23
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA
وَهَلْ أَتَاكَ نَبَأُ الْخَصْمِ إِذْ تَسَوَّرُوا الْمِحْرَابَ ﴿٢١﴾
21. Na je, imekufikia habari ya wagombanao walipopindukia ukuta kuingia mihrabu.
إِذْ دَخَلُوا عَلَىٰ دَاوُودَ فَفَزِعَ مِنْهُمْ قَالُوا لَا تَخَفْ خَصْمَانِ بَغَىٰ بَعْضُنَا عَلَىٰ بَعْضٍ فَاحْكُم بَيْنَنَا بِالْحَقِّ وَلَا تُشْطِطْ وَاهْدِنَا إِلَىٰ سَوَاءِ الصِّرَاطِ ﴿٢٢﴾
22. Walipomuingilia Daudi, naye akawaogopa. Wakasema: Usiogope! Ni mahasimu wawili, mmoja wetu amemdhulumu mwenziwe. Basi tuhukumu kwa haki, wala usipendelee. Na utuongoze kwenye njia iliyo sawa.
إِنَّ هَـٰذَا أَخِي لَهُ تِسْعٌ وَتِسْعُونَ نَعْجَةً وَلِيَ نَعْجَةٌ وَاحِدَةٌ فَقَالَ أَكْفِلْنِيهَا وَعَزَّنِي فِي الْخِطَابِ ﴿٢٣﴾
23. Hakika huyu ndugu yangu ana kondoo wa kike tisini na tisa; na mimi nina kondoo mke mmoja. Akasema: Nipe huyo! Na amenishinda kwa maneno.
قَالَ لَقَدْ ظَلَمَكَ بِسُؤَالِ نَعْجَتِكَ إِلَىٰ نِعَاجِهِ وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ الْخُلَطَاءِ لَيَبْغِي بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَقَلِيلٌ مَّا هُمْ وَظَنَّ دَاوُودُ أَنَّمَا فَتَنَّاهُ فَاسْتَغْفَرَ رَبَّهُ وَخَرَّ رَاكِعًا وَأَنَابَ ﴿٢٤﴾
24. Akasema: Kweli amekudhulumu kwa kumtaka kondoo wako mmoja kuongezea kwenye kondoo wake. Na hakika washirika wengi hudhulumiana wao kwa wao. Isipokuwa walioamini na wakatenda mema. Na hao ni wachache. Na Daud akaona kuwa tumemfanyia mtihani. Basi akamwomba maghufira Mola wake na akaanguka kunyenyekea na kutubia.
فَغَفَرْنَا لَهُ ذَٰلِكَ وَإِنَّ لَهُ عِندَنَا لَزُلْفَىٰ وَحُسْنَ مَآبٍ ﴿٢٥﴾
25. Basi tukamghufiria kwa hayo. Naye kwa hakika anao ukuruba na marejeo mazuri kwetu.
Aya 21 – 25
Baadhi ya wafasiri, wakifafanua Aya hii, wamemnasibishia Nabii Daud mambo ambayo si laiki hata ya mtu wa kawaida mwenye murua na haya; sikwambii tena mtume aliye maasumu. Wakataja kisa kirefu kutoka katika Biblia kitabu cha 2 Samweli: 11 na 12, kutoka agano la kale ambalo mahala pake pamechukuliwa na hukumu ya Qur’an. Nukuu za agano lenyewe kuhusiana na hilo haziingiliki akili.
Muhtasari wa kisa chenyewe ni kuwa Daud alimtamani mke wa mmoja wa watumishi wake aliye pia mwanajeshi wake. Basi akamfanyia hila ya kumuua ili amchukue mkewe. Biblia inasema kuwa Mwenyezi Mungu alikasirika sana na kumkemea kwa kitendo kibaya alichokifanya; miongoni mwa aliyoyasema ni “…Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe ukamtwaa mkewe awe wako… Basi sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau…Nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili. Maana wewe ulifanya jambo hili kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israil wote na mbele ya jua” (2 Samweli 12:9-12.).
Katika 1 Wafalme 1 imeelezwa kuwa jina la mke wa Uria ni Bath-sheba naye ndiye mama yake Suleiman bin Daud.
Daud azini kwa siri na Mwenyezi Mungu, badala ya kumpa adhabu ya hadd ya zina au kumlaumu na kumtaka atubie, badala ya kumfanyia hivyo, anamtia adabu kwa kuwavunjia heshima wakeze wawe uchi na wafanye machafu hadharani kweupe mchana kadmanasi!
Haya ndio maandiko matakatifu yanavyomsifu muumba kwa sifa za unyama. Mwenyezi Mungu Mtukufu ametakata kabisa na hayo wanayomsifu nayo. Huu ni mfano mmoja kati ya mifano kadhaa. Soma kuhusu kupigana miereka Mwenyezi Mungu na Ya’qub na kushindikana kupatikana mshindi, mpaka Ya’qub akalazimika kupiga mfupa wa paja wa Mwenyezi Mungu.
Vile vile soma yaliyoandikwa kwenye biblia, Kumbukumbu la Torat, 7, kwamba Mungu amewahalalishia Mayahudi kula mataifa yote, bila ya huruma. Baadhi ya wafasiri wametegemea Hadith hizi za kiisrail, katika kufasiri Aya za Qur’an yenye mawaidha, biashara na maonyo; ikiwemo hii tuliyo nayo. Kwa hiyo ni juu ya msomaji kuzikabili kauli zao na tafsiri zao kwa jicho la hadhari sana.
Na je, imekufikia habari ya wagombanao walipopindukia ukuta kuingia mihrabu. Walipomuingilia Daudi, naye akawaogopa.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamsilmulia Nabii wake mtukufu kisa cha Daud, kwamba siku moja Daud alipokuwa amemwelekea Mola wake kwenye mswala wake, ghafla watu wawili wakajitokeza mbele yake ana kwa ana. Basi kushtukiza huku kulimshtua; tena kuingia kwao kwa njia isiyokuwa ya kawaida.
Hata hivyo kuingia kwao huko, kusikokuwa kwa kawaida, hakufahamishi lolote kuwa ni malaika; kama walivyolitolea dalili baadhi ya wafasiri. Kwa sababu hata binadamu pia anaweza kuingia nyumbani kwa njia isiyokuwa ya kawaida kutokana na sababu fulani. Pia Aya haikuashiria kuwa ni malai- ka. Kwa hiyo hakuna sababu ya kuleta taawili ya kuwa ni malaika.
Wakasema: Usiogope! Ni mahasimu wawili, mmoja wetu amemdhulumu mwenziwe. Basi tuhukumu kwa haki, wala usipendelee. Na utuon- goze kwenye njia iliyo sawa.
Walipoona hofu iliyomjaa, haraka sana wakamtuliza na kusema, sisi tumekuja kwako kuhukumiwa, basi utuhukumu kwa uadilifu na utuongoze kwenye haki wala usikengeuke nayo. Kisha mmoja wao akasema:
Hakika huyu ndugu yangu ana kondoo wa kike tisini na tisa; na mimi nina kondoo mke mmoja. Akasema: Nipe huyo! Na amenishinda kwa maneno.
Hapa hakuna haja yoyote ya kuleta taawili. Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa tukio hili lilitokea wakati wa zama za Nabii Daud; nalo lina mfano wake katika kila zama na kila wakati; hasa wakati wetu huu wa sasa. Kwa hiyo ni wajibu kuichukulia dhahiri yake na kuitumia.
Akasema: Kweli amekudhulumu kwa kumtaka kondoo wako mmoja kuongezea kwenye kondoo wake.
Daud aliyasema haya kabla ya kusikiliza ushahidi kutoka kwa mdai na kujibu mdaiwa.
Na hakika washirika wengi hudhulumiana wao kwa wao.
Hapa itabidi kuchukulia majazi neno washirikia, kuwa na maana ya wenye mabavu. Kwa sababu hakukua na ushirika wowote kati ya wale mahasimu wawili.
Isipokuwa walioamini na wakatenda mema. Na hao ni wachache.
Nguvu inakuwa ni ya haki ikiwa kwa watu wema, lakini ikiwa kwa waovu basi, bila shaka yoyote, itakuwa dhidi ya haki. Na watu wema ni wachache kwa idadi, lakini wana nguvu katika maadili yao na sifa zao.
Na Daud akaona kuwa tumemfanyia mtihani. Basi akamwomba maghufira Mola wake na akaanguka kunyenyekea na kutubia
Baada ya Daud kutoa hukumu, alitanabahi kuwa amehukumu kabla ya kutaka dalili upande wa pili. Kwa hiyo akajuta na akamuomba msamaha Mwenyezi Mungu.
Basi tukamghufiria kwa hayo. Naye kwa hakika anao ukuruba na marejeo mazuri kwetu.
Mwenyezi Mungu alimsamehe Daud kwa vile alikuwa ni miongoni mwa waliotangulia kumtii Mwenyezi Mungu na kutaka radhi yake.
Katika kitabu Uyunil-akhbar, imeelezwa kuwa mtu mmoja alimuuliza Imam Ar-Ridha(a.s ) kuhusu kisa cha Daud na Uria na mkewe, Imam akapinga yanayonasibishiwa Daud. Muulizaji akauliza: Kosa lake lilikuwa nini ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu? Basi akajibu kwa jawabu refu, miongoni mwake ni: “Daud alifanya haraka kusema: “Kweli amekudhulumu kwa kumtaka kondoo wako mmoja kuongezea kwenye kondoo wake,” bila ya kumuuliza yule mwingine unasemaje? Basi hilo likuwa ni kosa la rasimu ya mahakama, sio kosa la wanavyosema watu.
Kwani hukusikia Mwenyezi Mungu Mtukufu alivyomwambia Daud: “Basi wahukumu watu kwa haki, wala usifuate matamanio Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya uwe Khalifa ardhini.”
Unaweza kuuliza : Vipi Daud alihukumu bila ya ushahidi, na tunajua kuwa mitume wamehifadhiwa na makosa (ni maasumu).
Jibu : kuwa maasumu hakumaanishi kuwa na maumbile mengine yasiyokuwa ya kibinadamu, hapana! Maasumu ni mtu kama watu wengine. Maana ya isma ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamlinda wakati wowote; hata wakijaribu watu kumhadaa kwa mandhari ya uzuri, basi Mwenyezi Mungu mara moja humwongoza kwenye haki na uhakika, kabla ya kuiingia mtegoni. Na hivyo ndivyo ilivyomtokea Daud. Mwenye kondoo mmoja alijaribu kumhadaa kwa namna yake ya kutaka kuhurumiwa, lakini Mwenyezi Mungu alimpa ilhamu ya uhakika kabla ya kutoa hukumu, akafahamu na akatubia.
Mtume alitokewa na yaliyo karibu na haya na akakurubia kuhadaiwa lau si Mwenyezi Mungu kumwimarisha kwa kumwambia: “Hakika tumekuteremshia Kitabu kwa haki ili upate kuhukumu baina ya watu kwa alivyokufahamisha Mwenyezi Mungu; wala usiwe mtetezi wa wenye kufanya hiyana. Na muombe maghufira Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu. Wala usiwatetee wale ambao wamezihini nafsi zao...” Juz. 5 (4:105 – 107).
Na akasema Mwenyezi Mungu kumwambia Mtume wake Mtukukufu:
وَلَوْلَا أَن ثَبَّتْنَاكَ لَقَدْ كِدتَّ تَرْكَنُ إِلَيْهِمْ شَيْئًا قَلِيلًا ﴿٧٤﴾
“Lau sikukuweka imara ungelikurubia kuwaelekea kidogo.” Juz. 15 (17:74).
Kuna Hadith isemayo: “Mimi ni mtu kama nyinyi, isipokuwa ninapewa wahyi tu. Na nyinyi mnakuja kuamuliwa kwangu. Pengine mmoja wenu anaweza kuwa hodari wa kusema kuliko mwingine na nikahukumu kulingana na nilivyosikia.
Ikiwa mtu nitamuhukumia kumpatia kitu katika haki ya ndugu yake, basi ajue ninampatia kipande cha Moto.”
Ingawaje Hadith hii haingii moja kwa moja kwenye maudhui haya tuliyo nayo, lakini tunaweza kuiunganisha nayo. Ama toba ya manabii na kutaka kwao maghufira ya dhambi, hiyo ni aina ya ibada na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t). Hilo tumeliashiria mara kadhaa.
يَا دَاوُودُ إِنَّا جَعَلْنَاكَ خَلِيفَةً فِي الْأَرْضِ فَاحْكُم بَيْنَ النَّاسِ بِالْحَقِّ وَلَا تَتَّبِعِ الْهَوَىٰ فَيُضِلَّكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ إِنَّ الَّذِينَ يَضِلُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ بِمَا نَسُوا يَوْمَ الْحِسَابِ ﴿٢٦﴾
26. Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya uwe Khalifa ardhini. Basi wahukumu watu kwa haki, wala usifuate matamanio, yakakupoteza Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika wanaopotea Njia ya Mwenyezi Mungu, watapata adhabu kali kwa sababu ya kusahau kwao Siku ya Hisabu.
وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا بَاطِلًا ذَٰلِكَ ظَنُّ الَّذِينَ كَفَرُوا فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ كَفَرُوا مِنَ النَّارِ ﴿٢٧﴾
27. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake bure. Hiyo ni dhana ya waliokufuru. Ole wao walio kufuru kwa Moto.
أَمْ نَجْعَلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَالْمُفْسِدِينَ فِي الْأَرْضِ أَمْ نَجْعَلُ الْمُتَّقِينَ كَالْفُجَّارِ ﴿٢٨﴾
28. Je! Tuwafanye walioamini na wakatenda mema kama wafisadi katika ardhi? Au tuwafanye wenye takua kama waovu?
كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٢٩﴾
29. Hiki ni Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili.
Aya 26 – 29
Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya uwe Khalifa ardhini.
Kila mtu aliyeko, au atakayekuweko, ardhini basi huyo ni khalifa wa Mwenyezi Mungu ardhini; kwa maana yakuwa ana majukumu mbele ya Mwenyezi Mungu ya kufanya mambo ya heri duniani na Akhera katika maisha haya.
Hayo ndio maana ya ukhalifa ardhini kwa hali yoyote ile; isipokuwa watu wanatofautiana kulingana na majukumu yenyewe; ambapo kila mmoja anatakiwa atekeleze kulingana na uwezo na wadhifa wake.
Kwa kuwa wadhifa wa manabii ni kutoa bishara na hadhari, ili watu wasiwe na hoja mbele ya Mwenyezi Mungu, basi imekuwa ni wajibu kwao kuwahukumu watu kwa haki na wengine wawasikilize wao.
Basi wahukumu watu kwa haki, wala usifuate matamanio, kwa sababu unabii uko hivyo kimaumbile.
Kwa maneno mengine ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamchagulia wahyi wake yule anayeiamini haki na kuitumia na inakuwa ni muhali kwake kukosea.
Yakakupoteza Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika wanaopotea Njia ya Mwenyezi Mungu, watapata adhabu kali kwa sababu ya kusahau kwao Siku ya Hisabu.
Muovu zaidi katika watu ni yule mwenye kumhalifu Mola wake na akafuata matamanio yake. Kuna Hadith isemayo: “Hakika ninalolihofia zaidi kwenu ni hawaa na tamaa nyingi. Hawaa inaipinga haki na tamaa nyingi inasahauliza akhera.”
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo kati yake bure.
Lau katika kuumbwa mbingu na ardhi kungelikua na chembe ya mchezo au hivi hivi tu, basi ulimwengu usingeendelea na nidhamu kwa mamilioni ya miaka.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:191).
Hiyo ni dhana ya waliokufuru. Ole wao waliokufuru kwa Moto.
Hiyo inaashiria kuwa hakuna tofauti kati ya aneyepinga kuweko Mwenyezi Mungu kabisa na yule anayekubali, lakini akapinga kuweko hekima katika kuumba kwake. Kwa sababu dalili zake ni wazi na alama zake ziko kweupe.
Imam Ali(a.s ) anasema:“Amekadiria aliyoumba akapangilia makadirio yake; akapangilia akafanya kwa uangalifu mipangilio yake; akaelekeza kwa maelekezo yake, lakini hakupetuka mpaka wa cheo chake wala hakupunguza ukomo wa lengo lake.”
Je! Tuwafanye walioamini na wakatenda mema kama wafisadi katika ardhi? Au tuwafanye wenye takua kama waovu?
Tofauti baina ya mwema na mfisadi na baina ya mwenye takua na muovu ni sawa na tofauti baina ya kipofu na mwenye kuona. Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (5:100) na Juz. 7 (6:50).
Katika kitabu Ahkamul-qur’an cha Kadhi Abi Bakri, ambaye ni maarufu kwa jina la Ibnul-arabiy, amesema: “Aya hii iliwashukia bani Hashim; na kwamba walioamini na kuwa na takua ni Ali bin Abi Twalib, ndugu yake Ja’far, Ubayda bin Tufayl, Al-harth bin Tufayl, Ummu ayman na wengineo, na kwamba wafisadi na waovu ni Bani Abd Shams.
Hiki ni Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili.
Hapa anaambiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) . Kitabu ni Qur’an, nayo ina baraka kwa kila mwenye kuiamini, ni dawa ya ukafiri na hulka mbaya na ni uokovu wa shirki na maangamizi. Kwenye Nahjul-Balagha imeelezwa:“Itakeni nasaha kwa nafsi zenu na mzituhumu rai zenu kwayo na mtake uokofu wa hawa zenu ndani yake.”