18
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI
وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ إِنَّنِي بَرَاءٌ مِّمَّا تَعْبُدُونَ ﴿٢٦﴾
26. Na pale Ibrahim alipomwambia baba yake na kaumu yake: Hakika mimi ninajitenga mbali na hayo mnayoyaabudu.
إِلَّا الَّذِي فَطَرَنِي فَإِنَّهُ سَيَهْدِينِ ﴿٢٧﴾
27. Isipokuwa yule aliyeniumba, kwani Yeye ataniongoza.
وَجَعَلَهَا كَلِمَةً بَاقِيَةً فِي عَقِبِهِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٢٨﴾
28. Na akalifanya liwe neno lenye kubaki katika vizazi vyake ili warejee.
بَلْ مَتَّعْتُ هَـٰؤُلَاءِ وَآبَاءَهُمْ حَتَّىٰ جَاءَهُمُ الْحَقُّ وَرَسُولٌ مُّبِينٌ ﴿٢٩﴾
29. Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka ikawafikia Haki na Mtume anayebainisha.
وَلَمَّا جَاءَهُمُ الْحَقُّ قَالُوا هَـٰذَا سِحْرٌ وَإِنَّا بِهِ كَافِرُونَ ﴿٣٠﴾
30. Na ilipowafikia Haki wakasema: Huu ni uchawi, na sisi hakika tunaukataa.
وَقَالُوا لَوْلَا نُزِّلَ هَـٰذَا الْقُرْآنُ عَلَىٰ رَجُلٍ مِّنَ الْقَرْيَتَيْنِ عَظِيمٍ ﴿٣١﴾
31. Na walisema: Kwa nini Qur’an hii haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili hii?
أَهُمْ يَقْسِمُونَ رَحْمَتَ رَبِّكَ نَحْنُ قَسَمْنَا بَيْنَهُم مَّعِيشَتَهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَرَفَعْنَا بَعْضَهُمْ فَوْقَ بَعْضٍ دَرَجَاتٍ لِّيَتَّخِذَ بَعْضُهُم بَعْضًا سُخْرِيًّا وَرَحْمَتُ رَبِّكَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ ﴿٣٢﴾
32. Kwani wao ndio wanaogawa rehema za Mola wako? Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawainua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya wengine wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayoyakusanya.
وَلَوْلَا أَن يَكُونَ النَّاسُ أُمَّةً وَاحِدَةً لَّجَعَلْنَا لِمَن يَكْفُرُ بِالرَّحْمَـٰنِ لِبُيُوتِهِمْ سُقُفًا مِّن فِضَّةٍ وَمَعَارِجَ عَلَيْهَا يَظْهَرُونَ ﴿٣٣﴾
33. Na lau isingekuwa watu watakuwa kundi moja tungeliwajaalia wanaomkufuru Mwingi wa rehema nyumba zao zina dari ya fedha, na ngazi zao pia wanazopandia.
وَلِبُيُوتِهِمْ أَبْوَابًا وَسُرُرًا عَلَيْهَا يَتَّكِئُونَ ﴿٣٤﴾
34. Na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyoegemea juu yake.
وَزُخْرُفًا وَإِن كُلُّ ذَٰلِكَ لَمَّا مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةُ عِندَ رَبِّكَ لِلْمُتَّقِينَ ﴿٣٥﴾
35. Na mapambo. Na hayo yote si chochote ila ni starehe ya maisha ya dunia tu, na Akhera iliyoko kwa Mola wako ni ya wenye takua.
Aya 26 – 35
Na pale Ibrahim alipomwambia baba yake na kaumu yake: Hakika mimi ninajitenga mbali na hayo mnayoyaabudu, isipokuwa yule aliyeniumba, kwani Yeye ataniongoza.
Kaumu ya Ibrahim, akiwemo baba yake, kama inayvofahamisha dhahiri ya Aya, walikuwa wakiabudu masanamu. Basi akawakataza na akatangaza kujitenga nayo, na kwamba yeye anamwabudu aliyemuumba na atamuongoza kwenye lile lililo na heri na masilahi naye.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:73), Juz. 16 (19: 41-44), Juz. 17 (21:51-56), Juz. 19 (26:69-82) na Juz. 23 (37:83-85).
Kusema kwake: ‘Kwani Yeye ataniongoza,’ kunaonyesha yakini yake na kumtegemea kwake Mwenyezi Mungu. Hivi ndivyo anavyokuwa kila mwenye kuitafuta haki na mwongozo kwa nia safi. Anaamini kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja naye, atamtosha na atamwongoza. Hiyo inatokana na kauli zake Mwenyezi Mungu Mtukufu zifuatazo:-
وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ ﴿٣٦﴾
“Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye takua.” Juz. 10 (9:36).
إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٣﴾
“Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri” Juz.2 (2:153).
وَإِنَّ اللَّـهَ لَمَعَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٦٩﴾
“Na hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wema” Juz. 21 (29:69).
Na akalifanya liwe neno lenye kubaki katika vizazi vyake.
Alilolifanya ni hilo neno la Tawhid, likiashiriwa na kauli yake: ‘Hakika mimi najitenga mbali na hayo mnayoyaabudu.’
Makusudio ya kulifanya ni kuliusia; kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na Ibrahim akawausia haya wanawe na Yaqub: Enyi wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu amewachagulia dini; basi msife ila nanyi ni waislamu.” Juz. 1 (2:131).
Ili warejee.
Hii ndio sababu yake Ibrahim kuwazuia wanawe; kwa maana ya kuwa aliwausia neno la Tawhid, ili walijue. Na kama mmoja wao akishirikisha au akijaribu basi akumbuke wasia wa baba yake na aambiwe kuwa wewe umehalifu wasia wa Ibrahim.
Na hilo lilitokea hasa: “Sema: amesem kweli Mwenyezi Mungu. Basi fuateni mila ya Ibrahim aliyeshikamana na haki; wala hakuwa katika washirikina.” Ni mila ya baba yenu Ibrahim. Yeye aliwaita waislamu zamani. Juz. 4 (3:95) Juz. 17 (22:78).
Mwaka 1389 nilifunga Ramadhan tukufu Dubai kwa mwaliko kutoka huko. Vijana wakawa wananiuliza maswali mengi; miongoni mwayo ni: Kwa nini wanapotajwa maswahaba sunni wanasema: Radhiallah a’nhu (Mwenyezi Mungu awe Radhi naye) na Shia anapotajwa Imam wanasema : Alyhis salaam (Amani ishuke juu yake).
Nikajibu kuwa wote wamechukua kutoka kwenye Qur’an:
رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ﴿١١٩﴾
“Awe radhi nao Mwenyezi Mungu na wao wawe radhi naye” Juz. 7 (5:119).
قُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ وَسَلَامٌ عَلَىٰ عِبَادِهِ الَّذِينَ اصْطَفَى ﴿٥٩﴾
“Sema: Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu (Alhamdu lillah) na amani ishuke juu ya waja wake aliowateua” Juz. 19 (27:59).
Kwa hiyo Shia wamechukua hii na Sunni wakachukua ile.
Nilipofikia kufasiri kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Ili warejee,’ nikasoma kwenye Tafsir Ruhul-bayan ya Sheikh Ismail Haqqi, katika ulama wa kisunni, ninamnukuu: “Wamesema baadhi katika kutukuzwa uso wa Ali bin Abu Twalib, kwa kusemwa: Karramallahu wajhah (Mwenyezi Mungu autukuze uso wake), kwamba imenukuliwa kutoka kwa mama yake, Fatima bint Asad, kwamba yeye (Fatma) alipokuwa akitaka kusujudia sanamu, Ali akimzuia akiwa tumboni.”
Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka ikawafikia Haki na Mtume anayebainisha.
Hawa ni washirikina wa kiquraishi, ambao ni kizazi cha Ibrahim(a.s ) . Makusudio ya haki hapa ni Qur’an na Mtume ni Muhammad(s.a.w.w) . Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemsifu kuwa anabainisha, kwa sababu risala yake iko wazi dalili na muujiza wake umemziba mdomo kila mpingaji.
Maana ni kuwa vigogo wa kiquraishi walimshirikisha Mwenyezi Mungu na wakaupinga wasia wa baba yao Ibrahim(a.s ) wa Tawhid, lakini Mwenyezi Mungu akawapa muda na akawaneemesha fadhila zake, lakini iliwatamalaki ghururi wakapituka mipaka, mpaka alipowajia Mtume kutokana na wao wenyewe na Kitabu cha Mwenyezi Mungu kinachowapa mwito wa Tawhid ambayo ni mila ya baba yao Ibrahim.
Na ilipowafikia Haki wakasema: Huu ni uchawi, na sisi hakika tunaukataa.
Waliikataa Qur’an na wakasema ni uchawi uliozushwa na wakamkataa Mtume wakasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِي نُزِّلَ عَلَيْهِ الذِّكْرُ إِنَّكَ لَمَجْنُونٌ ﴿٦﴾ لَّوْ مَا تَأْتِينَا بِالْمَلَائِكَةِ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٧﴾
“Ewe uliyeteremshiwa ukumbusho! Wewe ni mwendawazimu. Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli?” Juz. 14 (15:6-7).
Na walisema tena: Kwa nini Qur’an hii haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili hii?
Muhammad ni fukara ati anasema: Nimeteremshiwa Qur’an si ajabu hii! Mwenyezi Mungu anaweza kumchagulia risala yake mtu mkubwa; kama vile Walid bin Al-Mughira wa Makka na Urwa bin Mas’ud Athaqafi wa Taif. Mmoja wa hawa ndio angefaa kuteremshiwa Qur’an.
Hivi ndivyo walivyoipinga risala ya Muhammad(s.a.w. w ) ; si kwa lolote ila ni kwa vile hamiliki pesa wala ardhi. Hawajui kuwa mali inamilikiwa na mwema au muovu na mumin au kafiri. Lakini risala ni wakfu wa aliye kufu na na aliyesafi kati ya wasafi.
Hakuna tofauti mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baina ya anayepinga utume wa Muhammad kwa sababu ya ufukara wake na yule anayemtukuza na kumweshimu tajiri kwa sababu ya mali yake na utajiri wake na kumdharau fukara kwa sababu ya ufukara wake. Hakuna tofauti kabisa baina ya hawa wawili; hata mmoja wao akitamka shahada mbili. Isipokuwa tu, atakayetamka duniani atachukuliwa kama mwislamu, lakini huko Akhera atakuwa pamoja na wapinzani na washirikina.
Kwani wao ndio wanaogawa rehema za Mola wako?
Makusudio ya rehema hapa ni utume. Maana ni kuwa, je jambo la utume liko mikononi mwa wapenda anasa, ndio wachague wanayemtaka na wamzuie wasiyemtaka? Kwani utume ni udiwani au ubunge? Hapana! Utume unatoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume anafanya kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ndiye msemaji wake na mbainifu wake.
Sasa wapenda anasa ndio wasemaji rasmi wa Mwenyezi Mungu? Je, wao wanaweza kumruhusu mtu awe msemaji wao rasmi bila ya idhini yao? Vipi wanamfanyia Mwenyezi Mungu ambayo wao hawawezi kujifanyia?
Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawainua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya wengine wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayoyakusanya.
Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye, hilo halina shaka, lakini Yeye vile vile ametaka kutoruzuku hivi hivi isipokuwa kwa sababu:
هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ ذَلُولًا فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِن رِّزْقِهِ ﴿١٥﴾
“Yeye ndiye aliyeidhaliisha ardhi kwa ajili yenu, basi tembeeni katika pande zake na kuleni katika riziki zake.” (67:15).
Sababu hizi za riziki au mahangaiko katika ardhi yako aina nyingi; miongoni mwazo ni; viwanda, kilimo, biashara, utumishi, kama ilivyosema Qur’an: ‘Baadhi yao wanawafanya wengine wawatumikie,’ kama watumishi wa serikali, viwandani, madukani au hospitalini nk. Katika ufahamu wa watu nikuwa bosi yuko juu zaidi ya wengine, lakini mbele ya Mwenyezi Mungu mtukufu na na aliye juu zaidi ni yule mwenye takua zaidi.
إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿١٣﴾
“Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni aliye na takua zaidi katika nyinyi” (49:13)
“Na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, imeandaliwa wenye takua.”
Kwenye Nahjul-balagha Imam Ali(a.s ) anasema:
“Alikuwa na njaa Mtume katika dunia pamoja na umahasusi wake – yaani umahasusi mbele ya Mola wake-na alijiweka mbali na vivutio vya dunia pamoja na kuwa karibu navyo. Basi naatazame mwenye akili, je, Mwenyezi Mungu amemtukuza Muhammad kwa hilo au amemtweza? Akisema amemtweza – basi Wallahil-adhim – atakuwa muongo (anayesema hivyo) na akisema amemtukuza basi naajue kwamba Mwenyezi Mungu amemtweza mwenginewe aliyemkunjulia dunia.”
Unaweza kuuliza : utaifanyaje kauli: ‘Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawainua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi’ inayoonyesha wazi kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anayefukarisha na kutajirisha, na anayemfanya huyu ni mfanyikazi na yule ni mfanyiwa kazi?
Jibu : kauli yake hii Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kusimulia hali halisi waliyo nayo watu na ameyategemeza hayo kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa sababu kutofautiana kunatokana na sababu zake za kimaumbile moja kwa moja na zinatoka kwake kwa kupitia kwengine, kwa vile Yeye ndiye muumba wa ulimwengu.
Maana haya yanafahamishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu mwisho wa Aya: ‘Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayoyakusanya.’ Ambapo kukusanya mali amekutegemeza kwa watu.
Hapa ndio zinaafikiana Aya zinazoamrisha kuhangaikia riziki na zile zilizoitegemeza rizi kwa Mwenyezi Mungu moja kwa moja. Katika Juzuu hii tuliyo, kwenye (42:27), tumeashiria kwamba Mwenyezi Mungu mara nyingine anawapa baadhi ya waja wake tawfiki na kuwaruzuku kingi kutokana na kichache.
Na lau isingekuwa watu watakuwa kundi moja tungeliwajaalia wanaomkufuru Mwingi wa rehema nyumba zao zina dari ya fedha, na ngazi zao pia wanazopandia na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyoegemea juu yake na mapambo.
Yaani ngazi, milango na vitanda vyote vinatokana na madini ya fedha. Aya inamjibu anayesema kuwa ufukara hauendani na utume, eti kwa sababu ufukara ni hulka pungufu.
Ufupi wa jawabu ni kuwa dunia, mbele ya Mwenyezi Mungu, hailingani hata na bawa la mbu, na Akhera ni bora mbele ya Mola wako na ni yenye kubaki, lakini watu wanaathirika na dunia kuliko Akhera na wanakwenda nayo popote wanapoelekea. Lau si hivyo basi Mwenyezi Mungu angeliwapa makafiri nyumba zenye sakafu za fedha na pia milango, ngazi na samani. Na angeliwazidishia mapambo ya dunia kwa kuidharau. Mtaalamu mmoja alisema: “Watu wamepondokea dunia, lakini Mwenyezi Mungu hakulifanya hilo, je ingelikuwaje lau angelifanya. Aya hii inafahamisha kwamba Mwenyezi Mungu anawachukulia upole waja wake na kuwafanyia yale yatakayowakurubisha kwake na kuwaweka mbali na maasi. Kwa uchache kabisa ni kuwa hawafanyii yatakayowahadaa kwenye maasi.
Lakini hayo si chochote ila ni starehe ya maisha ya dunia tu.
Yaani neema za dunia, kwa vyovyote itakavyokuwa basi itaisha tu. Katika Aya nyingine dunia imeitwa upuzi, mchezo na ghururi. Na Akhera iliyoko kwa Mola wako ni ya wenye takua ambao wamemfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu katika kauli zao na vitendo vyao.