15
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI
وَلَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ كُلٌّ لَّهُ قَانِتُونَ ﴿٢٦﴾
26. Ni vyake vilivyo katika mbingu na ardhi. Vyote vinamtii.
وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ وَلَهُ الْمَثَلُ الْأَعْلَىٰ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢٧﴾
27. Naye ndiye ambaye anaanzisha uumbaji kisha ataurudisha, na jambo hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano bora katika mbingu na ardhi. Na yeye ndiye Mwenye uwezo, Mwenye hekima.
ضَرَبَ لَكُم مَّثَلًا مِّنْ أَنفُسِكُمْ هَل لَّكُم مِّن مَّا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُم مِّن شُرَكَاءَ فِي مَا رَزَقْنَاكُمْ فَأَنتُمْ فِيهِ سَوَاءٌ تَخَافُونَهُمْ كَخِيفَتِكُمْ أَنفُسَكُمْ كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿٢٨﴾
28. Amewapigia mfano kutokana na nafsi zenu. Je, katika hao iliyowamiliki mikono yenu ya kuume mnao washirika katika hivyo tulivyowaruzuku, mkawa nyinyi katika hivyo ni sawasawa, mkawahofia kama mnavyohofiana? Namna hiyo tunazipambanua Aya zetu kwa watu wenye akili.
بَلِ اتَّبَعَ الَّذِينَ ظَلَمُوا أَهْوَاءَهُم بِغَيْرِ عِلْمٍ فَمَن يَهْدِي مَنْ أَضَلَّ اللَّـهُ وَمَا لَهُم مِّن نَّاصِرِينَ ﴿٢٩﴾
29. Bali waliodhulumu wamefuata hawa zao pasi na kujua. Basi ni nani atamwongoa ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza?
Aya 26 – 29
Ni vyake vilivyo katika mbingu na ardhi. Vyote vinamtii.
Ulimwengu na vilivyomo ndani yake ni miliki ya Mwenyezi Mungu na vinakwenda kulingana na utashi wake; hata wale wanaomuasi pia anawafanya atakavyo, bila ya mpinzani.
Naye ndiye ambaye anaanzisha uumbaji kisha ataurudisha, na jambo hili ni jepesi zaidi kwake.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameumba ulimwengu, kisha atauondoa, tena ataurudisha mara nyingine.
Makusudio ya wepesi zaidi hapa ni wepesi tu; sio kuwa kuna mengine ni mepesi kidogo na mengine zaidi; kama vile kusema Mwenyezi Mungu ni Mkubwa zaidi, haimaanishi kuwa kuna mwingine aliye mkubwa na yeye ni mkubwa zaidi. Kwa sababu ambaye hana mfano wa kitu chochote, mambo yote kwake ni sawa. Haifai kusema ni mkubwa zaidi ya mwingine wala hili ni jepesi zaidi ya mengine.
Naye ndiye mwenye mfano bora katika mbingu na ardhi. Na yeye ndiye Mwenye uwezo, Mwenye hekima.
Makusudio ya mfano bora hapa ni sifa bora ambazo hashirikianai na yeyote katika sifa hizo. Nazo ni kuwa: Hakuna Mola isipokuwa yeye na Yeye ndiye Mwenye nguvu ambaye hashindwi na mwenye hekima asiyefanya mchezo.
Amewapigia mfano kutokana na nafsi zenu. Je, katika hao iliyowamiliki mikono yenu ya kuume mnao washirika katika hivyo tulivyowaruzuku, mkawa nyinyi katika hivyo ni sawasawa, mkawahofia kama mnavyohofiana?
Mfano huu, Mwenyezi Mungu (s.w.t), anaupiga kwa mataghuti wapenda anasa ambao wanamiliki watumwa na mali na wanadai kuwa Mwenyezi Mungu ana washirika katika kuumba kwake. Ufafanuzi wake ni kuwa: Angalieni enyi washirikina wapenda anasa.
Nyinyi mna watumwa na mali, lakini hamuwashirikishi kwenye mali zenu, wala hamkubali wazitumie ila kwa idhini yenu; wala hamuwahofii, wakati mnapowatumia, kama mnavyowahofia washirika wenu wasiokuwa watumwa na hali ya kuwa wale ambao mmewafanya watumwa sio milki yenu hasa.
Sasa vipi wale ambao ni milki ya Mwenyezi Mungu hasa mmewafanya ni washirika wake katika miliki yake na kuumba kwake. Vipi mnamnasibishia Mwenyezi Mungu yale ambayo nyinyi hamyaridhii. Nyinyi mnachukia kuwa na ushirika na wale mnaodai ni watumwa wenu, lakini Mwenyezi Mungu asichukie kuwa na ushirika na viumbe wake. Ole wenu! Mnahukumu vipi?
Hii ni sawa na kusema kwao kuwa Mwenyezi Mungu ana watoto wasichana na sisi tuna wavulana:
“Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu mabinti. Ametakata na hayo! Na hali wao hupata wanavyovitamani. Na mmoja wao akibashiriwa msichana uso wake unasawijika naye amejaa chuki.” Juz. 14 (16: 57 – 58).
Namna hiyo tunazipambanua Aya zetu kwa watu wenye akili.
Mfano huu ni wazi kabisa kuwa Mwenyezi Mungu hana mshirika, wala hawapofuki na mfano huu ispokuwa watu wa masilahi na matamanio.
Bali waliodhulumu wamefuata hawa zao pasi na kujua.
Ambapo haki iko katika hawa zao na uadilifu uko katika wanayoyatamani. Huu ndio ujinga wa mwisho na upotevu ulio wazi.
Basi ni nani atamwongoa ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza?
Mwenyezi Mungu amewapoteza kwa vile wameamua kufuata njia ya upotevu. Kila mwenye kufuata njia atafika; iwe njia ya kheri au ya shari; ya kuokoka au ya kuangamia.
Nao hawatakuwa na wasaidizi.
Vipi wawe na usaidizi na hali wao wameamua kufuata njia ya maangamizi kutokana na uchaguzi wao mbaya, wala hawakuonyeka au kukoma na makemeo yoyote.
فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا لَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّـهِ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٠﴾
30. Basi uelekeze uso wako sawa-sawa kwenye dini–ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo dini ya sawasawa, lakini watu wengi hawajui.
مُنِيبِينَ إِلَيْهِ وَاتَّقُوهُ وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَلَا تَكُونُوا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٣١﴾
31. Muwe wenye kurejea kwake na mcheni. Na simamisheni Swala wala msiwe katika washirikina.
مِنَ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ ﴿٣٢﴾
32. Katika wale walioigawa dini yao na wakawa makundi makundi. Kila kundi hufurahia waliyo nayo.
Aya 30 – 32
Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye dini–ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo dini ya sawasawa, lakini watu wengi hawajui.
Aya hii, mara nyingi, inakuwa vinywani mwa mahatibu na kwenye kalamu za waandishi. Kuna wale wanaotosheka na kuitolea dalili tu. Wengine wanaipamba wakisema: Hii ndio dini iliyo sahihi iliyo kubwa n.k.
Bila shaka Aya hii inathibisha msingi unaotiliwa mkazo na itikadi ya Kiislamu na sharia yake. Na inafahamisha wazi kwamba mafunzo ya dini kuanzia alifu mpaka ye (a mpaka z) yanaongoza kwenye uongofu na utekelezaji wa matakwa ya maisha, ukuaji na maendeleo yake.
Kwanza tutanza kufasiri misamiati iliyo katika Aya hii, kisha tutaja maana kijumla.
Neno umbile kwa ujumla linamanisha tabia iliyo ndani ya mtu, inayoikubali kheri inapoijua kuwa ni kheri na kulazimiana nayo kwa vile tu kheri inakubalika. Na tabia hiyo inaikataa shari inapoijua kuwa ni shari, si kwa jingine ila ni kwamba shari inakataliwa na kuepukwa.
Hii ni itakapokuwa umbile la mtu ni safi, halina takataka za desturi na uuigizaji wala halikuchafuliwa na hawaa. Mwanchuoni mkuu Hilli (Allama Hilli) ameipigia mfano tabia hii kwa kusema: “Lau mwenye akili atahiyarishwa kusema ukweli na apewe pesa au aseme uwongo pia apewe pesa, basi atachagua ukweli.”
Tabia hii inayochagua ukweli kuliko uongo ndio ile aliyoizungumzia Mwenyezi Mungu pale aliposema: “Je, mimi si Mola wenu? Wakasema: Kwa nini!” Juz. 9 (7:152). Pia ndiyo iliyokusudiwa na Hadith mashuhuri iliyopokewa kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) : “Kila anayezaliwa anazaliwa na umbile mpaka wazazi wake wamfanye Yahudi au Mnaswara.”
Ama neno ‘kwenye dini’ hapa linamanisha msimamo wa umbile ambalo Mwenyezi Mungu amewaumbia watu la kuwa mbali na hawaa za nafsi.
Makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu,” ni kuwa dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuthibiti kwa msingi wa kimaumbile, hauepukani nayo.
Neno ‘Hiyo’ ni ishara ya yale aliyoyawajibisha Mwenyezi Mungu kwa waja kulazimiana nayo kwa kauli na vitendo. Kwa sababu ndiyo dini ya kisawasawa isiyokuwa na kombokombo.
Ama kwa ujumla wake inafahamisha kuwa dini inafungamana na maumbile ya mtu, lakini hii haimaanishi kuwa umbile ndilo muamrishaji na mkatazaji na dini ielezee hukumu zake, hapana! Mwenyezi Mungu ambaye ameumba dini na maumbile ndiye muweka sharia wa kwanza. Ni Yeye pekee mwenye kuamrisha na kukataza.
Hakika makusudio ya Aya ni kuelezea kipimo tunachopimia dini ya Mwenyezi Mungu na kwamba itikidi, sharia na maadili yake yanenda sambamba na umbile la watu na masilahi yao; na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuweka hukumu kwa waja wake kupingana na manufaa ya mtu binafsi au jamii.
Huu ndio udhibiti na tofauti iliyoko baina ya hukumu ya Mwenyezi Mungu na hukumu nyinginezo, tofauti baina ya sharia ya haki na sharia ya batili. Ama kauli za maulama wa fiqih, tafsir na falsafa sio msingi wa Uislamu, wala haifai kuwategemea kama dalili ya sharia. Kwa sabau kauli zao hizo zinaakisi tu juhudi na fahamu zao katika dini ya Mwenyezi Mungu na hukumu zake, wala haziakisi uhakika na uhalisi wa dini.
Kwa ufupi ni kuwa Uislamu haukatai yote yaliyo katika dini na madhehbu mengineyo; bali unaangalia kwa mtazamo wa undani na usanifu. Unakubaliana yale yanayoafikiana na umbile la Mwenyezi Mungu na kukataa yasiyokuwa hayo.
Muwe wenye kurejea kwake na mcheni . Rudini kwenye dini hii na mtii hukumu zake zote.
Na simamisheni Swala kwani inawakumbusha Mwenyezi Mungu; wala msiwe katika washirikina.
Mfanyieni ikhlasi Mwenyezi Mungu peke yake kwenye kauli zenu na vitendo vyenu.
Katika wale walioigawa dini yao na wakawa makundi makundi. Kila kundi hufurahia waliyo nayo.
Umepita mfano wake katika Juz. 8 (6:158) na Juz. 18 (23:53).
وَإِذَا مَسَّ النَّاسَ ضُرٌّ دَعَوْا رَبَّهُم مُّنِيبِينَ إِلَيْهِ ثُمَّ إِذَا أَذَاقَهُم مِّنْهُ رَحْمَةً إِذَا فَرِيقٌ مِّنْهُم بِرَبِّهِمْ يُشْرِكُونَ ﴿٣٣﴾
33. Watu yakiwagusa madhara humwomba Mola wao wakiwa wanarejea kwake. Kisha akiwaonjesha rehema kutoka kwake, mara kikundi miongoni mwao humshirikisha Mola wao.
لِيَكْفُرُوا بِمَا آتَيْنَاهُمْ فَتَمَتَّعُوا فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ ﴿٣٤﴾
34. Ili wapate kuyakana tuliyowapa. Basi stareheni. Mtakuja jua.
أَمْ أَنزَلْنَا عَلَيْهِمْ سُلْطَانًا فَهُوَ يَتَكَلَّمُ بِمَا كَانُوا بِهِ يُشْرِكُونَ ﴿٣٥﴾
35. Au tumewateremshia hoja inayowaambia juu ya yale wamshirikishayo nayo?
وَإِذَا أَذَقْنَا النَّاسَ رَحْمَةً فَرِحُوا بِهَا وَإِن تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ إِذَا هُمْ يَقْنَطُونَ ﴿٣٦﴾
36. Na watu tunapowaonjesha rehema huifurahia. Na ukiwasibu uovu kwa iliyoyatanguliza mikono yao wenyewe, mara wanakata tamaa.
أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٣٧﴾
37. Je, hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humkunjia. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaoamini.
فَآتِ ذَا الْقُرْبَىٰ حَقَّهُ وَالْمِسْكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ ذَٰلِكَ خَيْرٌ لِّلَّذِينَ يُرِيدُونَ وَجْهَ اللَّـهِ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿٣٨﴾
37. Basi mpe jamaa haki yake na masikini na mwananjia. Hayo ni kheri kwa wale watakao radhi ya Mwenyezi Mungu na hao ndio wenye kufanikiwa.
وَمَا آتَيْتُم مِّن رِّبًا لِّيَرْبُوَ فِي أَمْوَالِ النَّاسِ فَلَا يَرْبُو عِندَ اللَّـهِ وَمَا آتَيْتُم مِّن زَكَاةٍ تُرِيدُونَ وَجْهَ اللَّـهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُضْعِفُونَ ﴿٣٩﴾
39. Na mnachokitoa katika riba ili kiongezeke katika mali ya watu, basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mlichokitoa Zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio watakaozidishiwa.
اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَكُمْ ثُمَّ رَزَقَكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ هَلْ مِن شُرَكَائِكُم مَّن يَفْعَلُ مِن ذَٰلِكُم مِّن شَيْءٍ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٤٠﴾
40. Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaumba, kisha akawaruzuku, kisha atawafisha na kisha atawafufua. Je katika mnaowashirikisha yuko awezaye kufanya lolote katika hayo? Ametakasika na ametukuka na hayo wanayomshirikisha nayo.
Aya 33 – 40
Watu yakiwagusa madhara humwomba Mola wao wakiwa wanarejea kwake. Kisha akiwaonjesha rehema kutoka kwake, mara kikundi miongoni mwao humshirikisha Mola wao.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:12) na Juz. 15 (17:67).
Ili wapate kuyakana tuliyowapa. Basi stareheni. Mtakuja jua.
Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii (29:66).
Au tumewateremshia hoja inayowaambia juu ya yale wamshirikishayo nayo?
Au hapa ni kwa maana ya mbali. Maana ni kuwa Je, kuna wahyi au akili yoyote inayoshuhudia kuwa ushirikina mlio nao ni sawa na haki? Makusudio ya swali hili ni kupinga na kukemea.
Na watu tunapowaonjesha rehema huifurahia. Na ukiwasibu uovu kwa iliyoyatanguliza mikono yao wenyewe, mara wanakata tamaa.
Huyu ndiye binadamu. Akipata heri anafurahi na kujifaharisha na akipat- wa na shari anakata tamaa. Umetangulia mfano wake katika Juz. 12 (11:9).
Je, hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humkunjia. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaoamini.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:26) na Juz. 15 (17:30).
Basi mpe jamaa haki yake na masikini na mwananjia.
Jamaa aliye fukara ana haki kwa jamaa yake aliye tajiri ya kumpa cha kusitiri haja. Shafii na Shia Imamiya wamesema kuwa ni wajibu kumtunza jamaa akiwa ni baba na kuendelea juu na mtoto na kuendelea chini.
Malik akasema: “Hakuna wajibu isipokuwa kwa wazazi na watoto wa karibu tu, sio baba wa baba au mtoto wa mtoto.”
Hambali anasema: “Ni wajibu kumtunza ndugu kwa sharti ya kuwa mtunzaji awe ni mrithi wa anayemtunza.” Ama Hanafi wanaona kuwa sharti la msingi ni kuwa ndugu aliye maharimu kuoana naye. Ufafanuzi uko katika Kitabu chetu Alfiqh ala madhahibil-khamsa (Fiqh ya madhehebu matano).
Ama masikini na mwananjia yametangulia maelezo yao katika Juz. 10 (9:60).
Hayo ni kheri kwa wale watakao radhi ya Mwenyezi Mungu na hao ndio wenye kufanikiwa.
‘Hayo’ ni ishara ya kutoa - kwamba ni wajibu kuwe ni kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, kama ilivyo kwa watu wema na wa kufaulu.
Na mnachokitoa katika riba ili kiongezeke katika mali ya watu, basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kuna kundi la wafasiri waliosema kuwa makusudio ya riba hapa ni ile riba ya haramu. Wengine wakasema makusudioa yake ni riba ya halali; kama vile mtu kumpa zawadi tajiri ili arudishe zawadi kubwa zaidi.
Vizuri ni kuichukulia Aya kwa yote mawili – kwamba zote mbili hazina thawabu mbele ya Mwenyezi Mungu; isipokuwa ya kwanza ina adhabu na ya pili haina thawabu wala adhabu.
Lakini mlichokitoa Zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio watakaozidishiwa.
Yaani watazidishiwa thawabu na malipo. Maana ya kiujumla ni kuwa mwenye kutoa kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenyezi Mungu humzidishia mali yake duniani na thawabu zake akhera. Imam Ali(a.s) anasema:“Mkifilisika basi fanyeni biashara na Mwenyezi Mungu.” Kauli hii imechukuliwa kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu:“Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, ili amzidishie ziada nyingi?” Juz. 2 (2:245).
Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaumba, kisha akawaruzuku, kisha atawafisha na kisha atawafufua. Je katika mnaowashirikisha yuko awezaye kufanya lolote katika hayo?
Mnavifanyia ubakhili alivyowapa Mwenyezi Mungu na mnataka riziki kwa wengine; na hali Yeye Mwenyezi Mungu ndiye aliyewafanya muweko baada ya kuwa hamko, akawamiminia baraka zake nyingi. Yeye ndiye anayewafisha na kuwapa uhai kisha awakusanye kwa ajili ya hisabu na malipo? Je, katika hao mnaowatarajia fadhila zao na kutarajia kuwanufaisha kuna anayeweza kutoa uhai na kufisha? Tukikadiria kuwa wanaweza kufanya baadhi ya mambo katika maisha haya, je kesho wataweza kunufaisha na kudhuru?
Ametakasika na ametukuka na hayo wanayomshirikisha naye.
Kuna hadith isemayo: “Shirki imejificha zaidi kuliko kutambaa kwa chungu.” Hapa kuna ishara kwamba shirki ziko aina nyingi, ikiwemo ile ya kumtegemea muumbwa badala ya Muumba.