18
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA
إِنَّهُمْ أَلْفَوْا آبَاءَهُمْ ضَالِّينَ ﴿٦٩﴾
69. Hakika waliwakuta baba zao wamepotea.
فَهُمْ عَلَىٰ آثَارِهِمْ يُهْرَعُونَ ﴿٧٠﴾
70. Na wao wakafanya haraka kufuata nyayo zao.
وَلَقَدْ ضَلَّ قَبْلَهُمْ أَكْثَرُ الْأَوَّلِينَ ﴿٧١﴾
71. Na hakika walikwishapotea kabla yao wengi wa watu wa zamani.
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا فِيهِم مُّنذِرِينَ ﴿٧٢﴾
72. Na hakika tuliwapelekea waonyaji.
فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُنذَرِينَ ﴿٧٣﴾
73. Basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale walioonywa.
إِلَّا عِبَادَ اللَّـهِ الْمُخْلَصِينَ ﴿٧٤﴾
74. Isipokuwa waja wa Mwenyezi Mungu waliosafishwa.
وَلَقَدْ نَادَانَا نُوحٌ فَلَنِعْمَ الْمُجِيبُونَ ﴿٧٥﴾
75. Na hakika Nuh alituita, na Sisi ni bora wa waitikiaji.
وَنَجَّيْنَاهُ وَأَهْلَهُ مِنَ الْكَرْبِ الْعَظِيمِ ﴿٧٦﴾
76. Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa.
وَجَعَلْنَا ذُرِّيَّتَهُ هُمُ الْبَاقِينَ ﴿٧٧﴾
77. Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia.
وَتَرَكْنَا عَلَيْهِ فِي الْآخِرِينَ ﴿٧٨﴾
78. Na tukamwachia kwa walio baadaye.
سَلَامٌ عَلَىٰ نُوحٍ فِي الْعَالَمِينَ ﴿٧٩﴾
79. Amani kwa Nuh ulimwenguni kote!
إِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿٨٠﴾
80. Kwa hakika hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.
إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُؤْمِنِينَ ﴿٨١﴾
81. Hakika yeye ni katika waja wetu walio waumini.
ثُمَّ أَغْرَقْنَا الْآخَرِينَ ﴿٨٢﴾
82. Kisha tukawagharikisha wale wengine.
WALIPOTEA KABLA YAO WATU WENGI WA ZAMANI
Aya 69 – 82
Hakika waliwakuta baba zao wamepotea. Na wao wakafanya haraka kufuata nyayo zao.
Wanazungumziwa washirikina wa kiarabu waliofuata nyayo za mababu zao bila ya kufanya utafiti wowote au mazingatio. Aya inaashiria kwamba mpotevu na mpotezaji wako sawa katika maasi na kustahili adhabu. Ama yule anayefuata uongofu na utengenevu anakuwa katika amani na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Hilo linafahamishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Husema: Bali tuta- fuata yale tuliyowakuta nayo baba zetu. Je, hata kama baba zao walikuwa hawafahamu chochote wala hawakuongoka?” Juz. 2 (2:170). Maana yake ni kuwa, lau baba zao wangelikuwa kwenye uongofu, ingelifaa kuwafuata. Kwa maelezo zaidi tazama Juz.2 (2:168 – 170) kifungu cha ‘Kufuata na misingi ya itikadi.’
Na hakika walikwishapotea kabla yao wengi wa watu wa zamani. Na hakika tuliwapelekea waonyaji.
Ikiwa watakukadhibisha ewe Muhammad na kupotea na haki, basi walikwishapotea kabla yao wengi katika umma, ingawaje Mwenyezi Mungu aliwapeleka mitume na wabashiri; wakawatimizia hoja na kuwabainishia mapenzi yake na machukivu yake, wakaacha hayo wakafuata yale. Basi likastahili kwao neno la adhabu.Basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale walioonywa walivyohizika na kubomolewa;isipokuwa waja wa Mwenyezi Mungu waliosafishwa, amewaokoa Mwenyezi Mungu (s.w.t) na adhabu yake na akawalipa ujira wake na thawabu zake.
Na hakika Nuh alituita, na Sisi ni bora wa waitikiaji.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaashiria yale yaliyoelezwa kwenye Aya nyingine: “Na akasema Nuh: Mola wangu! Usiache Katika ardhi mkazi yeyote katika makafiri” (71:26).
Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa.
Mwenyezi Mungu alimnusuru Nuh na watu wake kutokana na mataghuti. Akawangamiza wote bila ya kubakia, kwa kuitikia maombi ya Nabii wake Nuh. Kwa hiyo akamuokoa yeye na walikouwa pamoja naye na udhia wa ukafiri muovu na kumuhifadhi na msiba na majanga.
Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia, peke yao baada ya tufani.
Katika Tafsir Tabariy imesemwa: “Dhuria wa Nuh ndio waliobakia katika ardhi baada ya kuangamia kaumu yake. Na watu wote baada yake, mpaka leo, ni wa kizazi cha Nuh.
Waajemi na waarabu wanatokana na watoto wa Sam bin Nuh,Waturuki na Waslovenia ni watoto wa Yafith na weusi ni watoto wa Ham. Ulama na mapokezi yameeleza hivyo.”
Tabari alifariki mwaka 310 (A.H.), yaani zaidi ya miaka elfu moja iliyopita. Waliomtangulia na waliokuja baada yake walimbandika jina la sheikh wa wafasiri.
Katika Kamusi ya Kitabu kitakatifu imeandikwa: “Sam ni jina la kiebrania likiwa na maana ya isimu (jina). Yeye ndiye mtoto mkubwa wa Nuh. Kizazi chake ni waarabu, Waarmenia, waashwar na wayahudi. Ndio maana lugha zao wote hao zinatiwa Saamiya, kwa kunasibishwa naye; mfano: lugha ya kiarabu na kiebrania…Yafith huenda maana yake ni uzuri… kizazi chake ni wakazi wa kuanzia magharibi mwa Najad, kusini mwa Bahari ya Kazwin (Caspian sea) na Bahari nyeusi (Black sea) hadi fukwe na visiwa vya Bahri ya kati (Mediterranean Sea) katika asili ya wahindi wa Ulaya–katika hawa wanaingia waturuki na waslovania aliowaashiria Tabariy-Na ham ni jina la kiebrania yaani mwenye kuchemka naye ni mdogo wa watoto wa Nuh”
Na tukamwachia kwa walio baadaye.
Yaani tukamwachia utajo wa sifa katika uhai wake
Amani kwa Nuh ulimwenguni kote!
Yeye yuko kwenye amani ya Mungu kwa kutotajwa na mabaya. Mitume walikuwa wakimwomba Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwa na utajo mzuri kwa watu wakiondoka. Ibrahim(a.s ) alisema:
وَاجْعَل لِّي لِسَانَ صِدْقٍ فِي الْآخِرِينَ ﴿٨٤﴾
“Na unijaalie kutajwa kwa wema na wengine” Juz. 19 (26:84).
Kwa hakika hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.
Yaani atawafanyia wema Mwenyezi Mungu kwa vile hapotezi amali ya yeyote mwenye kutenda, awe mume au mke.
Hakika yeye ni katika waja wetu walio waumini.
Kwa sababu alifanya wema katika matendo yake, akapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa jihadi yake ya haki. Hii ndio nembo na dalili ya mumin.
Kisha tukawagharikisha wale wengine duniani na akhera watakuwa na adhabu chungu kwa yale waliyokuwa wakiyafanya.
وَإِنَّ مِن شِيعَتِهِ لَإِبْرَاهِيمَ ﴿٨٣﴾
83. Na hakika Ibrahim alikuwa katika kundi lake.
إِذْ جَاءَ رَبَّهُ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٤﴾
84. Alipomjia Mola wake kwa moyo ulio salama.
إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَاذَا تَعْبُدُونَ ﴿٨٥﴾
85. Alipomwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini?
أَئِفْكًا آلِهَةً دُونَ اللَّـهِ تُرِيدُونَ ﴿٨٦﴾
86. Je, kwa kuzua tu mnataka miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu?
فَمَا ظَنُّكُم بِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٨٧﴾
87. Mnamdhania nini Mola wa walimwengu wote?
فَنَظَرَ نَظْرَةً فِي النُّجُومِ ﴿٨٨﴾
88. Kisha akapiga jicho kutazama nyota.
فَقَالَ إِنِّي سَقِيمٌ ﴿٨٩﴾
89. Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa!
فَتَوَلَّوْا عَنْهُ مُدْبِرِينَ ﴿٩٠﴾
90. Nao wakamuacha, wakampa kisogo.
فَرَاغَ إِلَىٰ آلِهَتِهِمْ فَقَالَ أَلَا تَأْكُلُونَ ﴿٩١﴾
91. Basi akaiendea miungu yao kwa siri.
مَا لَكُمْ لَا تَنطِقُونَ ﴿٩٢﴾
92. Akaiambia: Mbona hamli? Mna nini hata hamsemi?
فَرَاغَ عَلَيْهِمْ ضَرْبًا بِالْيَمِينِ ﴿٩٣﴾
93. Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kuume.
فَأَقْبَلُوا إِلَيْهِ يَزِفُّونَ ﴿٩٤﴾
94. Basi wakamjia upesi upesi.
قَالَ أَتَعْبُدُونَ مَا تَنْحِتُونَ ﴿٩٥﴾
95. Akasema: Je, mnaviabudu vitu mnavyovichonga?
وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ ﴿٩٦﴾
96. Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaumba nyinyi na mnavyovifanya!
قَالُوا ابْنُوا لَهُ بُنْيَانًا فَأَلْقُوهُ فِي الْجَحِيمِ ﴿٩٧﴾
97. Wakasema: Mjengeeni jengo, kisha mtupeni motoni.
فَأَرَادُوا بِهِ كَيْدًا فَجَعَلْنَاهُمُ الْأَسْفَلِينَ ﴿٩٨﴾
98. Basi walitaka kumfanyia vitimbi, lakini tukawafanya wao ndio wa chini.
وَقَالَ إِنِّي ذَاهِبٌ إِلَىٰ رَبِّي سَيَهْدِينِ ﴿٩٩﴾
99. Na akasema: Hakika mimi nakwenda kwa Mola wangu atakayeniongoza.
Aya 83 – 99
Neno kundi limefasiriwa kutokana na neno la kiarabu shia’ lenye maana ya mfuasi anayefuta dini na njia ya yule anayemfuata. Kisha neno hili shia likazoeleka kuwa na maana ya mfuasi wa Imam Ali (a.s.) na yule aliyechukua nafasi yake katika watoto wake.
Na hakika Ibrahim alikuwa katika kundi lake.
Kundi lake, yaani kundi la Nuh. Maana ni kuwa Ibrahim alifuata njia ya Nuh kiitikadi na kimatendo. Mfasiri mmoja wa kale anasema kuwa baina ya Nuh na Ibrahim kulikuwa na miaka 2640. mwenye kauli hii hakutege- meza kwenye rejea za kutegemewa.
Alipomjia Mola wake kwa moyo ulio salama.
Mwenye moyo huu ni yule aliyemfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu peke yake katika kauli zake na vitendo vyake vyote. Kuna Hadith isemyo: “Imani ya mja haisimami sawa mpaka usimame sawa moyo wake.” Kwenye Nahjul-balgha kuna maneno haya: “Heri zote ni za moyo ulio salama uliomtii anayeuongoza na kujiepusha na anayeudekeza.”
Alipomwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini? Je, kwa kuzua tu mnataka miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu?
Ibrahim alipinga ibada ya masanamu kwa watu wake akawakabili na kauli ya haki kwa kusema kuwa mnataka uzushi na batili kwa kumrejea asiyekuwa Mwenyezi Mungu na kujikurubisha kwa ibada kwa asiyekuwa Yeye? Umetangulia mfano wake katika Juz.7 (6:74).
Mnamdhania nini Mola wa walimwengu wote?
Je, mnamdhania kuwa ni jiwe au nyota naye ameumba ulimwengu? Je, akili yenu haiamki hata kidogo au kuzinduka kutokana na ujinga huu?
Katika Juz. 13 (13:16), kifungu cha ‘akili za watu haziwatoshelezi,’ tumebinisha kwa nini washirikina waliabudu mawe yanayokojolewa na mambwa na vicheche?
Kisha akapiga jicho kutazama nyota, akiwapa dhana watu wake kuwa anatafuta muumba wa ulimwengu, kwa vile wao walikuwa wakiabudu miungu mingi; hasa Nanar, mungu wa mwezi na mkewe Nanjal; kama ilivyoelezwa katika Kamusi ya Kitabu kitakatifu.
Maana ya Aya hii yamekuja katika Juz. 7 (6:74-79).
Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa!
Wafasiri wana kauli nyingi kuhusu makusudio ya ugonjwa. Yenye nguvu zaidi ni ile inayosema kuwa makusudio ya ugonjwa hapa ni shaka. Na maana yanakuwa kwamba Ibrahim aliwaambia watu wake, mimi hivi sasa nimedangana natafuta ukweli na uhakika ili niweze kuongoka kuweza kumjua muumbaji.
Nimeangalia masanamu nikapata uhakika kuwa hayawezi kuwa miungu; kisha nikaangalia nyota na sikupata mwongozo wowote; nimebaki kwenye shaka na kudangana.
Mfumo wa Aya unasaidia maana haya au angalau unayapa nguvu, kwa sababu yanaunganisha baina ya kuangalia kwenye nyota na kuwa mgonjwa.
Wala kauli yake hii ya kusema ana shaka hatuwezi kusema kuwa ni uwongo, kwa sababu ni katika hali ya kwenda na mbishani ili kumchukua kwenye hoja na kumkatia nyudhuru zote.
Nao wakamwacha, wakampa kisogo.
Walimwacha na wakajiendea zao.
Basi akaiendea miungu yao kwa siri.
Alichukua fursa ya kuondoka kwao na kwenda haraka kwenye masanamu. Walikuwa wameyawekea chakula ili yakibariki, akaiambia:
Mbona hamli? Mna nini hata hamsemi?
Alisema hivi kwa kuibeza na kutoa hoja kwa anayeiabudu na kutabaruku nayo.
Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kuume.
Aliavunja masanamu vipande vipande kwa mkono wake wa kuume na kabakisha kubwa lao, angalau waweze kurejea.
Basi wakamjia upesi upesi.
Watu walikuja haraka kwa Ibrahim na kuanza kumuuliza: wewe ndiwe uliyeifanyia hivi miungu yetu?
Akasema: Je, mnaviabudu vitu mnavyo vichonga?
Yaani ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu uwongo. Hakika Mola ni Muumba sio muumbwa na Mwenye kuruzuku sio mwenye kuruzukiwa. Nyinyi mmeyatengeneza masanamu haya kwa mikono yenu na mnayalinda, vipi yatakuwa miungu?
Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaumba nyinyi na mnavyovifanya!
Yeye ndiye Muumba wa kila kitu na marejeo ni kwake.
Wakasema: Mjengeeni jengo, kisha mtupeni motoni.
Walishindwa kuikabili hoja kwa hoja, wakakimbila maguvu; kama ilivyo hali ya mataghuti, huwasha moto na kuwatupa humo wapigania haki na kheri; kama ilivyokuwa zamani. Na elimu ya uvunjaji ilipoondelea sasa wanautupa moto kwa wananchi wanyonge pamoja na wanawake na watoto wao.
Basi walitaka kumfanyia vitimbi, lakini tukawafanya wao ndio wa chini, pale alipoufanya moto ni baridi na salama kwa Ibrahim.
Na akasema: Hakika mimi nakwenda kwa Mola wangu ndiye atakayeniongoza.
Baada ya Mwenyezi Mungu kumwokoa Ibrahim na vitimbi vya watu wake, alihama kutoka mji wake wa Urulkaldaniyya (Chaldeans) – Babilon – kwenda Sham.
Katika Kamusi ya Kitabu kitakatifu imeandikwa: “Yaligunduliwa mabaki na michoro ya mika elfu mbili kabla ya miladi (B.C.).
Lilikutwa jina la Ibrahim kwa mfumo wa Abramu au Abrama. Ugunduzi wa historia wa sasa umedhihirisha hali ya mji wa Uru, aliouhama Ibrahim, kama ulivyokuwa wakati huo.”
Umetangulia mfano wake kwa ufafunizi kidogo kwenye Juz. 17 (21:51-60).