8
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
قَالَ قَدْ أُوتِيتَ سُؤْلَكَ يَا مُوسَىٰ ﴿٣٦﴾
36. Akasema: Hakika umepewa maombi yako ewe Musa
وَلَقَدْ مَنَنَّا عَلَيْكَ مَرَّةً أُخْرَىٰ ﴿٣٧﴾
37. Na hakika tulikwisha kuneemesha mara nyingine
إِذْ أَوْحَيْنَا إِلَىٰ أُمِّكَ مَا يُوحَىٰ ﴿٣٨﴾
38. Pale tulipompa wahyi mama yako yale yaliyotolewa wahyi
أَنِ اقْذِفِيهِ فِي التَّابُوتِ فَاقْذِفِيهِ فِي الْيَمِّ فَلْيُلْقِهِ الْيَمُّ بِالسَّاحِلِ يَأْخُذْهُ عَدُوٌّ لِّي وَعَدُوٌّ لَّهُ وَأَلْقَيْتُ عَلَيْكَ مَحَبَّةً مِّنِّي وَلِتُصْنَعَ عَلَىٰ عَيْنِي ﴿٣٩﴾
39. Kwamba mtie katika kisanduku kisha kitupe mtoni na mto utamfikisha ufukweni. Atamchukua adui yangu na adui yake. Na nimekutilia mapenzi kutoka kwangu na ili ulelewe machoni mwangu
إِذْ تَمْشِي أُخْتُكَ فَتَقُولُ هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَىٰ مَن يَكْفُلُهُ فَرَجَعْنَاكَ إِلَىٰ أُمِّكَ كَيْ تَقَرَّ عَيْنُهَا وَلَا تَحْزَنَ وَقَتَلْتَ نَفْسًا فَنَجَّيْنَاكَ مِنَ الْغَمِّ وَفَتَنَّاكَ فُتُونًا فَلَبِثْتَ سِنِينَ فِي أَهْلِ مَدْيَنَ ثُمَّ جِئْتَ عَلَىٰ قَدَرٍ يَا مُوسَىٰ ﴿٤٠﴾
40. Dada yako alipokwenda na akasema: Je, niwajulishe mtu wa kuweza kumlea? Basi tukakurujesha kwa mama yako, ili macho yake yaburudike wala asihuzunike, Na ulimuua mtu nasi tukakuokoa katika dhiki. Na tukakujaribu kwa majaribio. Ukakaa miaka kwa watu Madyana. Kisha ukaja kama ilivyokadiriwa ewe Musa
وَاصْطَنَعْتُكَ لِنَفْسِي ﴿٤١﴾
41. Na nimekuchagua kwa ajili yangu.
Aya 36 – 41
Akasema: Hakika umepewa maombi yako ewe Musa, ya kukunjuliwa kifua, kufanyiwa wepesi kazi, kufunguka ulimi, kuongezewa nguvu kwa nduguyo na kushirikishwa kwenye utume pamoja nawe. Imam Aliy(a.s) anasema: “Kuwa kwenye lile usilolitaraji kuwa unalitarajia zaidi kuliko lile unalolitaraji. Kwani Musa Bin Imran alitoka akitafuta moto, akazungumza na Mwenyezi Mungu akarejea akiwa ni Mtume”
Na hakika tulikwisha kuneemesha mara nyingine.
Neema za Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa Musa zilkuwa nyingi; miongoni mwazo ni hizi zifuatazo:-
Pale tulipompa wahyi mama yako yale yaliyotolewa wahyi. Kwamba mtie katika kisanduku kisha kitupe mtoni na mto utamfikisha ufukweni. Atamchukua adui yangu na adui yake. Na nimekutilia mapenzi kutoka kwangu na ili ulelewe machoni mwangu
Makusudio ya wahyi hapa ni ilham – msukumo wa kufanya jambo. Macho ya Mwenyezi Mungu ni ulinzi wake.
Firauni alikuwa akimchinja kila anayezaliwa wa kiume katika waisrail na akizaliwa wa kike humfanya mjakazi. Mke wa Imran alipomzaa Musa alihofia Firauni, ndipo Mwenyezi Mungu akampa ilhamu ya kumweka kwenye sanduku kisha alitupe kwenye mto Nile, naye akafanya. Mungu akampa uthabiti wa moyo, Mto Nile ukalibebea sanduku hadi ufukweni. Inasemekana kuwa wajakazi wa Asiya, Mke wa Firaun, walitoka kwenda kuoga, wakakuta sanduku, wakalichukua. Mara tu mke wa Firauni alipolifungua na kuona mtoto, Mungu alimtia mahaba katika moyo wake:
وَقَالَتِ امْرَأَتُ فِرْعَوْنَ قُرَّتُ عَيْنٍ لِّي وَلَكَ لَا تَقْتُلُوهُ عَسَىٰ أَن يَنفَعَنَا أَوْ نَتَّخِذَهُ وَلَدًا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٩﴾
“Na mkewe Firauni akasema: Atakuwa kibirudisho cha macho kwangu na kwako. Msimuuwe! Huenda akatufaa au tumpange kuwa mtoto wetu” (28:9).
Kwa hiyo Faruni akambakisha na akalelewa katika kasri yake akilindwa na Mwenyezi Mungu.
Dada yako alipokwenda na akasema: Je, niwajulishe mtu wa kuweza kumlea? Basi tukakurujesha kwa mama yako, ili macho yake yaburudike wala asihuzunike.
Mwenyezi Mungu alitaka Musa arejee kwa mama yake, ili asiwe mbali naye na asiwe na wasiwasi, Mungu akitaka jambo, huliandalia sababu zake, Alizuwiya matiti yote yasiweze kumnyonyesha Musa, kiasi ambacho Firauni alihangaika.
Akaenda dada yake kwenye kasri ya Firauni na kusema mimi nitawafahamisha atakayemnyonyesha. Ndio akaenda na mama yake akakubali matiti yake, Firauni akamkabidhi na akampa ujira wake.
Na ulimuua mtu nasi tukakuokoa katika dhiki.
Siku moja Musa alikuwa akipita njiani, akawaona watu wawili wakipigana; mmoja ni wa upande wa Firaun na mmoja ni wa upande wake. Huyu wa upande wake akataka usaidizi kwa Musa, Akampiga ngumi yule mpin- zani, bila ya kukusudia kumuua, lakini akamuua, Musa akahofia kulipiziwa kisasi; Mwenyezi Mungu akamuondolea dhiki hiyo ya kisasi.
Haya yameashiriwa na Aya isemayo:
فَوَجَدَ فِيهَا رَجُلَيْنِ يَقْتَتِلَانِ هَـٰذَا مِن شِيعَتِهِ وَهَـٰذَا مِنْ عَدُوِّهِ فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ فَوَكَزَهُ مُوسَىٰ فَقَضَىٰ عَلَيْهِ ﴿١٥﴾
“Akakuta humo watu wawili wanapigana – mmoja ni katika kundi lake na mwengine ni katika maadui zake, Yule mwenzake akamtaka msaada dhidi ya adui, Musa akampiga ngumi akammaliza.” (28:15).
Na tukakujaribu kwa majaribio.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) humjaribu mja wake kwa furaha na dhiki. Mwenye kushukuru hayo na akavumilia haya, humkurubisha na kumpa thawabu. Na ambaye hazijali neema na akakufuru wakati wa shida, Mwenyezi Mungu humweka mabali na rehema yake. Mwenyezi Mungu (s.w.t) Alimjaribu Musa kwa aina nyingi ya shida na misukosuko, akampata ni mwenye kuvumilia na mwenye kumkumbuka Mungu, ndipo Mwenyezi Mungu akamtukuza kwa utume na kamuinua daraja ya juu.
Ukakaa miaka kwa watu Madyana
Hapo ni baada ya kuchunga wanyama wa Shuayb, kama ilivyoashiria kauli yake Mwenyezi Mungu:
فَإِنْ أَتْمَمْتَ عَشْرًا فَمِنْ عِندِكَ ﴿٢٧﴾
“Kama ukitimiza kumi ni hiyari yako” (28:27)
Na aliitimiza kumi, kama inavyoelezwa katika baadhi ya riwaya.
Kisha ukaja kama ilivyokadiriwa ewe Musa.
Umekuja mahali hapa, kwenye jangwa takatifu la Tuwa; umekuja wakati ule alioukadiria Mwenyezi Mungu kukutuma wewe kwa utume.
Na nimekuchagua kwa ajili yangu.
Yaani nimekuchagua kwa ajili ya wahyi wangu na risala yangu. Kutegemezwa Musa kwa Mwenyezi Mungu ni ukomo wa utukufu na hes- hima; ambapo inaashiria kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemjalia ni katika watu wake mahususi.
اذْهَبْ أَنتَ وَأَخُوكَ بِآيَاتِي وَلَا تَنِيَا فِي ذِكْرِي ﴿٤٢﴾
42. Nenda wewe na nduguyo pamoja na ishara zangu, wala msichoke kunikumbuka.
اذْهَبَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ إِنَّهُ طَغَىٰ ﴿٤٣﴾
43. Nendeni kwa Firauni, hakika yeye amepituka mipaka.
فَقُولَا لَهُ قَوْلًا لَّيِّنًا لَّعَلَّهُ يَتَذَكَّرُ أَوْ يَخْشَىٰ ﴿٤٤﴾
44. Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa.
قَالَا رَبَّنَا إِنَّنَا نَخَافُ أَن يَفْرُطَ عَلَيْنَا أَوْ أَن يَطْغَىٰ ﴿٤٥﴾
45. Wakasema: ewe Mola wetu! Hakika sisi tunaogopa asije akapindukia mipaka juu yetu au kufanya jeuri.
قَالَ لَا تَخَافَا إِنَّنِي مَعَكُمَا أَسْمَعُ وَأَرَىٰ ﴿٤٦﴾
46. Akasema: msiogope! Hakika mimi niko pamoja nanyi. Nasikia na ninaona.
فَأْتِيَاهُ فَقُولَا إِنَّا رَسُولَا رَبِّكَ فَأَرْسِلْ مَعَنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ وَلَا تُعَذِّبْهُمْ قَدْ جِئْنَاكَ بِآيَةٍ مِّن رَّبِّكَ وَالسَّلَامُ عَلَىٰ مَنِ اتَّبَعَ الْهُدَىٰ ﴿٤٧﴾
47. Basi mwendeeni na mumwambie: hakika sisi ni wajumbe wa Mola wako, basi tuachie wana wa israil wala usiwaadhibu. Tumekuletea ishara itokayo kwa Mola wako, Na amani itakuwa juu ya aliyefuata uongofu.
إِنَّا قَدْ أُوحِيَ إِلَيْنَا أَنَّ الْعَذَابَ عَلَىٰ مَن كَذَّبَ وَتَوَلَّىٰ ﴿٤٨﴾
48. Hakika tumepewa wahyi kwamba adhabu itampata anayekadhibisha na akapu- uza.
Aya 42-48
Nenda wewe na nduguyo pamoja na ishara zangu, wala msichoke kunikumbuka.
Makusudio ya ishara hapa ni miujiza, amabayo ni fimbo, mkono mweupe na miujiza mingineyo, tuliyoiashiria katika Juz. 15 (17:101). Maana ya msichoke kunikumbuka ni msipuuze risala yangu na kukumbusha amri yangu na makatazo yangu.
Nendeni kwa Firauni, hakika yeye amepituka mipaka.
Nendeni ni kusisitiza ile kauli ya ‘nenda wewe na nduguyo.’ Umetangulia mfano wa Aya hii katika Aya ya 23 ya sura hii tuliyo nayo.
Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa.
Kama wenye mashirika ya ukandamizaji watazingatia na kuogopa, basi Firauni angelizingatia na kuogopa.
Aya hii inapangilia mfumo wa kutoa mwito wa dini ya Mwenyezi Mungu. Kwa usahihi zaidi; inapanga mfumo wa kukinaisha haki. Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ﴿١٢٥﴾
“Waite kwenye njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora.” Juz. 14(16:125).
Mawaidha mazuri ni kujua mwenye hatia, makosa yake na mpotevu kujua ubaya wake na kujiona kuwa yuko mbali na haki na hali halisi ya mambo:
وَقَالُوا لَوْ كُنَّا نَسْمَعُ أَوْ نَعْقِلُ مَا كُنَّا فِي أَصْحَابِ السَّعِيرِ ﴿١٠﴾
“Na watasema: lau tungelikuwa tunasikia au kuwa na akili, tusingelikuwa katika watu wa motoni” (67:10)
Sharti la kwanza la mawaidha mazuri ni kutotaka lolote anayetoa mwaid- ha, zaidi ya kutengeneza. Kwamba lengo la kwanza na la mwisho liwe ni kuongoza na kurekebisha.
Sharti la pili ni kuwa mawaidha kwa kauli laini. Miongoni mwa aliyoyasema Musa kwa Firauni ni: Je, unapenda kujitakasa? Nami nitakuongoza kwa Mola wako upate kumcha.(79:19).
Wakasema: Ewe Mola wetu! Hakika sisi tunaogopa asije akapindukia mipaka juu yetu au kufanya jeuri.
Ewe Mola wetu unajua ubabe wa Firauni na kwamba hakuna anayeweza kumzuia akiamrisha tuuawe kabla hata hajasikia dalili na hoja tutaka- zomwambia, Je unaweza kutuongeza kitu kitakachohakikisha usalama wetu?
Akasema: msiogope! Hakika mimi niko pamoja nanyi. Nasikia na ninaona.
Mimi ninadhamini usalama wenu, ‘Mwenyezi Mungu ni tosha wa kuhi- fadhi na kunusuru’ Unaweza kuuliza kuwa dhamiri ya wakasema: ni ya wawili, Musa na Harun, na inajulikana kuwa Harun hakuwa na Musa katika majibizano, sasa je, kuna wajihi gani wa hilo?
Baadhi ya wafasiri wamejibu kuwa kauli hii ilikuwa ni ya Musa kwa kusema na ya Harun kwa kihali; Kwa sababu Harun anamfuata Musa. Inawezekana kauli hii inatokana na wote wawili pamoja baada ya kuondoka Musa kwenda Misr na kuungana na nduguye, kabla hawajakwenda kwa Firani. Ni kawaida ya Qur’an kuacha maneno ambayo yatafahamika kutokana na mazingira au na maneno mengine.
Basi mwendeeni na mumwambie: hakika sisi ni wajumbe wa Mola wako, basi tuachie wana wa israil wala usiwaadhibu kwa kuwachukua mateka, kuwadhalilisha, kuwachinja watoto wao wa kiume na kuwatumia watoto wao wa kike. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz.9 (7:104 –105).
Tumekuletea ishara itokayo kuwa Mola wako, kwa dalili za kutosha na hoja mkataa juu ya ukweli wetu.
Na amani itakuwa juu ya aliyefuata uongofu.
Uingofu ni dini ya Mwenyezi Mungu na amani ni kusalimika na adhabu yake. Yaani mwenye kuingia dini ya Mwenyezi Mungu amesalimika na adhabu ya kuungua.
Hakika tumepewa wahyi kwamba adhabu itampata anayekadhibisha na akapuuza.
Ni makemeo na maonyo kwa Firauni kuwa ataangamia na kubomoka kama atampuuz Musa na Harun kwa kuukana utume wao na kuenedelea kwenye upotevu wake na jeuri yake.
قَالَ فَمَن رَّبُّكُمَا يَا مُوسَىٰ ﴿٤٩﴾
49. Akasema: Basi Mola wenu ni nani ewe Musa?
قَالَ رَبُّنَا الَّذِي أَعْطَىٰ كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَىٰ ﴿٥٠﴾
50. Akasema: Mola wetu ni yule aliyekipa kila kitu umbo lake kisha akakiongoza
قَالَ فَمَا بَالُ الْقُرُونِ الْأُولَىٰ ﴿٥١﴾
51. Akasema Nini hali ya karne za mwanzo?
قَالَ عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي فِي كِتَابٍ لَّا يَضِلُّ رَبِّي وَلَا يَنسَى ﴿٥٢﴾
52. Akasema: Elimu yake iko kwa Mola wangu katika Kitabu, Mola wangu hapotei wala hasahau.
الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ مَهْدًا وَسَلَكَ لَكُمْ فِيهَا سُبُلًا وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجْنَا بِهِ أَزْوَاجًا مِّن نَّبَاتٍ شَتَّىٰ ﴿٥٣﴾
53. Ambaye amewafanyia ardhi kuwa tandiko, Na akawapitishia humo njia, Na akateremsha kutoka mbinguni maji, Na kwayo tukatoa namna mbali mbali za mimea.
كُلُوا وَارْعَوْا أَنْعَامَكُمْ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّأُولِي النُّهَىٰ ﴿٥٤﴾
54. Kuleni na mchunge wanyama wenu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa wenye akili
مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ ﴿٥٥﴾
55. Kutokana nayo tumewaumba na humo tumewarudisha na kutoka humo tutawatoa mara nyingine.
وَلَقَدْ أَرَيْنَاهُ آيَاتِنَا كُلَّهَا فَكَذَّبَ وَأَبَىٰ ﴿٥٦﴾
56. Hakika tulimwonyesha ishara zetu zote, lakini alikadhibisha na akakataa.
Aya 49 -56
Akasema: Basi Mola wenu ni nani ewe Musa?
Musa na Harun walikwenda kwa Firauni kama walivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu, wakamwambia kuwa sisi ni mitume wa Mola wako, tumekujia na hoja na dalili kuthibitisha ukweli wetu. Basi ukiingia kwenye dini ya Mwenyezi Mungu utasalimika na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake; vinginevyo, utakuwa miongoni mwa watakaoangamia.
Hii ilikuwa mara ya kwanza Firauni kusikia neno ‘Mola wako’ kwa sababu yeye hakubali kuwa kuna mola; kama anavyodai kuwa yeye ndiye Mola Mtukufu. Ndio maana akauliza: Ni nani huyo Mola aliyekutuma kwangu?
Akasema: Mola wetu ni yule aliyekipa kila kitu umbo lake kisha akakiongoza
Musa alimjibu Firauni swali lake, kuwa Mola wetu ni yule aliyeumba viumbe akavipa sura na akazifanya nzuri sura zake bila ya kuwa na msaidizi kwenye hilo. Ndiye ambaye amekifanya kila kiumbe kibakie na hali yake. Amesema Imam Aliy(a.s) : “Je, hamuangalii kile kidogo jinsi Mungu alivyokiumba na akapingilia vizuri umbile lake, akakiumbia usikizi na uoni na akakifanyia mifupa na nyama.
Ni kama kwamba Musa anamwambia Firauni: Hakika Mola ni yule aliyeumba vitu kutokana na kutokuwa na chochote. Sasa wewe ni wapi na wapi na huyu? Ni kama ilivyomtokea Ibrahim na Namrud:
قَالَ إِبْرَاهِيمُ فَإِنَّ اللَّـهَ يَأْتِي بِالشَّمْسِ مِنَ الْمَشْرِقِ فَأْتِ بِهَا مِنَ الْمَغْرِبِ فَبُهِتَ الَّذِي كَفَرَ ﴿٢٥٨﴾
“Ibrahim akasema: Hakika Mwenyezi Mungu hulichomoza jua mashariki, basi wewe lichomoze magharibi, Akafedheheka yule aliyekufuru” Juz; 3 (2:258)
Akasema – Firauni – Nini hali ya karne za mwanzo?
Karne za mwanzo anakusudia watu wa Nuh, A’d, Thamud na wengineo ambao walikuwa wakiabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu. Firauni alitaka, kwa jawabu hili, kumrudi Musa, kwamba lau kungelikuwa na Mungu kwa sifa amabazo umezitaja, basi wangelimwabudu watu waliopita, na tunajua kuwa wao walikuwa wakiabudu masanamu.
Jawabu hili linajipinga lenyewe; Kwa sababu kutoa dalili ya kutokuweko Mungu kwa ibada ya masanamu, ni sawa na poponundu, na upofu wake, kupinga kuweko jua.
Akasema: Elimu yake iko kwa Mola wangu katika Kitabu; Mola wangu hapotei wala hasahau.
Musa alimjibu Firauni kuwa mimi sina ujuzi wa ghaibu mpaka nikupe habari za uma zilizopita. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye ujuzi wa kila kitu na ujuzi wake daima hauingiliwi na mabadiliko wala kugeuka:
يَوْمَ يَبْعَثُهُمُ اللَّـهُ جَمِيعًا فَيُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا أَحْصَاهُ اللَّـهُ وَنَسُوهُ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ ﴿٦﴾
“Siku atakapowafufua Mwenyezi Mungu awaambie yale waliyokuwa wakaiyatenda, Mwenyezi Mungu ameyadhibiti na wao wameyasahau, Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kushuhudia kila kitu” (58:6).
Unaweza kuuliza kuwa : Musa alikuwa na uhakika kuwa waabudu masanamu walikuwa katika upotevu, kwanini hakumwambia Firauni kuwa walikuwa kwenye upotevu na badala yake akamwambia Mwenyezi Mungu ndiye ajuye hali yao?
Jibu : Lau angelisema kuwa watu wa karne za kwanza walikuwa wapotevu, Firauni angelimtaka dalili ya kuwakinaisha waliopo au awe na hoja ambayo wasingeweza kuipinga na wakati huo Musa hakuwa nayo. Ndio maana akamjibu Firauni yale ambayo asingeyatakia dalili.
Ambaye amewafanyia ardhi kuwa tandiko.
Umekwishatangulia ufafanuzi wa kutandikwa ardhi na kufanywa kwake tandiko katika Juz.13 (13:3)
Na akawapitishia humo njia ya kufuatia matumizi yenu, Na akateremsha kutoka mbinguni maji; Na kwayo tukatoa namna mbali mbali za mimea
Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:99).
Kuleni na mchunge wanyama wenu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa wenye akili
Makusudio ya ishara ni dalili za kuweko Mwenyezi Mungu Mtukufu. Wenye akili ni wale wenye busara. Mwenyezi Mungu amewahusisha kuwataja hapa kwa sababu wao wanaipata haki wakiwa wamejiepusha na hawa na matamanio.
Kuna Hadith ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), kwamba yeye amesema: “Hakika wabora wenu ni wale wenye akili. Wakasema: Ninani hao wenye akili ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema ni wale wenye khulka njema, walio makini, wenye kuwapatiliza mafukara, mayatima na majirani, wanawalisha chakula na wanadhihirisha maamkuzi kwa watu”
Kutokana nayo tumewaumba na humo tumewarudisha na kutoka humo tutawatoa mara nyingine.
Mtu ni mtoto wa ardhi kwa mwili wake. Ndiyo mada ya kuumbwa kwake na humo mnatoka chakula chake na kinywaji chake na juu yake anakwenda na kurudi. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anasema:“Ardhi ni mama yenu na ni mlezi wenu.”
Ni mama yetu kwa vile tumetokana nayo na ni mlezi wetu kwa vile inatulisha, kama anavyonyonyesha mama mtoto wake. Kisha tutarudi ardhini baada ya kufa, tuwe mchanga kama ilivyokuwa mwanzo, tena tuwe hai mara ya pili kwa ajili ya hisabu na malipo.
Hakika tulimwonyesha ishara zetu zote, lakini alikadhibisha na akakataa.
Aliyeonyeshwa ni Firauni. Makusudio ya ishara ni miujiza aliyoidhihirisha Mwenyezi Mungu mikononi mwa Musa na ikafahamisha waziwazi juu ya ukweli wa utume wake. Lakini itafaa wapi miujiza na maonyo yakigongana na masilahi na manufaa?