11
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI
وَلُوطًا إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ إِنَّكُمْ لَتَأْتُونَ الْفَاحِشَةَ مَا سَبَقَكُم بِهَا مِنْ أَحَدٍ مِّنَ الْعَالَمِينَ ﴿٢٨﴾
28. Na Lut alipowaambia watu wake: Hakika nyinyi mnafanya uchafu ambao hajawatangulia yeyote kwa hilo katika walimwengu.
أَئِنَّكُمْ لَتَأْتُونَ الرِّجَالَ وَتَقْطَعُونَ السَّبِيلَ وَتَأْتُونَ فِي نَادِيكُمُ الْمُنكَرَ فَمَا كَانَ جَوَابَ قَوْمِهِ إِلَّا أَن قَالُوا ائْتِنَا بِعَذَابِ اللَّـهِ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٢٩﴾
29. Je, mnawaendea wanaume na mnakata njia na katika mikusanyiko yenu mnafanya uovu? Basi halikuwa jibu la watu wake isipokuwa kusema: Tuletee adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni katika wakweli.
قَالَ رَبِّ انصُرْنِي عَلَى الْقَوْمِ الْمُفْسِدِينَ ﴿٣٠﴾
30. Akasema: Mola wangu! Ninusuru juu ya watu hawa mafasiki.
وَلَمَّا جَاءَتْ رُسُلُنَا إِبْرَاهِيمَ بِالْبُشْرَىٰ قَالُوا إِنَّا مُهْلِكُو أَهْلِ هَـٰذِهِ الْقَرْيَةِ إِنَّ أَهْلَهَا كَانُوا ظَالِمِينَ ﴿٣١﴾
31. Na wajumbe wetu walipomjia Ibrahim na bishara, walisema: Hakika sisi tutawaangamiza watu wa mji huu, kwani hakika watu wake wamekuwa madhalimu.
قَالَ إِنَّ فِيهَا لُوطًا قَالُوا نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَن فِيهَا لَنُنَجِّيَنَّهُ وَأَهْلَهُ إِلَّا امْرَأَتَهُ كَانَتْ مِنَ الْغَابِرِينَ ﴿٣٢﴾
32. Akasema: Hakika humo yumo Lut. Wakasema: Sisi tunajua zaidi nani aliyemo humo. Bila shaka tutamwokoa yeye na ahli zake, isipokuwa mkewe, aliye miongoni mwa waliobaki.
وَلَمَّا أَن جَاءَتْ رُسُلُنَا لُوطًا سِيءَ بِهِمْ وَضَاقَ بِهِمْ ذَرْعًا وَقَالُوا لَا تَخَفْ وَلَا تَحْزَنْ إِنَّا مُنَجُّوكَ وَأَهْلَكَ إِلَّا امْرَأَتَكَ كَانَتْ مِنَ الْغَابِرِينَ ﴿٣٣﴾
33. Na wajumbe wetu walipomfikia Lut, aliwahuzunikia na akapata dhiki kwa ajili yao. Wakasema: Usihofu wala usihuzunike. Hakika sisi tutakuokoa na ahli zako isipokuwa mkeo aliye miongoni mwa wenye kubaki katika adhabu.
إِنَّا مُنزِلُونَ عَلَىٰ أَهْلِ هَـٰذِهِ الْقَرْيَةِ رِجْزًا مِّنَ السَّمَاءِ بِمَا كَانُوا يَفْسُقُونَ ﴿٣٤﴾
34. Hakika sisi ni wenye kuteremsha kwa watu wa mji huu adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya ufuska wanaoufanya.
وَلَقَد تَّرَكْنَا مِنْهَا آيَةً بَيِّنَةً لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿٣٥﴾
35. Hakika tumeacha katika mji huo ishara iliyo wazi kwa watu wanaotumia akili.
Aya 28 – 35
Mwenyezi Mungu alimtuma Nuh kwa jamii ambayo haina mfano wake katika historia mbaya. Wakiwaendea wanaume kwa matamanio badala ya wanawake na ujambazi wa kupora watu njiani. Vikao vyao havikujua kitu isipokuwa uchafu na uovu.
Ndipo Lut akawahadharisha na kuwaonya na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Hayo ndiyo aliyokuwa akiyaweza na kuyamiliki. Lakini wakamkejeli na kumwambia tuonyeshe adhabu ndio tutakuamini. Akamkimbilia Mwenyezi Mungu kumwomba msaada kutokana na watu hao mafasiki.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwitikia maombi yake, akamsadia kwa Malaika wakali na wenye nguvu, waliopitia kwa Ibrahim na kumpa habari njema ya kupata mtoto kutokana na mkewe kikongwe na wakamwelezea hukmu ya Mwenyezi Mungu kwa kaumu ya Lut.
Akasema; itakuwaje na humo yumo mja mwema Lut. Wakamwambia yeye na wafuasi wake watakuwa katika amani, isipokuwa mkewe ambaye alijitokeza na kupanga njama na makafiri.
Malaika wakaingia kwa Lut kwa nyuso angavu. Akawa na wasiwasi wasivunjiwe heshima na watu wake waovu. Basi wakamfichulia makusudio yao na likatimia neno la adhabu kwa wafisadi, wakabaki ni athari na mazingatio kwa wenye busara.
Baada ya maelfu ya miaka, historia ya ulawiti na ufisadi inajirudia tena katika bunge la Uingereza, lilipothibitisha na kuhalalisha uchafu huu ambao haufanywi hata na wanyama na wadudu. Sisi tuna uhakika kwam- ba aina ya adhabu itaifikia jamii hii na mfano wake, hivi sasa au baadaye; sawa na ilivyowafikia waliokuwa kabla yao.
Katika kamusi ya Kitabu Kitakatifu imeesemwa: “Tunajua kutokana na ugunduzi wa Jiolojia kwamba sehemu za kusini mwa bahari ya chumvi kulichipuka chumvi, huenda sababu ya kuchipuka huku chini ya ardhi kulitokana na tendo la kimungu.”
Aya hizi zimekwishatangulia katika Juz. 8 (7:80 – 87) na Juz. 12 (11:69–83).
وَإِلَىٰ مَدْيَنَ أَخَاهُمْ شُعَيْبًا فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَارْجُوا الْيَوْمَ الْآخِرَ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ ﴿٣٦﴾
36. Na kwa wamadyana (tulimpeleka) ndugu yao Shua’yb, akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu! Na itarajieni siku ya Akhera wala msiende katika ardhi mkifanya ufisadi.
فَكَذَّبُوهُ فَأَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ ﴿٣٧﴾
37. Wakamkadhibisha, ukawanyakuwa mtetemeko wakawa wameanguka majumbani mwao hawajimudu.
وَعَادًا وَثَمُودَ وَقَد تَّبَيَّنَ لَكُم مِّن مَّسَاكِنِهِمْ وَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَصَدَّهُمْ عَنِ السَّبِيلِ وَكَانُوا مُسْتَبْصِرِينَ ﴿٣٨﴾
38. Na kina A’d na Thamud na hakika maskani zao zimewabainikia na shetani aliwapambia vitendo vyao na akawazuilia njia na hali walikuwa wenye kuona.
وَقَارُونَ وَفِرْعَوْنَ وَهَامَانَ وَلَقَدْ جَاءَهُم مُّوسَىٰ بِالْبَيِّنَاتِ فَاسْتَكْبَرُوا فِي الْأَرْضِ وَمَا كَانُوا سَابِقِينَ ﴿٣٩﴾
39. Na Qaruni na Firauni na Haman. Na hakika aliwajia Musa na ishara wazi wazi, lakini wakafanya kiburi katika nchi wala hawakuwa ni wenye kushinda.
فَكُلًّا أَخَذْنَا بِذَنبِهِ فَمِنْهُم مَّنْ أَرْسَلْنَا عَلَيْهِ حَاصِبًا وَمِنْهُم مَّنْ أَخَذَتْهُ الصَّيْحَةُ وَمِنْهُم مَّنْ خَسَفْنَا بِهِ الْأَرْضَ وَمِنْهُم مَّنْ أَغْرَقْنَا وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿٤٠﴾
40. Kila mmoja tulimtesa kwa dhambi yake; miongoni mwao wapo tuliowapelekea kimbunga cha changarawe;. Na miongoni mwao wapo walionyakuliwa na ukelele na miongoni mwao wapo tuliowadidimiza katika ardhi na miongoni mwao wapo tuliowagharikisha; Wala Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu wenyewe.
Aya 36 – 40
Na kwa wamadyana (tulimpeleka) ndugu yao Shua’yb, akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu! Na itarajieni siku ya Akhera wala msiende katika ardhi mkifanya ufisadi.
Shua’yb ni mwarabu, kama Hud na Swaleh na watu wa Madyana pia ni waarabu; nayo iko pembeni mwa Sham. Jina hili halipatikani katika Biblia wala kwenye kamusi ya Kitabu kitatatifu; isipokuwa kwamba Yethro ni jina la mmadyani naye ni kuhani wa Madyan, baba mkwe wa Musa[5] ambaye pia anaitwa Rawail. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:85).
Wakamkadhibisha, ukawanyakuwa mtetemeko wakawa wameanguka majumbani mwao hawajimudu.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:78).
Na kina A’d na Thamud na hakika maskani zao zimewabainikia na shetani aliwapambia vitendo vyao na akawazuilia njia na hali walikuwa wenye kuona.
Yaani wanayo macho na akili ambayo inawaongoza kwenye haki, lakini wakamfuata shetani wakawa ni wenye kuangamia. Na nyinyi enyi washirikina mna akili, kama A’d na Thamud na mmeona dalili za kuangamia kwao, jambo ambalo linaweza kuwapa mawaidha na mazingatio. Hivi hamuwaidhiki mkaacha kumfuata shetani?
Na Qaruni na Firauni na Haman. Na hakika aliwajia Musa na ishara wazi wazi, lakini wakafanya kiburi katika nchi wala hawakuwa ni wenye kushinda.
Yaani wenye kuokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu kama walivyookoka waliotangulia.
Qaruni ni yule aliyekuwa na hazina ambazo funguo zake ziliwaelemea kundi la watu wenye nguvu. Firauni ni yule aliyesema: “Mimi ndiye Mola wenu mkubwa,” na Haman ni waziri wake. Hawa wote walijiwa na Musa na miujiza , lakini kujitukuza kwa dhambi, kuliwaangamiza wote.
Kila mmoja tulimtesa kwa dhambi yake; miongoni mwao wapo tuliowapelekea kimbunga cha changarawe; kama vile kaumu ya Lut.Na miongoni mwao wapo walionyakuliwa na ukelele; kama Thamud.Na miongoni mwao wapo tuliowadidimiza katika ardhi; kama Qarun.
Na miongoni mwao wapo tuliowagharikisha; kama kaumu ya Nuhu, Firauni na Haman.
Wala Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu wenyewe.
Kwa nini Mwenyezi Mungu awadhulumu watu? Je, ni kwa kuwa Yeye ana haja ya kudhulumu na hali yeye ni mwenye kujitosheleza na walimwengu? Vipi atawadhulumu waja wake na hali Yeye ndiye aliyesema:
أَن لَّعْنَةُ اللَّـهِ عَلَى الظَّالِمِينَ ﴿٤٤﴾
“Kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu.” Juz. 8 (7:44).
مَثَلُ الَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ أَوْلِيَاءَ كَمَثَلِ الْعَنكَبُوتِ اتَّخَذَتْ بَيْتًا وَإِنَّ أَوْهَنَ الْبُيُوتِ لَبَيْتُ الْعَنكَبُوتِ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٤١﴾
41. Mfano wa wale ambao wamewafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni kama mfano wa buibui aliyejitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu zaidi ni nyumba ya buibui, lau wangelikuwa wanajua.
إِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٤٢﴾
42. Hakika Mwenyezi Mungu anajua kila kitu wanachokiomba badala yake. Na Yeye ndiye mwenye nguvu, mwenye hekima.
وَتِلْكَ الْأَمْثَالُ نَضْرِبُهَا لِلنَّاسِ وَمَا يَعْقِلُهَا إِلَّا الْعَالِمُونَ ﴿٤٣﴾
43. Na hiyo ni mifano tunawapigia watu na hawaitii akilini ila wenye elimu.
خَلَقَ اللَّـهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٤٤﴾
44. Mwenyezi Mungu ameumba mbingu na ardhi kwa haki. Hakika katika hayo kuna ishara kwa waumini.
Aya 41 – 44
Mfano wa wale ambao wamewafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni kama mfano wa buibui aliyejitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu zaidi ni nyumba ya buibui, lau wangelikuwa wanajua.
Kwanza ni lazima tuwajue ni akina nani hao waliowafanya wengine kuwa walinzi badala ya Mwenyezi Mungu? Je ni waabudu mawe na mizimu tu, au ni zaidi ya hao?
Kabla ya kulijibu swali hili, kwanza tukumbuke kauli mbili za Mwenyezi Mungu Mtukufu:
مَن كَانَ يُرِيدُ الْعِزَّةَ فَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ جَمِيعًا ﴿١٠﴾
“Mwenye kutaka utukufu basi utukufu wote uko kwa Mwenyezi Mungu.” (35:10).
أَيَبْتَغُونَ عِندَهُمُ الْعِزَّةَ فَإِنَّ الْعِزَّةَ لِلَّـهِ جَمِيعًا ﴿١٣٩﴾
“Je wanataka kwao utukufu? Basi hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu.” Juz. 5 (4:139).
Maana ni kuwa hakuna utukufu wa nguvu ya mali, elimu, utawala wala kwa kitu chochote ila ikiwa utasimama kwa misingi ya kumcha Mungu (takua) na radhi yake na yakawa matokeo yake ni kumtii Yeye na matakwa yake.
Elimu ni nguvu, heri na imani ya Mwenyezi Mungu na ubinadamu, ikiwa inaunga mkono haki na uadilifu na nyenzo za kuendeleza maisha. Elimu ni udhaifu, shari na kumkufuru Mungu na ubinadamu, ikiwa ni nyenzo ya dhulma, uchokozi, uvunjaji na uharibifu. Pia mali, utawala n.k. Ni hivyo hivyo.
Baada ya utangulizi huu, tutakuwa tumejua kuwa wale waliowafanya walinzi wengine badala ya Mwenyezi Mungu, ni waabudu masanamu, wanaompinga Mwenyezi Mungu kwa kughurika na mali, elimu au utawala na wenye kufanya ufisadi katika ardhi.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amezifananisha nguvu za hawa na nyumba ya buibui ambayo ni dhaifu, isiyoweza kuhimili chochote; hata upepo pia unaweza ukaibomoa.
Kwa maneno mengine ni kuwa kila mwenye kumpinga Mwenyezi Mungu kwa kutegemea mizimu, elimu, mali au utawala, huyo ni katika waliowafanya wengine ni walinzi badala ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kufanya hivyo huyo ni miongoni mwa waliopata hasara.
Anasema Jahidh, katika Kitabu lhayawan (kitabu cha wanyama): “Mtoto wa buibui anaweza kutanda utandabui pale tu anapozaliwa kwa kutumia vitu vya nje sio vinavyotoka ndani mwake na kwamba yeye hutumia utando wake kulitanda windo lake.”
Kila mwenye akili anapaswa kujiuliza nafsi yake na akili yake: Ni nani aliyemjulisha buibui malighafi ya kuweza kutengeneza utando mara tu anapozaliwa? Ni mhandisi gani aliyemchorea nyumba hii yenye umbo la mtego wa wadudu? Je, yote haya yamekuja kwa sadfa? Ikiwa sadfa inaweza kuja mara mbili au tatu, je inaweza kukaririka kwa kila buibui wasio na idadi wanaozaliwa?
Hapana! Hakika Yeye ameumba kila kitu akakilinganisha sawa na akakikadiria na akakiongoza. Ametakata Mwenyezi Mungu Mtukufu na hayo wayasemayo wazushi.
Hakika Mwenyezi Mungu anajua kila kitu wanachokiomba badala yake.
Yaani katika mizimu na mengineyo wanayoyategemea badala ya Mwenyezi Mungu; kama vile mali na utawala. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anajua hakika ya vitu hivi wanavyojikuza navyo na kwamba hivyo haviwatoshi na chochote.
Na Yeye ndiye mwenye nguvu, mwenye hekima.
Mwenye nguvu kwa uweza wake na mwenye hekima katika mipangilio yake.
Na hiyo ni mifano tunawapigia watu na hawaitii akilini ila wenye elimu.
Mifano hiyo ni ile ya buibui na mfano wake na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu anawatanabahisha watu kwenye utukufu wake na umoja wake, lakini mifano hii na mingineyo, katika ishara za Mwenyezi Mungu hawaifahamu isipokuwa wenye akili na busara.
Mwenyezi Mungu ameumba mbingu na ardhi kwa haki.
Yaani kwa njia ya hekima na masilahi; na wala hakuziumba burebure na kwa mchezo. Hekima ya kuumbwa kwake ni kukaliwa na viumbe, wanufaike nayo na wapate dalili, kutokana na usanii wake na maajabu yake juu ya umoja wa Mwenyezi Mungu na utukufu wake.
Hakika katika hayo kuna ishara kwa waumini.
Hayo ya mpangilio na nidhamu ya kuumbwa mbingu na ardhi. Mpangilio huu ni dalili mkataa juu ya umoja wa Mwenyezi Mungu na utukufu wake kwa wale wanaoitafuta haki na kuiamini haki kwa ajili ya haki.