7
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO
وَقُل لِّعِبَادِي يَقُولُوا الَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِنَّ الشَّيْطَانَ يَنزَغُ بَيْنَهُمْ إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلْإِنسَانِ عَدُوًّا مُّبِينًا ﴿٥٣﴾
53. Waambie waja wangu waseme maneno mazuri. Kwani shetani huchochea baina yao. Hakika shetani ni adui aliye dhahiri kwa mtu.
رَّبُّكُمْ أَعْلَمُ بِكُمْ إِن يَشَأْ يَرْحَمْكُمْ أَوْ إِن يَشَأْ يُعَذِّبْكُمْ وَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ وَكِيلًا ﴿٥٤﴾
54. Mola wenu anawajua vilivyo, akipenda atawarehemu na akipenda atawaadhibu. Na hatukukutuma ili uwe mlinzi juu yao.
وَرَبُّكَ أَعْلَمُ بِمَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَقَدْ فَضَّلْنَا بَعْضَ النَّبِيِّينَ عَلَىٰ بَعْضٍ وَآتَيْنَا دَاوُودَ زَبُورًا ﴿٥٥﴾
55. Na Mola wako anawajua vilivyo waliomo mbinguni na waliomo ardhini. Na hakika tumewafadhilisha baadhi ya manabii kuliko wengine; na Daud tulimpa Zaburi.
قُلِ ادْعُوا الَّذِينَ زَعَمْتُم مِّن دُونِهِ فَلَا يَمْلِكُونَ كَشْفَ الضُّرِّ عَنكُمْ وَلَا تَحْوِيلًا ﴿٥٦﴾
56. Sema: Waombeni hao mnaodai badala Yake; hawawezi kuwaondolea madhara wala kuyabadilisha.
أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ وَيَخَافُونَ عَذَابَهُ إِنَّ عَذَابَ رَبِّكَ كَانَ مَحْذُورًا ﴿٥٧﴾
57. Hao wanawaomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya kujikurubisha kwa Mola wao, hata walio karibu miongoni mwao, na wanataraji rehema zake na wanaihofu adhabu yake. Hakika adhabu ya Mola wako ni ya kuhofiwa.
WAAMBIE WAJA WANGU WASEME MANENO MAZURI
Aya 53 – 57
Waambie waja wangu waseme maneno mazuri.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwamrisha Mtume wake mtukufu awaamrishe waumini au watu wote waseme maneno mazuri, watamke haki na uadilifu kwa thamani yoyote itakayokuwa, Angali Juz; 13 (14: 24–26).
Kwani shetani huchochea baina yao.
Shetani hutafuta makosa ya ulimi ili ayafanye ni kuni za moto wa uadui na chuki baina ya watu. Makosa ya ulimi hayawi tu kwa kutukana bali pia kwa kusifu pasipokuwa mahali pake na kwenye matamshi ya ufuska na uovu.
Hakika shetani ni adui aliye dhahiri kwa mtu.
Uadui huu aliubainisha wazi pale aliposema:
قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ ﴿١٦﴾ ثُمَّ لَآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَائِلِهِمْ ﴿١٧﴾
“Kwa kuwa umenipoteza, basi hakika nitawakalia katika njia yako iliyonyooka; kisha hakika nitawaendea kwa mbele yao na nyuma yao na kuumeni kwao na kushotoni kwao” Juz; 8 (7:16-17).
Mola wenu anawajua vilivyo, akipenda atawarehemu na akipenda atawaadhibu.
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwadilifu na Mwenye hekima. Anajua hali za waja wake, yale yaliyo na masilahi nao na yale yenye ufisadi na anawachukulia kwa uadilifu wake na hekima yake.
Atamrehemu anayestahiki rehema naye ni yule anayefuata amri na mtiifu; Na atamwadhibu anayestahiki adhabu; naye ni yule muasi jeuri. Hiyo ni baada ya kuwawekea hoja kwa kuwafikishia yaliyo halali na yaliyo haramu kupitia kwa Mtume mtukufu.
Na hatukukutuma ili uwe mlinzi juu yao , bali ni mfikishaji:
فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَعَلَيْنَا الْحِسَابُ ﴿٤٠﴾
“Basi ni juu yako kufikisha na juu yetu hisabu,” Juz.13: (13:40).
Na Mola wako anawajua vilivyo waliomo mbinguni na waliomo ardhini. Na hakika tumewafadhilisha baadhi ya manabii kuliko wengine; na Daud tulimpa Zaburi.
Mwenyezi Mungu anawajua watu wa mbinguni na wa ardhini na anajua uwezo wa kila mmoja wao. Kwa misingi hiyo ndio huwachagua wajumbe kwenda kwa mitume wake; kama vile Jibril(a.s) . Na hupeleka mitume wabashiri na waonyaji kwa watu.
Kama alivyowafadhilisha baadhi ya Malaika kuliko wengine; vilevile Mitume, baadhi amaewafadhilisha kuliko wengine.
Unaweza kuuliza kuwa : Uislamu unasimama kwenye misingi ya usawa ;sasa kuna maana gani ya ubora huu kwa baadhi kuliko wengine? Kisha ubora huu utapatikana vipi kwa Malika na Mitume na hali tunajua kuwa wote ni waja wa Mwenyezi Mungu wenye kutukuzwa, hawamtangulii kwa jambo lolote na wanafanya kulingana na amri yake?
Jibu : Ndio ni kweli kuwa hakuna tofauti kwa msingi wa utiifu, isma, na utawala kama ulivyo; isipokuwa kwa upande wa sifa; kama vile dhahabu tunajua kuwa yote ina thamani, lakini kuna baadhi inathamani zaidi kuliko nyingine. Vile vile vitu vingine vizuri vinatofautiana kulingana na uzuri wake na daraja yake, sio katika kuwa kwake na hakika yake. Ndio maana ikasemwa: ‘Nuru juu ya nuru’ au ‘kheri juu ya kheri’
Swali la pili : imekuwaje Mwenyezi Mungu kumtaja Daud peke yake kuwa amempa Zaburi na tunajua kuwa Musa alimpa Tawrat, Isa Injil na Muhammad akampa Qur’an?
Amemtaja peke yake kuwarudi washirikina waliosema: vipi Muhammad atakuwa ni mtume na yeye ni yatima fukara. Njia ya kuwarudi ni kuwa Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaujalia ujumbe wake kwa yule anayestahiki - awe yatima aliyefukara, kama Muhammad au tajiri, kama Daud. Katika vitabu vingi vya sera na tarikh, hutajwa Mfalme Daud.
Sema: Waombeni hao mnaodai badala Yake, hawawezi kuwaondolea madhara wala kuyabadilisha.
Wafasiri wengi wamesema kuwa Aya hii na inayofuatia zilishuka kwa ajili ya wale wanaoabudu malaika, Isa na Uzayr. Na kwamba wanokusudiwa hapa sio waabudu masanamu, kwa sababu Mwenyezi Mungu amewataja hao waabudiwa kwa kusema: ‘wao wenyewe wanatafuta njia ya kujikuru- bisha kwa Mola wao,’ na kutafuta nji hakuelekeani na masanamu.
Kwa hiyo maana ni kuwa ewe Muhammad! Waambie wale wanaoabudu Malaika, Isa na Uzayr: yakiwapata madhara, kama ufukara na maradhi, basi waaombeni wale manowaabudu wawaondolee, kisha muangalie, je wanaweza kuwakinga au kuwabadilishia? Hakuna mwenye shaka ya kushindwa kwao, kwa vile wao wenyewe hawawezi kujikinga itakuwaje kwa mwengine?
Hao wanawaomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya kujikurubisha kwa Mola wao.
Yaani hao ambao mnawaabudu enyi washirikina wanatafuta kujikuruku- bisha kwa Mwenyezi Mungu kwa twaa, hawajitii kiburi kwa waja wengine, wanamtakasa na kumsujudia Mungu, sasa vipi nyinyi mnawaabudu.
Hata walio karibu miongoni mwao, na wanataraji rehema zake na wanaihofu adhabu yake.
Yaani kila mmoja kati ya Malaika, Isa na Uzayr anajitahidi, kumwabudu Mwenyezi Mungu na kumfanyia ikhlasi ili awe karibu na msamaha wake na rehema zake na awe mbali na machukivu yake.
Hiyo ni kwa vile Hakika adhabu ya Mola wako ni ya kuhofiwa.
Wanaihofia manabii na mawalii, je, wengine? Kila mwenye akili ni lazima ahofie mwisho na kuuandalia maandalizi, kwa hali yoyote atakavyokuwa na cheo na daraja; hasa ikiwa mwenye kuchukua hisabau anajua siri na yaliyofichikana.
وَإِن مِّن قَرْيَةٍ إِلَّا نَحْنُ مُهْلِكُوهَا قَبْلَ يَوْمِ الْقِيَامَةِ أَوْ مُعَذِّبُوهَا عَذَابًا شَدِيدًا كَانَ ذَٰلِكَ فِي الْكِتَابِ مَسْطُورًا ﴿٥٨﴾
58. Hapana mji wowote ila Sisi tutauangamiza kabla ya Siku ya Kiyama au kuupa adhabu kali, Haya yamekwishaandikwa kwenye Kitabu.
وَمَا مَنَعَنَا أَن نُّرْسِلَ بِالْآيَاتِ إِلَّا أَن كَذَّبَ بِهَا الْأَوَّلُونَ وَآتَيْنَا ثَمُودَ النَّاقَةَ مُبْصِرَةً فَظَلَمُوا بِهَا وَمَا نُرْسِلُ بِالْآيَاتِ إِلَّا تَخْوِيفًا ﴿٥٩﴾
59. Na hapana kinachotuzuia kupeleka miujiza ila ni kuwa watu wa zamani waliikanusha. Na wathamudi tuliwapa ngamia jike kuwa ni dalili inayoonekana, lakini wakamdhulumu. Nasi hatupeleki ishara ila kwa ajili ya kuhadharisha.
وَإِذْ قُلْنَا لَكَ إِنَّ رَبَّكَ أَحَاطَ بِالنَّاسِ وَمَا جَعَلْنَا الرُّؤْيَا الَّتِي أَرَيْنَاكَ إِلَّا فِتْنَةً لِّلنَّاسِ وَالشَّجَرَةَ الْمَلْعُونَةَ فِي الْقُرْآنِ وَنُخَوِّفُهُمْ فَمَا يَزِيدُهُمْ إِلَّا طُغْيَانًا كَبِيرًا ﴿٦٠﴾
60. Na tulipokwambia: hakika Mola wako amekwishawazunguka hao watu. Na hatukuifanya ndoto tuliyokuonyesha ila ni fitna (majaribu) kwa watu na mti uliolaaniwa katika Qur’an. Na tunawahadharisha, lakini haiwazidishii ila uasi mkubwa.
Aya 58 – 60
Hapana mji wowote ila Sisi tutauangamiza kabla ya siku ya Kiyama au kuupa adhabu kali, Haya yamekwishaandikwa kwenye Kitabu.
Dhahir ya Aya inafahamisha kuwa watu wote watatoweka kabla ya siku ya kiyama, ambapo itafika siku kwenye ardhi kutakuwa hakuna yoyote kabisa; na kwamba jambo hili limekwishaandikwa katika kadha na kadari ambayo haiepukiki. Kuna jamii itatoweka kwa mauti ya kawaida na nyingine kwa adhabu kali, lakini Mwenyezi Mungu hakubainisha wasifa wa hawa wala wale.
Hiyo ndiyo dhahir ya Aya, lakini wafasiri wamesema kuwa jamii njema itatoweka kwa mauti ya kawaida na jamii ya ufisadi itatoweka kwa adhabu kali. Lakini haya hayaafikianai na kauli yao katika kufasiri Aya za mwanzo za sura Hajj:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ إِنَّ زَلْزَلَةَ السَّاعَةِ شَيْءٌ عَظِيمٌ ﴿١﴾ يَوْمَ تَرَوْنَهَا تَذْهَلُ كُلُّ مُرْضِعَةٍ عَمَّا أَرْضَعَتْ وَتَضَعُ كُلُّ ذَاتِ حَمْلٍ حَمْلَهَا وَتَرَى النَّاسَ سُكَارَىٰ وَمَا هُم بِسُكَارَىٰ وَلَـٰكِنَّ عَذَابَ اللَّـهِ شَدِيدٌ ﴿٢﴾
“Enyi watu! Mcheni Mola wenu, Hakika tetemeko la Saa (ya Kiyama) ni jambo kuu. Siku mtakapoiona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau amnyonyeshae na kila mwenye mimba ataharibu mimba yake na utawaona watu wamelewa kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali,” (22:1-2).
Tuonavyo sisi mji alioukusudia katika kauli yake hii ni mji ambao watu wake ni madhalimu; yaani jamii yenye ufisadi tu; na kwamba Yeye ataiangamiza jamii hii au ataiadhibu kabla ya Siku ya Kiyama, wala hawatabakia ispokua watu wema tu, wote wakiwa wanaishi kwenye twaa ya Mwenyezi Mungu wakiwa na amani ya nafsi zao na vitu vyao vyote.
Kuna Hadith nyingi zinazozungumzia suala hilo; miongoni mwazo ni hizi:-
Hadith iliyoko kwenye Sunan Abi Daud As-sasjsataniy, kikiwa ni mojawapo ya Sahih sita kwa masunni, Juzuu ya pili chapa ya mwaka 1952, uk. 422:
“Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) : Lau haitabaki isipokuwa siku moja ya dunia, basi Mwenyezi Mungu atairefusha siku hiyo mpaka amlete mtu kutokana na watu wa nyumba yangu (Ahli bayti), Jina lake linafanana na jina langu na jina la baba yake ndio jina la baba yangu, ataijaza ardhi usawa na uadilifu; kama ilivyojazwa dhulma baada kujazwa usawa na uadilifu.”
Hadith iliyoko katika Sunan Ibn Maja, Pia nayo ni miongoni mwa sahih sita, juzuu ya pili chapa ya mwaka 1952, Hadith namba: 4083: Amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu: “Atakuwa katika umma wangu Mahdi, utaneemeka uma wangu neema ambayo haujaneemeka mfano wake.”
Mapinduzi na kujitoa mhanga kwa kujilipua (intifada), kila mahali kwa ajili ya kujikomboa na dhulma, ufisadi, ujinga na umasikini, yana fahamisha waziwazi kuwa hilo litakuwa tu karibuni au baadaye.
Na hapana kinachotuzuia kupeleka miujiza ila ni kuwa watu wa zamani waliikanusha. Na wathamudi tuliwapa ngamia jike kuwa ni dalili inayoonekana, lakini wakamdhulumu.
Washirikina walipendekeza kwa Mtume awaletee muujiza wanaoutaka wao. Miongoni mwa waliyoyasema ni: Tuchimbulie chemchem kutoka ardhini, tuletee Mungu na Malaika, tuletee kitabu kutoka mbinguni tukisome na mengineyo.
Ndio Mwenyezi Mungu akawajibu katika Aya hii, kwamba yeye amekwishapitisha katika kadha na kadari yake, kuwang’owa kwa adhabu kila kaumu iliyokadhibisha miujiza iliyokuja kwa maombi yao.
Wathamudi walimwomba Mtume wao awapatie ngamia wa muujiza. Alipowajia na sifa zile walizozitaka, walimkanusha na wakamchinja. Ukawanyakua ukelele wakawa ni wenye kuangamia; Yametangulia maelezo ya ngamia katika Juz; 8 (7:73 –79).
Imekwishapitisha kadari yake kutowang’oa Makuraishi, kutokana na mapendekezo waliyoyapendekeza kwa Mtume. Kwa sababu watapatikana watu watakaotubia na kuamini, watazaliwa wengine wapigania jihadi kwa Mwenyezi Mungu. zaidi ya hayo kadari ya Mwenyezi Mungu imepitisha kuwa uma wa Muhammad na sharia yake ubakie mpaka siku ya ufufuo. Kwa sababu hii na nyinginezo, Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuitikia maombi ya makuraishi.
Nasi hatupeleki ishara ila kwa ajili ya kuhadharisha.
Hakuna ishara yoyote inayodhihiri mikononi mwa Mtume ila ina malengo; yakiwemo: mawaidha, makaripio na kuhadharisha adhabu isiyokuwa na kinga wala kafara; sasa vipi wao wanaharakia kutoa maombi ya adhabu?
Na tulipokwambia: hakika Mola wako amekwishawazunguka hao watu.
Imeelezwa hapo juu kuwa makuraishi walimtaka Mtume awalete muujiza na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimpa wahyi Mtume wake kuwa lau atawaitikia maombi yao na wakaasi, wataangamia.
Lakini jawabu hili halikuwakinaisha washirikina na wakamwambia kuwa lau ungelikuwa ni Mtume ungelituletea yale tunayotaka, ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia mtume wake kuwa wewe endelea tu, wala usiwajali wale wanaofanya inadi na kiburi. Sisi tunawajua zaidi watu na wanayoy- afanya na tumewadhibiti.
Katika maana ya Aya hii ni ile isemayo:
وَاللَّـهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ ﴿٦٧﴾
“Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu,” Juz. 6 (5:67).
Na hatukuifanya ndoto tuliyokuonyesha ila ni fitna (majaribu) kwa watu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema kuwa alimuonyesha Mtume wake ndoto usingizini na kwamba ndoto yenyewe ni fitna, lakini hakubainisha ilikuwa ya aina gani wala makusudio ya hiyo fitna au majaribu.
Ndio maana wafasiri wakatofautiana katika maana yake, Akataja Razi kati- ka Tafsiri al-kabir, Abu Hayan Al-andalusi katika Al-bahrul-muhit, Muhammad bin Ahmad Al-kalabiy, katika Attas-hil na wengineo, wametaja kauli kadhaa katika tafsiri ya ndoto na fitna.
Miongoni mwazo ni mtume(s.a.w.w) aliota kuwa yeye ataingia Makka pamoja na swahaba, lakini alipotaka kuingia makuraishi walimzuia katika mwaka wa Hudaybiya.
Akaingiwa na shaka mwenye shaka miongoni mwa waislamu kuhusu ndoto ya Mtume, akamwambia: “Si umesema kuwa tutaingia Makka kwa amani?” Akasema: “Ndio, kwani nimesema tutaingia mwaka huu?” Akasema: “Hapana” Mtume(s.a.w.w) akasema: “Inshallah tutaingia” wakaingia mwaka uliofuatia.
Miongoni mwa kauli nyingine zinazotokana na tafsiri ni kuwa Mtume(s.a.w.w) aliona kwenye ndoto bani Umayya wakiiparamia mimbari yake kama anavyoparamia nyani, akahuzunika na akawa hana raha, na hakuonekana akicheka.
Kikundi miongoni mwa swahaba wako kwenye tafsiri hii; miongoni mwao ni Said bin Al-musabbib na Ibn Abbas; kama ilivyo katika Tafsiru-rrazi. Pia Sahal bin Sa’d; kama ilivyo katika Tafsir Al-bahr al-muhit.
Katika Sahih Al-bukhari Juzuu ya tisa Kitabu Al-fitan, imeelezwa kuwa Mtume(s.a.w.w) alisema: “Kuangamia kwa umma wangu kutakua mikononi mwa wafidhuli wa kikuraishi,” Riwaya hii inatia nguvu tafsiri ya ndoto kuhusu Bani Umayya.
Kwa hiyo makusudio yaNa mti uliolaaniwa katika Qur’an ni Bani Umayya. Katika Tafsiru-rrazi imeelezwa kuwa kuna kundi la wafasiri wanasema: “Mti uliolaaniwa katika Qur’an ni mayahudi.” Matukio ya Historia ya kale na ya sasa yamethibitisha kuwa mayahudi ndio mzizi wa fitina.
Na tunawahadharisha, lakini haiwazidishii ila uasi mkubwa.
Mwenyezi Mungu amewahadharisha wanafiki kwa mifumo mbalimbali, lakini haikufaa kitu; bali hizo hadhari ziliwazidishia upotevu, kwa sababu wao hawataharaki isipokuwa kwa wahyi wa masilahi na manufaa. Ama hoja, maadili na misimamo, kwao ni maneno na njozi tu.