11
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١٠٦﴾
106. Anayemkufuru Mwenyezi Mungu baada ya imani yake, Isipokuwa aliyelazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetua juu ya imani. Lakini aliyekifungulia kifua chake ukafiri, basi hao ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yao na watapata adhabu kubwa.
ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ وَأَنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ ﴿١٠٧﴾
107. Hiyo ni kwa sababu wao wamestahabu maisha ya dunia kuliko ya akhera, Na kwamba Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ طَبَعَ اللَّـهُ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ وَسَمْعِهِمْ وَأَبْصَارِهِمْ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ ﴿١٠٨﴾
108. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amepiga chapa juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao; na hao ndio wenye kughafilika.
لَا جَرَمَ أَنَّهُمْ فِي الْآخِرَةِ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿١٠٩﴾
109. Hapana shaka kwamba wao ndio wenye kuhasirika Akhera.
ثُمَّ إِنَّ رَبَّكَ لِلَّذِينَ هَاجَرُوا مِن بَعْدِ مَا فُتِنُوا ثُمَّ جَاهَدُوا وَصَبَرُوا إِنَّ رَبَّكَ مِن بَعْدِهَا لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١١٠﴾
110. Kisha hakika Mola wako kwa wale waliohajiri baada ya kusumbuliwa kisha wakafanya jihadi na wakasubiri, bila shaka Mola wako baada ya hayo ni Mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.
يَوْمَ تَأْتِي كُلُّ نَفْسٍ تُجَادِلُ عَن نَّفْسِهَا وَتُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَّا عَمِلَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿١١١﴾
111. Siku ambayo kila nafsi itakuja jitetea, Na kila nafsi italipwa sawa na yale iliyoyafanya, nao hawatadhulumiwa.
Aya 106 –111
Anayemkufuru Mwenyezi Mungu baada ya imani yake.
Tabari ametaja njia nne za irab ya jumla hii. Razi ametaja njia nne na akachagua moja kuwa iko mahali pa maf ’ul; kwa maana ya kukadiriwa kuwa, ninamkusudia kumtaja anayemkufuru...
Ama sisi tumechagua kuwa iko mahali pa mubdata (jumla ya kuanzia maneno) na Khabar yake (ukamailisho wake) ni jumla inayokadirwa kuwa, anayemkufuru Mwenyezi Mungu baada ya imani yake basi ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yake. Jumla hii inafahamika kutokana na jumla iliyo mwishoni mwa Aya hiyo hiyo: ‘Basi ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yao.
Isipokuwa aliyelazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetua juu ya imani.
Hii inafahamisha kuwa iko ruhusa ya kutamka neno la kufuru kwa ajili ya kujiokoa na kuuuliwa ikiwa mwenye kutamka ni muumini wa kweli.
Imeelezwa katika tafsiri ya Razi: Watu walilazimishwa neno la kufuru. Miongoni mwao ni Ammar na wazazi wake Yasir na Summayya. Vilevile Suhayb, Bilal, Khabbab na Salim, Wote hao waliaadhibiwa.
Summayya alifungwa baina ya ngamia wawili na akachomwa mkuki moyoni mwake na Yasir naye pia akauawa, lakini Ammar aliwapatia kile walichotaka kwa ulimi wake, akiwa amelazimika kufanya hivyo. Baadhi ya watu wakasema: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hakika Ammar amekufuru.
Mtume(s.a.w.w) akasema: Hapana! Hakika Ammar imani imemmjaa kuanzia utosini mwake hadi nyayoni mwake.
Ammar akamajia Mtume huku akilia, Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) akawa anampangusa machozi na kumwambia: Kwani una nini? Wakikurudia, rudia uliyosema, Yametangulia maelezo ya Taqiya katika Juz, 3 (3:28).
Lakini aliyekifungulia kifua chake ukafiri, basi hao ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yao na watapata adhabu kubwa.
Baada ya Mwenyezi Mungu kumtaja muumini halisi aliyedhihirisha kufu- ru, kuwa yeye anakubaliwa udhuru mbele ya Mwenyezi Mungu; sasa anamtaja yule kafiri wa kweli asiyekuwa na jengine zaidi ya kupendelea ukafiri. Hakuna malipo kwa huyu isipokuwa ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake kali.
Hiyo ni kwa sababu wao wamestahabu maisha ya dunia kuliko ya Akhera.
Hiyo ni ishara ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Wamestahabu, yaani wameathirika zaidi, Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawaondolea makafiri rehema yake na atawaadhibu kwa moto wake, kwa sababu wao wameathirika zaidi na maisha ya dunia na starehe zake.
Maana ya yote haya ni kuwa kila mwenye kuathirika na matamanio kuliko haki na mambo ya sasa kuliko yajayo, basi huyo mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama kafiri na mshirikina katika kustahiki ghadhabu na adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Na kwamba Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
Kwa maana ya kuwa Mwenyezi Mungu hawazingatii kuwa ni wenye kuongoka baada ya kustahabu ukafiri kuliko imani. Vilevile hawaongozi kwa maana ya kuwa hawalipi thawabu. Hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu amewaongoa kwa maana ya kuwa amewawekea dalili za kutosha juu ya kuweko kwake Mwenyezi Mungu na utume wa mitume yake. Mwenyezi Mungu anasema:
وَأَمَّا ثَمُودُ فَهَدَيْنَاهُمْ فَاسْتَحَبُّوا الْعَمَىٰ ﴿١٧﴾
Na ama Thamud tuliwaongoa, wakastahabu upofu kuliko uongofu” (41:17).
Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amepiga chapa juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao; na hao ndio wenye kughafilika.
Umetangulia mfano wa Aya hii pamoja na tafsiri yake katika Juz. 1 (2:2).
Hapana shaka kwamba wao ndio wenye kuhasirika Akhera.
Wala hapana hasara kubwa zaidi kuliko ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.
Kisha hakika Mola wako kwa wale waliohajiri baada ya kusumbuliwa kisha wakafanya jihadi na wakasubiri, bila shaka Mola wako baada ya hayo ni Mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.
Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja waumini halisi na makafiri dhahiri, hapa sasa anataja wale waliokuwa wamemwamini Mtume, lakini wakabakia Makka na wasihame naye kwenye Hijra, Wakawapa washirikina baadhi ya waliyoyataka. Kisha wakatubia, wakahama kwa Mtume na wakasubiri kwa kupigania jihadi dhidi ya washirikina na wafisadi. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amebainisha hukumu ya ya hawa kwa kusema: “Bila shaka Mola wako baada ya hayo ni Mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.”
Makusudio ya baada ya hayo ni hayo waliyoyatenda; kama unavyofahamisha mfumo wa maneno. Inawezekana pia ni kwa maana ya baada ya kutubia kwao pamoja na kuhama, jihadi na subira.
Katika tafsiri nyingi imeeelezwa kuwa Aya hii ilishuka kwa sababu ya jamaa fulani katika maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) waliokuwa wamebaki nyuma Makka na wasihame pamoja na Mtume. Washirikina wakawapa shida sana mpaka baadhi yao wakafitinishwa na dini yao; kisha wakajuta, lakini wakahofia kuwa toba yao haitatakabaliwa; ndipo ikashuka Aya hii.
Siku ambayo kila nafsi itakuja jitetea.
Yaani kila mtu siku ya Kiyama atajitetea mwenyewe, wala hatajishuguhulisha na mwingine:
لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ ﴿٣٧﴾
Kila mtu siku hiyo atakuwa na jambo linalomshughulisha, (80:37).
Na kila nafsi italipwa sawa na yale iliyoyafanya, nao hawatadhulumiwa.
Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٢٢﴾
“Na ili ilipwe kila nafsi kwa yale iliyoyachuma, nao hawatadhulumiwa” (45:22)
na pia kauli yake:
كُلُّ نَفْسٍ بِمَا تَسْعَىٰ ﴿١٥﴾
Ili kila nafsi ilipwe kwa iliyoyahangaikia, (20:15).
Yamekaririka maana ya Aya hii katika Aya nyingi.
وَضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا قَرْيَةً كَانَتْ آمِنَةً مُّطْمَئِنَّةً يَأْتِيهَا رِزْقُهَا رَغَدًا مِّن كُلِّ مَكَانٍ فَكَفَرَتْ بِأَنْعُمِ اللَّـهِ فَأَذَاقَهَا اللَّـهُ لِبَاسَ الْجُوعِ وَالْخَوْفِ بِمَا كَانُوا يَصْنَعُونَ ﴿١١٢﴾
112. Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mji uliokuwa na amani na utulivu, riziki yake ikiufikia kwa nafasi kutoka kila mahali. Lakini ukazikufuru neema za Mwenyezi Mungu; kwa hiyo Mwenyezi Mungu akauvika vazi la njaa na hofu kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyafanya.
وَلَقَدْ جَاءَهُمْ رَسُولٌ مِّنْهُمْ فَكَذَّبُوهُ فَأَخَذَهُمُ الْعَذَابُ وَهُمْ ظَالِمُونَ ﴿١١٣﴾
113. Na alikwishawajia Mtume kutoka miongoni mwao, lakini wakamkadhibisha, basi ikawafikia adhabu hali ya kuwa wamedhulumu.
Aya 112 – 113
Wafasiri wametofautiana kuhusu mji uliotajwa kuwa, je, ni mji hasa au ni kiasi cha kukadiria tu kwa ajili ya kupigia mfano? Razi amenukuu kutoka kwa wafasiri wengi kuwa makusidio ya mji huo ni Makka.
Vyovyote iwavyo, sifa hizi zinafanana na Makka na watu wake. Kwa sababu watu walikuwa na amani ya nafsi na mali zao; hawakuwa na hofu ya vita wala ujambazi; kama ilivyokuwa kwa miji mingine ya waarabu.
Pia wakazi wa hapo hawakuwa na haja ya kuhemea chakula, kwa sababu riziki ilkuwa ikiwajia kutoka kila mahali, kutokana na kuitikiwa dua ya Ibrahim(a.s) :
رَبَّنَا لِيُقِيمُوا الصَّلَاةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ ﴿٣٧﴾
Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao na uwaruzuku matunda. Juz; 13: (14:37).
Lakini watu wa Makka walizikufuru neema za Mwenyezi Mungu kwa kumkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) na wakaazimia kumuua mpaka akalazimika kuuhama mji wake.
Watu wa Makka walipatwa na njaa kwa dua ya Mtume(s.a.w.w) , pale aliposema: “Ewe Mola wangu! Wadhikishe kwa madhara na uajaalie miaka (ya shida) kama miaka ya Yusuf, Basi Mwenyezi Mungu akaitikia maombi yake. Wakapatwa na shida mpaka wakawa wanakula mizoga, majibwa, mifupa iliyochomwa, manyani na ngozi iliyochanganywa na damu.
Mtu alikuwa akiangalia mbinguni na kuona moshi kutokana na njaa. Ama hofu iliyowapata ni pale nchi ilipowatingisha wakaanguka ni mateka wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) .
فَكُلُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّهُ حَلَالًا طَيِّبًا وَاشْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّهِ إِنْ كُنْتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ {114 }
114. Basi kuleni katika vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu vilivyo halali na vizuri. Na shukuruni neema ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnamwabudu Yeye tu.
إِنَّمَا حَرَّمَ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةَ وَالدَّمَ وَلَحْمَ الْخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١١٥﴾
115. Hakika amewaharamishia mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilichosomewa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Basi aliyefikwa na dharura bila kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwengi maghufira, Mwenye kurehemu.
وَلَا تَقُولُوا لِمَا تَصِفُ أَلْسِنَتُكُمُ الْكَذِبَ هَـٰذَا حَلَالٌ وَهَـٰذَا حَرَامٌ لِّتَفْتَرُوا عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ إِنَّ الَّذِينَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ لَا يُفْلِحُونَ ﴿١١٦﴾
116. Wala msiseme uwongo kwa kuropokwa na ndimi zenu: Hiki ni halali na hiki ni haramu, mkimzulia uwongo Mwenyezi Mungu, Hakika wanaomzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafaulu.
مَتَاعٌ قَلِيلٌ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿١١٧﴾
117. Ni starehe ndogo nao watapata adhabu chungu.
وَعَلَى الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا مَا قَصَصْنَا عَلَيْكَ مِن قَبْلُ وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿١١٨﴾
118. Na wale waliokuwa mayahudi tuliwaharamishia tuliyokusimulia kabla, Na hatukuwadhulumu, laikini walijidhulumu wenyewe.
ثُمَّ إِنَّ رَبَّكَ لِلَّذِينَ عَمِلُوا السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ تَابُوا مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَأَصْلَحُوا إِنَّ رَبَّكَ مِن بَعْدِهَا لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١١٩﴾
119. Kisha hakika Mola wako kwa waliotenda uovu kwa ujinga kisha wakatubu baada ya hayo na wakatengenea, hakika Mola wako ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Aya 114 – 119
Basi kuleni katika vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu vilivyo halali na vizuri. Na shukuruni neema ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnamwabudu Yeye tu. Hakika amewaharamishia mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilichosomewa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Basi aliyefikwa na dharura bila kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwengi maghufira, Mwenye kurehemu.
Umetangulia mfano wa Aya hizi na tafsiri zake katika Juz. 2 (2:173) na katika Juz. 6 (5: 3)
Wala msiseme uwongo kwa kuropokwa na ndimi zenu: Hiki ni halali na hiki ni haramu.
Watu wa jahilia walikuwa wakijihalalalishia na kujiharamishia wao wenyewe tu; kisha wananasibisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu; kama kuhalalisha nyamafu, damu, nyama ya nguruwe na mnyama aliyechinjwa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Vilevile kusema kuwa aliye tumboni mwa mnyama huyu ni wa wanaume tu na ni haramu kwa wanawake na mengineyo yaliyotajwa katika Juz, 8 (6: 139 – 139).
Ndipo Mwenyezi Mungu akawakataza hayo na kusema kuwa ni uwongo na uzushi:Mkimzulia uwongo Mwenyezi Mungu.
Kila mwenye kumtegemezea Mwenyezi Mungu hukumu, kauli au jambo lolote bila dalili mkataa basi atakuwa amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo.
Hakika wanaomzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafaulu. Vipi watafaulu na Mwenyezi Mungu amewakasirikia na amewaandalia adhabu chungu?
Ni starehe ndogo nao watapata adhabu chungu.
Manufaa yoyote katika dunia hayalingani hata na ile adhabu ndogo ya akhera, sikwambi tena ikiwa ni ahabu kubwa:
نُمَتِّعُهُمْ قَلِيلًا ثُمَّ نَضْطَرُّهُمْ إِلَىٰ عَذَابٍ غَلِيظٍ ﴿٢٤﴾
Tunawastarehesha kidogo kisha tutawasukuma kwenye adhabu ngumu. (31:24).
Na wale waliokuwa mayahudi tuliwaharamishia tuliyokusimulia kabla.
Maneno haya anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) , Mwenyezi Mungu anamkumbusha yale aliyomwambia hapo nyuma: “Na kwa wale walio mayahudi tuliharamisha kila mwenye kucha. Na katika ng’ombe na mbuzi na kondoo tukawaharamishia mafuta yao; isipokuwa yale iliyobeba migongo yao, au matumbo, au iliyochanganyika na mifupa, Juz. 8 (6:146).
Na hatukuwadhulumu, laikini walijidhulumu wenyewe.
Kwa sababu wao walimwasi Mwenyezi Mungu na wakapetuka mipaka, ndipo akawaadhibu kwa uharamisho huu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
فَبِظُلْمٍ مِّنَ الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا عَلَيْهِمْ طَيِّبَاتٍ أُحِلَّتْ ﴿١٦٠﴾
“Basi kwa dhuluma ya ambao ni mayahudi tuliwaharamishia vitu vizuri walivyohalalishiwa,” Juz.6 (4:160).
Kisha hakika Mola wako kwa waliotenda uovu kwa ujinga kisha wakatubu baada ya hayo na wakatengenea, hakika Mola wako ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Umepita mfano wa Aya hii pamoja na tafsiri yake katika Juz.7 (6: 54).