7%

22

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ لَيَقُولُونَ ﴿٣٤﴾

34. Hakika hawa wanasema:

إِنْ هِيَ إِلَّا مَوْتَتُنَا الْأُولَىٰ وَمَا نَحْنُ بِمُنشَرِينَ ﴿٣٥﴾

35. Hapana ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi hatu- fufuliwi.

فَأْتُوا بِآبَائِنَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٣٦﴾

36. Basi warudisheni baba zetu, ikiwa mnasema kweli.

أَهُمْ خَيْرٌ أَمْ قَوْمُ تُبَّعٍ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ أَهْلَكْنَاهُمْ إِنَّهُمْ كَانُوا مُجْرِمِينَ ﴿٣٧﴾

37. Je, wao ni bora au watu wa Tubbaa’ na walio kuwa kabla yao? Tuliwaangamiza. Hakika hao walikuwa wakosefu.

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا لَاعِبِينَ ﴿٣٨﴾

38. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake kwa mchezo.

مَا خَلَقْنَاهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٩﴾

39. Hatukuviumba ila kwa haki. Lakini wengi wao hawajui.

إِنَّ يَوْمَ الْفَصْلِ مِيقَاتُهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٤٠﴾

40. Hakika siku ya Upambanuzi ni wakati uliowekwa kwa wao wote.

يَوْمَ لَا يُغْنِي مَوْلًى عَن مَّوْلًى شَيْئًا وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ ﴿٤١﴾

41. Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala hawatanusuriwa.

إِلَّا مَن رَّحِمَ اللَّـهُ إِنَّهُ هُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿٤٢﴾

42. Isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu atamrehemu Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

JE, WAO NI BORA AU WATU WA TUBBAA’

Aya 34 – 42

MAANA

Hakika hawa wanasema: Hapana ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi hatufufuliwi.

‘Hawa’ ni ishara ya washirikina wa Makka, walisema hakuna uhai wala ufufuo baada ya mauti na wakatoa hoja kwa kusema:Basi warudisheni baba zetu, ikiwa mnasema kweli. Wao hawaamini kuwa Mwenyezi Mungu anaweza kuwafufua wafu ila wakiona hilo kwa macho; wakasahau umbile la kwanza, kwamba yule aliyeleta mwanadamu, aliyekuwa hayuko, ndiye huyo huyo mwenye uweza wa kufufua mifupa iliyosagika.

Je, wao ni bora au watu wa Tubbaa’ na walio kuwa kabla yao? Tuliwaangamiza. Hakika hao walikuwa wakosefu.

Watubba’ walikuwa na dola yenye nguvu katika Yemen, na walikuwa na mali na hali nzuri zaidi kuliko makuraishi. Walipoasi amri ya Mola wao, Mwenyezi Mungu aliwakamata na akawaangamiza; kama alivyowaangamiza watu wa Nuh, A’d na Thamud kutokana na kufuru na ufisadi. Lau wangelizingatia wangeliona na wakaamini, lakini wao ni watu wasiofahamu.

Na hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo kati yake kwa mchezo. Hatukuviumba ila kwa haki.

Mwenyezi Mungu ni mwenye hikima na mwenye hikima hawezi kufanaya mchezo. Kwa hiyo haumbi kitu ila kwa masilahi yanayorudia kuumba. Lengo la kuumbwa mtu ni kuishi maisha mema ya milele yasiyokuwa na mwisho. Kwa hiyo basi hakuna budi kuweko na ufufuo; vinginevyo itakuwa kuumbwa mtu ni kwa mchezo tu. Tazama Juz. 21 (31:33-34) kifungu cha: ‘Kwa nini Mungu akamuumba mtu?’

Lakini wengi wao hawajui kwamba Mwenyezi Mungu ameumba ulimwengu na vilivyomo ndani yake kwa hikima na malengo sahihi.

Hakika siku ya Upambanuzi ni wakati uliowekwa kwa wao wote.

Siku ya upambanuzi ni siku ya Kiyama ambayo Mwenyezi Mungu atawakusanya watu wote kwa ajili ya kuangalia hisabu na malipo. Kuwekewa wakati kwa wote ni ahadi ya huko kukusanywa kwa hisabu na malipo.

Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala hawatanusuriwa.

Si cheo, mali, nasabu, urafiki wala chochote kitakachoweza kufaa siku hiyo, isipokuwa matendo mema. Hayo peke yake ndiyo yatakayoweza kusaidia mbele ya Mwenyezi Mungu.

Isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu atamrehemu, lakini Mwenyezi Mungu atamrehemu yule anayestahiki kurehemiwa; kama yule mwenye vitangulizi vya kumkurubisha kwa muumba wake.

Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. Hakuna mwenye kunusuru wala kurehemu kesho isipokuwa Mwenyezi Mungu. Yeye ni mwenye nguvu na rehema, viumbe wananyenyekea nguvu yake na wanahitajia rehema yake.

إِنَّ شَجَرَتَ الزَّقُّومِ ﴿٤٣﴾

43. Hakika Mti wa Zaqqum.

طَعَامُ الْأَثِيمِ ﴿٤٤﴾

44. Ni chakula cha mwenye dhambi.

كَالْمُهْلِ يَغْلِي فِي الْبُطُونِ ﴿٤٥﴾

45. Kama mafuta mazito, hutokota matumboni,

كَغَلْيِ الْحَمِيمِ ﴿٤٦﴾

46. Kama kutokota kwa maji ya moto.

خُذُوهُ فَاعْتِلُوهُ إِلَىٰ سَوَاءِ الْجَحِيمِ ﴿٤٧﴾

47. Mkamateni na mburuzeni mpaka katikati ya Jahannamu!

ثُمَّ صُبُّوا فَوْقَ رَأْسِهِ مِنْ عَذَابِ الْحَمِيمِ ﴿٤٨﴾

48. Kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayochemka.

ذُقْ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْكَرِيمُ ﴿٤٩﴾

49. Onja! Hakika wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu!

إِنَّ هَـٰذَا مَا كُنتُم بِهِ تَمْتَرُونَ ﴿٥٠﴾

50. Hakika haya ndiyo mliyokuwa mkiyatilia shaka.

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي مَقَامٍ أَمِينٍ ﴿٥١﴾

51. Hakika wenye takua watakuwa katika mahali pa amani.

فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ ﴿٥٢﴾

52. Katika mabustani na chem-chem.

يَلْبَسُونَ مِن سُندُسٍ وَإِسْتَبْرَقٍ مُّتَقَابِلِينَ ﴿٥٣﴾

Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana.

كَذَٰلِكَ وَزَوَّجْنَاهُم بِحُورٍ عِينٍ ﴿٥٤﴾

54. Ndio kama hivyo! na tutawaoza mahurilaini

يَدْعُونَ فِيهَا بِكُلِّ فَاكِهَةٍ آمِنِينَ ﴿٥٥﴾

55. Humo watataka kila aina ya matunda, na wakae kwa amani.

لَا يَذُوقُونَ فِيهَا الْمَوْتَ إِلَّا الْمَوْتَةَ الْأُولَىٰ وَوَقَاهُمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ ﴿٥٦﴾

56. Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na atawalinda na adhabu ya Jahannamu.

فَضْلًا مِّن رَّبِّكَ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿٥٧﴾

57. Ni fadhila zitokazo kwa Mola wako. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

فَإِنَّمَا يَسَّرْنَاهُ بِلِسَانِكَ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ ﴿٥٨﴾

58. Basi tumeifanya nyepesi hii kwa ulimi wako, ili wapate kukumbuka.

فَارْتَقِبْ إِنَّهُم مُّرْتَقِبُونَ ﴿٥٩﴾

59. Basi ngoja tu, na wao wanangoja.

CHAKULA CHA MWENYE DHAMBI NA CHA MWENYE TAKUA

Aya 43 – 59

MAANA

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwataja wakosefu, katika Aya iliyotangulia, na kwamba ahadi yao ni siku ya Kiyama, sasa anataja hali yao itakavyokuwa, kama ifuatavyo:

Hakika Mti wa Zaqqum, Ni chakula cha mwenye dhambi, ambaye dhambi zake na makosa yake yalikithiri duniani. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameyasifu matunda ya mti huu kuwa ni kama mafuta mazito, hutokota matumboni kama kutokota kwa maji ya moto.

Sio mbali kuwa hiki ni kinaya cha uchungu wa adhabu na ukali wake. Mulla Sadra anasema katika Al-asfar: Mti wa Zaqqum ni itikadi za ubatilifu na tabia mbaya zinazompeleka mtu kwenye moto. Baadhi ya mapokezi yanaeleza kuwa ubakhili ni mti miongoni mwa miti ya Motoni na ukarimu ni mti miongoni mwa miti ya Peponi.

Mkamateni na mburuzeni mpaka katikati ya Jahannamu!

Yaani wataambiwa Malaika wa motoni mburuzeni hadi katikati ya Jahannam,kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayochemka.

Hii inaashiria kuwa kwenye Jahannam kuna matunda, hamamu na mavazi, lakini yote yanatokana na moto.

Onja! Hakika wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu! Hakika haya ndiyo mliyokuwa mkiyatilia shaka.

Malaika wa adhabu watamwambia taghuti mwenye dhambi: wewe ulipinga siku ya ufufuo na ukadai kuwa ni mkubwa na mtukufu, basi hivi sasa onja malipo ya kujitukuza kwako na kiburi chako.

Kadiri ninavyotia shaka, lakini siwezi kutia shaka yoyote kuwa wale wanaopora mali za watu na kuzitengenezea silaha za maangamizi kwa ajili ya kuwaua wasiokuwa na hatia, wakiwemo wanawake na watoto, na wala wasione haki wala uadilifu isipokuwa yale wanayoyataka na kuyatamani, sitii shaka kabisa kwamba hawa wanastahiki aina hii ya adhabu; bali wanastahiki zaidi ya adhabu hii kama ingeliokuwako. Tazama Juz. 13 (14:46-52), kifungu cha ‘Jahannam na silaha za maangamizi.’

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kubainisha hali za wakosefu, sasa anaashiria hali za wenye takua siku ya Kiyama, kwa Aya zinazofuatia:

Hakika wenye takua watakuwa katika mahali pa amani, hawatakuwa na hofu wala kuhuzunika. Katika mabustani na chemchem, wakistarehe kadiri watakavyo.

Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana.

Nguo zao ni hariri laini na nzito na watakaa kwenye viti wakielekeana wao kwa wao, wakibarizi huku wanashukuru kwa kukumbuka neema ya Mwenyezi Mungu na radhi zake.

Ndio kama hivyo! na tutawaoza mahurulaini, ambao hajawagusa mtu kabla yao wala jinni.

Humo watataka kila aina ya matunda, na wakae kwa amani.

Watataka matunda bila ya kuhofia kuwa yataisha.

Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na Mwenyezi Munguatawalinda na adhabu ya Jahannamu.

Kila mtu atakufa mauti ya kwanza na baadae ataguria Peponi au Motoni, hakuna kufa huko, lakini kufa ni bora sana kuliko uhai katikati ya Jahannam.

Ni fadhila zitokazo kwa Mola wako. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

Kuna kufuzu gani kukubwa zaidi ya kuokoka na adhabu ya moto na ghad- habu ya Mwenyezi Mungu?

Basi tumeifanya nyepesi hii kwa ulimi wako, ili wapate kukumbuka.

Iliyofanywa nyepesi ni Qur’an. Wanaotakiwa kukumbuka ni waarabu na ulimi ni wa Mtume. Maana ni kuwa tumeiteremsha Qur’an kwa kiarabu ili waarabu wanufaike na mafunzo yake na mawaidha.

Basi ngoja tu, na wao wanangoja.

Ngoja kidogo ewe Muhammad, utaona mwisho utakuwa wako. Wao wanakuduia ufikwe na mabaya, lakini: “Ameaangamia mwenye kuduia na amerudi utupu mwenye kuzua na mwenye kuigeukia haki ameangamia,” kama anavyosema Imam Ali.(a.s) .

MWISHO WA SURA YA ARUBAINI NA NNE: SURAT AD-DUKHAN