4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ إِلَّا أَن يُؤْذَنَ لَكُمْ إِلَىٰ طَعَامٍ غَيْرَ نَاظِرِينَ إِنَاهُ وَلَـٰكِنْ إِذَا دُعِيتُمْ فَادْخُلُوا فَإِذَا طَعِمْتُمْ فَانتَشِرُوا وَلَا مُسْتَأْنِسِينَ لِحَدِيثٍ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ يُؤْذِي النَّبِيَّ فَيَسْتَحْيِي مِنكُمْ وَاللَّـهُ لَا يَسْتَحْيِي مِنَ الْحَقِّ وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ وَمَا كَانَ لَكُمْ أَن تُؤْذُوا رَسُولَ اللَّـهِ وَلَا أَن تَنكِحُوا أَزْوَاجَهُ مِن بَعْدِهِ أَبَدًا إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمًا ﴿٥٣﴾
53. Enyi ambao mmeamini! Msiingie majumba ya Mtume ila mkipewa ruhusa ya kwenda kula, sio kungojea kiive. Lakini mtakapoitwa, basi ingieni. Na mkisha kula, tawanyikeni wala msiweke mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii, naye anawastahi nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu hastahi kwa haki. Na mnapowaomba chombo cha nyumbani, basi waulize nyuma ya mapazia. Hilo linasafisha zaidi nyoyo zenu na nyoyo zao. Haiwafalii nyinyi kumuudhi Nabii wala kuwaoa wake zake kabisa. Hakika hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
إِن تُبْدُوا شَيْئًا أَوْ تُخْفُوهُ فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٥٤﴾
54. Mkidhihirisha chochote au mkikificha, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
لَّا جُنَاحَ عَلَيْهِنَّ فِي آبَائِهِنَّ وَلَا أَبْنَائِهِنَّ وَلَا إِخْوَانِهِنَّ وَلَا أَبْنَاءِ إِخْوَانِهِنَّ وَلَا أَبْنَاءِ أَخَوَاتِهِنَّ وَلَا نِسَائِهِنَّ وَلَا مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ وَاتَّقِينَ اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدًا ﴿٥٥﴾
55. Hapana ubaya kwao kwa baba zao, wala watoto wao, wala kaka zao, wala watoto wa kaka zao, wala watoto wa dada zao, wala wanawake wao, wala wale waliomilikiwa na mikono yao ya kuume. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kushuhudia kila kitu.
Aya 53 – 55
Enyi ambao mmeamini! Msiingie majumba ya Mtume ila mkipewa ruhusa ya kwenda kula, sio kungojea kiive. Lakini mtakapoitwa, basi ingieni. Na mkisha kula, tawanyikeni wala msiweke mazungumzo.
Yaani msikae kabisa si kwa mazungumzo wala kwa jambo jingine. Yametajwa mazungumzo kwa vile mara nyingi mtu anakaa kwa kupiga gumzo.
Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa baadhi ya maswahaba walikuwa wakiingia nyumba ya Mtume(s.a.w. w ) bila ya idhini kama ilivyo ada ya kijahiliya; na kwamba wakiona chakula kinapikwa basi wanakingoja na baada ya kula walikuwa wakipiga gumzo.
Hakuna mwenye shaka kwamba aina hii ya upuzi na kukosa adabu inamuudhi binadamu yeyote, awe Mtume au si Mtume. Ni kwa ajili hii Mtume(s.a.w. w ) aliwafundisha adabu mswahaba na wengineo kuwa wasiingie nyumba yoyote bila ya idhini ya wenyewe - hayo yamedokezwa kwenye Juz. 18 (24:28) – na kwamba wasiende kula ila wakiitwa, tena chakula kiwe kimeandaliwa na wakishamaliza kula wasingoje tena.
Haya hayahusiki na nyumba ya Mtume peke yake; isipokuwa Mwenyezi Mungu amemtaja yeye kwa vile ndio sababu ya kushuka Aya. Mara nyingi tumesema kuwa sababu ya kushuka Aya haiifungi na hilo lililoishukia.
Hakika hayo yanamuudhi Nabii, naye anawastahi nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu hastahi kwa haki.
Makusudio ya haki aliyokuwa akiistahi Mtume ni haki yake ya kiutu – kuwatoa wapuuzi nyumbani kwake. Mtume aliwanyamazia kwa kuwaonea haya; ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akatanabahisha kwamba kubaki kwao baada ya chakula kunamuudhi Mtume, vile vile kuingia kwao nyumbani kwake bila ya idhini yake.
Kuna Hadith isemayo: “Haya ni tawi la imani na asiyekuwa na haya hana dini.” Kuna Hadith nyingine isemayo:“Hakukubakia katika mifano ya mitume isipokuwa kauli ya watu: Kama huna haya basi fanya utakavyo.”
Katika maelezo ya wasifu wa Mtume(s.a.w. w ) ni kuwa yeye alikuwa na haya kuliko mwanamwali kwenye ushungi wake. Katika Nahjul-balagha imesemwa:“Hakuna imani kama haya na subira.” Farazdaq katika kumsifu Imam Zaynul-abdin anasema:
Hufumba macho kwa haya kwa haiba yake. Hazungumzi ila kuonekana tabasamu yake Maajabu ni yale yaliyoandikwa kwenye kitabu Muhadharatul-udabai cha Asfahaniy:
“Doezi mmoja alilaumiwa kwa kudoea kwake, akasema akijitetea: “Ala! Ikiwa bani Israil walimdoea Mungu, je sisi tusidoee watu?”
Na mnapowaomba chombo cha nyumbani, basi waulize ni nyuma ya mapazia. Hilo linasafisha zaidi nyoyo zenu na nyoyo zao.
Yaani mnapowaomba haja wakeze Mtume. Kutaja chombo cha chumbani ni kutolea mfano tu, sio kuhusisha na kuondoa hukumu kwa vingine. Hilo linafahamishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Hilo linasafisha zaidi nyoyo zenu na nyoyo zao.” Inayotambulisha kuwa kuchanganyika na kuondoa pazia baina ya wanawake na wanaume kunaleta ufisadi na fitna.
Maana yake ni kuwa kuchanganyika ni haramu, au angalau ni bora kuacha. Hapa inatubainikia kuwa kuchanganyika ni sababu ya kuleta matamanio ya kijinsiya, na wala sio kumtia adabu mwanamke na kumkandamiza; kama wanavyodai wale wasemao: “Mungu amesema hivyo na mimi nasema hivi” Ni nani aliye mkweli zaidi kwa mazungumzo kuliko Mwenyezi Mungu?
Haiwafalii nyinyi kumuudhi Nabii wala kuwaoa wake zake kabisa. Hakika hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Hukumu hii inamuhusu Mtume tu peke yake. Kwa sababu wakeze wako katika daraja ya mama wa waumini. Imeelezwa katika Tafsir Arrazi na Ruhul-bayan ya Ismail Haqiy: “Hakika Aya hii ilishuka pale aliposema Twalha bin Abdallah Attaymiy:“Akifa Muhammad(s.a.w. w ) nitamuoa Aisha.”
Hilo linataliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu:
Mkidhihirisha chochote au mkikificha, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Hilo ni karipio kwa yule aliyedhamiria kuoa wake za Mtume baada yake.
Hapana ubaya kwao kwa baba zao, wala watoto wao, wala kaka zao, wala watoto wa kaka zao, wala watoto wa dada zao, wala wanawake wao, wala wale waliomilikiwa na mikono yao ya kuume. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kushuhudia kila kitu.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuamrisha kuzungumza na wanawake nyuma ya pazia (hijabu) hapa anavua wale ambao hawawezi kuoana nao, ambao ni: baba, mtoto, kaka, mtoto wa kaka na mtoto wa dada, mtumwa na wanawake. Lakini Mwenyezi Mungu amesema wanawake wao, yaani wanawake wenzao walio waumini, kwa sababu wasiokuwa waumini watawasifia wanaume zao.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 18 (24:31).
إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾
56. Hakika Mwenyezi Mungu na malaika wake wanamswalia Nabii. Enyi ambao mmeami- ni! Mswalieni na mumsalimu kwa salamu.
إِنَّ الَّذِينَ يُؤْذُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ لَعَنَهُمُ اللَّـهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَأَعَدَّ لَهُمْ عَذَابًا مُّهِينًا ﴿٥٧﴾
57. Hakika wale ambao wanamuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu amewalaani duniani na Akhera, na amewaandalia adhabu ya kufedhehesha.
وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ بِغَيْرِ مَا اكْتَسَبُوا فَقَدِ احْتَمَلُوا بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا ﴿٥٨﴾
58. Na wale ambao wanawaudhi waumini wanaume na waumini wanawake pasi na wao kufanya, hakika wamebeba dhulma kubwa na dhambi kubwa.
Aya 56 – 58
Hakika Mwenyezi Mungu na malaika wake wanamswalia Nabii. Enyi ambao mmeamini! Mswalieni na mumsalimu kwa salamu.
Makusudio ya Mwenyezi Mungu kumsalia Mtume ni kumridhia kumrehe- mu na kumsifu kwa kila kheri, swala ya malaika ni kumsifu, na kutoka kwa waumini ni kumwombea dua ya kuwa na daraja ya juu. Imam Ar-Ridha(a.s) aliulizwa kuhusu maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu: malaika na waumini humswalia Mtume, akasema:“Swala kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni rehema, kutoka kwa malaika ni kumsifu na kutoka kwa waumni ni kumwombea.”
Kuswaliwa huku hakuhusiki na risala ya Muhammad(s.a.w. w ) peke yake. Kila mtu anayetumia desturi ya risala ya Muhammad(s.a.w. w ) , kuifundisha au kuijulisha au kutaja fadhila yoyote katika fadhila zake basi atakuwa amemswalia, awe mumin au sio mumin, akitaka hilo au asitake.
Imam Ja’far As-Sadiq(a.s) anasema: “Mtu kumswalia Muhammad(s.a.w. w ) ni kama kusema:“Subhanallah walhamdulillah walailaha illaha wallahu akbar” (Kutakasika ni kwa Mwenyezi Mungu na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu na hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni mkubwa).
Imam hapa anakusudia kuwa thawabu za kumswalia Mtume ni sawa na thawabu za tasbih, tahmid, tahlil na takbir. Imepokewa Hadith kutoka kwa Mtume mtukufu(s.a.w. w ) , amesema:“Bakhili wa kweli ni yule ambaye nikitajwa mbele yake haniswalii” .
Katika Sahih Al-Bukhariy Juz. 8, mlango wa kumswalia mtume, Tafsir At- Tabariy, Tafsir Ar-Raziy, Tafsir Al-Maraghi na wafasiri wengineo, pia katika vitabu vya Hadith, kuna maelezo haya: “Mtume aliulizwa: Vipi tutakuswalia ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?Akasema: semeni:
Allahumma swalli a’la muhammdi wa a’la aali Muhammad, kama swal-layta a’la Ibrahima wa a’laa aali Ibrahim, Innaka hamidum majiid Allahumma barik ala muhammdi wa a’la ali Muhammad, kama barakta a’la Ibrahima wa a’la ali Ibrahim, Innaka hamidum majid.
(Ewe Mwenyezi Mungu mswalie Muhammad na kizazi cha Muhammad, kama ulivyomswalia Ibrahim na kizazi cha Ibrahim, hakika wewe ni mwenye kusifiwa mwenye kutukuzwa. Ewe Mwenyezi Mungu mbariki Muhammad na kizazi cha Muhammad, kama ulivyombariki Ibrahim na kizazi cha Ibrahim. Hakika wewe ni Mwenye kusifiwa Mwenye kutukuzwa. )
Katika tafsir Ruhul-bayan ya Ismail Haqiy, amesema: “Inatakikana mwenye kuswali aseme: Allhumma swali a’la Muhammad wa a’la AliMuhammad” kwa kulirudia neno ‘a’la’; kwani Sunni wanaweka neno hilo kabla ya aali, kuwapinga Shia ambao hawaliweki neno hilo.
Sisi hatuoni tofauti yoyote baina ya anayesema: neno hilo na asiyelisema. Ama kuhusu ile Hadith isemayo:“Mwenye kutenganisha baina yangu na kizazi changu, hatapata shafaa yangu,” Mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi usahihi wake.
Imam Shafii naye amesema katika shairi lenye maana hii: Enyi watu wa nyumba ya Mtume pendo lenu ni faradhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu amelieleza katika Qur’an. Inawatosha kuwa ni cheo kikuu kwamba nyinyi asiyewaswalia hana Swala
Hakika wale ambao wanamuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake Mwenyezi Mungu amewalaani duniani na Akhera, na amewaandalia adhabu ya kufedhehesha.
Makusudio ya kumuudhi Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kumghadhabisha, na sababu yenye kuwajibisha hilo ni kumpinga, kumnasibishia mshirika au mtoto, au kuasi hukumu miongoni mwa hukumu zake. Na kuumuudhi Mtume(s.a.w. w ) ni kupinga utume wake au kupuuza mwenendo wake.
Laana kutoka kwa Mungu ni kwa kuwekwa mbali na rehema yake na kutoka kwa watu ni shutuma na kuombewa mabaya. Katika Nahjul-balagha imeelezwa:“Mwenyezi Mungu amewalaani wanaoamrisha mema na kuacha kuyatenda na wanaokataza maovu na wanayoyatenda.”
Na wale ambao wanawaudhi waumini wanaume na waumini wanawake pasi na wao kufanya, hakika wamebeba dhulma kubwa na dhambi kubwa.
Pasi na wao kufanya, yaani kufanya kosa linalostahili udhia. Kuudhi kunakuwa ni kwa kusengenya, vitimbi, uzushi n.k. Kuna Hadith zisemazo:
“Mwislamu ni yule ambaye watu wamesalimika na mkono wake na ulimi wake.”
“Utukufu wa mumin ni kwa kujizuia na kuwaudhi watu.”
“Aliye dhalili zaidi katika watu ni yule anayewadharau watu.”
Imam Ali(a.s) anasema:“ Mwenye hali mbaya zaidi katika watu ni yule asiyemwaamini yeyote kwa dhana zake mbaya, na asiyeaminiwa na yeyote kwa vitendo vyake vibaya.”