7%

11

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ ﴿٣٠﴾

30. Hakika wale ambao wamesema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakawa na msimamo. Huwateremkia Malaika: Msiwe na hofu, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa.

نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ ﴿٣١﴾

31. Sisi ni mawalii wenu katika maisha ya dunia na katika Akhera, na humo mtapata kinachotamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata mtakavyovitaka.

نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ ﴿٣٢﴾

32. Ni takrima itokayo kwa mwingi wa Maghufira, Mwenye kurehemu.

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّـهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ ﴿٣٣﴾

33. Na ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa Mwenyezi Mungu na akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni katika Waislamu?

وَلَا تَسْتَوِي الْحَسَنَةُ وَلَا السَّيِّئَةُ ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِي بَيْنَكَ وَبَيْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِيٌّ حَمِيمٌ ﴿٣٤﴾

34. Mema na maovu hayawi sawa. Zuia uovu kwa lilio jema zaidi. Mara yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki mkubwa.

وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ ﴿٣٥﴾

35. Lakini hawapewi hayo ila wanaosubiri, wala hawapewi ila wenye bahati kubwa.

وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٣٦﴾

36. Na kama Shetani akikuchochea kwa uchochezi basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

WALISEMA MOLA WETU NI MWENYEZI MUNGU KISHA WAKAWA NA MSIMAMO

Aya 30 – 36

MWENYEZI MUNGU NA MTU NA MATENDO

Mwenye kufuatilia Aya za Qur’ani yenye hekima, atakuta kwamba mantiki yake yote na ufahamu wake unajulisha kuwa matendo na imani ndio kila kitu kwa mtu. Hebu angalia dalili zifuatazo:

1. Aya zinazofahamisha kuwa lengo la kwanza na hekima kubwa ya kuweko mtu ni kutenda mambo mema; miongoni mwa Aya hizo ni:

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ ﴿٢﴾

“Ambaye ameumba mauti na uhai ili kuwajaribu ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi” (67:2).

Tazama Juz. 21 (31:33) kifungu ’Kwa nini Mungu akamuumba mtu?’

2. Aya zinazofahamisha kuwa matendo ndio mizani ya kumpima mtu kwenye msingi wake; mfano kauli hizi za Mwenyezi Mungu mtukufu:

كُلُّ امْرِئٍ بِمَا كَسَبَ رَهِينٌ ﴿٢١﴾

“Kila mtu atalipwa alichokichuma” (52:21)

وَمَا تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٣٩﴾

“Na hamtalipwa ila mliyokuwa mkiyafanya” Juz. 23 (37:39)

وَلِكُلٍّ دَرَجَاتٌ مِّمَّا عَمِلُوا وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا يَعْمَلُونَ ﴿١٣٢﴾

“Na wote wana daraja mbalimbali kutokana na yale waliyoyatenda” (Juz. 8 (6:132) na nyinginezo.

3. Ama kauli yake Mwenyezi mungu Mtukufu:Hakika wale ambao wamesema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakawa na msimamo, ni dalili wazi na mkataa kwamba vitendo ndio dhahiri ya pekee inayoakisi imani ya kweli ya Mwenyezi Mungu iliyo halisi na kwamba yeyote mwenye kusema kuwa mimi ni mumin bila ya kuitafsiri imani yake kwa vitendo katika mfungamano wake na wa muumba wake na nafsi yake na jamii yake, basi huyo atakuwa ni muongo mzushi.

Kuongezea zaidi ni kuwa makusudio ya Qur’ani kuhusu matendo ni matendo ya kujenga yenye kuzaa matunda. Tumezungumzia kwa ufafanuzi zaidi kuhusu msimamo katika Juz. 12 (11: 110 – 115) kifungu cha ’Msimamo.’

4. Zaidi ya yote ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amefahamisha kuweko kwake na utukufu wake kwa matendo. Anasema:

سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ ﴿٥٣﴾

“Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli.” (41:53)

Kisha akataja Mwenyezi Mungu (s.w.t) Aya kadhaa zinazohusiana na haya, tutatosheka na hizi tu:

خَلَقَ الْإِنسَانَ ﴿٣﴾ عَلَّمَهُ الْبَيَانَ ﴿٤﴾ الشَّمْسُ وَالْقَمَرُ بِحُسْبَانٍ ﴿٥﴾

“Amemuumba mtu, akamfundisha kubaini. Jua na mwezi (huenda) kwa hisabu” (55:3-5).

Huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiwe na hofu, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa.

Kila jambo lina muda maalum. Utakapokuja muda wa wale waliokuwa na msimamo katika njia ya Mwenyezi Mungu, Malaika watawateremkia na rehema kwa utulivu na habari njema kwamba Mwenyezi Mungu ameyaona matendo yao na kuridhia mahangaiko yao. Kwa hiyo amewaandalia makazi ya heshima aliyowaahidi kupitia kwa manabi na mitume wake.

Sisi ni mawalii wenu katika maisha ya dunia na katika Akhera, na humo mtapata kinachotamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata mtakavyovitaka.

Ni takrima itokayo kwa Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Bado yanaendelea mazungumzo baina ya Malaika wa rehema na wale waliokuwa na msimamo. Yaani watiifu na wenye msimamo watakuwa kwa Mola wao Mwenye kurehemu na watapata kila wakitakacho kutokana na riziki ya ukarimu.

Ibn Al-arabi katika Futahitil-Makkiya anasema kuhusu Aya hii, kwamba Malaika watawaambia wenye ikhlasi kabla ya kutoka kwenye makazi ya kuisha kwenda kwenye makazi ya kudumu: Sisi tumekuwa mawalii wenu duniani kwa sababu shetani aliwajaribu kuwahadaa muache njia iliyonyooka na sisi tukiwakataza na mlikuwa mkitusikiliza. Vile vile sisi ni mawalii wenu Akhera kwa sababu tunawatolea ushahidi wa imani na msimamo mbele ya Mwenyezi Mungu.

Na ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa Mwenyezi Mungu na akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni katika Waislamu?

Tukiunganisha Aya hii na ile isemayo “Hakika wale ambao wamesema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu kisha wakawa na msimamo,” tutapata maana kuwa imani ya kweli iko sehemu tatu: Kwanza, kutangaza kumwamini Mwenyezi Mungu. Pili, kutenda kwa mujibu wa sharia ya Mwenyezi Mungu. Na matendo yaliyo muhimu na adhimu zaidi ni kuwahudumia watu. Tatu, ni kutoa mwito wa Mwenyezi Mungu.

I. Ya kwanza inafahamishwa na kauli: “Wale ambao wamesema Mola wetu ni Mwenyezi Mungu;” yaani wamelitangaza hilo mbele ya watu.

II. Ya pili inafahamishwa na kauli: “Kisha wakawa na msimamo.”

III. Na ya tatu: “Aitaye kwa Mwenyezi Mungu.” Mwenye kukusanya sifa tatu hizi anayo haki ya kusema “Hakika mimi ni katika Waislamu.” Lakini atakayesema hivyo bila ya kumwamini Mwenyezi Mungu au amemuamini Mwenyezi Mungu bila ya kuwahudumia watu na bila ya kulingania kwa Mwenyezi Mungu, basi huyo si Mwislamu kitu; ingawaje duniani anachukuliwa kama Mwislamu.

Mema na maovu hayawi sawa. Zuia uovu kwa lilio jema zaidi. Mara yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki mkubwa.

Makusudio ya mema hapa ni mema ya mjumbe anayelingania kwa Mwenyezi Mungu ambayo ni jihadi yake na uvumilivu wake wa maudhi kwenye njia hii. Na makusudio ya uovu ni uovu wa safihi aliye mjinga wa dini.

Maana ni kuwa tofauti ni kubwa baina yako wewe Muhammad, ukiwa unalingania kwa Mwenyezi Mungu na unavumilia maudhi kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, na yule ambaye ameitika mwito wako kwa upinzani, maudhi na kukuzulia. Matendo yako ni baraka na wema na matendo yao ni uovu na laana. Lakini pamoja na yote hayo ni juu yako kuwachukulia kwa upole na kuwasamehe, ukivumilia usafihi wao, kwani miongoni mwao wako ambao lau utawakabili kwa namna hii basi wanaweza kurudi kwa Mola wao na uadui ukageuka kuwa mahaba na chuki ikawa mapenzi.

Mtu yeyote anaweza kupata marafiki watakaomsaidia kwa maneno mazuri na anaweza kujitengenezea maadui kwa maneno machafu. Maneno ya watu wema yameweza kuwaongoza waovu wengi na kutatua matatizo mengi. Lau si hayo basi mito ingelijaa damu.

Lakini hawapewi hayo ila wanaosubiri, wala hawapewi ila wenye bahati kubwa.

Hayo ni hayo ya kuzuia uovu kwa wema. Mwenye bahati kubwa ni yule anayeridhiwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Maana ni kuwa kuzuia uovu kwa wema ni daraja kubwa ambayo haipati isipokuwa mwenye kuwa mvumilivu wa shida na akawa ana mwelekeo wa Mwenyezi Mungu.

Kwenye Nahjul-balagha imesemwa:“Subira katika imani ni kama kichwa katika mwili. Hakuna kheri katika mwili usiokuwa na kichwa wala katika imani isiyokuwa na subira.” Imesemwa tena:“Iondoe shari iliyoko kifuani kwa mwenzako kwa kuing’oa kifuani mwako.”

Na kama Shetani akikuchochea kwa uchochezi basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w. w ) . Tukiibia Aya ufahamu wake ni kuwa inapaswa mtu achukue hadhari wala asijione ni msafi hata akiwa na dini, elimu au akili kiasi gani. Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 9 (7:200).