12%

16

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

إِنَّ لِلْمُتَّقِينَ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴿٣٤﴾

34. Hakika wenye takua watakuwa na Bustani za neema kwa Mola wao.

أَفَنَجْعَلُ الْمُسْلِمِينَ كَالْمُجْرِمِينَ ﴿٣٥﴾

35. Kwani tutawafanya Waislamu kama wakosefu?

مَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ ﴿٣٦﴾

36. Mna nini? Mnahukumu vipi?

أَمْ لَكُمْ كِتَابٌ فِيهِ تَدْرُسُونَ ﴿٣٧﴾

37. Au mnacho kitabu ambacho ndani yake mnasoma?

إِنَّ لَكُمْ فِيهِ لَمَا تَخَيَّرُونَ ﴿٣٨﴾

38. Kuwa mtapata humo mnayo yachagua?

أَمْ لَكُمْ أَيْمَانٌ عَلَيْنَا بَالِغَةٌ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ إِنَّ لَكُمْ لَمَا تَحْكُمُونَ ﴿٣٩﴾

39. Au mna viapo juu yetu vinavyofika Siku ya Kiyama ya kuwa mtapata mnayo­jihukumia?

سَلْهُمْ أَيُّهُم بِذَٰلِكَ زَعِيمٌ ﴿٤٠﴾

40. Waulize: Ni nani miongoni mwao mdhamini wa hayo?

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ فَلْيَأْتُوا بِشُرَكَائِهِمْ إِن كَانُوا صَادِقِينَ ﴿٤١﴾

41. Au wanao washirika? Basi wawalete washirika wao waki­wa wanasema kweli.

يَوْمَ يُكْشَفُ عَن سَاقٍ وَيُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ فَلَا يَسْتَطِيعُونَ ﴿٤٢﴾

42. Siku utakapowekwa wazi muundi, na wataitwa kusu­judu, lakini hawataweza.

خَاشِعَةً أَبْصَارُهُمْ تَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ وَقَدْ كَانُوا يُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ وَهُمْ سَالِمُونَ ﴿٤٣﴾

43. Macho yao yatanyenyekea fedheha itawafunika. Na hakika walikuwa wakiitwa wasujudu walipokuwa salama.

KWANI TUTAWAFANYA WAISLAMU KAMA WAKOSEFU?

Aya 34 – 43

MAANA

Hakika wenye takua watakuwa na Bustani za neema kwa Mola wao.

Katika Aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaahidi wakosefu adhabu kubwa, na katika Aya hii anawaahidi wanaomcha Mwenyezi Mungu kuwa na milki ya daima na neema ya kudumu. Namna hii Mwenyezi Mungu analinganisha mwisho wa wakosefu na wa wenye takua; kwa kuvutia na kuhadharisha.

Kwani tutawafanya Waislamu kama wakosefu? Mna nini? Mnahukumu vipi?

Makusudio ya waislamu hapa sio kila mwenye kusema: Lailaha ilallah muhammadur-rasulullah[ (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu); bali makusudio ni wanaom­cha Mwenyezi Mungu. Kwa sababu mazungumzo hapa yanahusiana na wao na yale waliyo nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya Pepo yenye neema.

Unaweza kuuliza : hatudhani kama kuna yeyote anayehukumu kuwa wenye takua wako sawa na wakosefu; sasa kuna haja gani ya Mwenyezi Mungu kusema: mnahukumu vipi?

Jibu : Ni kweli kuwa hakuna anayehukumu kuwa wakosefu na wenye takua wako sawa, lakini mara nyingi wakosefu wanajiona kuwa ni wacha Mungu na kwamba wao wanastahiki malipo na tahawabu wanazostahiki wenye takua.

Basi ndio Mwenyezi Mungu akalipinga hilo na kuwaambia, vipi mnajifanya mko sawa na wenye takua na kati yenu na wao kuna umbali wa mashriki na magharibi? Linalofahamisha maana haya kuwa ndio makusudio ni maswali haya yafuatayo:

Au mnacho kitabu ambacho ndani yake mnasoma? Kuwa mtapata humo mnayoyachagua?

Je, mna Kitabu kutoka mbinguni au ardhini mnachokisoma kwamba nyi­nyi duniani mtapata mnachokipenda na Akhera mpate mnachokitamani? Wasifu uko sawa na ule wa mayahudi na wanaswara: “Na Mayahudi na Manaswara wanasema: Sisi ni wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake.” Juz. 6 (5:18).

Makusudio ya Aya tunayoifasiri ni ya vigogo wa kikuraishi. Ingawaje wao hawakudai kuwa na Kitabu, lakini lengo ni kuwanyamazisha, kwamba hakuna dalili wa mfano wa dalili kuwa wako sawa na wenye takua na kwamba wao watapata wanayoyataka.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 22 (35:30) na Juz. 25 (43:21)

Au mna viapo juu yetu vinavyofika Siku ya Kiyama ya kuwa mtapata mnayojihukumia?

Je, Mwenyezi Mungu amewaapia kiapo kizito na kuwapa ahadi msisitizo kuwa atawaingiza Peponi pamoja na wanaomcha Mungu? Kwamba hatabadilisha ahadi mpaka siku ya Kiyama?

Waulize: Ni nani miongoni mwao mdhamini wa hayo?

Yaani waulize wewe Muhammad! Ni nani aliyeahidiana nao kutekelezewa madai yao?

Au wanao washirika? Basi wawalete washirika wao wakiwa wanase­ma kweli.

Makusudio ya washirika hapa ni masanamu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: “Sema: nionyesheni wale mliowaunganisha naye kuwa washirika.” Juz. 22 (34:27).

Maana ni kuwa haya nawalete hao washrikina waungu wanaowaabudu ili washuhudie kwamba wao watapata Pepo pamoja na wenye takua.

Msawali yote aliyoyaelekeza Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa washirikina ni kuwa hakuna kitu kinachofahamisha kwa karibu wala mbali kwamba washirikina wana chochote. Aina hii ya hoja ni katika nyenzo nzuri sana ya kumnyamazisha hasimu, wakati huo ikielimisha na kuleta uhakika.

Siku utakapowekwa wazi muundi, na wataitwa kusujudu, lakini hawataweza.

Waarabu wanaiita siku ngumu na yenye shida kuwa siku ya kufunuka muundi. Ndio maana siku ya Kiyama imeitwa hivyo. hakuna atakayetaki­wa kusujudi siku hiyo wala kufanya ibada nyingineyo, kwa sababu hiyo ni siku ya hisabu na malipo sio siku ya taklifa na matendo. Kwa hiyo basi kutakiwa kusujudi ni kwa njia ya kutahayariza, sio kwa sharia na taklifa.

Kwa hiyo makusudio ya kutoweza kusujudi siku hiyo ni kwamba hakutawafaa kitu kwa sababu siku hiyo ni ya malipo sio ya kufanya amali. Maana ni kuwa wale ambao wamepituka mipaka au wakafanya uzembe duniani walipokuwa na uwezo wa kufanya, watatahayarizwa na kuadhibi­wa siku ya Kiyama ambayo hakuna hila wala njia ya kuwakurubisha kwa Mwenyezi Mungu.

Macho yao yatanyenyekea.

Kunyenyekea ni sifa ya moyo, lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu ameileta kwa kinaya cha udhalili wao na utwevu wao uliodhahiri machoni mwao. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:fedheha itawafunika , ni tafsiri na ubainifu wa hilo.

Na hakika walikuwa dunianiwakiitwa wasujudu, lakini walikataa kwa kiburi.walipokuwa salama, bila ya kizuizi chochote. Baada ya kuiona adhabu sasa ndio wanataka kusujudi, lakini wakati umekwishapita.

فَذَرْنِي وَمَن يُكَذِّبُ بِهَـٰذَا الْحَدِيثِ سَنَسْتَدْرِجُهُم مِّنْ حَيْثُ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٤٤﴾

44. Basi niache na wanaokad­hibisha maneno haya! Tutawavuta kidogo kidogo kwa mahali wasipopajua.

وَأُمْلِي لَهُمْ إِنَّ كَيْدِي مَتِينٌ ﴿٤٥﴾

45. Na ninawapa muda; hakika hila zangu ni imara.

أَمْ تَسْأَلُهُمْ أَجْرًا فَهُم مِّن مَّغْرَمٍ مُّثْقَلُونَ ﴿٤٦﴾

46. Au wewe unawaomba ujira, kwa hiyo wanalemewa na gharama?

أَمْ عِندَهُمُ الْغَيْبُ فَهُمْ يَكْتُبُونَ ﴿٤٧﴾

47. Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wanaandika?

فَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ وَلَا تَكُن كَصَاحِبِ الْحُوتِ إِذْ نَادَىٰ وَهُوَ مَكْظُومٌ ﴿٤٨﴾

48. Basi ingojee hukumu ya Mola wako, wala usiwe kama sahibu wa samaki, aliponadi naye amezongwa.

لَّوْلَا أَن تَدَارَكَهُ نِعْمَةٌ مِّن رَّبِّهِ لَنُبِذَ بِالْعَرَاءِ وَهُوَ مَذْمُومٌ ﴿٤٩﴾

49. Kama isingelimfikia neema kutoka kwa Mola wake, bila ya shaka angeli tupwa ufuk­weni naye ni mwenye kulau­miwa.

فَاجْتَبَاهُ رَبُّهُ فَجَعَلَهُ مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٥٠﴾

50. Lakini Mola wake alimteua na akamfanya miongoni mwa watu wema.

وَإِن يَكَادُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَيُزْلِقُونَكَ بِأَبْصَارِهِمْ لَمَّا سَمِعُوا الذِّكْرَ وَيَقُولُونَ إِنَّهُ لَمَجْنُونٌ ﴿٥١﴾

51. Na waliokufuru hukaribia kukutelezesha kwa macho yao, wanaposikia mawaidha, na wanasema: Hakika yeye ni mwendawazimu.

وَمَا هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِّلْعَالَمِينَ ﴿٥٢﴾

52. Na hayakuwa haya, ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote.

NIACHENI NA WANAOKADHIBISHA

Aya 44 - 52

MAANA

Basi niache na wanaokadhibisha maneno haya!

Wanaokadhibisha ni washirikina wa kiarabu. Maneno ni Qur’an. Neno ‘niache na’ ni lakutangaza vita nao kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwam­ba Mwenyezi Mungu Yeye mwenyewe atatekeleza kuwaadhibu; apumue Nabii na wale walio pamoja naye kutokana nao na shari yao, kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akabainisha, vipi na kwa njia gani atawatesa pale aliposema:

Tutawavuta kidogo kidogo kwa mahali wasipopajua. Na ninawapa muda; hakika hila zangu ni imara.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anawapa muda wala hawafanyii haraka. Vile vile anawapa mali na watoto na kuwatoa kwenye hali nzuri hadi kwenye hali nzuri zaidi katika dhahiri ya maisha ya dunia, lakini wao kwa undani, wanagurishwa kutoka kwenye hali mbaya hadi kwenye hali mbaya zaidi; mpaka wakifikia kujiona kuwa wako katika ngome madhubuti, ndipo Mwenyezi Mungu huwapatiliza kwa mpatilizo wa mwenye nguvu mwenye uweza. Ili hilo liwe ni la kuumiza zaidi na kutia uchungu moyoni.

Mwenyezi Mungu amekuita huku kuvuta kidogo kidogo kuwa ni hila kwa sababu kunafanana na hila kwa dhahiri; vinginevyo ni kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kutakata na hila na vitimbi. Vipi isiwe hivyo na hali hakimbilii kwake ila mwenye kushindwa, na Mwenyezi Mungu husema kukiambia kitu ‘kuwa kikawa.’ Zaidi ya haya lengo la kutajwa vitimbi ni asihadaike mtu na dunia ikimkabili na kumpa tabasamu. Anatakikana awe na hadhari na yanayojificha.

Au wewe unawaomba ujira, kwa hiyo wanalemewa na gharama? Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wanaandika?

Je, unawataka mali inayokuwa na uzito kwao kuitoa, au wamejua ilimu ya siri kwa hiyo wakafuta yale wanayotakiwa kuamini. Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 27 (40-41).

Basi ingojee hukumu ya Mola wako, wala usiwe kama sahibu wa samaki, aliponadi naye amezongwa.

Sahibu wa samaki ni Nabii Yunus ambaye alipata dhiki na watu wake na akawaacha kwa hasira. Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:97), Juz. 17 (21:87) na.Juz. 23 (37:140). Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemuusia Nabii wake mtukufu(s.a.w.w) kuwa na subira na adha ya watu wake, wala asifanye haraka, kama alivyofanya Yunus, aliyemezwa na samaki, akanadi akiwa tumboni mwa samaki:

أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٨٧﴾

“Hapana Mola isipokuwa wewe, umetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.” Juz. 17 (21:87).

Kama isingelimfikia neema kutoka kwa Mola wake, bila ya shaka angeli tupwa ufukweni naye ni mwenye kulaumiwa.

Yunus alimwomba Mola wake akiwa tumboni mwa samaki, akamwitikia dua yake kwa kumuhurumia, akatemwa na samaki akiwa si mwenye kulau­miwa. Lau si dua yake na kuhurumiwa na Mola wake angelikuwa katika wenye kulaumiwa; bali angelibakia tumboni mwa samaki hadi siku ya ufu­fuo. Ilivyo hasa nikuwa kulaumiwa hapa ni kwa sababu ya kuacha lilo bora sio kwa sababu ya dhambi na uasi.

Lakini Mola wake alimteua na akamfanya miongoni mwa watu wema.

Miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu kwa Yunus ni kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu alimtoa tumboni mwa samaki, akiwa radhi naye, na akamrudisha kwa watu wake akiwa Nabii; kama alivyokuwa hapo mwanzo; wakanufaika naye na kwa mawaidha yake.

Lau angelibakia kati­ka tumbo la samaki hadi siku ya ufufuo, unabii wake usingelikuwa na athari yoyote. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “akamfanya mion­goni mwa watu wema,” ni kuwa atamfufua kesho pamoja na manabii.

Na waliokufuru hukaribia kukutelezesha kwa macho yao, wana­posikia mawaidha

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Maana ni kuwa washirikina wanaposikia Qur’an kutoka kwa Muhammad(s.a.w.w) wanamtazama kwa mtazamo wa kiuadui na chuki, na miguu ya Mtume(s.a.w.w) inakurubia kuteleza kutokana na mtazamo wao mkali kama mshale. Razi anasema: “Waarabu wanasema: Amenitazama kwa kwa mtazamo unaokaribia kuniangusha na kunila. Mshairi anasema: wakikutana macho huyazungusha, mtazamo wa nyoyo kuziangusha

Na wanasema: Hakika yeye ni mwendawazimu.

Walimtazama Mtume kwa mtazamo mkali, vile vile wakamtupia maneno makali, kama kusema kwao: Yeye ni mwendawazimu mwenyezi Mungu (s.w.t) amewarudi, mwanzo mwanzo mwa sura hii tuliyo nayo, kwa kuse­ma: “Kwa neema ya Mola wako wewe si mwendawazimu.”

Na hayakuwa haya, ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote.

Makusudio ya ukumbusho ni ukumbusho wa heri na mwongozo wa njia yake. Maana ni kuwa Qur’an ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliouteremsha kwa Muhammad(s.a.w.w) ili awaongoze watu wote, kila mahali na kila wakati.

MWISHO WA SURA YA SITINI NA NANE: SURAT AL- QALAM