7%

14

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA

إِنَّ أَصْحَابَ الْجَنَّةِ الْيَوْمَ فِي شُغُلٍ فَاكِهُونَ ﴿٥٥﴾

55. Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi.

هُمْ وَأَزْوَاجُهُمْ فِي ظِلَالٍ عَلَى الْأَرَائِكِ مُتَّكِئُونَ ﴿٥٦﴾

56. Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fahari.

لَهُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ وَلَهُم مَّا يَدَّعُونَ ﴿٥٧﴾

57. Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakachokitaka.

سَلَامٌ قَوْلًا مِّن رَّبٍّ رَّحِيمٍ ﴿٥٨﴾

58. Salaam! Ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mwenye kurehemu.

وَامْتَازُوا الْيَوْمَ أَيُّهَا الْمُجْرِمُونَ ﴿٥٩﴾

59. Na jitengeni leo enyi wakosefu.

أَلَمْ أَعْهَدْ إِلَيْكُمْ يَا بَنِي آدَمَ أَن لَّا تَعْبُدُوا الشَّيْطَانَ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿٦٠﴾

60. Je, sikuagana nanyi, enyi wanadamu, kuwa msimuabudu Shet’ani? Hakika yeye ni adui dhahiri kwenu.

وَأَنِ اعْبُدُونِي هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ ﴿٦١﴾

61. Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia iliyonyooka.

وَلَقَدْ أَضَلَّ مِنكُمْ جِبِلًّا كَثِيرًا أَفَلَمْ تَكُونُوا تَعْقِلُونَ ﴿٦٢﴾

62. Na hakika yeye amewapoteza viumbe wengi miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkim- tia akili?

هَـٰذِهِ جَهَنَّمُ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ ﴿٦٣﴾

63. Hii ndiyo Jahannamu mliyokuwa mkiahidiwa.

اصْلَوْهَا الْيَوْمَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ ﴿٦٤﴾

64. Ingieni leo kwa vile mlivyokuwa mkikufuru.

الْيَوْمَ نَخْتِمُ عَلَىٰ أَفْوَاهِهِمْ وَتُكَلِّمُنَا أَيْدِيهِمْ وَتَشْهَدُ أَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٦٥﴾

65. Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyokuwa wakiyachuma.

وَلَوْ نَشَاءُ لَطَمَسْنَا عَلَىٰ أَعْيُنِهِمْ فَاسْتَبَقُوا الصِّرَاطَ فَأَنَّىٰ يُبْصِرُونَ ﴿٦٦﴾

66. Na lau tungelipenda tungeliyafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wangeionaje?

وَلَوْ نَشَاءُ لَمَسَخْنَاهُمْ عَلَىٰ مَكَانَتِهِمْ فَمَا اسْتَطَاعُوا مُضِيًّا وَلَا يَرْجِعُونَ ﴿٦٧﴾

67. Na lau tungelitaka tungewageuza hapo hapo walipo, basi wasingeweza kwenda wala kurudi.

وَمَن نُّعَمِّرْهُ نُنَكِّسْهُ فِي الْخَلْقِ أَفَلَا يَعْقِلُونَ ﴿٦٨﴾

68. Na tunayempa umri tunampindua katika umbo. Basi je! hawatii akilini?

WATU WA PEPONI NA WATU WA MOTONI

Aya 55 – 68

MAANA

Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi. Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fahari. Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakachokitaka.

Anachotamani mtu zaidi ni siha, amani, utulivu wa moyo kutokana na tabu na mihangaiko na kupata kuburudika na chakula na kinywaji, maskani, mavazi, kustarehe na wanawake na kuwa na bustani yenye miti na mito. Haya yote yanapatikana Peponi.

Zaidi ya hayo ni Salaam! Ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mwenye kurehemu.

Salaam ya Mwenyezi Mungu ni amani na rehema. Na radhi yake ndio ukomo wa wema na neema. Ndio maana Imam Ali(a.s ) akasema:“Kila neema isiyokuwa Pepo ni upuzi na kila balaa isiyokuwa moto ni faraja.”

Na jitengeni leo enyi wakosefu.

Wakosefu walikuwa duniani wakijionyesha ni watu wema, wakivaa nguo za utawa na kuchanganyika na watu wa takua na wa heri. Hali halisi haikuwa ikijulikana na watu wengi. Ama leo – siku ya hukumu na malipo, Mwenyezi Mungu atawaweka mbali na watu wema na kuwaambia, ingieni motoni pamoja na watakaoingia:

يُعْرَفُ الْمُجْرِمُونَ بِسِيمَاهُمْ فَيُؤْخَذُ بِالنَّوَاصِي وَالْأَقْدَامِ ﴿٤١﴾

“Watajulikana wakosefu kwa alama zao, basi watashikwa kwa nywele za utosi na kwa miguu” (55:41).

Je, sikuagana nanyi, enyi wanadamu, kuwa msimuabudu Shet’ani? Hakika yeye ni adui dhahiri kwenu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwahadharisha waja kutokana na shetani na wasiwasi wake na akwakataza wasimtii; akawaongoza kwenye njia ya heri na uongofu. Lakini wengi wamemtii Shetani na kumuasi Mwingi wa rehe- ma. Hili ameliashiria kwa kusema:

Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia iliyonyooka.

Na hakika yeye amewapoteza viumbe wengi miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkitia akili?

Kila mwenye kufuata njia ya walioangamia baada ya kuhadharishwa na kuonywa, basi huyo ni katika vipofu wa nuru ya akili na muongozo wake. Wala hakuna malipo ya mfano huu isipokuwa adhabu ambayo amaeiashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kusema:

Hii ndiyo Jahannamu mliyokuwa mkiahidiwa, kupitia midomoni mwa mitume; mkaidharau na mkawadharau. BasiIngieni leo kwa vile mlivyokuwa mkikufuru, na huu ndio mwisho wa kila mpotevu na aliyepituka mipaka.

Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyokuwa wakiyachuma.

Kila kiungo cha muasi kesho kitatamka kumtolea ushahidi mtu wake yale maovu aliyoyafanya. Mkono utatoa ushahidi kwa ulivyopiga, kuiba, kuandika na kuashiria. Mguu kwa ulivyohangaika. Jicho kwa lililoona n.k.Unaweza kuuliza : Utachanganya vipi kauli hii ‘Tutaziba vinywa vyao’ na ile isemayo:

يَوْمَ تَشْهَدُ عَلَيْهِمْ أَلْسِنَتُهُمْ ﴿٢٤﴾

“Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao” Juz. 18 (24:24).

Ambapo ya kwanza imekanusha kutamka na hii ikathibitisha.

Jibu : Kesho waja watakuwa wana hali tofauti, wengine wataruhisiwa kuzungumza na wengine hawataruhusiwa:

يَوْمَ يَأْتِ لَا تَكَلَّمُ نَفْسٌ إِلَّا بِإِذْنِهِ ﴿١٠٥﴾

“Siku itakapofika, nafsi yoyote haitasema ila kwa idhini yake.” Juz. 13 (11:105).

Na lau tungelipenda tungeliyafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wangeionaje? Na lau tungelitaka tungewageuza hapo hapo walipo, basi wasingeweza kwenda wala kurudi.

Makusudio ya kufutilia mbali macho yao ni kuwa kipofu. Maana ni lau Mwenyezi Mungu angelitaka kuwaadhibu wakosefu dunianai angeliwapofusha macho yao na wasingeweza kuongoka na angeliwageuza wakawa wameganda bila ya kuwa na harakati wala uhai.

Na tunayempa umri tunampindua katika umbo. Basi je! hawatii akilini?

Kupindua kitu ni kukifanya juu chini. Binadamu kila anavyoendelea kuwa na umri mrefu anarudi nyuma: anakuwa mdhaifu baada ya kuwa na nguvu.

Lengo la ubainifu huu ni kuashiria kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amempa maisha ya kutosha ili aongoke na afanye mambo mema. Na lau angelipewa umri zaidi ya kawaida, basi maradhi yangelimweka chini, na umri mrefu ungelikuwa ni balaa na shari:

أَوَلَمْ نُعَمِّرْكُم مَّا يَتَذَكَّرُ فِيهِ مَن تَذَكَّرَ وَجَاءَكُمُ النَّذِيرُ فَذُوقُوا فَمَا لِلظَّالِمِينَ مِن نَّصِيرٍ ﴿٣٧﴾

“Je, hatukuwapa umri wa kutosha kukumbuka mwenye kukumbuka, na akawajia mwonyaji? Basi onjeni Na madhalimu hawana wa kuwanusuru” Juz. 22 (35:37).

وَمَا عَلَّمْنَاهُ الشِّعْرَ وَمَا يَنبَغِي لَهُ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ وَقُرْآنٌ مُّبِينٌ ﴿٦٩﴾

69. Wala hatukumfundisha mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur’an inayobainisha.

لِّيُنذِرَ مَن كَانَ حَيًّا وَيَحِقَّ الْقَوْلُ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴿٧٠﴾

Ili imwonye aliye hai, na ihakikike kauli juu ya makafiri.

HATUKUMFUNDISHA MASHAIRI

Aya 69 – 70

MAANA

Maadui wa Mwenyezi Mungu walijaribu kwa nyenzo zote kumkadhibisha Muhammad(s.a.w. w ) . Miongoni mwazo ni kauli yao kuwa ni mwenda wazimu, lakini mmoja wao, Walid bin Al-Mughira, aliyekufa akiwa kafiri, akasema: “Hapana, hakika kauli yake – yaani Qur’an – ina utamu na ina mvuto na kwamba juu yake kuna matunda na chini yake kumejaa. Hakika iko juu na haishindwi” Basi wakabadilisha kumtusi na wazimu na kusema: “Huyu ni mchawi muongo” (38:4.) Ilipowabainikia kuwa wao ndio waongo wakasema ni kuhani anakosea na anapatia au ni malenga mwenye kutunga mashairi kwa mawazo.

Ilivyo hasa ni kuwa kutuhumu kwao kuwa Mtume(s.a.w. w ) ni mshairi kunafahamisha kwamba mashairi kwa waarabu si lazima yawe na vina na uzani, bali yana upana zaidi. Ni fani iliyo na uzuri wake; iwe na uzani au la. Hali ni hiyo hiyo hata kwa wanafalsafa wa kale.

Mwenye Tafsir Ruhul-bayani amesema: “Mashairi ya watu wa kale hayakuwa na uzani wala vina wala hivyo sio nguzo ya ushairi.” Fikra hii imeenea leo kwenye somo la fasihi na uchambuzi.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewarudi wanaomtuhumu Mtume Mtukufu kuwa ni mshairi au kuhani kwenye Aya nyingi; miongoni mwazo ni:

إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ﴿٤٠﴾ وَمَا هُوَ بِقَوْلِ شَاعِرٍ قَلِيلًا مَّا تُؤْمِنُونَ ﴿٤١﴾ وَلَا بِقَوْلِ كَاهِنٍ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ ﴿٤٢﴾

“Kwa hakika hiyo ni kauli ya Mtume mwenye heshima. Wala si kauli ya mshairi. Ni machache mnayoamini, wala si kauli ya kuhani. Ni machache mnayokumbuka. (69:40 – 42).

فَذَكِّرْ فَمَا أَنتَ بِنِعْمَتِ رَبِّكَ بِكَاهِنٍ وَلَا مَجْنُونٍ ﴿٢٩﴾ أَمْ يَقُولُونَ شَاعِرٌ ﴿٣٠﴾

Na wewe kwa neema ya Mola wako si kuhani wala mwendawazimu. Au wanasema ni mshairi (52:29 – 30).

Na wakisema:

وَيَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَّجْنُونٍ ﴿٣٦﴾

“Hivi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mshairi mwendawazimu?” (37:36).

“Bali huyo ni mshairi.” Juz. 17 (21:5). Aya hizi tulizo nazo:

Wala hatukumfundisha mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur’an inayobainisha. Ili imwonye aliye hai, na ihakikike kauli juu ya makafiri.

Makusudio ya aliye hai hapa, ni yule ambaye akili yake iko hai kiuzingatiaji, kutaamali na kufungua moyo wake kwa haki na kheri. Na makusudio ya kauli hapa ni adhabu; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَلَـٰكِنْ حَقَّتْ كَلِمَةُ الْعَذَابِ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴿٧١﴾

“Lakini limekwishahakika neno la adhabu juu ya makafiri.” (39:71).

Washirikina walisema kuwa Qur’an aliyokuja nayo Muhammad si chochote ila ni mashairi yanayoelezea fikra yake na mawazo yake; na wala sio wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawarudi, kwa kuwaambia, kuwa shairi linajikita zaidi kwenye fikra hawa na mapendeleo ya mshairi; anamtetea anayempenda hata kama hana haki na anapamabana na anayemchukia hata kama ana haki. Na Qur’an ni kauli yenye hadhi na ya upambanuzi, na wala si kauli ya hawa na mzaha.

Ni Kitabu cha itikadi na sharia, maadili na mawaidha, ndani yake mna ilimu na fikra. Sasa wapi na wapi ushairi na hayo.

Kama ingelikuwa Qur’an imetengenezwa na Muhammad(s.a.w.w) , angeliweka humo machungu yake na huzuni yake, maisha yake na maazimio; sawa na walivyo malenga.

Kilichobakia ni kudokeza kuwa; hata hivyo Mtume(s.a.w.w) alikuwa akithamini na akiheshimu ushairi, kama fani iliyo na athari nzuri katika kuelezea mapendeleo na matakwa ya watu na amani yao.

Kuna kauli mshuhuri aliyoisema: “Katika baadhi ya ubainifu kuna uchwi na katika baadhi ya mshairi kuna hekima.” Alikuwa akiwaombea tawfiki malenga wanaoipigania haki na watu wa haki.

Aliwahi kumvulia kashida yake Ka’ab bin Zuheir kwa kumtuza, pale alipomsifu kwa kaswida yake iliyo maarufu kwa jina la Burda (kashida); miongoni mwa beti zake ni:

Haki ni nuru rasuli, kwaye twaangaziwa, Upanga wenye makali, wa Mola umechomozwa.

Tazama Juz. 22 (36:4) kifungu cha ‘Mdundo wa ndani katika Qur’an’ na Juz. 19 (26:224).