7%

10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

وَإِبْرَاهِيمَ إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاتَّقُوهُ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿١٦﴾

16. Na Ibrahim pale alipowaambia watu wake: Muabuduni Mwenyezi Mungu na mcheni Yeye. Hayo ni kheri kwenu ikiwa mnajua.

إِنَّمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ أَوْثَانًا وَتَخْلُقُونَ إِفْكًا إِنَّ الَّذِينَ تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَا يَمْلِكُونَ لَكُمْ رِزْقًا فَابْتَغُوا عِندَ اللَّـهِ الرِّزْقَ وَاعْبُدُوهُ وَاشْكُرُوا لَهُ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿١٧﴾

17. Hakika nyinyi mnaabudu masanamu kinyume na Mwenyezi Mungu na mnazua uzushi. Hakika mnao waabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu hawamilikii riziki yoyote. Takeni riziki kwa Mwenyezi Mungu na mumwabudu na mumshukuru; kwake mtarudishwa.

وَإِن تُكَذِّبُوا فَقَدْ كَذَّبَ أُمَمٌ مِّن قَبْلِكُمْ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿١٨﴾

18. Na kama mkikadhibisha basi zimekwisha kadhibisha umma kabla yenu. Na si juu ya Mtume ila kufikisha.

IBRAHIM

Aya 16 – 18

MAANA

Na Ibrahim pale alipowaambia watu wake: Muabuduni Mwenyezi Mungu na mcheni Yeye. Hayo ni kheri kwenu ikiwa mnajua. Hakika nyinyi mnaabudu masanamu kinyume na Mwenyezi Mungu na mnazua uzushi. Hakika mnaowaabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu hawamilikii riziki yoyote. Takeni riziki kwa Mwenyezi Mungu na mumwabudu na mumshukuru; kwake mtarudishwa. Na kama mkikadhibisha basi zimekwisha kadhibisha umma kabla yenu. Na si juu ya Mtume ila kufikisha.

Hakika mwito wa Ibrahim(a.s) ni mwito wa kila Nabii – Ikhlasi katika kila jambo na kuiondoa shirki kwa sura zake zote, kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mwanzilishi na ndiye mrejeshaji; mkononi mwake ndio kuna madhara na manufaa. Mwenye kukadhibisha na akaukataa mwito huu atakuwa amejidhulumu nafsi yake.

Katika kamusi ya Kitabu Kitakatifu, imeelezwa kuwa Ibrahim ni mwana wa Tarih kutokana na kizazi cha Sam bin Nuhu, yeye anatoka katika mji ulio baina ya mito miwili: mto Dijla na mto Furat na kwamba yeye alikaa hapo miaka 75, kisha akahama pamoja na mkewe na Lut hadi ardhi ya Kanani. Mtungaji wa Kamusi hiyo anasema: “Haiwezekani kuainisha kwa mpangilio tarehe aliyoishi Ibrahim, lakini yeye alizaliwa, kulingana na tarehe aliyoielezea Ashir, kuwa ni kwenye mwaka 1996 kabla ya Kuzaliwa Nabii Isa.”

Yametangulia maelezo kuhusu Ibrahim katika Juz. 7 (6:74 – 84 , Juz. 16 (19:41 – 50) na Juz. 17 (21:52 – 72).

أَوَلَمْ يَرَوْا كَيْفَ يُبْدِئُ اللَّـهُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ ﴿١٩﴾

19. Je, hawaoni jinsi Mwenyezi Mungu anavyoanzisha uumbaji na kisha akaurudisha. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni rahisi.

قُلْ سِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ بَدَأَ الْخَلْقَ ثُمَّ اللَّـهُ يُنشِئُ النَّشْأَةَ الْآخِرَةَ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٢٠﴾

20. Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyoanzisha kuumba, kisha Mwenyezi Mungu ndiye atakayeumba umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.

يُعَذِّبُ مَن يَشَاءُ وَيَرْحَمُ مَن يَشَاءُ وَإِلَيْهِ تُقْلَبُونَ ﴿٢١﴾

21. Humwadhibu amtakaye, Na humrehemu amtakaye; na kwake mtapelekwa.

وَمَا أَنتُم بِمُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ وَمَا لَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ ﴿٢٢﴾

22. Wala nyinyi si wenye kushinda ardhini wala mbinguni. Wala hamna mlinzi wala msaidizi isipokuwa Mwenyezi Mungu.

وَالَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ وَلِقَائِهِ أُولَـٰئِكَ يَئِسُوا مِن رَّحْمَتِي وَأُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٢٣﴾

23. Na wale ambao wamezikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye. Hao wamekata tamaa na hao watakaopata adhabu chungu.

فَمَا كَانَ جَوَابَ قَوْمِهِ إِلَّا أَن قَالُوا اقْتُلُوهُ أَوْ حَرِّقُوهُ فَأَنجَاهُ اللَّـهُ مِنَ النَّارِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٢٤﴾

24. Basi halikuwa jawabu la watu wake ila ni kusema: Muuweni au mchomeni moto! Mwenyezi Mungu akamwokoa na moto. Hakika katika halo kuna ishara kwa watu wanaoamini.

وَقَالَ إِنَّمَا اتَّخَذْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ أَوْثَانًا مَّوَدَّةَ بَيْنِكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ثُمَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُ بَعْضُكُم بِبَعْضٍ وَيَلْعَنُ بَعْضُكُم بَعْضًا وَمَأْوَاكُمُ النَّارُ وَمَا لَكُم مِّن نَّاصِرِينَ ﴿٢٥﴾

25. Na alisema: Hakika nyinyi mmeyashika masanamu badala ya Mwenyezi Mungu kwa mapenzi baina yenu katika maisha ya dunia. Kisha siku ya Kiyama mtakataana nyinyi kwa nyinyi na mtalaniana nyinyi kwa nyinyi. Na makazi yenu ni motoni wala hamtapata wa kuwanusuru.

فَآمَنَ لَهُ لُوطٌ وَقَالَ إِنِّي مُهَاجِرٌ إِلَىٰ رَبِّي إِنَّهُ هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ {26 }

26. Akamwamini Lut na akasema: Hakika mimi ninahamia kwa Mola wangu. Hakika Yeye ni mwenye nguvu mwenye hekima.

وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَجَعَلْنَا فِي ذُرِّيَّتِهِ النُّبُوَّةَ وَالْكِتَابَ وَآتَيْنَاهُ أَجْرَهُ فِي الدُّنْيَا وَإِنَّهُ فِي الْآخِرَةِ لَمِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٢٧﴾

27. Na tulimtunukia yeye Is-haq na Ya’qub na tukajaalia katika kizazi chake Unabii na Kitabu na tukampa ujira wake katika dunia. Naye hakika katika Akhera, bila shaka atakuwa katika wema.

MWENYEZI MUNGU NDIYE MWANZILISHI NA MRUDISHAJI

Aya 19 – 27

MAANA

Je, hawaoni jinsi Mwenyezi Mungu anavyoanzisha uumbaji na kisha akaurudisha. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni rahisi.

Maana ya hawaoni ni hawajui. Maana yanafupika kwa kauli ya Imam Ali(a.s) :“Namstaajabu anayepinga uumbaji wa mwisho naye anaona uuum- baji wa kwanza.”

Wajihi wa kuungana maumbo haya mawili ni kwa kisababishi ambacho ni uweza wa aliyeyafanya. Kwani aliyeweza kukifanya kitu bila ya kuweko kitu, vile vile anaweza kukifanaya baada ya kutawanyika; bali huko kukufanya ni kwepesi zaidi. Tunasema hivi tukijua kuwa kwa Mwenyezi Mungu hakuna jepesi wala zito, na kwamba yeye anafanya kikubwa na kidogo kwa neno ‘Kuwa.’ Maelezo haya tumeyakariri kwa kukaririka Aya. Angalia Juz.1 (2:28 – 29), Juz. 5 (4:85 – 87) na Juz. 13 (13:5 – 7).

QUR’AN NA FIKRA

Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyoanzisha kuumba, kisha Mwenyezi Mungu ndiye atakayeumba umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.

Qur’an imekataza kuiga na ikaamrisha kufanya utafiti na uchunguzi. Imewasifu wataalamu na wenye kufanya jitihada. Hakuna mwenye shaka kwamba utafiti na uchunguzi ni katika alama za uhai na njia ya kuuen- deleza na kutatua matatizo yake, ikiwa utafiti na uchunguzi utaambatana na subira na kuamua kufikia kwenye malengo hata kama kutakuwa na vikwazo vya namna gani.

Subira na imani inashinda nguvu zote. Binadamu wa zama hizi ameamua kufika mwezini; akajitahidi na akafanya bidii mpaka akakanyaga kwenye uso wa mwezi kwa unyayo wake. Kesho au kesho kutwa atakanyaga mirikh na sayari nyinginezo.

Kwa hiyo, hakuna nguvu isiyoshindwa na binadamu isipokuwa nguvu ya muumba tu. Ndio maana ikasemwa: hakuna zaidi ya binadamu isipokuwa muumba wake.

Kama mtu ataniuliza: Ni kiwango gani cha binadamu? Nitamjibu: Kiwango chake ni kuwa hakuna kiwango cha nguvu zake na maandalizi yake. Ujinga na kuiga ndiko kunakoingilia kati baina ya mtu na mkabala wake na kumtenganisha na nafsi yake na uhalisi wake.

Ndio maana Qur’an ikaharamisha kuiga na kuamrisha kuchunguza na kufuata akili katika hukumu zake zote na kukupa jina la nuru uongofu na dalili.

Unaweza kuuliza : Ni kweli Qur’an imekataza kuiga na kuamrisha kufanya utafiti na uchunguzi, pia ikawasifu wataalamu.

Lakini mfumo au sababu iliyowajibisha kushuka Aya inayohusiana na maudhui haya inafahamisha wataalamu wa dini ndio waliosifiwa kuwa watu wa elimu ya Mwenyezi Mungu na kujua halali yake na haramu yake na kwamba Yeye ameamrisha kuchunguza na kufikiri katika kuumbwa vilivyoko ili mtu aishilie kwa hilo kwenye imani ya Mungu na Siku ya Mwisho, aweze kufuzu kwa kupata pepo na neema zake na kuokoka na moto na ukali wake.

Mfano mzuri wa hayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

أَفَرَأَيْتُم مَّا تَحْرُثُونَ ﴿٦٣﴾ أَأَنتُمْ تَزْرَعُونَهُ أَمْ نَحْنُ الزَّارِعُونَ ﴿٦٤﴾ لَوْ نَشَاءُ لَجَعَلْنَاهُ حُطَامًا فَظَلْتُمْ تَفَكَّهُونَ ﴿٦٥﴾

“Je, mmeona mnayolima. Je, nyinyi mmeiotesha au tumeiotesha sisi? Lau tungelitaka tungeifanya makapi mkabaki mnastaajabu.” (56:63 – 65).

Ni mwenye akili gani atakayeweza kusema kuwa Aya hii inahimiza elimu ya kilimo?

Jibu :Kwanza : kuna Aya zilizobariki na kusifu kila linalowanufaisha watu; kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَأَمَّا مَا يَنفَعُ النَّاسَ فَيَمْكُثُ فِي الْأَرْضِ ﴿١٧﴾

“Ama povu linakwenda bure; ama kinachowafaa watu hukaa kwenye ardhi.” Juz. 13 (13:17).

Hakuna kitu kinachowafaa zaidi watu kama elimu; bali hakuna maisha bila elimu katika zama hizi. Zaidi ya hayo kuna Aya kadhaa zinazohimiza kufanya amali njema na kuwazingatia watendaji wake kuwa ni viumbe bora. Mwenyezi Mungu anasema:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَـٰئِكَ هُمْ خَيْرُ الْبَرِيَّةِ ﴿٧﴾

“Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema, hao ndio bora ya viumbe” (98:7)

Na elimu inajitokeza kuwa ni katika matendo mema.

Pili : Ni kweli kuwa sababu za kushuka Aya zilizoamrisha utafiti na uchunguzai au nyingi katika hizo ni kumrudi yule anayemkufuru Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, lakini sababu ya kushuka hailifungi neno na sababu hiyo hiyo peke yake.

Tatu : Elimu yenye manufaa ni nzuri katika mtazamo wa akili. Ndio, elimu ina daraja mbali mbali, zinazopimwa kutokana na faida na manufaa yake.

Elimu ya sharia ya kiislamu na sharia yake ndiyo iliyo na manufaa zaidi kidunia na akhera. Kidunia ni kwa kuwa inaelekeza kila kitu kwenye heri ya watu na masilahi yao. Ama kiakhera, hiyo ndio njia ya kuokoka na hasira za Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Ndio maana waislamu wakamwita mwanachuoni wa kidini: ‘Mwanachuoni huru’ na ‘Mwanachuoni aliyefungwa’ kuwa ni yule wa kidunia.

Nne : wameafikiana mafakihi wa kiislamu kwa kauli moja kwamba kila elimu inayohitajika katika maisha basi ni wajib kifaya.

Kuna hadith isemayo: “ Hakuna Mwislamu yoyote aliyepanda mti au kupanda mbegu, akala humo ndege au mnyama au mtu, ila huwa ni kama sadaka, “Tafuteni elimu katika machimbuko yake ya kidini na kidunia” na “Tafuteni elimu hata kama ni China.”

Kimsingi ni kuwa elimu ya dini inatafutwa katika Kitabu na Sunna sio China!

Humwadhibu amtakaye, katika wanaostahiki adhabu,Na humrehemu amatakaye, katika wanaostahiki rehema.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mwadilifu na hakimu, atailipa kila nafsi iliyoyachuma.

Na kwake mtapelekwa . Mtarudishwa siku ya Kiyama kwa hisabu na malipo.

Wala nyinyi si wenye kushinda ardhini wala mbinguni.

Yaani wala aliyeko mbinguni. Katika Nahjul-balagha imeelezwa: “Hamshindi anayemtafuta wala hamponyoki anayemkimbia.”

Wala hamna mlinzi wala msaidizi isipokuwa Mwenyezi Mungu.

Hakuna wa kuzuia hukumu yake wala kumkimbia.

Na wale ambao wamezikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye. Hao wamekata tamaa na hao watakaopata adhabu chungu.

Kukata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu ni natija ya kumkana Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na malipo ya mwenye kukata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu, kwa ukafiri na inadi, ni kuonja adhabu ya kuungua.

Basi halikuwa jawabu la watu wake ila ni kusema: Muuweni au mchomeni moto! Mwenyezi Mungu akamwokoa na moto.

Zinarudi simulizi za Ibrahim(a.s) na sera yake pamoja na watu wake ambao walijaribu kuepukana naye na mwito wake kwa kumuua au kumchoma.

Haya ndio mantiki ya mataghuti kila wakati na mahali. Wanashindwa na hoja wazi basi wanahofia vyeo vyao. Kwa hiyo wanakuwa hawana jingine isipokuwa dhulma waliyo nayo. Hapo wanaanza kutoa amri ya: Wafungeni, waadhibuni, wanyang’anyeni mali, vunjeni majumba, nyongeni, chomeni n.k.

Hapa ndio unaingia uokovu wa Mwenyezi Mungu. Unaweza kuwa ni kwa kuokoka mdhulumiwa kutoka mikononi mwa dhalimu, kuadhibiwa dhalimu na Mwenyezi Mungu au kupitia kwa wanamapinduzi, wakombozi. Umepita mfano wake katika Juz. 17 (21:68).

Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaoamini.

Yaani wanaonufaika na maonyo, kuwaidhika na mazingatio, kuitafuta haki kwa ajili ya haki ili waiamini na kutenda kwa ikhlasi.

Na alisema: Hakika nyinyi mmeyashika masanamu badala ya Mwenyezi Mungu kwa mapenzi baina yenu katika maisha ya dunia.

Ibrahim aliwaambia watu kuwa nyinyi mnayaabudu haya masanamu mkiwa na yakini kuwa hayadhuru wala hayanufaishi, lakini mmeyatukuza kwa kuwaiga mnaowapenda katika maisha haya na kesho haya mapenzi yatabadilika kuwa uadui na chuki.

Kisha siku ya Kiyama mtakataana nyinyi kwa nyinyi na mtalaaniana nyinyi kwa nyinyi.

Imam Ali(a.s) anasema:“Mfuatwa atajitenga na mfuasi, na kiongozi na muongozwa; watafarikiana kwa chuki na watalaaniana wakati wa kukutana.”

Na makazi yenu ni motoni wala hamtapata wa kuwanusuru.

Huu ndio mwisho wa kila mwenye kuipinga haki awe mfuasi au mwenye kufuatwa.

Akamwamini Lut na akasema: “Hakika mimi ninahamia kwa Mola wangu. Hakika Yeye ni mwenye nguvu mwenye hekima.”

Lut ni mtoto wa nduguye Ibrahim. Kundi katika wafasiri wamesema: “Hakuongoka yoyote katika kaumu ya Ibrahim au kumwamini isipokuwa Lut peke yake.” Yakushangaza ni yale yaliyoandikwa katika Biblia Mwanzo: (19:30 – 38)

Imeelezwa kuwa mabinti wawili wa Lut walimlewesha baba yao pombe, wakalala naye na wakashika mimba. Mkubwa akazaa mtoto wa kiume aliyemwita Moabu na mdogo pia akazaa mtoto wa kiume aliyemwita Binamu.

Na tulimtunukia Is-ahq na Ya’qub na tukajaalia katika kizazi chake Unabii na Kitabu na tukampa ujira wake katika dunia. Naye hakika katika Akhera, bila shaka atakuwa katika wema.

Aliyetunukiwa ni Ibrahim(a.s) . Aya hii ni dalili ya wazi kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakutuma mtume baada yake ila anatokana na uti wake wa mgongo.

Tukiiunganisha Aya hii na Hadith isemayo: “Jambo hili liko kwa makuraish... Watu wanawafuata makuraishi Maimamu ni katika makraishi...” tunapata natija ya kuwa mitume wote na maimamu wanatokana na kizazi cha Ibrahim. Kwa sababu nasaba ya Kuraishi inakomea kwake.

Umepita mfano wake katika Juz. 16 (19: 49) na Juz. 17 (21: 72 - 73).