyote katika starehe za dunia. Hakuna mwenye shaka kwamba huyu amefanya dhambi kwa kutaka kwake sio kwa maumbile yake. Hayo ndiyo aliyoyakusudia Mwenyezi Mungu aliposema:

Hakika mtu ni dhalimu mkubwa mwingi wa kukufuru.

Ni wazi kuwa kupondokea haramu hakuifanyi kuwa ni halali, madamu iko nafasi ya kuweza kufanya subira na kushinda mapondokeo haya. Tumetangulia kueleza yanayoambatana na utafiti huu katika kufasiri Juz. 12 (11:9).

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ اجْعَلْ هَـٰذَا الْبَلَدَ آمِنًا وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الْأَصْنَامَ ﴿٣٥﴾

35. Na Ibrahim aliposema: Ewe Mola wangu! Ujaalie mji huu uwe wa amani na uniepushe mimi na wanangu na kuabudu masanamu.

رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ فَمَن تَبِعَنِي فَإِنَّهُ مِنِّي وَمَنْ عَصَانِي فَإِنَّكَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣٦﴾

36. Ewe Mola wangu! Hakika hayo yamewapoteza watu wengi, Basi atakayenifuata, hakika huyo ni katika mimi na atakayeniasi basi hakika wewe ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُوا الصَّلَاةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ ﴿٣٧﴾

37. Ewe Mola wetu! Hakika mimi nimeweka baadhi ya dhuria zangu katika bonde lisilokuwa na mmea, kwenye nyumba yako takatifu, ewe Mola wetu, ili wasimamishe Swala. Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao na uwaruzuku matunda ili wapate kukushukuru.

رَبَّنَا إِنَّكَ تَعْلَمُ مَا نُخْفِي وَمَا نُعْلِنُ وَمَا يَخْفَىٰ عَلَى اللَّـهِ مِن شَيْءٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ ﴿٣٨﴾

38. Ewe Mola wetu! Hakika wewe unajua tunayoyaficha na tunayoyafichua, na hapana kitu kinachofichikana mbele ya Mwenyezi Mungu katika ardhi wala mbingu.

الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي وَهَبَ لِي عَلَى الْكِبَرِ إِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ إِنَّ رَبِّي لَسَمِيعُ الدُّعَاءِ ﴿٣٩﴾

39. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliyenipa juu ya uzee wangu Ismail na Is-haq. Hakika Mola wangu ni mwenye kusikia sana dua.

رَبِّ اجْعَلْنِي مُقِيمَ الصَّلَاةِ وَمِن ذُرِّيَّتِي رَبَّنَا وَتَقَبَّلْ دُعَاءِ ﴿٤٠﴾

40. Ewe Mola wangu! Nijaalie niwe mwenye kuisimamisha Swala na katika dhuria zangu pia. Ewe Mola wetu! Na utakabalie dua yangu.

رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ ﴿٤١﴾

41. Ewe Mola wetu! Nighufirie mimi na wazazi wangu wawili na waumini siku ya kusimama hisabu.

EWE MOLA WANGU UJAALIE MJI HUU UWE WA AMANI

AYA 35-41

Na Ibrahim aliposema: Ewe Mola wangu! Ujaalie mji huu uwe wa amani.

Ibrahim na Ismail ndio waliojenga Al-ka’ba Makka. Angalia Juz. 1 (2:127).

Ibrahim na Ismail walimwomba Mola wao awajalie watu wawe na amani, na akawaitikia dua yao. Walikuwa na wanaendelea kuwa maadui wanakutana bila ya kuhofiana. Katika hili Mwenyezi Mungu ameashiria kwa kusema:

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا جَعَلْنَا حَرَمًا آمِنًا وَيُتَخَطَّفُ النَّاسُ مِنْ حَوْلِهِمْ ﴿٦٧﴾

“Je hawaoni kuwa tumeifanya nchi takatifu iwe ya amani na hali watu wengine wananyakuliwa kwa majirani zao? ” (29:67)

Na uniepushe mimi na wanangu na kuabudu masanamu.

Ni muhali kabisa kwa Ibrahim kuabudu masnamu. Itakuwaje ayaabudu naye aliyavunja kwa mikono yake na akawaambia:

أُفٍّ لَّكُمْ وَلِمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٦٧﴾ قَالُوا حَرِّقُوهُ وَانصُرُوا آلِهَتَكُمْ إِن كُنتُمْ فَاعِلِينَ ﴿٦٨﴾

Je, mnaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yasiyofaa chochote wala kuwadhuru, Kefle yenu! Na mnavyoviabudu badala ya Mwenyezi Mungu, Je, hamtii akili? (21:67-68).

lakini mitume wa Mwenyezi Mungu na manabii wake – pamoja na isma yao – wanaogopa maasi, Hofu hii ndiyo daraja ya juu ya utiifu. Anayejiona ni mtakatifu basi amemfungulia shetani madirisha.

MITUME NA KUITIKIWA DUA

Unaweza kuuliza : kuwa Ibrahim alimuomba Mola wake kuwa watoto wake wawe waumini, asimshirikishe Mwenyezi Mungu hata mmoja wao; na inajulikana kuwa wengi katika kizazi chake walimshirikisha Mwenyezi Mungu, wakaabudu masanamu, wakiwemo maquraish ambao wao ni katika kizazi chake?

Razi amenukuu majibu matano kutoka kwa wafasiri, lakini bado swali liko palepale linataka jawabu.

Tuonavyo sisi ni kuwa dua ni maombi na matarajio; ni sawa iwe inatoka kwa Nabii au mwinginewe. Inaweza kuwa hekima yake Mwenyezi Mungu inataka kuyakubali maombi na wakati mwingine kuyakataa. Wala hiyo haimaanishi kuwa aliyekataliwa maombi hana uzito wowote mbele ya Mungu kuweza kudhuru cheo cha utume na isma yake.

Hapana! Kwani kukataliwa maombi hakummaanishi hasira za mwenye kuombwa kwa muombaji; bali inawezekana kuwa ni mapenzi zaidi kwake na kuchunga masilahi yake. Nuhu(a.s) alimtaka Mwenyezi Mungu kumuokoa mtoto wake kutokana na kuangamia, Mola wake akamjibu kwa kusema: “Basi usiniombe usilo na ujuzi nalo” Juz.12 (11:46).

Kwa maneno mengine ni kuwa dua ya Nabii Ibrahim haina tafsiri nyingine zaidi ya hamu yake na mapenzi. Hakuna mwenye shaka kwamba manabii wana hamu na wanapendelea watu wote waamini na waongoke kwenye haki. Pamoja na hayo Mwenyezi Mungu alimwambia Bwana wa mitume aliyeadhimu:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ ﴿٥٦﴾

Hakika wewe huwezi kumwongoza umpendae, lakini Mwenyezi Mungu humuongoza amtakaye (28:56)

Lau yangehakikia kila wanayoyataka mitume basi asingelipatikana hata kafiri mmoja duniani na mitume wasingelisumbuka; hasa yule bwana wao na wa mwisho wao ambaye alisema: “Hakuudhiwa mtume kama nilivyoudhiwa mimi”

Ewe Mola wangu! Hakika hayo yamewapoteza watu wengi.

Makusudio ya hayo ni ya masanamu. Maana ni kuwa wengi katika watu wamepotea kwa sababu ya ibada ya masanamu; sawa na kusema: mali imempoteza fulani; yaani amepotea kwa sababu yake.

Basi atakayenifuata, katika kizazi changu,hakika huyo ni katika mimi kinasabu na kidini.Na atakayeniasi basi hakika wewe ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Atakayemuasi Ibrahim(a.s) basi yuko mbali naye sana hata kama ndiye aliyekaribu zaidi kiudugu kuliko watu wengine; Kwa sababu atakayemuasi atakuwa amemuasi Mwenyezi Mungu.

Lakini, pamoja na hayo, Ibrahim ni mpole mno mwenye kurudi kwa Mwenyezi Mungu; kama alivyomsifu yule aliyemchagua kuwa kipenzi na akamtakasa. Ndio maana hakuwatakia adhabu waasi katika kizazi chake, bali alimwachia Mwenyezi Mungu mambo yao kwa masamaha wake na maghufira yake.

Ilivyo ni kuwa akili haizuwii kusamehewa washirikina, kwa sababu adhabu ya washirikina ni haki ya Mwenyezi Mungu. Akitaka atwaadhibu na akitaka atawasamehe. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: “Hakika Mwenyezi Mungu hasamei kufanyiwa mshirika, lakini husamehe yasiyokuwa hayo” Juz.5 (4:48), ni dalili ya kiusikilizaji si dalili ya kiakili, Angalia tafsiri yetu huko, tumefafanua zaidi.

Ewe Mola wetu! Hakika mimi nimeweka baadhi ya dhuria zangu katika bonde lisilokuwa na mmea, kwenye nyumba yako takatifu, ewe Mola wetu, ili wasimamishe Swala.

Aliyasema haya Ibrahim(a.s) pale alipomwacha Ismail na mama yake Makka, pakiwa ni bonde kavu, halina chochote, si maji wala mmea; isipokuwa nyumba tu inayosimamishwa swala ndani yake na kukaririwa talbiya. Ni kwa lengo hili Ibrahim aliiweka baadhi ya famila yake mahali hapa pa kame. Lakini binadamu haishi kwa swala peke yake, bali hana budi apate mkate vile vile, ndipo Ibrahim akasema:

Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao na uwaruzuku matunda ili wapate kukushukuru.

Ikiwa kwenye nyumba ya Mwenyezi Mungu hakuna mmea wala kiwele, basi watu waelekee huko kwa ibada au biashara wakiwa na mkate na matunda, ili familia ya Ibrahim nayo ipate kula na kuweza kuswali na kushukuru.

Musa(a.s) alisema: “Mola wangu! Hakika mimi ni muhitaji wa heri utakyoiteremsha” (28:24). Imam Ali(a.s) anasema:“Wallahi hakumuomba isipokuwa mkate atakokula” Alisema mshairi aliye faqih: Fadhila ni za mkate lau si huo kamwe hata siku hakuna aabaduo.

Ewe Mola wetu! Hakika wewe unajua tunayoyaficha na tunayoyafichua, na hapana kitu kinachofichikana mbele ya Mwenyezi Mungu katika ardhi wala mbingu.

Baada ya Ibrahim kuuomba watu wafike nyumbani kwake wakiwachukulia familia yake mkate na matunda ili wapate nguvu na uchangamfu wa kuabudu, baada ya haya alisema maombi yangu haya si lolote ila ni unyenyekevu na kukiri kuwa wewe ni Muumba Mwenye kuruzuku. Ama haja yetu na masilahi yetu wewe unayajua zaidi kuliko sisi; tuwe tumekuomba au hatukuomba.

Kwa hiyo kauli ya Ibrahim ‘tunayofichua’ maana yake ni tunayoyaomba na maana ya ‘tunayoyaficha’ ni yale tusiyoyaomba.

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliyenipa juu ya uzee wangu Ismail na Is-haq. Hakika Mola wangu ni mwenye kusikia sana dua.

Shukrani hii kutoka kwa Ibrahim imechanganya maombi ya msaada wa Mwenyezi Mungu kwa wanawe, Ismaili na Is-haq. Kwa vile Ibrahim amekwishakuwa mzee na muda wake umekurubia, ndipo akawakilisha mambo ya familia yake kwa Mwenyezi Mungu; wala hakuwabainishia kitu au kuwalimbikizia mali watoto wake ili wastarehe na kuwanyima wengine.

Ewe Mola wangu! Nijaalie niwe mwenye kuisimamisha Swala na kati- ka dhuria zangu pia. Ewe Mola wetu! Na utakabalie dua yangu.

Swala ya Ibrahim sio aina ya hii swala tunayoiswali sisi; bali ni katika aina ya swala amabyo Mwenyezi Mungu ameiainisha kwa kusema:

إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ ﴿٤٥﴾

Hakika Swala huzuia mambo machafu na maovu (29:45).

Ndio hapa mafakihi wakaigawanya swala katika mafungu mawili: Swala ya kutekeleza wajibu tu, lakini mtekelezaji halipwi kitu; na Swala ya kutekeleza wajibu na mtekelezaji analipwa. Hiyo ni ile ambayo inaleta ikhlasi katika matendo na ukweli katika kuamiliana na watu.

Ewe Mola wetu! Nighufirie mimi na wazazi wangu wawili na waumini siku ya kusimama hisabu.

Tumetangulia kueleza katika Juz, 7 (6:74) tofauti baina ya Sunni na Shia kuhusu imani ya baba wa Ibrahim Al-khalil(a.s) . Miongoni mwa tuliyoyasema ni kuwa mzozo huu na mfano wake ni tasa, na kwamba linalotakikana kwa Mwislamu ni kuitakidi isma ya mitume, Ama kuamini kuwa mababa zao walikuwa waumini si itikadi ya uislamu kabisa.

Lau mtu atasema mimi ninamwamini Mungu na umoja wake, mitume na isma yao na siku ya mwisho na hisabu, lakini sithibitishi wala si kanushi imani ya mababa wa Mitume, Atakayesema hivi, tutamwambia kuwa wewe ni Mwislamu, unastahiki wanyostahiki waislamu nawe unawajibu wa kuwafanyia wanayostahiki waislamu wenzako.