4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU
Sura Ya Arubaini Na Saba: Surat Muhammad. Ina Aya 38. Aya zote au nyingi zimeshuka Madina.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ أَضَلَّ أَعْمَالَهُمْ ﴿١﴾
1. Wale waliokufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu, Yeye atavipotoa vitendo vyao.
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَآمَنُوا بِمَا نُزِّلَ عَلَىٰ مُحَمَّدٍ وَهُوَ الْحَقُّ مِن رَّبِّهِمْ كَفَّرَ عَنْهُمْ سَيِّئَاتِهِمْ وَأَصْلَحَ بَالَهُمْ ﴿٢﴾
2. Na wale walioamini, na wakatenda mema, na wakaamini aliyoteremshiwa Muhammad - nayo ni Haki iliyotoka kwa Mola wao - atawafutia maovu yao na ataitengeneza hali yao.
ذَٰلِكَ بِأَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا اتَّبَعُوا الْبَاطِلَ وَأَنَّ الَّذِينَ آمَنُوا اتَّبَعُوا الْحَقَّ مِن رَّبِّهِمْ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّـهُ لِلنَّاسِ أَمْثَالَهُمْ ﴿٣﴾
3. Hayo ni kwa sababu wale waliokufuru wamefuata upotovu, na walioamini wamefuata Haki iliyotoka kwa Mola wao. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowapigia watu mifano yao.
فَإِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا فَضَرْبَ الرِّقَابِ حَتَّىٰ إِذَا أَثْخَنتُمُوهُمْ فَشُدُّوا الْوَثَاقَ فَإِمَّا مَنًّا بَعْدُ وَإِمَّا فِدَاءً حَتَّىٰ تَضَعَ الْحَرْبُ أَوْزَارَهَا ذَٰلِكَ وَلَوْ يَشَاءُ اللَّـهُ لَانتَصَرَ مِنْهُمْ وَلَـٰكِن لِّيَبْلُوَ بَعْضَكُم بِبَعْضٍ وَالَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَلَن يُضِلَّ أَعْمَالَهُمْ ﴿٤﴾
4. Basi mnapokutana na waliokufuru wapigeni shingo, mpaka mkiwadhoofisha wafungeni pingu. Tena waachilieni kwa hisani au wajikomboe, mpaka vita vitue mizigo yake. Ndio hivyo. Na lau angelitaka Mwenyezi Mungu angeliwashinda mwenyewe, lakini haya ni kwa sababu awatie katika mitihani nyinyi kwa nyinyi. Na waliouliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu hatazipoteza amali zao.
سَيَهْدِيهِمْ وَيُصْلِحُ بَالَهُمْ ﴿٥﴾
5. Atawaongoza na awatengezee hali yao.
وَيُدْخِلُهُمُ الْجَنَّةَ عَرَّفَهَا لَهُمْ ﴿٦﴾
6. Na atawaingiza katika Pepo aliyowajulisha.
Aya 1 – 6
Wale waliokufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu, Yeye atavipotoa vitendo vyao.
Neno ‘kuzuilia’ tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu ‘swaddu’ lenye maana ya kupinga na pia lina maana ya kuzuuilia. Likifasiriwa kwa maana ya kwanza, itakuwa kukufuru na kupinga ni kwa maana moja na uungan- ishi utakuwa ni wa kitafsiri. Ikiwa litafasiriwa ‘kuzuiliwa’ maana yake itakuwa wao hawakuamini na pia wamewazuia watu wengine wasiamini. Hii ndio dhahiri inayofahamishwa na Aya.‘Kuvipotoa vitendo vyao,’ ni kuvibatilisha; kama kwamba havikuwaokoa.
Maana ni kuwa mwenye kuupinga Uislamu na akawazuia watu wengine wasiuamini, Mwenyezi Mungu hatamkubalia chochote. Kwa sababu Uislamu ni sharti la msingi la thawabu za Akhera. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
وَمَا مَنَعَهُمْ أَن تُقْبَلَ مِنْهُمْ نَفَقَاتُهُمْ إِلَّا أَنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ وَبِرَسُولِهِ ﴿٥٤﴾
“Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao, ila ni kwamba wao wamemkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake.” Juz. 10 (9:54).
Na wale walioamini, na wakatenda mema, na wakaamini aliyoteremshiwa Muhammad - nayo ni Haki iliyotoka kwa Mola wao - atawafutia maovu yao na ataitengeneza hali yao.
Neno hali hapa tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu ‘bal’ ambalo pia lina maana ya moyo.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kusema kuwa hatawakubalia makafiri, sasa anasema kuwa mwenye kufanya amali njema akiwa anamwamini Mwenyezi Mungu na Qur’an isiyo na shaka, atamkubalia na atamsamehe dhambi zake akitubia na pia atamtengenezea vizuri mambo yake duniani kwa tawfiki na heri na Akhera atamtia Peponi.
Hayo ni kwa sababu wale waliokufuru wamefuata upotovu, na walioamini wamefuata Haki iliyotoka kwa Mola wao.
‘Hayo’ ni hayo ya thawabu za watenda mema na adhabu ya watenda uovu. Maana ni kuwa haki ina wenyewe na batili ina wenyewe. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) atamlipa kila mmoja stahiki yake, hakika yeye ana habari ya wanayoyafanya.
Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowapigia watu mifano yao akibainisha thawabu za mtenda mema na mfano wa watenda mema wenzake, ili awe na yakini ya wema wake na uongofu wake na kumbainishia muovu mfano wa adhabu ya waovu wenzake, ili aweze kujikanya na kuongoka.
Basi mnapokutana na waliokufuru wapigeni shingo mpaka mkiwadhoofisha wafungeni pingu. Tena waachilieni kwa hisani au wajikomboe, mpaka vita vitue mizigo yake.
Aya hii ni miongoni mwa mama wa Aya na katika Aya zilizo wazi wazi na maudhui yake ya vita ni muhimu. Kwa hiyo kwanza tutafsiri misamiati yake kisha tubainishe maana yanayopatikana:
Makusudio ya kukutana ni kupamabana na maadui wa Uislamu katika vita. Kupiga shingo ni kinaya cha kuua; iwe ni kwa kukata shingo au vinginevyo. Mwenyezi Mungu amehusisha kutaja shingo kwa vile ni katika viungo muhimu. Kuwadhoofisha ni kuwaua sana na kuwakamata.
Kufunga pingu ni kuwafunga imara au kutia jela ili wasikimbie wakawarudishia mpira nyinyi. Kuwachilia kwa hisani ni kuwaachilia kwa fidia au bila ya kutoa fidia. Kutua vita mizio yake ni adui kusalimu amri na kutupa silaha. Kwa sababu mizigo ya vita ni silaha.
Maana ya Aya kwa ujumla ni maadui wa dini waking’ang’ania kufuru na mkapambana nao kwa vita, basi wapigeni ili isiwashike huruma na mpambane nao kwa uimara mpaka muwakamate.
Mkishawakamata basi muwazuie barabara ili wasiwaponyoke wasije wakawageukia. Baada ya hapo mwenye hiyari atakuwa ni Mtume au naibu wake, kuwaachia mateka kwa fidia au bila fidia kulingana na masilahi yalivyo wakati huo.
Ilivyo hasa maana ya Aya hii na ile simayo:
مَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَكُونَ لَهُ أَسْرَىٰ حَتَّىٰ يُثْخِنَ فِي الْأَرْضِ ﴿٦٧﴾
“Haimfalii Nabii yoyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda sawasawa katika ardhi.”
Juz. 10 (8:67),
Ni moja tu; yaani hakuna mateka ila baada ya kuwashinda vitani.
Ndio hivyo. Na lau angelitaka Mwenyezi Mungu angeliwashinda mwenyewe, lakini haya ni kwa sababu awatie katika mitihani nyinyi kwa nyinyi.
‘Ndio hivyo,’ ni ishara ya aliyoyabainisha Mwenyezi Mungu – kupigana na maaduia wa Mwenyezi Mungu na kuwachukua mateka. Maana ni kuwa lau Mwenyezi Mungu angelitaka kuwatesa maadui zake katika dunia bila ya vita angeliweza kuwaangamiza kwa askari wa kutoka mbinguni, lakini Mwenyezi Mungu amewaamuru waumini kupigana jihadi na kuwajaribu kwa makafiri, ili vidhihirike vitendo vya yule mwenye kustahiki thawabu na adhabu.
Na waliouliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu hatazipoteza amali zao.
Mwenyezi Mungu anapigana vita na mwenye kumuasi kwa kumtumia mwenye kumtii. Akiuliwa mtiifu, damu yake haiendi bure. Vipi isiwe hivyo na hali atakuwa shahidi wa njia ya Mwenyezi Mungu na kwa ajili yake? Ni nani anayemtekelezea Mwenyezi Mungu kuliko yule aliyemafanyia ikhlasi na akafanya kwa ajili yake?
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amebainisha ujira wa waliofanya kwa ajili yake kwa kusema: “Hatapoteza amali zao,” bali itawarudia wao heri. Hiyo ni kwa kuwaAtawaongoza peponi kwenye mashukio yao, sawa na walivyokuwa wakiongoka kwenye nyumba zao za dunianina awatengezee hali yao, siku ile mtu atakapomkimbia ndugu yake na mama yake na wanawe.
Na atawaingiza katika Pepo aliyowajulisha mito yake, matunda yake, makasri yake, mahurilaini wake na mengineyo yanayotamaniwa na nafsi na yale yanayoburudisha macho.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّـهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ ﴿٧﴾
7. Enyi mlioamini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atawanusuru ataithibitisha miguu yenu.
وَالَّذِينَ كَفَرُوا فَتَعْسًا لَّهُمْ وَأَضَلَّ أَعْمَالَهُمْ ﴿٨﴾
8. Na waliokufuru, basi kwao ni maangamizo, na atavipoteza vitendo vyao,
ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَرِهُوا مَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأَحْبَطَ أَعْمَالَهُمْ ﴿٩﴾
9. Hayo ni kwa sababu waliyachukia aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi akaviangusha vitendo vyao.
أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ دَمَّرَ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ وَلِلْكَافِرِينَ أَمْثَالُهَا ﴿١٠﴾
10. Je, hawatembei katika ardhi wakaona ulikuwaje mwisho wa waliokuwa kabla yao? Mwenyezi Mungu aliwaangamiza. Na kwa makafiri hawa itakuwa mfano wa hayo.
ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ مَوْلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَأَنَّ الْكَافِرِينَ لَا مَوْلَىٰ لَهُمْ ﴿١١﴾
11. Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walioamini. Na makafiri hawana mlinzi.
إِنَّ اللَّـهَ يُدْخِلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ وَالَّذِينَ كَفَرُوا يَتَمَتَّعُونَ وَيَأْكُلُونَ كَمَا تَأْكُلُ الْأَنْعَامُ وَالنَّارُ مَثْوًى لَّهُمْ ﴿١٢﴾
12. Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza ambao wameamini na wakatenda mema katika Bustani zipitiwazo na mito chini yake. Na ambao wamekufuru hujifurahisha na hula kama walavyo wanyama, na Moto ndio makazi yao.
وَكَأَيِّن مِّن قَرْيَةٍ هِيَ أَشَدُّ قُوَّةً مِّن قَرْيَتِكَ الَّتِي أَخْرَجَتْكَ أَهْلَكْنَاهُمْ فَلَا نَاصِرَ لَهُمْ ﴿١٣﴾
13. Na miji mingapi iliyo kuwa na nguvu zaidi kuliko mji wako huu uliokutoa; nao tuliwateketeza na wala hawakuwa na wa kuwanusuru.
أَفَمَن كَانَ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّهِ كَمَن زُيِّنَ لَهُ سُوءُ عَمَلِهِ وَاتَّبَعُوا أَهْوَاءَهُم ﴿١٤﴾
14. Je, mwenye kuwa na dalili kutoka kwa Mola wake ni kama aliyepambiwa uovu wa vitendo vyake, na wakafuata hawa zao?
MKIMNUSURU MWENYEZI MUNGU ATAWANUSURU
Aya 7 – 14
Enyi mlioamini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atawanusuru ataithibitisha miguu yenu.
Kuithibitisha miguu ni kinaya cha uimara. Aya hii ni dalili wazi kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) yuko pamoja na watu wa haki na uadilifu; anawasaidia na kuwashika mkono. Maana ya Aya hii yako kwenye Aya nyingi; kama vile:
فَإِنَّ حِزْبَ اللَّـهِ هُمُ الْغَالِبُونَ ﴿٥٦﴾
“Basi kundi la Mwenyezi Mungu ndio watakaoshinda.” Juz. 6 (5:56).
إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الَّذِينَ اتَّقَوا وَّالَّذِينَ هُم مُّحْسِنُونَ ﴿١٢٨﴾
“Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye uchamungu Na wale ambao wanatenda mema” Juz. 14 (16:128),
إِنَّ اللَّـهَ يُدَافِعُ عَنِ الَّذِينَ آمَنُوا ﴿٣٨﴾ وَلَيَنصُرَنَّ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٤٠﴾
“Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini. Na hakika Mwenyezi Mungu humnusuru yule anayemnusuru Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mtukufu.” Juz. 17 (22:38,40).
Nusra inayotoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) iko namna nyingi; miongoni mwazo ni hizi zifutazo:
• Kuwashinda maadui kwa vita na nguvu ya silaha; kama alivyowashinda Mtume wa Mwenyezi Mungu vigogo wa kikuraishi na dhulma yao na wengineo.
• Kushinda kwa adhabu itokayo mbinguni; kama vile kimbunga tufani n.k.
• Kushinda kwa nguvu ya hoja na dalili katika mijadala.
• Kushinda kwa shani na utajo wa kudumu duniani.
• Nusra ya Akhera siku ile zitakosawijika nyuso.
وَتَرَى الْمُجْرِمِينَ يَوْمَئِذٍ مُّقَرَّنِينَ فِي الْأَصْفَادِ ﴿٤٩﴾
“Na utawaona wahalifu siku hiyo wamefungwa katika minyororo.” Juz. 13 (14:49).
Kwa vile katika Aya tuliyo nayo nusra haikufungwa na sifa ya aina yoyote, basi inatubainikia kuwa makusudio ya nusura katika Aya hii ni nusra yoyote. Hakuna mwenye shaka kuwa itakuwa tu, hata kama ni huko Akhera kusiko na shaka. Kwa hiyo basi hakuna nafasi ya kutaaradhi au kuuliza kuwa vipi Mwenyezi Mungu amewaahidi wenye haki nusra yake, lakini historia imejaa dhulma na ujeuri waaliofanyiwa wema na wenye ikhlasi.
Yametangulia maelezo kuhusu maudhui haya katika Juz. 17 (22:38) kifungu cha “Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini.”
Kwa mnasaba wa Aya hii tutadokeza yafuatayo: Kuna vikundi siku hizi vinadai kusimamisha dola ya Kiislamu. Ni mwislamu gani leo, mwenye ikhlasi ya Mwenyezi Mungu anayekataa Uislamu uwe na serkali yake inayotekeleza hukumu za Qur’an na waislamu wawe na umoja utakaowaokoa na utengano?
Lakini tujiulize: Je, dola hii itapatikana kwa kiasi tu cha kusimamisha bendera na kuinua nembo? Au kwa kuweko vilemba vingi kwenye vichwa vya wajinga na wenye undani?
Je, inawezekana kuwaunganisha Waislamu milioni 700 walioenea mashariki na magharibi mwa ardhi huku wakiwa na makabila, madhehebu na siasa mbalimbali; hawa wameukumbatia ujamaa, wale ubepari na wengine wakiwa na siasa zisizofungamana na upande wowote?
Kama itapatikana dola hiyo ya waarabu au wasiokuwa waarabu je, itaweza kukabili majukumu yake na kutatua matatizo ya waislamu katika nchi nyingine. Kisha je, dola hii ni ya kisunni au kishia au ya wote wawili?
Majibu ya maswali haya tuwachie wataalamu wenye ikhlasi[2] .
Hakika waislamu wamepatwa na udhalili mwingi na kushindwa. Kule kushindwa mnamo tarehe 5 June inatosha kuwa ni udhalili na utwevu. Sababu ya kwanza na ya mwisho ya kushindwa huko ni utengano. Dawa pekee ya hilo ni maarufu kwa wote – kusimama safu moja dhidi ya maadui wenye ushirikiano waliojipanga na kujitokeza kwenye vita vya mwezi June.
Mwenye kumfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu na akataka kuwanasihi waislamu kwa ukweli kabisa basi na afanye juhudi zake zote kwa ajili ya kuwasaidia waislamu kujikomboa na nguvu ya ufisadi ya ndani na nje.
Wakishajikomboa na kuwa na uhuru kamili, hapo ndipo wenye ikhlasi wanaweza kufikiria serikali ya kiislamu au nyingine yenye kuridhiwa na Mwenyezi Mungu na yenye masilahi kwa waislamu.
Ishara yetu hii inatiliwa nguvu na kauli ya Imam Ali(a . s) :“Hakika uzushi wenye kutatiza ni maangamizi na katika utawala wa Mungu kuna hifadhi ya mambo yenu basi upeni utiifu wenu au Mwenyezi Mungu atawaondolea utawala wa kiislamu.”
Ikiwa utawala wa kiisalamu uliwaondokea wahenga kwa sababu ya utengano wao, je utaweza kuturudia sisi tuliotengana zaidi.
Unaweza kuuliza : Je, ni kweli yanayosemwa kuwa chimbuko la fikra ya dola ya kiislamu ni uzayuni ili kuitakasa dola yake ya kidini na ya kibaguzi? Ili waweze kusema kuwa hata waislamu nao pia wanataka dola ya kidini?
Jibu : Hakika dini ya kiyahudi ni dini ya uadui wa maisha na ubinadamu. Kwa sababu, katika itikadi yao, Mwenyezi Mungu ni Mungu wa kikabila, hajishughulishi na walimwengu wengine wote isipokuwa Israil peke yake, na kwamba watu wengine wote wameumbwa kuwatumikia wao; kama ilivyoelezwa katika kitabu Alkanzul marsud cha Dkt. Yussuf Hanna Naasrullah na kitabu Albaqau lilyahud cha mzayuni Rose Marine.
Ama Uislamu ni dini ya maisha, huruma na ubaindamu kwa ujumla. Hakuna kitu kinachofahamisha hivyo zaidi kuliko Aya na Hadithi zinazotangaza waziwazi kuwa uislamu unaongoza kwenye usawa zaidi na kwamba unatilia mkazo kwenye akili na maumbile na ni wajibu kuitikia mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume, kwa sababu ni mwito wa maisha bora.
Maana ni kuwa Uislamu ni dini ya kilimwengu ya kiakili; yaani unajishughulisha na mtu kama mtu wa namna yeyote, hata kama ni myahudi, kwa sharti ya kutomfanyia uadui nduguye mtu.
Sasa haya ni wapi kwa wapi na dini ya Mayahudi waliojiita taifa teule la Mwenyezi Mungu?
Na waliokufuru, basi kwao ni maangamizo, hawataona isipokuwa hizaya na maangamizina atavipoteza vitendo vyao, haitawarudia heri yoyote.
Hayo ni kwa sababu waliyachukia aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi akaviangusha vitendo vyao.
Walimchukia Mtume(s.a.w. w ) na Qur’an si kwa lolote ila ni kwa vile aliwatakia haki na wao wanaichukia, basi wakawa ni wenye hasara. Kupotea na kuanguka kuna maana moja, nako ni kupotea na kutofaa amali. Mwenyezi Mungu amekariri ili kuashiria kuwa kuikufuru Qur’an na kuichukia ni kupotea amali.
Je, hawatembei katika ardhi wakaona ulikuwaje mwisho wa waliokuwa kabla yao?
Jinsi washirikina walivyokadhibisha risala ya Muhammad(s.a.w. w ) , huku wakiona athari ya waliopita na wakisikia kuwa Mwenyezi Mungu aliwaadhibu walipowakadhibisha mitume?
Aya hii imetangulia kwa herufi zake katika Aya kadhaa.
Mwenyezi Mungu aliwaangamiza wao, watoto wao, wake zao na mali zao.
Na kwa makafiri hawa itakuwa mfano wa hayo.
Hukumu ya Mwenyezi Mungu kwa mataghuti ni moja – ikiwa atawaangamiza wa mwanzo kwa sababu ya uasi wao, basi wengine pia atawaangamiza kwa sababu hiyo hiyo.
Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walioamini. Na makafiri hawana mlinzi.
‘Hayo’ ni hayo ya kuangamizwa. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwaangamiza makafiri wakiwa hawana wa kuwasaidia, lakini waumini, msimamizi wao ni Mwenyezi Mungu, akiwakinga na kuwaaneemesha.
Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza ambao wameamini na wakatenda mema katika Bustani zipitiwazo na mito chini yake.
Maana yako wazi na imekwishatangulia katika Aya kadhaa huko nyuma.
Na ambao wamekufuru hujifurahisha na hula kama walavyo wanyama, na Moto ndio makazi yao.
Wao ni sawa na wanyama, wanakula tu na wala hawafikirii chochote. Kwa hiyo mwisho wao ni Jahannam makazi mabaya kabisa.
Imam Ali(a . s) anasema:“Mimi sikuumbwa ili nijishughulishe na kula vizuri. kama mnyama aliyefungwa ambaye hamu yake ni lishe yake tu, au asiyefungwa ambaye shughuli yake kuu ni kuchakura majaa kwa ajili ya lishe yake na kucheza nayo anavyotaka.”
Na miji mingapi iliyo kuwa na nguvu zaidi kuliko mji wako huu uliokutoa; nao tuliwateketeza na wala hawakuwa na wa kuwanusuru.
Hili ni karipio kwa wale waliopanga njama za kumuua Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) , akalazimika kuuhama mji wake wa Makka na kuelekea Madina. Tazama Juz. 9 (8:30).
Katika Tafsir Attabariy, imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas, kwamba Mtume alipotaka kuutoka mji wa Makka alisema: ‘’Wewe ni mji wa Mwenyezi Mungu unaopendeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu. Na wewe ni mji wa Mwenyezi Mungu unaopendeza zaidi kwangu. Lau sikuwa washirikina wamenitoa nisingelikutoka.’’ Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akateremsha Aya hii.
Je, mwenye kuwa na dalili kutoka kwa Mola wake ni kama aliyepambiwa uovu wa vitendo vyake, na wakafuata hawaa zao?
Yule mwenye kuichukua haki kutoka katika chimbuko lake na akawa na busara, hayuko sawa mbele ya Mwenyezi Mungu na yule anayeipima haki kwa hawaa yake na malengo yake, huku akijiona kuwa yeye ndiye mtu mwenye matendo mema zaidi kuliko wengine.