20
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI
Sura Ya Thelathini Na Tatu: Surat Ahzab. Imeshuka Madina, Ina Aya 73.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ اتَّقِ اللَّـهَ وَلَا تُطِعِ الْكَافِرِينَ وَالْمُنَافِقِينَ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿١﴾
1. Ewe Nabii! Mche Mwenyezi Mungu wala usiwatii makafiri na wanafiki. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
وَاتَّبِعْ مَا يُوحَىٰ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا ﴿٢﴾
2. Na fuata uliyoletewa wahyi kutoka kwa Mola wako. Hakika Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.
وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ وَكِيلًا ﴿٣﴾
3. Na mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni wa kutegemewa.
Aya 1-3
Ewe Nabii! Mche Mwenyezi Mungu wala usiwatii makafiri na wanafiki. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hekima. Na fuata uliyoletewa wahyi kutoka kwa Mola wako. Hakika Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda. Na mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni wa kutegemewa.
Katika Aya hizi Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemwamrisha Nabii wake mtukufu, kuwa na takua, kumtegemea Yeye, kuutumia wahyi wake na kutowatii makafiri na wanafiki.
Wafasiri wamejiuliza kuwa Nabii ni maasumu, sasa kuna haja gani ya amri zote hizi na kukatazwa uasi?
Kuna waliojibu kuwa hii ni kusisitiza utiifu na unyenyekevu alio nao Nabii(s.a.w.w) . Wengine wakasema kuwa Abu Sufyan alimtaka Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) kutoyatukana masanamu wanayoyaubudu makauraishi. Abu Sufyani wakati huo alikuwa pamoja na kundi la makafiri na wanafiki.
Sisi huko nyuma tumesema mara kwa mara kuwa aliye juu ana uwezo wa kumwamrisha aliye chini na kumkataza maasi hata kama ni maasumu. Hivi sasa tunayaunganisha hayo na haya yafutayo:
Hakuna kitu kizito kwa yule asiyemuogopa Mwenyezi Mungu kuliko tamko la ‘mche Mungu;’ wala hakuna adui mkubwa kuliko atakayelisema tamko hilo kwake. Imenukuliwa kutoka kutoka kwa Abdul-Malik bin Marwani kwamba yeye alipotawala alisema katika hotuba: “Kuanzia leo, atakayeniambia: mche Mungu, nitamkata shingo yake.”
Ama yule mwenye kuhofia kukutana na Mola wake na akaikanya nafsi na matamanio, basi kwake yeye hilo ni tamko la mapenzi na huruma na hutamani lau angelisikia mara kwa mara; hata kama ni maasumu wa makosa na madhambi; bali huko kulipenda na kulisikilza kumetokana na umaasumu na utiifu wake. Mtu adhimu huwa anajituhumu kwa upunguvu kadiri atakavyoweza kujitahidi.
Kwa hiyo basi hakuna haja ya kuleta taawili na tafsiri nyingine. Kuongezea kuwa amri ya takuwa kwa bwana wa watu na majini ni hekima na somo kubwa kwa wenye vyeo na watawala, kwamba kwa vyovyote watakavyokuwa wakubwa, lakini hawako zaidi ya kuamrishwa uadilifu na takua.
Kwenye Nahjul balagha imeelezwa: “Ambaye itakuwa uzito kwake kuambiwa neno la haki au kuelezwa uadilifu basi itakuwa kuyafanya mawili hayo ni uzito zaidi.”
مَّا جَعَلَ اللَّـهُ لِرَجُلٍ مِّن قَلْبَيْنِ فِي جَوْفِهِ وَمَا جَعَلَ أَزْوَاجَكُمُ اللَّائِي تُظَاهِرُونَ مِنْهُنَّ أُمَّهَاتِكُمْ وَمَا جَعَلَ أَدْعِيَاءَكُمْ أَبْنَاءَكُمْ ذَٰلِكُمْ قَوْلُكُم بِأَفْوَاهِكُمْ وَاللَّـهُ يَقُولُ الْحَقَّ وَهُوَ يَهْدِي السَّبِيلَ ﴿٤﴾
4. Mwenyezi Mungu hakumwekea mwanamume nyoyo mbili ndani yake. Wala hakuwafanya wake zenu – mnaowalinganisha migongo yao na migongo ya mama zenu – kuwa ni mama zenu. Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu. Hiyo ni kauli yenu kwa vinywa vyenu tu. Na Mwenyezi Mungu anasema haki, naye huongoza njia.
ادْعُوهُمْ لِآبَائِهِمْ هُوَ أَقْسَطُ عِندَ اللَّـهِ فَإِن لَّمْ تَعْلَمُوا آبَاءَهُمْ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ وَمَوَالِيكُمْ وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَـٰكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥﴾
5. Waiteni kwa baba zao. Hilo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Kama hamuwajui mababa zao basi ni ndugu zenu katika dini na rafiki zenu. Si vibaya kwenu kwa mlivyokosea, lakini kwa yale ziliyoyakusudia nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
MWENYEZI MUNGU HAKUMWEKA MTU MMOJA NYOYO MBILI
Aya 4 – 5
Mwenyezi Mungu hakumwekea mwanamume nyoyo mbili ndani yake.
Hata mwanamke pia ni kama mwanamume. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemuhusu mwanmume hapa kwa sababu amemwamrisha Mtume(s.a.w.w) wake mtukufu kuwa na takua, kwa hiyo ikanasibiana kufuatishia amri hii kuwa mwanamume hawezi kuwa na moyo mmoja wa kumcha Mwenyezi Mungu na mwingine wa kucha watu.
Lengo ni Mwenyezi Mungu (s.w.t) anabainisha kuwa mtu hawezi kuamini mambo mawili yanayopingana kwa wakati mmoja; kwa mfano aamini dini inayokataza dhulma na uchokozi, Uislamu na Ukiristo, na wakati huo huo ahalalishe dhulma na uchokozi.
Ila ikiwa ana nyoyo mbili na nyuso mbili; kama waamerika ambao wameleta kununi mpya, kwamba mmarekani anaweza kuwa ni mwisrail na kupigana na mwarabu kwa jina la Israil na wakati huo bado ni raia wa Marekani.
Au itabidi tuseme kuwa Israil ni kambi ya jeshi la uchokozi la marekani na kwamba urai wa Israil ni jina tu; hata watawala pia; kwa vile ni kikosi tu cha kulinda masilahi ya ukoloni na unyonyaji.
Mtu mmoja alimwambia Imam Ali(a.s ) : “Mimi nakupenda wewe na ninampenda Muawiya.” Imam akamwambia:“Wewe ni chongo, sasa chagua ama uwe kipofu au upone chongo.”
Unaweza kuuliza : Utasemaje kuhusiana na anayesema; mimi ni mwislamu au mkristo kiitikadi, lakini kisiasa ninafuata siasa za mashariki au magharibi. Je inawezekana kuchanganya mawili haya?
Jibu : Mtu yoyote anayeamini haki kwa ukweli na usafi wa nia, inafaa, bali ni wajibu kumuunga mkono kila kwenye msimamo wa kuinusuru haki na uadilifu; awe ni wa mashariki au magharibi. Wala haijuzu kumuunga mkono tu, hivi hivi, bila ya msingi wowote. Kwa maana hiyo basi haiwezekeni kuchanganya baina ya itikadi ya kiislamu na kuunga mkono tu hivi hivi kwa hali yoyote.
Hii ni katika yanayohusiana na Uislamu. Ama yanayohusiana na itikadi ya kikiristo tunawaachia makasisi walio huru waliotangaza hasira zao kwa baba mtakatifu aliyekataa kukutana nao, lakini wakati huo huo akakutana na viongozi wa kimarekani.
Wakasema katika mateta yao: “Mkutano huu wa Baba mtakatifu na viongozi hawa unaonyesha wazi uhusiano wa nguvu ulioko baina ya kanisa kama tasisi ya dini na siasa za kiuchumi zinazosimamia ukandamizaji na dhulma dhidi ya watu wengi.” Makasisi hawa walitangaza kuwa wangejaribu kuuangamiza uhusiano huu[6] .
Wala hakuwafanya wake zenu – mnaowalinganisha migongo yao na migongo ya mama zenu – kuwa ni mama zenu.
Wakati wa ujahiliya mtu alikuwa akimwacha mkewe kwa kumwambia: Wewe kwangu ni kama mgongo wa mama yangu (Dhihar). Uislamu ukalikataza hilo, kwa sabau mke hawezi kuwa mama kwa kauli hii, na ukawajibisha kafara kwa atakayesema kauli hiyo, yakipatikana masharti yake, ambayo yatabainishwa mwanzoni mwa Juzuu ya 28. (inshaallah).
Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu.
Wakati wa ujahiliya mtu alikuwa akimchukua mtoto wa mwingine kumfanya mwanawe hasa na kumwingiza kwenye ukoo wake, anakuwa na hukumu ya mtoto wake halisi katika kila kitu na watu wakimwita kwa jina la baba aliyemchukua badala ya baba yake. Ndipo Uislamu ukakataza mtindo huu[7] .
Hiyo ni kauli yenu kwa vinwywa vyenu tu.
Na kauli haibadilishi uhalisi wa mambo.
Na Mwenyezi Mungu anasema haki naye huongoza njia.
Kauli ya haki na njia ya sawa ni kuwa mtoto wa kupanga sio mtoto wa kiuhakika; wala mke hawi ni mama kwa dhihari.
Waiteni kwa baba zao waliowazaa sio waliowapanga.Hilo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. yaani hilo la kuwaita kwa ubini wa baba zao.
Kama hamuwajui mababa zao basi ni ndugu zenu katika dini na rafiki zenu.
Neno rafiki limefasiriwa kutokana na neno mawla, pia lina maana ya huria; mtumwa aliyeachwa huru. Mtu alikuwa anaweza kuitwa huria wa fulani.
Wafsiri na watu wa sera wanasema kuwa Zayd Bin Haritha alitekwa nyara akiwa mdogo. Hakim bin Huzam akamnunua kwa ajili ya kumpatia shangazi yake Khadija Bint Khuwalid. Mtume(s.a.w.w) alipomuoa akapewa zawadi na mkewe. Baada ya kushuka wahyi kwa Nabii, akamlingania kwenye Uisalamu na akasilimu. Akamfanya ndugu na ami yake Hamza bin Abu Twalib.
Haritha, Baba yake Zayd, akaja siku moja kwa Mtume(s.a.w.w) na kumwambia, ama uniuzie mwanangu, au mwache huru. Mtume akamwacha huru na kumwambia nenda upendako. Basi akakataa kuachana na Mtume. Ndipo watu wakawa wanamwita Zayd bin Muhammad mpaka iliposhuka Qur’an kubatilisha hilo.
Si vibaya kwenu kwa mlivyokosea, lakini kwa yale ziliyoyakusudia nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Anayemwita mtu asiyekuwa baba yake kwa kufikiria kuwa ni baba yake, hana lawama; isipokuwa mwenye dhambi ni yule aliyejua na akakusudia: Mtume(s.a.w.w) anasema: “Umma wangu umeondolewa kukosea na kusahau na yale waliyolazimishwa na wasiyoyajua na wasiyoyaweza na wanayokuwa na dharura nayo,” kwa sharti la kutotokea hayo kwa uzembe na kupuuza.
النَّبِيُّ أَوْلَىٰ بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنفُسِهِمْ وَأَزْوَاجُهُ أُمَّهَاتُهُمْ وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ إِلَّا أَن تَفْعَلُوا إِلَىٰ أَوْلِيَائِكُم مَّعْرُوفًا كَانَ ذَٰلِكَ فِي الْكِتَابِ مَسْطُورًا ﴿٦﴾
6. Nabii ni aula kwa waumini kuliko nafsi zao. Na wake zao ni mama zao. Na ndugu wa tumbo ni aula wenyewe kwa wenyewe, katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kuliko waumini wengine na wahajiri. Ila muwe mnafanya wema kwa marafiki zenu. Hayo yamekwishaandikwa kitabuni.
وَإِذْ أَخَذْنَا مِنَ النَّبِيِّينَ مِيثَاقَهُمْ وَمِنكَ وَمِن نُّوحٍ وَإِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ وَأَخَذْنَا مِنْهُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا ﴿٧﴾
7. Na tulipochukua kwa manabii agano lao na kwako wewe na Nuh na Ibrahim na Isa mwana wa Maryam, na tulichukua kwao agano madhubuti.
لِّيَسْأَلَ الصَّادِقِينَ عَن صِدْقِهِمْ وَأَعَدَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿٨﴾
8. Ili awaulize wakweli juu ya ukweli wao. Na amewandaalia makafiri adhabu chungu.
NABII NI AULA KWA WAUMINI KULIKO NAFSI ZAO
Aya 6 – 8
Je, Nabii Ni Hakimu Kwa Amri Yake? Nabii Ni Aula Kwa Waumini Kuliko Nafsi Zao.
Neno aula tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu linalotamkwa hivyo hivyo awla lililonyumbuliwa kutokana na neno wilaya na walii, ambalo maana yake yanatofautiana kulingana na yule anayezungumziwa. Akizungumziwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) basi maana yake ni utawala na nguvu zisizoshindwa na yeyote. Akizungumziwa Nabii(s.a.w.w) inakuwa maana ni utiifu usiopingwa. Haya ndiyo maana yaliyokusudiwa hapa.
Sasa unaweza kuuliza: Si itakuwa maana yake ni kuwa Nabii ni hakimu na mtoa amri tu, mwengine hana uhuru. Tutalinganisha vipi hili na lile la msingi wa uhuru ambao ni haki ya kiasili ya kila mtu?
Jibu : Tutalinganisha uhuru wa mtu na utiifu wa Mwenyezi Mungu. Nabii(s.a.w. w ) anamsemea na kumbainishia Mwenyezi Mungu:
وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٣﴾ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ ﴿٤﴾
“Hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya ila ni wahyi uliofunuliwa” 53 (3 – 4).
Kuna Hadith sahihi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) amesema:“Haamini mmoja wenu mpaka matamanio yake yafuate yale niliyokuja nayo.” Kwa hiyo kufuata na kutii ni aliyokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu sio kutoka kwake.
Zaidi ya hayo uhuru ni kushikamana na njia ya usawa, kutumia haki na kubeba majukumu kwa utashi wake, huku akiipigania haki kwa nguvu zake zote. Lakini mwenye kuwa na msukumo wa mapendeleo bila ya kujali hisabu wala mchungaji, huyo ni mtumwa wa matamanio. Mwana falsafa mmoja mashuhuri alisema: “Uhuru sio kujifadhilisha kiundani kunakoruhusu tujifadhilishe sisi kuliko majukumu; isipokuwa ni uwezo wa kujenga mustakabali.”
Na wake zao ni mama zao.
Wake za mitume wana heshima na uharamu wa kuolewa baada yake sawa na mama, lakini kwenye mambo mengine ni watu kando kama wengine.
Na ndugu wa tumbo ni aula wenyewe kwa wenyewe, katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kuliko waumini wengine na wahajiri.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 10 (9:75).
Ila muwe mnafanya wema kwa marafiki zenu
Makusudio ya wema hapa ni wasia, na marafiki wanakuwa ni pamoja na walioachwa huru au ndugu wasiorithi. Maana ni kuwa mirathi ni ya ndugu wa karibu wa maiti, lakini wasia ni wa aliyeusiwa awe wa mbali au wa karibu.
Hayo yamekwishaandikwa kitabuni.
Yaani hukumu imekwishathibiti Kitabuni mbele ya Mwenyezi Mungu na mwenye kuiasi atakuwa miongoni mwa walioangamia.
Na tulipochukua kwa manabii agano lao na kwako wewe na Nuh na Ibrahim na Isa mwana wa Maryam, na tulichukua kwao ahadi ngumu.
‘Kwako wewe,’ anaambiwa Muhammad(s.a.w. w ) . Makusudio ya agano ni kufikisha (Tabligh) risala ya Mwenyezi Mungu kwa ukamilifu wake na kuwa na subira na yatakayowapata katika njia yake. Amehusisha kutaja Nuh, Ibrahim, Musa, Isa na Muhammad, baada ya kuwataja manabii kwa ujumla kwa vile wao ni bora ya manabii wote, na ametangulizwa Muhammad kwa vile yeye ni mbora wao hao watano.
Katika Juz. 26 (46:35) wameashiriwa mitume Ulul-azmi (wenye ustahamilivu). Sababu ya kuitwa hivyo, kama zilivyopokewa baadhi ya riwaya, ni kuwa kila Nabii baada ya Nuh alikwa akifuata sharia ya Nuh, kisha sharia yake ikafutwa na sharia ya Ibrahim nayo ikafutwa na sharia ya Musa, nayo ikafutwa na Isa, kisha ikafutwa na ya Muhammad (s.a.w.) ambayo haitafutwa hadi Kiyama, kwa vile hakuna Nabii mwingine baada yake.
Na tulichukua kwao agano madhubuti.
Hili ndilo agano la kwanza, na amerudia kulitaja ili alisifu kuwa ni imara na lenye nguvu. Mwenyezi Mungu ameyapa sifa ya maagano madhibuti katika sehemu tatu katika Kitabu chake kitukufu:
Kwanza, ni agano la ndoa aliposema: “Na hali wao wamechukua kwenu agano madhubuti?” Juz. 4 (4:21). Pili ni agano alilochukua na wana wa Israil aliposema: “Na tukachukua kwao agano madhubuti.” Juz. 6 (4:154). Agano la tatu ni hili la Manbii tunalolizungumzia.
Sheikh Mahmud Shaltut, alighafilika kidogo pale aliposema: “Wasifu wa agano madhubuti haukuja katika sehemu yoyote ile katika sehemu zake – yaani Qur’an - isipokuwa katika kufunga ndoa.” Kutokosea ni kwa Mungu.
Ili awaulize wakweli juu ya ukweli wao.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewatuma Manabii na akachukua kwao agano la kufikisha ujumbe ili wakawaulize wakweli, walikusudia nini kwenye ukweli wao. Je, walikusudia radhi ya Mwenyezi Mungu au ni kwa ajili ya kuwaambia watu kuwa wao ni wakweli na mengineyo ya kibinafsi.
Imam Ja’far Sadiq(a.s) anasema: “Mwenyezi Mungu akimuuliza mtu kuhusu ukweli wake ni kwa njia gani aliusema, basi atamlipa kulingana nao, je vipi hali ya muongo?”
Na amewandalia makafiri adhabu chungu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alipowataja mitume sasa anawataja makafiri kwa mkabala wa kuwataja wema.