10
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA
وَإِن يُكَذِّبُوكَ فَقَدْ كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَعَادٌ وَثَمُودُ ﴿٤٢﴾
42. Wakikukadhibisha, basi wamekadhibisha kabla yao kaumu ya Nuh na kina A’d na Thamud.
وَقَوْمُ إِبْرَاهِيمَ وَقَوْمُ لُوطٍ ﴿٤٣﴾
43. Na kaumu ya Ibrahim na kaumu ya Lut.
وَأَصْحَابُ مَدْيَنَ وَكُذِّبَ مُوسَىٰ فَأَمْلَيْتُ لِلْكَافِرِينَ ثُمَّ أَخَذْتُهُمْ فَكَيْفَ كَانَ نَكِيرِ ﴿٤٤﴾
44. Na watu wa Madyan na Musa alikadhibishwa. Nikawapa muda makafiri kisha nikawatia mkononi, basi kulikuwaje kukanya kwangu?
فَكَأَيِّن مِّن قَرْيَةٍ أَهْلَكْنَاهَا وَهِيَ ظَالِمَةٌ فَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا وَبِئْرٍ مُّعَطَّلَةٍ وَقَصْرٍ مَّشِيدٍ ﴿٤٥﴾
45. Na miji mingapi tuliyoiangamiza iliyokuwa ikidhulumu. Ikaangukiana mapaa yake na visima vilivyoachwa na makasri yaliyo madhubuti?
أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَتَكُونَ لَهُمْ قُلُوبٌ يَعْقِلُونَ بِهَا أَوْ آذَانٌ يَسْمَعُونَ بِهَا فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى الْأَبْصَارُ وَلَـٰكِن تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ ﴿٤٦﴾
46. Je, hawatembei katika ardhi ili wapate akili za kuzingatia na masikio ya kusikilia? Kwani hakika si macho yanayopofuka, lakini zinazopofuka ni nyoyo zilizomo vifuani.
وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالْعَذَابِ وَلَن يُخْلِفَ اللَّـهُ وَعْدَهُ وَإِنَّ يَوْمًا عِندَ رَبِّكَ كَأَلْفِ سَنَةٍ مِّمَّا تَعُدُّونَ ﴿٤٧﴾
47. Wanakuharakisha ulete adhabu na hakika Mwenyezi Mungu hakhalifu miadi yake. Na hakika siku moja kwa Mola wako ni kama miaka elfu mnavyohisabu.
وَكَأَيِّن مِّن قَرْيَةٍ أَمْلَيْتُ لَهَا وَهِيَ ظَالِمَةٌ ثُمَّ أَخَذْتُهَا وَإِلَيَّ الْمَصِيرُ ﴿٤٨﴾
48. Ni miji mingapi nimeipa muda na hali ilikuwa imedhu- lumu, kisha nikaitia mkononi? Na kwangu mimi ndio marejeo yote.
قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّمَا أَنَا لَكُمْ نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٤٩﴾
49. Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni muonyaji kwenu niliye dhahiri.
فَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٥٠﴾
50. Basi wale ambao wameamini na wakatenda mema, watapata maghufira na riziki za heshima.
وَالَّذِينَ سَعَوْا فِي آيَاتِنَا مُعَاجِزِينَ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ ﴿٥١﴾
51. Na wanaojitahidi kuzipinga Aya zetu hao ndio watu wa motoni.
Aya 42 -51
Wakikukadhibisha, basi wamekadhibisha kabla yao kaumu ya Nuh na kina A’d na Thamud na kaumu ya Ibrahim na kaumu ya Lut na watu wa Madyan na Musa alikadhibishwa.
Makuraishi walimkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) na wakamtoa nyumbani kwake, Mwenyezi Mungu akamwambia Mtume wake, kwa kumtuliza na kumpoza moyo, kwamba hakuna la ajabu katika yanayokutokea. Kila Nabii alipambana na hayo uliyopamabana nayo.
Kisha akamtajia idadi ya manabii, kwa njia ya mfano tu; akiwemo Hud na watu wake walioitwa A’d, Swaleh na watu wake walioitwa Thamud. Ama watu wa Madyana hao ni watu wa Shuayb. Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:34).
Nikawapa muda makafiri kisha nikawatia mkononi, basi kulikuwaje kukanya kwangu?
Makusudio ya kukanya hapa ni adhabu, kwa maana ya kukanya kwa vitendo sio kwa maneno. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwacheleweshea makafiri adhabu mpaka ulipofika muda wake, akawapatiliza kwa upatilizo wa mwenye uweza asiyeshindwa. Aya inaashiria kwamba mwenye akili hatakikani kuharakisha mambo kabla ya kufikia muda wake.
Na miji mingapai tuliyoiangamiza iliyokuwa ikidhulumu.
Baada ya Mwenyezi Mungu kusema kuwa anawapa muda makafiri mpaka wakati maalum, sasa anaishiria kuangamia kwa miji ambayo watu wake wamedhulumu, ambayo ni mingi, kama inavyoashiria kauli yake: ‘Miji mingapi?’ Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:4).
Ikaangukiana mapaa yake?
Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (2:259) na Juz. 15 (18:42).
Na visima vilivyoachwa na makasri yaliyo madhubuti.
Yote haya yameachwa bila watu; yaani miji ya madhalimu imekuwa mahame, haina watu, ambapo hapo zamani ilikuwa imesheheni wenyeji na wageni wanaoitembelea.
Je, hawatemebei katika ardhi ili wapate akili za kuzingatia na masikio ya kusikilia?
Wanaambiwa wale waliomkadhibisha Muhammad(s.a.w. w ) . Yaani hawapati funzo kwa waliyowafikia wakadhibishaji na kuona jinsi miji yao ilivyokuwa mitupu? Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:137) na Juz. 14 (16: 36).
Kwani hakika si macho yanayopofuka, lakini zinazopofuka ni nyoyo zilizomo vifuani.
Kuna faida gani ya kusikia na kuona ikiwa moyo umepofuka? Kwa sababu masikio na macho ni nyenzo na akili ndio asili.
Wanakuharakisha ulete adhabu.
Wanaohimiza ni washirikana na anayehimizwa ni Muhammad(s.a.w.w) . Mtume alikuwa akiwapa kiaga cha adhabu ikiwa watang’ang’ania ushirikina.
Walikuwa wakisema yale waliyosema waliowatangulia kuwaambia mitume kila wanapowakataza ushirikina: “Tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni mkweli.”
Na hakika Mwenyezi Mungu hakhalifu miadi yake.
Kuharakisha au kuchelewesha si muhimu madamu ahadi itakuwa. Kuwa hakika ni kuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu kuwapa thawabu watiifu ni haki ya wale watiifu, hawezi kuihalifu.
Ama ahadi yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ya adhabu kwa waasi, hiyo ni haki yake Mwenyezi Mungu, akitaka anaweza kuitekeleza na akipenda anaweza kusamehe, ila ikiwa imetanguliwa na neno ‘Hatahalifu’ kama ilivyo katika Aya hii tuliyo nayo; ambapo amekanusha kutotekeleza aliyowaahidi makuraishi kutokana na msimamo wao kwa Mtume wa rehema.
Na hakika siku moja kwa Mola wako ni kama miaka elfu mnavyohisabu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawaambia washirikina; kuna haja gani ya kuharakisha adhabu ya Akhera na siku moja kwake ni kali kwenu kuliko adhabu ya miaka elfu katika miaka ya kiduniani? Kwa ufupi ni kuwa miaka elfu ni fumbo la vituko vya siku ya mwisho.
Ni miji mingapi nimeipa muda na hali ilikuwa imedhulumu, kisha nikaitia mkononi? Na kwangu mimi ndio marejeo yote.
Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii na Sura hii tuliyo nayo Aya 45 na pia sehemu hii tuliyo nayo. Mwenyezi Mungu amerudia kwa kusisitiza na kutoa hadhari.
Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni muonyaji kwenu niliye dhahiri.
Huu ndio umuhimu wa mitume, kufikisha ujumbe na kutoa onyo kwa yule mwenye kuupinga. Maana haya yamekaririka kwa mifumo mbalimbali.
Basi wale ambao wameamini na wakatenda mema, watapata maghufira na riziki za heshima.
Maana yako wazi, na yametangulia kwenye Aya kadha, ikiwemo Juz. 1 (2:25).
Na wanaojitahidi kuzipinga Aya zetu hao ndio watu wa motoni.
Yaani washirikina wataingia motoni kwa muda usiokuwa na ukomo kwa sababu ya kumfanyia inadi Mtume na kujitahidi kumpinga kufikisha ujumbe wa Mola wake na kuwazuilia nao watu.
وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ وَلَا نَبِيٍّ إِلَّا إِذَا تَمَنَّىٰ أَلْقَى الشَّيْطَانُ فِي أُمْنِيَّتِهِ فَيَنسَخُ اللَّـهُ مَا يُلْقِي الشَّيْطَانُ ثُمَّ يُحْكِمُ اللَّـهُ آيَاتِهِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٥٢﴾
52. Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii anaposoma ila shetani hutumbukiza katika masomo yake. Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa anayoyatumbukiza shetani; kisha Mwenyezi Mungu huzi- makinisha Aya zake na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, mwenye hekima.
لِّيَجْعَلَ مَا يُلْقِي الشَّيْطَانُ فِتْنَةً لِّلَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ وَالْقَاسِيَةِ قُلُوبُهُمْ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ لَفِي شِقَاقٍ بَعِيدٍ ﴿٥٣﴾
53. Ili alifanye lile alilolitumbu iza shetani ni mtihani kwa wale wenye maradhi katika nyoyo zao na wale ambao nyoyo zao zimesusuwaa. Na hakika madhalimu wamo katika uasi wa mbali.
وَلِيَعْلَمَ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ أَنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ فَيُؤْمِنُوا بِهِ فَتُخْبِتَ لَهُ قُلُوبُهُمْ وَإِنَّ اللَّـهَ لَهَادِ الَّذِينَ آمَنُوا إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٥٤﴾
54. Ili wajue wale ambao wamepewa elimu kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wako na zinyenyekee kwake nyoyo zao. Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye awaongozaye wale ambao wameamini kwenye njia iliyonyooka.
وَلَا يَزَالُ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي مِرْيَةٍ مِّنْهُ حَتَّىٰ تَأْتِيَهُمُ السَّاعَةُ بَغْتَةً أَوْ يَأْتِيَهُمْ عَذَابُ يَوْمٍ عَقِيمٍ ﴿٥٥﴾
55. Na wale ambao wamekufuru hawataacha kuwa katika wasiwasi katika hilo mpaka saa iwafikie ghafla au iwafikie adhabu ya siku tasa.
الْمُلْكُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴿٥٦﴾
56. Ufalme siku hiyo ni wa Mwenyezi Mungu. Atahukumu baina yao. Basi wale ambao wameamini na wakatenda mema, watakuwa katika Bustani zenye neema.
وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا فَأُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿٥٧﴾
57. Na wale ambao wamekufuru na wakazikadhibisha ishara zetu watapata adhabu ifedheheshayo.
Aya 52 -57
Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii anaposoma ila shetani hutumbukiza katika masomo yake.
Wametofautiana wafasiri kuhusu neno Nabii na Mtume, (Nabiy na Rasul)[6] kuwa je, ni ibara zenye maana moja au kila moja ina maana yake?
Kauli iliyo karibu zaidi ni ile isemayo kuwa hakuna tofauti baina yake; kwa vile kila mmoja kati yao anatanabahishwa na Mwenyezi Mungu kwa lile analolitaka. Kwa hiyo akitanabahishwa na kuamrishwa kufikisha yale aliyotanabahishwa, huyo anaitwa Nabii kwa sababu Mwenyezi Mungu amemtanabahisha na pia anaitwa Mtume kwa sababu Mwenyezi Mungu amemtumma kufikisha.
Ikiwa amemtanabahisha tu bila ya kumwamuru kufikisha, basi huyo atakuwa ni Nabii tu. Hiyo ni kusema kuwa kila Mtume ni Nabii, lakini sio kila Nabii ni Mtume.
Kuna riwaya inayosema kuwa sababu ya kushuka Aya hii ni kwamba Mtume(s.a.w.w) aliwasomea makuraishi Sura Najm, alipofikia kwenye Aya isemayo:
أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ ﴿١٩﴾ وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ ﴿٢٠﴾
“Je, mmewaona Lata na Uzza na Manata mwingine wa tatu” (53: 19 – 20)
basi shetani aliingiza katika kisomo cha Mtume maneno haya: “Hao ni wazuri watukufu na kwamba maombezi yao bila shaka yanatarajiwa,” yani haya masanamu ni mazuri na uombezi wao unatarajiwa kwa Mwenyezi Mungu.
Maulama wahakiki wamekanusha riwaya hii na wakakata kauli kuwa hiyo ni miongoni mwa uzushi wa wazandiki wanaotaka kukitia ila Kitabu cha Mwenyezi Mungu na utume wa Muhammad(s.a.w.w) .
Wametegemea, katika hilo, kwenye dalili mkataa za kiakili na kinakili. Mtume ambaye ametumwa na Mwenyezi Mungu kupiga vita ushirikina na kuabudu mizimu, halafu huyo huyo arudi kuisifia kwa sifa za ukamilifu! Vipi iwe hivyo na ulimi wa Mtume unamtarjumu na kumbainisha Mwenyezi Mungu? Shetani anaweza kupata nafasi kwenye ubainifu na tafsiri hii ya kimungu?
Usahihi wa maana ya Aya ni kuwa ukomo wa usomaji wa Mtume yeyote, ni kuwafahamisha watu uhakika wa risala yake ili waweze kuifahamu na kuongoka nayo, lakini wenye tamaa wanaingilia kati kwa kuvungavunga na kueneza kila aina ya propaganda.
Haya tumeyashuhudia na kuyaona hasa. Haya ndio maana ya kutumbukiza shetani katika usomi wa Nabii. Nabii anawatakia heri watu na shetani muharibifu anawazuia wasiipate.
Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa anayoyatumbukiza shetani; kisha Mwenyezi Mungu huzimakinisha Aya zake na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, mwenye hekima.
Wabatilifu wanaunda njama na kuzitangaza, lakini Mwenyezi Mungu huondoa ubatilifu wao na kuufedhehi uwongo wao kwenye ndimi za wakweli na mikononi mwa wapigania jihadi. Aya nyingine yenye maana hii ni ile isemayo:
يُرِيدُونَ أَن يُطْفِئُوا نُورَ اللَّـهِ بِأَفْوَاهِهِمْ وَيَأْبَى اللَّـهُ إِلَّا أَن يُتِمَّ نُورَهُ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ ﴿٣٢﴾
“Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywavyao. Na Mwenyezi Mungu amekataa isipokuwa kuitimiza nuru yake, ijapokuwa makafiri wamechukia.” Juz.10 (9:32).
Ili alifanye lile alilolitumbukiza shetani ni mtihani kwa wale wenye maradhi katika nyoyo zao na wale ambao nyoyo zao zimesusuwaa.
Wenye maradhi katika nyoyo ni wezi wanaoishi kwa unyang’anyi, uporaji, ghushi na utapeli. Ama waliosusuwaa nyoyo zao ni wale ambao ni bendera hufuata upepo. Maana ni kuwa kampeni za uwongo hazina nafasi isipokuwa kwa wezi na walio na bendera.
Popote utakapoelekea utakuta picha hii waziwazi; hasa kwenye magazeti, idhaa, vitabu, michezo ya kuigiza na katika mazungumzo ya vibaraka na wale wanaodanganywa ambao wanaamini kila wanayoambiwa bila ya kuchunguza; tena ni wengi.
Kisha kampeni za uwongo, hata kama zitakuwa zina madhara kwa upande fulani, lakini zina manufaa kwa upande mwingine. Kwa sababu zinamtambulisha muhaini na mwenye ikhlasi, vile vile mjinga na mjuzi. Haya ndio makusudio ya neno mtihani.
Na hakika madhalimu wamo katika uasi wa mbali.
Kila mwenye kuvungavunga na akafanya uzushi basi ni dhalimu, na kila mwenye kuusadikisha uwongo na uzushi bila ya kuuchuunguza pia huyo ni dhalimu.
Ili wajue wale ambao wamepewa elimu kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wako na zinyenyekee kwake nyoyo zao.
Neno ‘hiyo’ hapa ni hiyo Qur’an. Pia inaweza kufasirika ‘huyo’ kwa maana ya huyo Nabii. Maana ni kuwa, ikiwa mtu atasadikisha uwongo juu ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi wenye maarifa na ikhlasi, wanajua hakika ya uwongo na uzushi huo; jambo ambalo linawazidishia imani na mshikamano kwa Mwenyezi Mungu, mitume yake na vitabu vyake na pia unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu.
Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye awaongozaye wale ambao wameamini kwenye njia iliyonyooka.
Anawaongoza Mwenyezi Mungu kwenye njia yake na kuifuata kwa kujikurubisha kwake hata kukiwa na kampeni za uwongo na vikwazo kiasi gani.
Na wale ambao wamekufuru hawataacha kuwa katika wasiwasi kati- ka hilo mpaka saa iwafikie ghafla au iwafikie adhabu ya siku tasa.
Makusudio ya saa ni ile saa ya kutoka watu kuelekea kwa Mola wao wakitokea makaburini (Kiyama). Siku tasa ni siku ya hisabu. Utasa ni kinaya cha makafiri kukata tamaa ya kuokoka.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kueleza, katika Aya iliyotangulia, kuwa wenye elimu wanaamini Qur’an na utume wa Muhammad(s.a.w.w) , kwenye Aya hii anasema kuwa makafiri wako katika shaka kuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu na watendelea kuwa katika shaka hiyo mpaka siku ya kufufuliwa kwao makaburini au siku ya kusimama kwao mbele ya Mwenyezi Mungu kwa hisabu.
Na hapo ndipo itawafichukia hakika yao na watajua kuwa wao walikuwa kwenye upotevu.
Ufalme siku hiyo ni wa Mwenyezi Mungu peke yake, hakuna kadhi au amiri wala raisi au waziri; kama ilivyo katika maisha haya ya duniani.Atahukumu baina yao . Yaani baina ya makafiri na waumini.
Basi wale ambao wameamini na wakatenda mema, watakuwa katika Bustani zenye neema. Na wale ambao wamekufuru na wakazikadhibisha ishara zetu watapata adhabu ifedheheshayo.
Hawa watapata hizaya na moto na wale watapata Pepo na raha. Mfano wa Aya hizi umekwishatangulia mara nyingi.