19
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI
وَمَن يَعْشُ عَن ذِكْرِ الرَّحْمَـٰنِ نُقَيِّضْ لَهُ شَيْطَانًا فَهُوَ لَهُ قَرِينٌ ﴿٣٦﴾
36. Anayeifanyia upofu dhikri ya Mwingi wa rehema tutamwekea Shetani kuwa ndiye rafiki yake.
وَإِنَّهُمْ لَيَصُدُّونَهُمْ عَنِ السَّبِيلِ وَيَحْسَبُونَ أَنَّهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٣٧﴾
37. Na hakika wao wanawazuilia njia na wenyewe wanadhani kuwa wameongoka.
حَتَّىٰ إِذَا جَاءَنَا قَالَ يَا لَيْتَ بَيْنِي وَبَيْنَكَ بُعْدَ الْمَشْرِقَيْنِ فَبِئْسَ الْقَرِينُ ﴿٣٨﴾
38. Hata atakapotujia atasema: Laiti ungelikuwako baina yangu na wewe umbali baina ya mashariki na magharibi. Ni urafiki mbaya ulioje?
وَلَن يَنفَعَكُمُ الْيَوْمَ إِذ ظَّلَمْتُمْ أَنَّكُمْ فِي الْعَذَابِ مُشْتَرِكُونَ ﴿٣٩﴾
39. Na kwa kuwa mlidhulumu, haitawafaa leo kwamba nyinyi mnashirikiana katika adhabu.
أَفَأَنتَ تُسْمِعُ الصُّمَّ أَوْ تَهْدِي الْعُمْيَ وَمَن كَانَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٤٠﴾
40. Je, unaweza kumsikilizisha kiziwi, au kumwongoza kipofu na aliyemo katika upotofu ulio wazi?
فَإِمَّا نَذْهَبَنَّ بِكَ فَإِنَّا مِنْهُم مُّنتَقِمُونَ ﴿٤١﴾
41. Na hata tukikuondoa, Sisi tutalipiza kisasi kwao.
أَوْ نُرِيَنَّكَ الَّذِي وَعَدْنَاهُمْ فَإِنَّا عَلَيْهِم مُّقْتَدِرُونَ ﴿٤٢﴾
42. Au tutakuonyesha tuliowaahidi. Nasi bila ya shaka tuna uweza juu yao.
فَاسْتَمْسِكْ بِالَّذِي أُوحِيَ إِلَيْكَ إِنَّكَ عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٤٣﴾
43. Basi yashike uliyopewa. Hakika wewe uko kwenye Njia iliyonyooka.
وَإِنَّهُ لَذِكْرٌ لَّكَ وَلِقَوْمِكَ وَسَوْفَ تُسْأَلُونَ ﴿٤٤﴾
44. Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakujaulizwa.
وَاسْأَلْ مَنْ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رُّسُلِنَا أَجَعَلْنَا مِن دُونِ الرَّحْمَـٰنِ آلِهَةً يُعْبَدُونَ ﴿٤٥﴾
45. Na waulize Mitume wetu tuliowatuma kabla yako: Je, tulifanya miungu mingine iabudiwe badala ya Mwingi wa rehma?.
Aya 36 – 45
Anayeifanyia upofu dhikri ya Mwingi wa rehema tutamwekea Shetani kuwa ndiye rafiki yake.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni mwadililifu na ni hakimu, hawezi kuwasilitia Shetani waja wake ili awadanganye kuwatia kwenye upotevu na uasi; kisha awaadhibu. Itakuwaje hivyo na hali Yeye ndiye aliyesema:
إِنَّ عِبَادِي لَيْسَ لَكَ عَلَيْهِمْ سُلْطَانٌ إِلَّا مَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْغَاوِينَ ﴿٤٢﴾
“Hakika waja wangu hutakuwa na mamlaka nao, ispokuwa wale wapotofu waliokufuata.”
Juz. 14 (15:42).
Akasema tena:
وَمَا رَبُّكَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴿٤٦﴾
“Na Mola wako si mwenye kuwadhulumu waja.” Juz. 24 (41:46).
Kwa hiyo basi maana ya Aya yatakuwa ni mwenye kuitupilia mbali dini ya Mwenyezi Mungu na sharia yake, akafuata matamanio na starehe, Mwenyezi Mungu atamwachia nafsi yake yenye kuamrisha mno uovu na mashetani watu na majini, wamfanye vile watakavyo na kumwongoza kwenye maangamizi. Mwenyezi Mungu hamkatazi mtu mambo maovu kwa nguvu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 24 (41:25).
Na hakika wao wanawazuilia Njia.
Yaani hao mashetani wanawazulia watu njia ya uwongofu.
Na wenyewe wanadhani kuwa wameongoka.
Mashetani wanawaongoza wafuasi wao kwenye upotevu na wafuasi wanadhani kuwa wako kwenye uwongofu kwa kuwafuata mashetani. Muovu zaidi katika watu ni yule anayefuata njia ya upotevu na mwenyewe anaitakidi kuwa yuko salama:
قُلْ هَلْ نُنَبِّئُكُم بِالْأَخْسَرِينَ أَعْمَالًا ﴿١٠٣﴾ الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا ﴿١٠٤﴾ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ وَلِقَائِهِ فَحَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فَلَا نُقِيمُ لَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَزْنًا ﴿١٠٥﴾
“Sema je, tuwaambie wale wenye hasara mno ya vitendo? Ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kuwa wanafanya kazi nzuri? Hao ndio ambao wamezikanusha ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye. Kwa hiyo vitendo vyao vimepomoka; na wala siku ya Kiyama hatutawapa uzito wowote.” Juz. 16 (18:103-105).
Hata atakapotujia atasema: Laiti ungelikuwako baina yangu na wewe umbali baina ya mashariki na magharibi. Ni urafiki mbaya ulioje?
Yaani kesho mfuasi atamwambia mfuaswa: afadhali ningekuwa mbali sana na wewe, kulikoni urafiki huu mbaya:
إِذْ تَبَرَّأَ الَّذِينَ اتُّبِعُوا مِنَ الَّذِينَ اتَّبَعُوا وَرَأَوُا الْعَذَابَ وَتَقَطَّعَتْ بِهِمُ الْأَسْبَابُ ﴿١٦٦﴾
“Pindi waliofuatwa watakapowakataa wale waliowafuata, na hali ya kuwa wamekwishaiona adhabu na kuwakatikia mafungamano.” Juz. 1 (2:166).
Na kwa kuwa mlidhulumu, haitawafaa leo kwamba nyinyi mnashirikiana katika adhabu.
Wanaambiwa wafuasi. Maana ni kuwa duniani mtu akipata adhabu na akamuona mwenzake naye anapata adhabu ile basi huwa anapoa kidogo (kifo cha wengi ni arusi), lakini sivyo kwa adhabu ya akhera; inakuwa sawa tu, iwe kwa wafuasi au wafuaswa-kushirikiana kwao hakuwezi kuwapun-guzia chochote wala kuwanufaisha.
Je! Unaweza kumsikilizisha kiziwi, au kumwongoza kipofu na aliyemo katika upotofu ulio wazi?
Starehe zimepiga muhuri kwenye macho yao, nyoyo zao na masikio yao, wataionaje haki na kusikia maneno yao? Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:42), Juz. 20 (27:80) na Juz. 21 (21:52).
Na hata tukikuondoa, Sisi tutalipiza kisasi kwao au tutakuonyesha tuliowaahidi. Nasi bila ya shaka tuna uweza juu yao.
Maneno yanaelekezwa kwa Mtume kuhusiana na washirikina. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hawaachi washirikina walivyo.
Ikiwa mtume atafariki kuelekea kwenye rehema ya Mola wake, kabla ya wao hawajasalimu amri, basi Mwenyezi Mungu atawaadhibu au ikiwa mtume yuko hai basi atampa ushindi juu yao na watanyenyekea amri yake watake wasitake.
Hiyo ilitokea hasa; pale mtume alipoiteka Makka na vigogo wake kusal- imu amri, baada ya kuwa wamemtoa huko kwa hofu na kujificha. Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:46), Juz. 13 (13:40) na Juz. 24 (24:77).
Basi yashike uliyopewa. Hakika wewe uko kwenye Njia iliyonyooka.
Shikamana na Qur’an ewe Muhammad, kwa sababu ni haki, na Mwenyezi Mungu yuko pamoja nawe kwa sababu uko kwenye njia yake iliyo ya sawa. Naye atakutoshea na wanaokufanyia istihzai na inadi.
Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako.
Yaani Qur’an ni heshima kwako na kwa waarabu, kwa sababu imewainua na ikaeneza utawala wao na lugha yao maghiribi mwa ardhi na mashariki yake; kama tulivyotaja katika Aya ya 4 kwenye Sura hii. Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (21:10).
Na mtakujaulizwa nyinyi waarabu jinsi mlivyoitumia Qur’an; na nyinyi hivi leo mnaipuuza sana; ndio maana mmekua chakula cha kila mwenye tamaa.
Na waulize Mitume wetu tuliowatuma kabla yako: Je! Tulifanya miungu mingine iabudiwe badala ya Mwingi wa rehma?
Waulize ewe Muhammad watu wa dini zilizotangulia na mitume kuwa je, wamewahi kumsikia Mtume yoyote aliyeruhusu ushirikina na kuhalisha kuabudiwa masanamu?
Ikiwa mitume wote walilingania Tawhid na kutupilia mbali ushirikina; kama alivyofanya Muhammad, basi kwanini mnanupiga vita mwito wake enyi washirikina?
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مُوسَىٰ بِآيَاتِنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ فَقَالَ إِنِّي رَسُولُ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٤٦﴾
46. Na hakika tulimtuma Musa kwa Ishara zetu aende kwa Firauni na waheshimiwa wake, na akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Mola wa walimwengu!
فَلَمَّا جَاءَهُم بِآيَاتِنَا إِذَا هُم مِّنْهَا يَضْحَكُونَ ﴿٤٧﴾
47. Lakini alipowajia na Ishara zetu wakaingia kuzicheka.
وَمَا نُرِيهِم مِّنْ آيَةٍ إِلَّا هِيَ أَكْبَرُ مِنْ أُخْتِهَا وَأَخَذْنَاهُم بِالْعَذَابِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٤٨﴾
48. Na hatukuwaonyesha Ishara yoyote ila hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko nyengineyo. Na tukawakamata kwa adhabu ili warejee.
وَقَالُوا يَا أَيُّهَ السَّاحِرُ ادْعُ لَنَا رَبَّكَ بِمَا عَهِدَ عِندَكَ إِنَّنَا لَمُهْتَدُونَ ﴿٤٩﴾
49. Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako kwa ile ahadi aliyokuahidi; hakika sisi tutakuwa wenye kuongoka.
فَلَمَّا كَشَفْنَا عَنْهُمُ الْعَذَابَ إِذَا هُمْ يَنكُثُونَ ﴿٥٠﴾
50. Basi tulipowaondolea adhabu hiyo, mara wakaingia kuvunja ahadi.
وَنَادَىٰ فِرْعَوْنُ فِي قَوْمِهِ قَالَ يَا قَوْمِ أَلَيْسَ لِي مُلْكُ مِصْرَ وَهَـٰذِهِ الْأَنْهَارُ تَجْرِي مِن تَحْتِي أَفَلَا تُبْصِرُونَ ﴿٥١﴾
51. Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi watu wangu! Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini yangu? Je, hamwoni?
أَمْ أَنَا خَيْرٌ مِّنْ هَـٰذَا الَّذِي هُوَ مَهِينٌ وَلَا يَكَادُ يُبِينُ ﴿٥٢﴾
52. Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala hawezi kusema waziwazi?
فَلَوْلَا أُلْقِيَ عَلَيْهِ أَسْوِرَةٌ مِّن ذَهَبٍ أَوْ جَاءَ مَعَهُ الْمَلَائِكَةُ مُقْتَرِنِينَ ﴿٥٣﴾
53. Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au hawakuja Malaika pamoja naye wakamwandama?
فَاسْتَخَفَّ قَوْمَهُ فَأَطَاعُوهُ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمًا فَاسِقِينَ ﴿٥٤﴾
54. Basi aliwachezea watu wake, na wakamtii. Kwa hakika hao walikuwa watu mafasiki.
فَلَمَّا آسَفُونَا انتَقَمْنَا مِنْهُمْ فَأَغْرَقْنَاهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٥٥﴾
55. Walipotukasirisha tuliwapatiliza tukawagharikisha wote.
فَجَعَلْنَاهُمْ سَلَفًا وَمَثَلًا لِّلْآخِرِينَ ﴿٥٦﴾
56. Kisha tukawafanya kuwa watangulizi na mfano kwa wa baadaye.
Aya 46 – 56
Na hakika tulimtuma Musa kwa Ishara zetu aende kwa Firauni na waheshimiwa wake, na akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Mola wa walimwengu wote! Lakini alipowajia na Ishara zetu wakaingia kuzicheka.
Hii ni mara ya kumi na sita kukaririka kisa cha Musa(a.s ) , mbali na zile Aya alizotajwa. Tumekwishazungumzia kisa hiki, mara nyingine kwa ufafanuzi zaidi na mara nyingine kwa ujumla.
Katika Juz. 16 (20:9) tumetaja sababu za kukaririka. Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa Mwenyezi Mungu mtukufu amekirudia kisa cha Musa hapa kwa sababu vigogo wa kikuraishi walimtia ila Muhammad(s.a.w. w ) , ndio akabainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwamba Yeye alimtuma Musa fukara kwa Firauni tajiri. Aya iliyotangulia inatilia nguvu hili.
Vyovyote iwavyo, maana ya Aya tuliyo nayo yako wazi. Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu alimtuma Musa kwa Firauni na watu wake na miujiza inayojulisha utume wake; kama vile fimbo na mkono mweupe, lakini wakamdharau yeye, mwito wake na miujiza yake.
Na hatukuwaonyesha Ishara yoyote ila hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko nyengineyo.
Makusudio ya ishara hapa ni adhabu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t):
فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمُ الطُّوفَانَ وَالْجَرَادَ وَالْقُمَّلَ وَالضَّفَادِعَ وَالدَّمَ آيَاتٍ مُّفَصَّلَاتٍ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا مُّجْرِمِينَ ﴿١٣٣﴾
“Basi tukawapelekea tufani na nzige na chawa na vyura na damu kuwa ishara mbalimbali, lakini wakatakabari na wakawa watu wakosefu.” Juz. 9 (7:133).
Na tukawakamata kwa adhabu ili warejee kutoka kwenye upotevu kwenda kwenye uongofu na kutoka kwenye ufisadi wa nchi hadi kwenye kuitengeneza, lakini ishara na maonyo hayakuwafuaa watu wasioona ispokuwa manufaa na chumo lao tu.
Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako kwa ile ahadi aliyokuahidi; hakika sisi tutakuwa wenye kuongoka.
Katika Aya hii Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasimulia kuwa watu wa Firauni walimwita Musa mchawi, na katika Juz.9 (7:134) walimwita kwa jina lake. Sio mbali kuwa kuna wakati walimwambia kwa jina lake na wakati mwingine walimwambia kwa kumwita mchawi. Hili ni jambo la kawaida katika mabishano ya watu.
Basi tulipowaondolea adhabu hiyo, mara wakaingia kuvunja ahadi.
Mwenyezi Mungu aliwakamata na adhabu kwa miaka, wakamtaka Musa awaombee kuondolewa adhabu na wakamwahidi kutubia, lakini waliivunja ahadi yao na wakaendelea na kufuru na upotevu baada ya kuondokewa na adhabu.
Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi watu wangu! Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini yangu? Je, hamwoni?
Chini yangu ni kinaya cha kuwa mito iko chini yake akiitumia vile atakavyo. Firauni anautolea dalili ukuu wake na cheo chake kwa mali na ardhi. Hii ndio hali iliyoenea kwa wengi kila wakati na kila mahali. Wenye mali hivi sasa ndio watawala kwenye nchi nyingi.
Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala hawezi kusema waziwazi?
Ni mnyonge eti kwa kuwa ni fukara na kutosema waziwazi ni kwa kuwa alikuwa ana kigugumizi, lakini Mwenyezi Mungu alikiondoa kwa dalili ya kauli yake Musa kumuomba Mola wake:
“Na ulifungue fundo lililo katika ulimi wangu.” Na Mwenyezi Mungu naye akamjibu: “Hakika umepewa maombi yako ewe Musa!” Juz.16 (20:27,36). Na Firauni alimwita Musa kwa alivyokuwa si kwa alivyo.
Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au hawakuja Malaika pamoja naye wakamwandama?
Yaani Malaika wawe wapambe wake; kama wanavyofanya viongozi kuwa na wapambe. Wafasiri wanasema kuwa ilikuwa ni desturi ya watu wa firauni wakimchagua kiongozi wao wanamvisha vikuku na mkufu wa dhahabu, kuwa ndio alama ya uongozi wake. Ndio maana Firauni akasema, atakuwaje Musa ni nabii na hali hana dhahabu mikononi mwake wala shingoni mwake. Lililompa ujasiri wa hilo ni ujinga wa watu wake, upotevu wao na udhaifu wa akili zao; kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t):
Basi aliwachezea watu wake, na wakamtii. Kwa hakika hao walikuwa watu mafasiki.
Mwaka uliopita nilimwita fundi wa umeme anirekebishie kwenye maktaba yangu. Basi alipoona vitabu vimetapakaa huku na huko, aliniambia: “Mke wangu ananichukia sana, nakuomba uniandikie dawa ya mapenzi.” Nikwambia mimi sijui fani hiyo. Akasema: “Kwa nini una vitabu vyote hivi?”
Walipotukasirisha kwa kumkadhibisha Mtume, kuvunja ahadi na kuendelea na ukafiri na upotevu,tuliwapatiliza tukawagharikisha wote, viongozi na wafuasi.
Kisha tukawafanya kuwa watangulizi wa motonina mfano kwa wa baadaye, wapate funzo na mawaidha wale watakaokuja baada yao.
Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَقَوْمَ نُوحٍ لَّمَّا كَذَّبُوا الرُّسُلَ أَغْرَقْنَاهُمْ وَجَعَلْنَاهُمْ لِلنَّاسِ آيَةً ﴿٣٧﴾
“Na watu wa Nuh walipowakadhibisha Mitume, tuliwagharikisha na tukawafanya ni ishara kwa watu: Juz. 19 (25:37).