7
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَن نُّؤْمِنَ بِهَـٰذَا الْقُرْآنِ وَلَا بِالَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الظَّالِمُونَ مَوْقُوفُونَ عِندَ رَبِّهِمْ يَرْجِعُ بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ الْقَوْلَ يَقُولُ الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا لِلَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا لَوْلَا أَنتُمْ لَكُنَّا مُؤْمِنِينَ ﴿٣١﴾
31. Na walisema waliokufuru: Hatutaiamini Qur’an hii, wala yaliyokuwa kabla yake. Na ungeliwaona madhalimu watakaposimamishwa mbele ya Mola wao wakirudishiana maneno! wale wanyonge wakiwaambia wale waliojifanya wakubwa: Lau si nyinyi bila shaka tungelikuwa waumini.
قَالَ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا لِلَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا أَنَحْنُ صَدَدْنَاكُمْ عَنِ الْهُدَىٰ بَعْدَ إِذْ جَاءَكُم بَلْ كُنتُم مُّجْرِمِينَ ﴿٣٢﴾
32. Wale waliojiona wakubwa watawaambia wale wanyonge: Kwani sisi ndio tuliowazuia na uongofu baada ya kuwafikia? Bali nyinyi wenyewe mlikuwa waovu. Kwani wanalipwa ila kwa waliokuwa wakiyatenda?
وَقَالَ الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا لِلَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا بَلْ مَكْرُ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ إِذْ تَأْمُرُونَنَا أَن نَّكْفُرَ بِاللَّـهِ وَنَجْعَلَ لَهُ أَندَادًا وَأَسَرُّوا النَّدَامَةَ لَمَّا رَأَوُا الْعَذَابَ وَجَعَلْنَا الْأَغْلَالَ فِي أَعْنَاقِ الَّذِينَ كَفَرُوا هَلْ يُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٣٣﴾
33. Na wale wanyonge watawaambia wale waliojifanya wakubwa: Bali ni vitimbi vyenu vya usiku na mchana, mlipokuwa mkituamrisha tumkufuru Mwenyezi Mungu na tumfanyie washirika, nao wataficha majuto watakapoiona adhabu. Na tutaweka minyororo shingoni mwa wale waliokufuru kwani wanalipwa ila kwa waliokuwa wakiyatenda?.
Aya 31-33
Na walisema waliokufuru: Hatutaiamini Qur’an hii, wala yaliyokuwa kabla yake, kama vile Tawrat na Injil. Walioyasema haya ni washirikina, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَقَالَ الرَّسُولُ يَا رَبِّ إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَٰذَا الْقُرْآنَ مَهْجُورًا {30 }
Na Mtume alisema: Ewe Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur’an ni mahame.” Juz. 19 (25:30).
Wameihama na kuikana kwa sababu inamfanya sawa mweusi na mweupe na ikawaambia:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَوْمٌ مِّن قَوْمٍ عَسَىٰ أَن يَكُونُوا خَيْرًا مِّنْهُمْ وَلَا نِسَاءٌ مِّن نِّسَاءٍ عَسَىٰ أَن يَكُنَّ خَيْرًا مِّنْهُنَّ وَلَا تَلْمِزُوا أَنفُسَكُمْ وَلَا تَنَابَزُوا بِالْأَلْقَابِ بِئْسَ الِاسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الْإِيمَانِ وَمَن لَّمْ يَتُبْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿١١﴾
“Enyi ambao mmeamini! Wanaume wasiwadharau wanaume wengine, huenda wakawa bora kuliko wao; wala wanawake kwa wanawake wengine, huenda wakawa bora kuliko wao. Wala msitiane kasoro, wala msiitane majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya imani.” (49:11).
Vile vile waliukana utume wa Muhammad(s.a.w. w ) kwa sababu alitaka kuwatoa kwenye ujinga na kurudi nyuma, waende kwenye elimu na maendeleo.
Mtaalamu mmoja wa Ulaya, Jack Rezler, aliyeandika kitabu kuhusu mwamko wa kiislamu na kingine kinachozungumzia maendeleo ya waarabu ambavyo vilichapishwa ufaransa mnamo 1962, alisema: “Hatua ya kwanza ya maendeleo ya waarabu ilianza kwa kujitokeza dini ya kiislamu.
Kuna sababu kadhaa zilizofanya maendeleo haya na kuenea kwake; sababu kubwa zaidi ni kuweko na roho ya kimaana kwa Waislamu kupitia dini hii mpya; jambo ambalo limeleta ushujaa, kiasi cha kufikia kuyadharau mauti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.”
Na ungeliwaona madhalimu watakaposimamishwa mbele ya Mola wao wakirudishiana maneno!
Baada ya Mtume(s.a.w. w ) kukata tamaa kuwa washirikina wataamini, Mola Mtukufu alimtuliza na kumwambia kuwa kesho utaona hawa waongo watakavyokuwa dhalili na kuhizika pale watakaposimama mbele ya Mwenyezi Mungu kwa hisabu, jinsi mfuasi atakavyomlaumu aliyemfuata kila mmoja atamtia makosani mwinginewale wanyonge wakiwaambia wale waliojifanya wakubwa: Lau si nyinyi bila shaka tungelikuwa waumini.
Wanyonge ni wale wafuasi; na waliojifanya wakubwa ni viongozi.
Wale waliojiona wakubwa watawaambia wale wanyonge: Kwani sisi ndio tuliowazuia na uongofu baada ya kuwafikia? Bali nyinyi wenyewe mlikuwa waovu, sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:
كَمَثَلِ الشَّيْطَانِ إِذْ قَالَ لِلْإِنسَانِ اكْفُرْ فَلَمَّا كَفَرَ قَالَ إِنِّي بَرِيءٌ مِّنكَ إِنِّي أَخَافُ اللَّـهَ رَبَّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦﴾
“Kama mfano wa shetani anapomwambia mtu: Kufuru. Na akikufuru humwambia: Mimi si pamoja nawe. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu. (59:16).
Sio mbali kuwa shetani katika Aya hii ni kinaya cha viongozi wapotevu wanaopoteza.
Na wale wanyonge watawaambia wale waliojifanya wakubwa: Bali ni vitimbi vyenu vya usiku na mchana, mlipokuwa mkituamrisha tumkufuru Mwenyezi Mungu na tumfanyie washirika.
Wafuasi na viongozi watakapokata tamaa ya kuokoka watatupiana lawama na kutuhumiana, kila kundi likijaribu kuwatupia makosa wengine; sawa na wezi wanapoafikiana kufanya uhalifu, lakini wanaposhikwa wanalaniana wao kwa wao.
Mwisho ushindi utakuwa ni wa wafuasi, kwa kuwakabili waliojifanya wakubwa kwa njama walizozifanya usiku na mchana na kuwadanga na ukafiri na ushirikina kwa njia mbalimbali.
Hata hivyo hilo halitawaondolea adhabu wala kuwapunguzia, maadamu walikuwa na akili na kulifanya hilo kwa hiyari yao: “Wa mwisho wao watawasema wa mwanzo wao: Mola wetu! Hawa ndio waliotupoteza basi uwape adhabu ya moto maradufu. Atasema: Itakuwa maradufu kwenu nyote, lakini hamjui.” Juz. 8 (7:38).
Nao wataficha majuto watakapoiona adhabu. Yaani wafuasi na waliofuatwa. Kila mwenye kuzembea na kupituka mipaka mwisho wake ni adhabu na majuto.
Na tutaweka minyororo shingoni mwa wale waliokufuru, viongozi na wafuasi wao.Kwani wanalipwa ila kwa waliyokuwa wakiyatenda? Kabisa! Mtu atalipwa kwa aliyoyafanya tu na Mola wako si mwenye kuwadhulumua waja.
وَمَا أَرْسَلْنَا فِي قَرْيَةٍ مِّن نَّذِيرٍ إِلَّا قَالَ مُتْرَفُوهَا إِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُم بِهِ كَافِرُونَ ﴿٣٤﴾
34. Na hatukumtuma mwonyaji yeyote kwenye mji ila walisema wapenda anasa wake: Hakika sisi tunayakataa hayo mliyotumwa nayo.
وَقَالُوا نَحْنُ أَكْثَرُ أَمْوَالًا وَأَوْلَادًا وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ ﴿٣٥﴾
35. Na wakasema: Sisi tuna mali nyingi zaidi na watoto, wala sisi hatutaadhibiwa.
قُلْ إِنَّ رَبِّي يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٦﴾
36. Sema: Hakika Mola wangu humkunjulia riziki amtakaye na huikunja, lakini watu wengi hawajui.
وَمَا أَمْوَالُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُم بِالَّتِي تُقَرِّبُكُمْ عِندَنَا زُلْفَىٰ إِلَّا مَنْ آمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ لَهُمْ جَزَاءُ الضِّعْفِ بِمَا عَمِلُوا وَهُمْ فِي الْغُرُفَاتِ آمِنُونَ ﴿٣٧﴾
37. Na si mali yenu wala watoto wenu watakaowajongeza kwetu muwe karibu, isipokuwa aliyeamini na akatenda mema. Hao basi watapata malipo maradufu, kwa waliyoyafanya nao watakuwa salama katika maghorofa.
وَالَّذِينَ يَسْعَوْنَ فِي آيَاتِنَا مُعَاجِزِينَ أُولَـٰئِكَ فِي الْعَذَابِ مُحْضَرُونَ ﴿٣٨﴾
38. Na wale ambao wanajitahidi kuzipinga ishara zetu, wakaona watashinda, hao watahudhurishwa kwenye adhabu.
قُلْ إِنَّ رَبِّي يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ لَهُ وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿٣٩﴾
39. Sema: Hakika Mola wangu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake na humkunjia. Na chochote mtakachotoa Yeye atakilipa. Naye ni Mbora wa wanaoruzuku.
وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ يَقُولُ لِلْمَلَائِكَةِ أَهَـٰؤُلَاءِ إِيَّاكُمْ كَانُوا يَعْبُدُونَ ﴿٤٠﴾
40. Na siku atakayowakusanya wote, kisha atawaambia Malaika: Je, hawa walikuwa wakiwaabudu?
قَالُوا سُبْحَانَكَ أَنتَ وَلِيُّنَا مِن دُونِهِم بَلْ كَانُوا يَعْبُدُونَ الْجِنَّ أَكْثَرُهُم بِهِم مُّؤْمِنُونَ ﴿٤١﴾
41. Watasema: Umetakasika! Wewe ndiye walii wetu sio hao. Bali walikuwa wakiwaabudu majini; wengi wao wakiwaamini hao.
فَالْيَوْمَ لَا يَمْلِكُ بَعْضُكُمْ لِبَعْضٍ نَّفْعًا وَلَا ضَرًّا وَنَقُولُ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا ذُوقُوا عَذَابَ النَّارِ الَّتِي كُنتُم بِهَا تُكَذِّبُونَ ﴿٤٢﴾
42. Na leo hii hawataweza baadhi yenu kuwaletea nafuu wengine wala kuwadhuru. Na tutawaambia wale ambao wamedhulumu: Onjeni adhabu ya Moto mliokuwa mkiukadhibisha.
Aya 34 – 42
Na hatukumtuma mwonyaji yeyote kwenye mji ila walisema wapenda anasa wake: Hakika sisi tunayakataa hayo mliyotumwa nayo. Na wakasema: Sisi tuna mali nyingi zaidi na watoto, wala sisi hatutaadhibiwa.
Hii ndio fikra ya wapenda anasa na hii ndio lugha yao. Mali ndio ya kwanza na ya mwisho; ndiyo bwana na wao ni watumwa.
Wanabeba bendera ya shari na uchokozi kwa watu kwa ajili ya mali, wanatawala masoko na vyakula, wanaanzisha vita moto na vita baridi, wanatafuta kila namna ya kutawala maisha na kila kitu wanakifungamanisha na chumo lao na faidia yao.
Kwao elimu sio chochote ila ikiwa inazidisha utajiri wao, dini ni ugaidi ila ikiwa inalinda masilahi yao, na amani ni wao wapore na wanayang’anye bila ya ya kuulizwa au kukemewa. Tazama Juz. 15: (17:16,90).
Sema: Hakika Mola wangu humkunjulia riziki amtakaye na huikunja, lakini watu wengi hawajui.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:26) kifungu cha ‘riziki na mtu.
Na si mali yenu wala watoto wenu watakaowajongeza kwetu muwe karibu, isipokuwa aliyeamini na akatenda mema. Hao basi watapata malipo maradufu, kwa waliyoyafanya nao watakuwa salama katika maghorofa.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) hapimi kheri na fadhila kwa mali na watoto, wala kwa vyeo na nasaba; bali ni kwa imani na matendo mema. Ni kwa mawili haya ndio mja anakuwa ni mwenye kuridhiwa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa thawabu zake na fadhila zake.
Imam Ali(a.s) anasema:“Heri sio kuwa nyingi mali yako na watoto, lakini heri ni kuwa nyingi elimu yako na kuwa na ustahamilivu mkubwa, na ushindane na watu kwa kumwabudu Mola wako. Ukifanya vizuri msifu Mwenyezi Mungu na ukifanya uovu muombe msamaha Mwenyezi Mungu; wala hakuna heri isipokuwa kwa watu wawili: Mtu aliyefanya dhambi akaiunganisha na toba, na mtu anayeharakisha kheri.”
Na wale ambao wanajitahidi kuzipinga ishara zetu, wakaona watashinda, hao watahudhurishwa kwenye adhabu.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (22:51).
Sema: Hakika Mola wangu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake na humkunjia.
Unaweza kuuliza : Kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekariri Aya hii, pamoja na kujua kuwa kuna mtengano wa Aya mbili tu?
Wafasiri wamejibu kwamba Aya ya kwanza inahusika na makafiri na ya pili ni ya waumini. Razi anasema: “Dalili ya hilo ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Aya ya pili amesema katika ‘waja wake’ na ya kwanza amesema ‘waja’ tu, na mja anayetegemezwa kwake Mwenyezi Mungu anakusudiwa muumini.”
Sio mbali kuwa makusudio ya kukaririka ni mawaidha na kuhimiza kutoa ambako Mwenyezi Mungu amekuashiria kwa kusema:
Na chochote mtakachotoa Yeye atakilipa. Naye ni Mbora wa wanaoruzuku.
Kuna Hadith ya Mtume mtukufu(s.a.w. w ) , amesema:“Kila usiku kuna mnadi anayenadi kwa kusema: “Ewe Mola wangu! Mlipe kila mtoaji. Na mnadi mwingine ananadi: Ewe Mola angu! Mlipe kila mzuiaji kuangamia.” kwenye Nahjul-Balagha imeelezwa:“Iteremsheni riziki kwa sadaka.”
Na siku atakayowakusanya wote, kisha atawaambia Malaika: Je, hawa walikuwa wakiwaabudu?
Makusudio ya kuelekeza swali hili kwa Malaika ni kuwatahayariza washirikina. Aya inafahamisha kuwa baadhi ya waarabu walikuwa wakiwaabudu malaika. Hayo yanaashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Je, Mola wenu amewachagulia watoto wa kiume na yeye akajichukulia watoto wa kike katika Malaika?” Juz. 15 (17:40).
Mwenye kumnasibishia Mwenyezi Mungu mwana basi amemfanya Mungu kuwa na mfano na mshirika katika uungu wake.
Watasema: Umetakasika! Wewe ndiye walii wetu sio hao.
Wewe ndiye bwana wetu na wao ni maadui zetu nasi tunajitenga nao.
Bali walikuwa wakiwaabudu majini; wengi wao wakiwaamini hao.
Kundi la wafasiri wamesema kuwa makusudio ya jini hapa ni mashetani na kwamba wao wanawapambia washirikina wawaabudu malaika na wengineo badala ya Mwenyezi Mungu.
Wengine wakasema kuwa ibada ya majini ilikuwa maarufu kwa waarabu; kwa hiyo maana ya Aya yatabaki kwenye dhahiri yake, wala hakuna haja ya kufanya taawili.
Iwe ni majini ndio waliokuwa wakiabudiwa au wengineo kwa kudanganywa na shetani, bado makusudio ya kwanza ya Aya ni kukanusha kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kwamba hakuna uombezi kwake ila kwa idhini yake. Vile vile hakuna kimbilio isipokuwa kwake yeye tu.
Ndio maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akafuatishia na kauli yake:
Na leo hii hawataweza baadhi yenu kuwaletea nafuu wengine wala kuwadhuru.
Si malaika, watu wala majini wanaoweza wao wenyewe kujikinga, sikwambii tena kuwasaidia wengine. Yeye peke yake ndiye mwenye ufalme na sifa njema, naye ni muweza wa kila kitu.
Na tutawaambia wale ambao wamedhulumu: Onjeni adhabu ya Moto mliokuwa mkiukadhibisha.
Walisema kuwa hakuna Pepo wala Moto, wala hatutauamini mpaka tutakapouona waziwazi. Basi ndio Mwenyezi Mungu akawachoma kuitikia matakwa yao.
Aya hii imenikumbusha wanaosema kuwa hakuna elimu wala maarifa ila kwa njia ya kushuhudia au majaribio; hata katika visivyoonekana na kuhisiwa.