NINANI KHALIFA ( KIONGOZI ) WA WAISLAMU KATIKA ZAMA HIZI?

KIONGOZI (KHALIFA) WA WAISLAMU KATIKA ZAMA HIZI NI IMAMULMAHDI(A.S)

Baada ya kuwa tumefahamu kuwa ahlisunnah, hawakutekeleza wadhifa wao wa wajibu, wa kumteua kiongozi wao wa zama hizi, na kwamba watakufa bila kuwa na baiyah shingoni mwao, tunaweza kusema kuwa:

Hakika Mashia wanao amini maimamu kumi na mbili, wanaamini kuwa kiongozi wa zama hizi ni Imamu Muhammadi bin Hasani Al-askari(a.s) .

Na kwakuwa swala hili, lilizua mjadala mkubwa ndani yake, hivyo tutalitolea ufafanuzi na maelezo katika pande tofauti:

SEHEMU YA KWANZA: TUTAMZUNGUMZIA IMAMU HUYO:

Imamu huyo ni; Muhammadi bin Hasani, bin Ali, bin Muhammadi, bin Ali Riza, bin Musa, bin Jaafar Swadiq, bin Muhamadi, bin Ali Zainul-abidina, bin Husaini, bin Ali, bin Abi Twalibi, sala na salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote.

Alizaliwa tarehe 15 mwezi Shaabani, mwaka; 255 hijiriya, katika mji wa Samarraa.

Na kupata uongozi tarehe: 8/3/260 hijiriya, akiwa na umri wa miaka mitano punde tu baada ya kufariki baba yake. Alitoweka katika macho ya watu mpaka mwaka 329 hiriya, ambako kulifahamika kwa Ghaibutu sughra, ambapo alikuwa akionekana kwa baadhi ya Mashia wake, na baada ya kufariki balozi wake wanne, alitoweka na kutooneka kwa watu mpaka leo hii, ambako kunajulikana kwa Ghaibutu kubra. Ataendelea kubakia hivo mpaka hapo Mwenyezi Mungu atakapo taka adhihiri, kwaajili ya kueneza uadilifu na usawa duniani, baada ya kujaa uovu na uonevu.

SEHEMU YA PILI: KUTHIBITISHA KUZALIWA KWAKE:

Baadhi ya Ahlusunnah, walikanusha kuzaliwa kwake, wakidai kuwa baba yake (Imamu Hsani Al-askari, a.s.) alifariki bila kuwa na mtoto.

Alisema ibun Hajari Alhaitami: wanazuoni wengi wanasema kuwa Hasani Al-askari hakuwa na mtoto, kwa sababu kaka yake, ambaye ni Jaafari, alidai urithi wake, hivyo kama angekuwa na mtoto, asingerithiwa na kaka yake[55] .

Shamsu Alddini Adhahabi nae pia alisema: alisema ibun Hajari, na ibun Qanii, na wengineo kuwa: Hasani bin Ali Al-askari hakuwa na mtoto[56] .

Lakini baada ya kusimama dalili sahihi zenye kuthibitisha kuzaliwa kwake, hayata kuwa na thamani maneno ya wenye kukanusha kuzaliwa kwake.

Hivyo tuta taja dalili za kiakili na hadithi zenye kuthibitisha kuzaliwa kwake.

MIONGONI MWA DALI ZA KIAKILI NI:

1 – Ikiwa hatuta kubali kuzaliwa kwa Imamu Almahdi(a.s) na kuendelea kuwa hai, basi hatuna budi kukubali kuwa; katika zama hizi hatuna Imamu atokanae na kizazi kitukufu cha Mtume, kama alivyo tueleza kuwa:

(إنّي تاركٌ فيكم الثقلين: كتاب الله وعترتي أهل بيتي، ما إن تمسّكتم بهما فلن تضلّوا من بعدي أبداً، وإنّهما لن يفترقا حتّى يَرِدَ عليّ الخوض، فانظروا كيف تخلفوني فيهما).

Hakika mimi nimekuachieni vizito viwili, kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi cha nyumba yangu, kamwe hamta potea, madamu mta shikamana navyo, na hakika vizito hivyo kamwe havita tengana, mpaka vitanirejea katika hauzi, tazameni ni vipi mtashikana navyo baada yangu[57] .

Hivyo ni kwa sababu kwamba; kama hatakuwepo, hakutakuwa na Imamu mwengine atokanae na kizazi kitukufu cha mtume, anayefaa kushikwa, na hadithi hii haitakuwa na maana yeyete katika zama hizi, na hivyo kuwa batili. Na hilo halikubaliki kwa sababu hadithi hiyo imeeleza kwa uwazi kuwa; wapo wenye vigezo vya kuwa Mamamu (viongozi) wa kila zama, mpaka sijku ya kiyama, kinyume na hivyo tungeona utengano kati ya vizito hivyo viliwi, jambo ambalo limekataliwa na hadithi hiyo.

2 – ikiwa hatuta kabali kuzaliwa kwa Imamu Almahdi(a.s) , na kuwepo kwake, na si Imamu wazama, hatunabudi kukubali kuwa; waislamu wote wa zama hizi na zama zilizo pita, wanakufa kifo cha kijahili, kwamujibu wa maneno ya mtume(s.a.w.w) kuwa:

( من مات وليس في عنقة بيعة مات ميتة جاهلية )

yeyote atakaye kufa bila kuwa na kiapo cha utii (bayia), shingoni mwaake, atakufa kifo cha kijahili [58] .

Kwa sababu waislamu wote hawatakuwa na Imamu (kiongozi), na hilo si sahihi kwa ijmau ya wote.

3 – Ikiwa hatuta kubali kuzaliwa kwa Imamu Almahdi(a.s) , na badala yake tukasema kuwa; Imamu Mahdi atazaliwa baadae, kama wanavyo itikadia Masunni, hilo litasababishia matatizo mengi, ambayo tutayataja mwishoni mwa kitabu.

4 – kwamba wanazuoni wengi wa Ahlusunnah, walikuri kuzaliwa kwake, tutakuja kuwa taja hivi punde panapo majaaliwa.

Hivyo ni upuuzi mkubwa, kukanusha kwazaliwa kwa mtu ambaye wamekiri kuzaliwa kweke, wanazuoni wengi, ambao hawatuhumiwi kufanya jama na watu wenye kuitikadia kuzaliwa kwake!!

NA MIONGONI MWA DALILI ZA HADITHI NI:

(ما رواه الكليني في كتاب الكافي بسند صحيح، عن محمد بن يحيى، عن أحمد بن إسحاق، عن أبي هاشم الجعفري قال: قلت لأبي محمد×: جلالتك تمنعني من مسألتك، أتأذن لي أن أسألك؟ فقال: سل. قلت: يا سيّدي هل لك ولد؟ فقال: نعم. فقلت: فإن حدَثَ بِكَ حدَثٌ فأين أسأل عنه؟ فقال: بالمدينة).

1 – Alipokea Kulaini, (Mungu amrehemu), katika kitabu cha Alkafi, kwa Sanadi sahihi, kutoka kwa Muhammadi bin Yahya, kutoka kwa Ahmadi bin Is’haqa, kutoka kwa Abi Hashimu Aljaafari kuwa alisema: nili mwambia Abi Muhammadi(a.s) : utukufu wako unanifanya nishindwe kukuuliza, je unaniruhusu ni kuulize? Akasema: uliza. Nika muuliza: bwana wangu, je unamtoto? Akanijibu: ndio. Nikamuuliza: je kama litakukuta la kukuta, nitamtafutia wapi? Akajibu: mtafute mjini[59] .

Watu wote wanapo taka kuthibitisha mazazi ya mtoto, hurejea kwa baba wa mtoto, hivyo kama atawathibitishia kuzaliwa kwake, kwa riwaya moja sahhihi, kuwa amethibisha kuwa anamtoto, hatunabudi kumsadiki na kukiri, na tunaangalia katika hadithi hapo juu, tunakuta kuwa; Imamu Al-askari, kakiri kuwa anamtoto.

Pia tutataja hapo mbele, hadidhi zingine, zinazo thibitisha kuzaliwa kwake.

2 – Wanazuoni wengi, pia waumini, na watu wema, walimuona Imamu Amahdi(a.s) , katika matukio mengi na maeneo tofauti, mpaka Mirza Nuri Altwabarasi (utukuke utajo wake) katika kitabu chake cha: (Jannatulmaawa fi dhikraa man faaza bi liqaailhujjah), alitaja visa nyingi vilivyo tajwa na watu walio muona Imamu Almahdi(a.s) .

Na kitabu hiki kimechapwa mwishoni mwa juzuu ya khamsini na tatu ya Biharul-anwari.

Hata baadhi ya wanazuoni wa Ahlusunnah, walikiri kuwa walimuona Imamu Almahdi(a.s) , miongoni mwao ni: Asshekhe Hasani Al-iraqi, kama alisema Abdulwahhabu Asshaarani, katika kibu chake cha: (Alyawaqiti wa Aljawahiri), pale alipo sema: mpaka itakapo kuwa dini ngeni kama ilivyo anza... hapo ndipo utangojwa ujio wa Almahdi(a.s) , ambaye ni katika watoto wa Imamu Hasani Al-askari(a.s) , na mazazi yake yalikuwa ni katika mwezi Shaabani tarehe 15, mwaka; 255 hijiria, nae ataendelea kuwa hai mpaka na kutana na Nabii Issa bin Maryamu(a.s) , hivyo umri wake mpaka sasa utakuwa miaka mia saba na sita. Hivi ndivyo alivyo niambia Asshekhe Hasani Al-iraqi, aliyezikwa katika baadhi ya miji inayo lindwa na Imamu Almahdi, pale alipo kutana nae, na pia bwana wangu Ali Alkhawasi [60] .

SEHEMU YA TATU; DALILI YA UIMAMU WAKE:

Dalili ya kwanza: Imamu (Kiongozi) wa waislamu nilazima awe Maasumu.

Na ushahidi juu ya hilo ni mambo ya fuatayo:

1 – Asiye kuwa Maasumu, maneno yake hayaaminiki, na nivigumu kutekeleza amri yake au hukumu yake, kwa sababu inawezekana akawa amekosea au kusahau, au kughafilika, au kusema uongo na kuto kuwa na maarifa. Hivyo hawezi kuwa chini ya maneno ya Mwenyezi Mungu yasemayo:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ﴿٥٩ ﴾

Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi [61] .

Kwani Mwenyezi Mungu mtukufu, ameiweka twa’a yake sawa na twa’a ya wenye madaraka, amabao ni Maimamu, kwa sababu ya kuto kuwa na makosa.

2 – Asiye kuwa Maasumu, anaidhulumu nafsi yake, kwa kufanya maasi, kwani kila mwenye kufanya maasi, anaidhulumu nafsi yake, kwaminajili hiyo hafai kuwa Imamu (kiongozi), kwa mujibu wa maneno ya Mwenyezi Mungu mtukufu, pale aliposema:

قَالَ وَمِن ذُرِّيَّتِي قَالَ لَا يَنَالُ عَهْدِي الظَّالِمِينَ ﴿١٢٤﴾

Akasema: Je, na katika vizazi vyangu pia? Akasema: Ahadi yangu haitawafikia wenye kudhulumu[62] .

Aya ilipotaja, kujidhulumu, inakusudia kujidhulumu mwenyewe, au kumdhulumu mwengine, na mana ya Ahadi, ni uimamu, kwa ushahidi wa maneno yaliyo tangulia katika Aya tajwa.

3 – Uimamu (uongozi) ambao dini au kunyoka mambo ya waislamu, vya tegemea Uimamu huo, hauwezi kupewa mtu ambaye, hukosea au kupatia, kwa sababu kufanya hivo, kutasababisha kubadilika sheria za dini, kwa kadiri watakavyo kuwa wakibadilika Maimamu. Kwa sababu hiyo, ndio mana Mwenyezi Mungu, aliwafanya mitume kuwa Maasumina, na kuwa epusha na makosa, kwa kuwa wao ndio wafikishaji wa Dini na sheria, na ili Dini ihifadhike na kubaki daima.

Baada ya kufahamika yote hayo, tunasema: Hakika Uimamu (uongozi), upo kwa Imamu Almahdi(a.s) , kwa sababu yeye ameepushwa na madhambi ya kila aina, kwa mujibu wa maneno ya mtukufu mtume(s.a.w.w) , pale aliposema:

(يملؤها قسطاً و عدلاً بعد ما ملئت ظلماً وجوراً)

Ataeneza uadilifu na usawa duniani, baada ya kujaa uovu na uonevu[63] .

Alisema Barzanji: Ama kuhusu isma ya Mahdi, ipo katika hukumu yake.

Kisha akasema: Imamu Mahadi, anahukumu kwa kile anacho funuliwa na malaika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Malaika ambaye alitumwa kumuongoza, na hiyo ndiyo sharia ongofu ya mtume Muahammadi, sheria ambayo, hata yeye angekuwa hai asinge hukumu kinyume na sheria hiyo... hayo aliyasema mtukufu mtume akimsifia kuwa:

(يقفو أثري لايخطئ)

Atafuata nyayo zangu bila kukosea. Hivyo tukafahamu kuwa; yeye ni mfuasi, na si mwenye kuongeza sheria, na kwamba ni Maasumu. Na haina maana awe maasumu katika hukumu, bila kuwa Maasumu katika makosa. Kwani hukumu ya Mtume, hainasibishwi na makosa, kwa sababu yeye hatamki kwa matamanio, bali ni ufunuo ulio funuliwa[64] .

Kwaminajili hiyo, ndio maana tukasema kuwa; Al’imamu Almahdi ni Maasumu, na kwamba yupo katika zama hizi, kama ambavyo uwepo wake unabaibisha uimamu wake, kwa sababu umma unakubali kuwa hakuna mwengine, mwenye sifa ya kuwa Maasumu katika zama hizi, ghairi yake, na maasumu hutangulizwa juu ya asiye kuwa maasumu, vinginevyo, tutakosa Imamu katika zama hizi, jambo amalo halikubaki.

Dalili ya pili: Imamu wa waislamu (kiongozi), ni lazima awe ameteuliwa kwa aya na hadithi;

Ushahidi juu ya hilo ni:

1 - Imethibiti kuwa; ni sharti Imamu awe maasumu, na isma ni swala la kinafsi, hawezi kulifahamu kila mtu, hivyo basi ni lazima ateuliwe na ambaye anayajua yaliyofichika vifuani na nyoni, ambaye ni Mwenyezi Mungu mtukufu.

2 – Kuacha kumteua kiongozi (Imamu), kuta fungua mlango wa Mifarakano na marumabano, kama ilivyo tokea katika Saqifah bani Saidah, (kwa madai kuwa mtukufu Mtume hakuteua kiongozi). Marumbano hayo haya kuishia hapo, bali yaliendelea mpaka leo hi, ambapo ni kinyume na maagizo ya Mwenyezi Mungu katika Qur’ani pale alipo tutaka kuwa pamoja, na kushikamana, kwa kusema:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا ﴿١٠٣ ﴾

Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane [65] .

Pia akasema: { لا تَنازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَ تَذْهَبَ ريحُكُمْ} Wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu[66] .

Hivyo hafai kwa Mwenyezi Mungu kuwafungulia waislamu mlango wa mizozano na mifarakano, kwa kuwaacha waislamu wajichagulie kiongozi.

3 – Kuteua Kiongozi kinyume na uteuzi wa Mwenyezi Mungu, kutapelekea kumteua Kiongozi asiyefaa, kwa sababu maranyingi huteuliwa kwa kuangalia maslahi binafsi, kufuata matamanio ya nafsi, au ubaguzi.

Hivyo kumuacha aliye bora, kama atakuwa mkali katika haki, au kuto kuwa na mali, Wasaidizi, na ukoo.

Hayo yote ni kama watu watamjua ni nani mbora, lakini, kuna wakati wanashindwa kujua ni nani bora, hususani kama atakuwa ya tukio la kumteua kiongozi huyo.

Kwaminajili hiyo, haifai kwa Mwenyezi Mungu mtukufu, awaachie watu swala muhimu la kumteua kiongozi, ambao wengi wao amewataja katika Qur’ani kwa sifa mbaya kwa kusema:

وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ﴿١١٦﴾

Na ukiwat'ii wengi katika hawa waliomo duniani watakupoteza na Njia ya Mwenyezi Mungu [67] .

وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ ﴿١٠٣﴾

Na wengi wa watu si wenye kuamini hata ukijitahidi vipi [68] .

وَأَكْثَرُهُمْ لِلْحَقِّ كَارِهُونَ ﴿٧٠﴾

Na wengi wao wanaichukia Haki [69] .

Hivyo hakuna njia zaidi ya kumuainisha kiongozi, kwani Mwenyei Mungu mtukufu, ndiye anaye jua maslahi ya viumbe wake, na nani anayefaa kuwa kiongozi, na kuwaongoza.

4 – Uimamu (Uongozi), ni khilafa ya Mwenyezi Mungu na mtume wake, hivyo basi, uongozi huo hauwezi kupatikana isipokuwa kwa uteuzi wao. Na ama uteuzi utakao fanyika kinyume na uteuzi wao, utakuwa kinyume na maagizo ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

5 – Qur’ani tukufu imebainisha kwa uwazi kuwa; Mwenyezi Mungu ndiye anayemteua nabii, imamu, waziri au khalifa, wala hatujaona aya hata moja katika Qur’ani, inayosema kuwa; uteuzi huo umeachwa kwa watu.

Ama ushahidi wa kuteuliwa manabi katika Qur’ani, ni pale aliposema Mwenyezi Mungu mtukufu katika aya zifuatazo:

اذْكُرُوا نِعْمَةَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ جَعَلَ فِيكُمْ أَنبِيَاءَ ﴿٢٠﴾

Kumbukeni Neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, alipo wateuwa Manabii kati yenu [70] .

وَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَكُلًّا جَعَلْنَا نَبِيًّا ﴿٤٩﴾

Tulimpa Is-haq na Yaaqub, na kila mmoja tukamfanya Nabii [71] .

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا وَإِبْرَاهِيمَ وَجَعَلْنَا فِي ذُرِّيَّتِهِمَا النُّبُوَّةَ وَالْكِتَابَ ﴿٢٦ ﴾

Na bila ya shaka tulimtuma Nuhu na Ibrahim, na tukaweka katika dhuriya zao Unabii na Kitabu [72] .

اللَّـهُ أَعْلَمُ حَيْثُ يَجْعَلُ رِسَالَتَهُ ﴿١٢٤﴾

Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi kuliko wote kujua wapi anaweka ujumbe wake [73] .

إِنَّا رَادُّوهُ إِلَيْكِ وَجَاعِلُوهُ مِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٧﴾

Hakika Sisi tutamrudisha kwako na tutamfanya miongoni mwa Mitume [74] .

Ama dalili kuhusu kumteua khalifa, au waziri, zinapatikana katika aya zifuatazo:

يَا دَاوُودُ إِنَّا جَعَلْنَاكَ خَلِيفَةً فِي الْأَرْضِ ...﴿٢٦﴾

Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya wewe uwe Khalifa katika nchi [75] .

وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَائِكَةِ إِنِّي جَاعِلٌ فِي الْأَرْضِ خَلِيفَةً ﴿٣٠﴾

Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi) [76] .

وَجَعَلْنَاهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا وَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِمْ فِعْلَ الْخَيْرَاتِ وَإِقَامَ الصَّلَاةِ وَإِيتَاءَ الزَّكَاةِ وَكَانُوا لَنَا عَابِدِينَ ﴿٧٣﴾

Na tukawafanya maimamu wakiongoa watu kwa amri yetu. Na tukawafunulia watende kheri, na washike Sala, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu [77] .

قَالَ إِنِّي جَاعِلُكَ لِلنَّاسِ إِمَامًا قَالَ وَمِن ذُرِّيَّتِي قَالَ لَا يَنَالُ عَهْد ِي الظَّالِمِينَ ﴿١٢٤﴾

Akasema: Je, na katika vizazi vyangu pia? Akasema: Ahadi yangu haitawafikia wenye kudhulumu[78] .

وَجَعَلْنَا مِنْهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا لَمَّا صَبَرُوا وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يُوقِنُونَ ﴿٢٤﴾

Na tukawafanya miongoni mwao waongozi wanao ongoa watu kwa amri yetu, walipo subiri na wakawa na yakini na Ishara zetu [79] .

Baada ya kufahamika hayo, tunasema kuwa; Hakika imamu Almahdi(a.s) kama atakuwa ndiye Imamu mteuliwa katika zama hizi, basi itathibiti kinacho kusudiwa. Na kama tutasema kuwa; hajazaliwa, na kwamba hayupo, ukiachia mbali kuteuliwa, basi inabidi tukubali kuwa zama hizi hazina kiongozi, kwa sababu ghairi ya imamu Mahdi, hakuna mwenye sifa ya kuwa kiongozi wa zama hizi. Na kubaki zama bila kuwa na kiongozi, ni kinyume na itifaki ya waislamu wote.

DALILI YA TATU: Ni hadithi ya vizito viwili; ambayo ime pokewa kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) kuwa:

(إنّي تركت فيكم الثقلين، ما إن أخذتم به لن تضلّوا بعدي: أحدهما أكبر من الآخر، كتاب الله حبل الله ممدود من السماء إلى الأرض، وعترتي أَهل بيتي، ألا وإنّهما لن يفترقا حتى يرد عليّ الحوض).

Hakika mimi nimekuachieni vizito viwili, kimoja ni kikubwa kuliko chengine, kitabu cha Mwenyezi Mungu, kamba iliyo nyoka kutoka mbingini mpaka ardhini, na kizazi cha nyumba yangu, kamwe hamta potea, madamu mta shikamana navyo, na hakika vizito hivyo kamwe havita tengana, mpaka vitanirejea katika hauzi[80] .

Hadithi hii inatuonyesha wazi, ulazima wa kushikamana na Imamu (kiongozi) Mwema, atokanae na nyumba ya Mtume(s.a.w.w) , na kwamba hata tofautiana na kitabu cha Mwenyezi Mungu, katika maneno yake na matendo yake, na yeye ndiye mwenye kuyafahamu maana za dhahiri na batini, za kitabu kitukufu.

Hivyo tunapo sema kuwa Imamu Mahdi yupo, maana yake, yeye ndiye kiongozi wa umma kwa zama hizi, vinginevyo hakuna mwengine anaye faa kushikwa, kutoka katika nyumba ya bwana Mtume katika zama hizi. Kwani umma umekubaliana kuwa; asiye kuwa yeye, anatofautiana na Qur’ani katika matendo yake na maneno yake, kutokana na kuwa si Maasumu.

DALILI YA NNE: wanazuoni wa kisunni, walitaja vigezo, ambavyo anatakiwa kuwa navyo khalifa wa waislamu, vigezo ambavyo anavyo Imamu Mahdi, kwa sababu yeye, ni katika makuraishi, kutokana na kwamba yeye ni katika kizazi cha Mtume(s.a.w.w) , Pia ni muadilifu, kwa mujibu wa maneno ya Mtume(s.a.w.w) pale aliposema: ( يملؤها قسطاً و عدلاً ), Ataeneza uadilifu na usawa duniani. Na kwamba yeye ni mjuzi wa wajuzi, kwa sababu atahukumu, kwa hukumu ya Mtume(s.a.w.w) , na wengine hawana sifa hizo, kama tulivyo taja huko nyuma.

Hivyo kama watasalimu kuwa yeye ndiye kiongozi mteule, basi itathibiti hoja yetu, na kama hawata salimu, basi ulimwengu utabakia bila Imamu, kwa sababu Ahlusunnah, hawana khalifa mwenye sifa za kuwa kiongozi, lakini pia Mashia, zaidi ya kuamini kuwa, imamu mahdi ndiye mwenye sifa hizo. Na kubakia zama bila kuwa na kiongozi, nikinyume na itifaki ya waislamu wote duniani.

DALILI YA TANO: kama Imamu Mahdi, hata kuwa Imamu wa zama, basi vifo vya waislamu wote, vitakuwa vya kijahili, hivyo umma mzima kuwa katika makosa, kitu ambacho ni batili, na hakikubaliki kwa wote, kwa sababu imesihi kwa wo te hadithi isemayo: ( لاتجتمع أمتي على ضلالة أو خطأ) , umma wangu hawezi kukosanyika katika upotevu au makosa.

Shubhat na jibu lake:

Waweza kusema kuwa: Imamu Almahdi, hajazaliwa, na wala hayupo, bali atazaliwa mwishoni mwa zama (akheri zamani), na si Muhammadi bin Hasani Al-askari, kama wanavyo dai Mashia.

JIBU LAKE:

1 – Tulithibisha huko nyuma, kuzaliwa kwake, na kuwepo kwake, na kwamba yeye ndie kiongozi wa zama hizi, vingine itatulazimu kuyakubali yote tuliyo yakanusha huko nyuma.

2 – Wanazuoni wengi wa kisunni, wamekiri kuwa; Almahdi anaye kusudiwa, ni Muhammadi Ibni Hasani Al-askari(a.s) , na kwamba bado yupo mpaka sasa. Itikadi hiyo, pamoja na kuwa inapingana , na itikadi ya wanazuoni wengi wa kisunni, hawakuacha kuitaja katika vitabu vyao, kwa kuwa ndiyo itikadi sahihi isipo.

Na miongoni mwa wanazuoni hao ni:

1 – Muhammdi bin Twalha Alsshafi’i: (582 – 652 hijiriya): katika kitabu chake (Matwalibu Assauli), malango wa kumi nambili, Alisema; Muhammadi bin Hasani Al-askari(a.s) , huitwa; Almahdi Alhujjah Alkhalafu Asswalehe.

Kisha akasema: Ama kuhusu mazazi yake; ilikuwa; tarehe ishirini na tatu, mwaka 258, hijiriya.. kisha akanukuu baadhi ya hadithi zinazo husu kuzaliwa kwake, kisha akataja baadhi ya shubuhati na kuzijibu.

2 – Muammadi bin Yusufu bin Muammadi Alkanji Asshafi’i( [81] ) (alifariki;658 hijiriya): katika mlango wa mwisho wa kitabu chake cha: (Albayani fi Akhbari Swaahibu Alzzamani): alitaja ushadi juu ya bakia hai Al-imamu Almahdi, tangu alipo toweka (ghaibah).

3 – Ali Ibni Muhammadi, afahamikae kwa; ibu Alswabbaghu Almaaliki( [82] ) (784 – 855): katika mlango wa kumi na mbili wa kitabu chake cha (Alfusulu Almuhimmah), Alisema kuwa: Abu Muhammadi Alhasani Al-askari, aliacha mtoto mmoja, ambaye ni; Alhujjah Alqaaimu, anayegojwa kusimamisha dola ya haki. Na alikuwa ameficha kuzaliwa kwake, kutokana na ugumu wa mazingira ya wakati ule, na kuhofia asiuliwe na wafalme wa zama zile[83] .

4 – Sibtwi Ibuni Aljauzi: katika; Tadhkiratul-khawaasu, malngo maalumu wa Imamu Almahdi, Alisema kuwa ni: Muhammadi Ibni Alhasani, Ibni Ali, bin Muhammadi, bin Ali, bin Musa Alriza, Ibni Jaafar, bin Muhammadi, Ibni Ali, Ibni Alhusaini, Ibni Ali, Ibni Abi Twalibi(a.s) , na kuniya yake, ni: Abulqaasimu, ambaye ni Alkhalafu Alhujjah, Swaahibu Alzzamani, Alqaaimu, Almuntazari, naye ndiye mwisho wa maimamu. Hivyio ndivyo alivyo tueleza Abdul-azizi Ibni Mahmudu Albazzazi, kutoka kwa ibun Amru, kutoka kwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu kuwa alisema:

(يخرج في آخر الزمان رجل من ولدي، اسمه كاسميو، وكنيته ككنيتي، يملأ الأرض عدلاً كما ملئت جوراً)

Katika zama za mwisho, atatokea mtu atokanae na kizazi changu, jina lake ni kama jina langu, na kuniya yake ni kama ya kwangu, Ataeneza uadilifu na usawa duniani, baada ya kujaa uovu na uonevu, huyo ndiye Mahdi.

Hadithi hii ni mashuhuri... mpaka mwisho wa maneno yake[84] .

5 – Abdulwahhabu Assha’arani[85] (892 – 973hijiriya): Aliyataja hayo katika mlango wa sitini na tano, wa kitabu chake cha (Alyawaakiti wa Aljawahir fi Aqaaidi Al-akabir).

6 – Muhyi Alddini ibun Arabi (560 – 638 h): katika kitabu chake cha (Alfutuhati Almakkiyah), mlango wa mia tatu na sitini nasaba, alisema kuwa: tambueni kuwa; Almahdi(a.s) , ni lazima atatokea... nae ni katika kizazi cha mjumbe wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , katika wana wa Fatwima (radhi za mola ziwe juu yake). Babu yake ni Huseini Ibni Ali, Ibni Abi Twalibi (radhi za mola ziwe juu yao). Na baba yake ni Hasani Al-askari, Ibni Imamu Ali Alnnaqiyu, Ibni Imamu Muhammadi Altaqiyu, Ibni Imamu Ali Alriza, Ibni Imamu Musa alkadhwimu[86] .

7 – Alhafidhu Khawaja Barsaa: katika kitabu chake cha (Faswilu Alkitwabu) Alisema kuwa: miongoni mwa maimamu wa Ahlulbayti wa toharifu, ni; Abu Muhammadi Alhasani Al-askari. Alizaliwa siku ya jumaa,tarehe; sita, mwezi wa; tatu, mwaka mia mbili thelathini na moja. Alizikwa pembeni ya baba yake... Aliacha mtoto mmoja ambae ni; Abalqaasimu, Muhammadi, Almuntadhwir. Ambae huitwa pia; Alqaaimu, Alhujjah, Almahadi, Swahibu alzzamani. Na ndie Mwisho wa maimamu kumi na mbili, kwa Mashia. Imamu huyo, alizaliwa tarehe; kumi na tano, mwezi; Shaabani, Mwaka; mia mbili khamsini na tano. Baba yake alifariki, akiwa na miaka mitano. Na Mama yake anaitwa; Narges, amabae alifahamika kwa; Ummu waladi. Abu Muhammadi; Alhasani Al-askari, na mwanae Muhammadi Almuntadhwir Almahdi (radhi za mola ziwe juu yao), ni maarufu kwa watu wa zama zile[87] .

8 – Swalahu Alddini Alsswafadi (797 – 764 hijiriya): Kunduzi katika kitabu chake cha; Yanaabiu Alisema kuwa: Alsshekh Alkabir Alkamil, mjuzi wa siri za herufi, Swalahu Alddini Alsswafadi katika kitabu cha; Sharhu Alddairah Alisema kuwa: Hakika Mahdi mtarajiwa, ni Imamu wa kumi na mbili, katika maimamu kumi na wa wili, ambapo wa kwanza kati yao ni, Bwana wetu Ali, na wa mwisho wao ni; Almahdi, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na kutunufaishe nao[88] .

9 – Muhammadi Ibni Ali Twuluni (880 – 953 hijiriya): katika kitabu chake cha (Al-aimatu Al-ithna Asharah), Alielezea kuhusu uwepo wa Imamu Almahdi, kwa Mashairi, ambayo ni:

عليك بالأئمة الاثنى عشَر من آل بيت المصطفى خير البشر

أبو ترابٍ، حسنٌ، حسينُ وبغضُ زينِ العابدين شين

محمدُ الباقر كم علمٍ درى والصّادق ادعُ جعفراً بين الورى

موسى هو الكاظم وابنه علي لقِّبه بالرضا وقدره علي

محمد التفيُّ قلبه معمور عليُّ النقيُّ دُرُّه المنثور

والعسكريُّ الحسن المطهَّر محمد المهديُّ سوف يظهر

Shikamana na Maimamu kumi na mbili watokanao na nyumba ya Mtume mbora wa vimbe.

Abu Turabu (Ali bin Abi Twalibi), Hasani, Huseini Na kumchukia Zainul-abidina ni vibaya.

Muhammadi Albaaqir, ni kiasi gani alikuwa na elimu Na Alsswadiq, aliyefahamika kwa viumbe Jaafar.

Musa Alkadhwimu na Mwanae Ali Ambae aliitwa Alrrizaa, na kadari yake ni Ali.

Muhammadi Altaqiy, Ali Annaqiy.

Na Al-askari Alhasani Almutwahharu Muhammadi Almahdi, ambae atadhihiri[89] .

10 – Sulaymani Alqunduzi Alhanafi: Hakika yeye katika kitabu chake cha; ( Yanaabiu Almawaddah) alijitahidi kuthibitisha kuwa Almahdi, mtarajiwa, ndie Muhamaadi Ibni Hasani Al-askari(a.s) . Na aliweka milango mbali mbali kwaajili ya kuthibitisha hilo, miongoni mwa milango hiyo ni; Mlango unaotaja mazazi ya Almahdi. Pi Mlango wa karama zilizo zidhihirika kwa watu, na kwamba baba yake Al-imamu Al-askari, aliwaonyesha baadhi ya Mashia wake mwanae Almahdi, na kuwajulisha kuwa yeye ndie atakuwa Imamu baada yake. Na mlango mwengine, ni kuhusu waliomuona Almahdi baada ya kutoweka. Na mlango wa mwisha, alitaja Maneno ya wanazuoni, yanayothibisha kuwa; Almahdi mtarajiwa ni mwana wa Al-imamu Alhasani Al-askari(a.s)[90] .

Almirza Huseini Annuri, katika kitabu chake cha (Kashfu Al-astaari), alitaja majina arobaini ya wanazuoni wa kisunni, ambao aliuta katika vitabu vyao kuwa; Al-imamu Muhammadi Ibni Alhasani Al-askari(a.s) , ndie Almahdi Almuntadhwar[91] .

3 – Hakika baadhi ya Masunni, walikiri kumuona Al-imamu Almahdi, na kuonana nae. Miongoni mwao ni; Asshekh Hasani Al-iraqey, kama tulivyo taja huko nyuma, kutoka kwa Abdulwahhabu Alssha’araani, katika kitabu chake cha: ( Alyawakitu wa Aljawahir).

TIJA: Ni kwamba; Al-imamu Almahdi, Muhammadi Ibni Alhasani Al-askari(a.s) , ndie Imamu (kiongozi) wa zama hizi, kwa mujibu wa dalili Sahihi tulizo zitaja huko nyuma. Ama wengine, hatuna ushahidi wa kuthibitisha uongozi wao.

NINANI KHALIFA ( KIONGOZI ) WA WAISLAMU KATIKA ZAMA HIZI?

USAHIHI WA HADITHI SAHIHI JUU YA KUZALIWA AL-IMAMU ALMAHDI

Kuna bwana mmoja, aliye jiita ( Ahmadi Alkatibu), alidai katika baaadhi ya vituo habari kuwa: hakukuta dalili hata moja ya kihistoria, inayothibisha kuzaliwa kwa Al-imamu Almahdi, Muhammadi Ibni Hasani Al-askari(a.s) . Na anacho kikusudia kunako dalili ya kihistiria, ni; hadithi sahihi zinazo thibisha kuzaliwa kwake, hatakama zitakuwa za kishia. Huku akiwa amejitia kuto zifahamu dalili za kiakili, zinazo thibitisha kuzaliwa kwake na kuwepo kwake. Lakini alidai kuwa aliwaomba wanazuoni wa kishia wamthibitishie hilo, lakini hakuma yeyote aliye jitokeza.

Ingawaje madai yake ni ya uongo, kwani yeye hana Maarifa yoyote juu ya hadithi sahihi. Nasi tutamthibishia uongo wake, ili wasije wakadanganyika baadhi ya watu na uongo wake; kwakusema:

1 - katika kuthibisha kuzaliwa kwa Imamu Almahdi, inabidi tuchukuwe hadithi sahihi, na wala hatupaswi kutosheka na dalili za kihistoria tu, kwa sababu kila dalili sahihi tunapaswa kuikubali, wala hatuna sababu ya kuzitangulizaa dalili za kihistoria juu ya zingine. Na mazazi ya Swahibu Alzzamani, yamethibiti kwa dalili mbali mbali sahihi. Ambazo za tosha kwa mwenye moyo salama, na kuwa tayari kuzipokea.

2 – Dalili zingine, zaweza kuwa za kiakili tu, au zilizo changanyika kati ya dalili za kiakili na za kihadithi, dalili hizo, ndizo zenye kutangulizwa kuliko dalili za kihistoria, kwa sababu baada ya kuthibiti dalili za kiakili, hakuna haja ya dalili za kihistoria zisizo za uhakika.

3 – Mazazi ya mtu hayathibiti kwa historia tu, kwani kama ingekuwa hivo, tusinge kubali mazazi ya watu wengi maarufu katika historia, kwani mazazi yao hajathibiti katika historia thabiti, na mutawatir.

4 – Watu wote wanapo taka kuthibitisha mazazi ya mtoto, hurejea kwa baba wa mtoto, hivyo kama atawathibitishia kuzaliwa kwake, hata kwa riwaya moja sahhihi, kuwa anamtoto, hatunabudi kumsadiki na kukiri. Na tutakuja kuthibisha huko mbeleni kuwa; Al-imamu Al-askari, alikiri kuwa anamtoto.

5 – Maneno ya wanazuoni na waumini wema,ya kuwa walimuona katika matukio mbali mbali, yatosha kuwa ushahidi wa kuzaaliwa kwake. Na tulitaja huko nyuma, kuwa; Almirza Alnnuri katika kitabu chake cha (Jannatu Alma’awa fi dhikri Man fazaa bi Liqaai Alhujjah), alikusanya majina khamsini na tisa, ya watu waliomuona Al-imamu Almahdi(a.s) .

Lakini pia tulitaja kutoka kwa; Asshekh Abdulwahhab Alssha’arani, katika kitabu chake cha; (Alyawaqitu wa Aljawahir), wanazuoni wengi wa kisunni, waliokiri kumuona Al-imamu Almahdi.

Je baada ya yote hayo, inafaa kwa mwenye busara, kuyakathibisha yote hayo, ukizingitia kwamba miongoni mwa wazuoni hao, ni masunni.

6 – Dalili za kihadithi, ambazo Ahamadi Alkatibu, alizitaja kuwa ni zakihistoria, ili kukadhibisha kuzaliwa kwa Al-imamu Al-mahdi, zinathibisha kuzaliwa kwa Imamu huyo, nazo twaweza kuzigawa katika makundi tofauti:

KUNDI LA KWANZA: hadithi zinazo thibisha kuwa Almahdi ni mtoto wa tisa wa Imamu Huseini(a.s) .

Amepokea Swaduqi, katika kitabu cha: Alkhiswalu wa kamalu Alddini, kwa sanadi sahihi, kutoka kwa baba yake, alisema: Alituahadithia Sa’adu Ibni Abdallah, kutoka kwa Yaaqubu Ibni Yazidi, kutoka kwa Hammaadi Ibni Isa, kutoka kwa Abdallah Ibni Maskaani, kutoka kwa Abaani Ibni Taghlibu, kutoka kwa Sulaymu Ibni Qaisi Alhilali, kutoka kwa Salmani Ibni Farisi kuwa alisema: " Siku moja niliingia kwa mtume(s.a.w.w) , mara Huseini akawa amekaa juu ya mapaja ya mtume (s.a.w.w), huku mtume akiyabusu macho na midomo yake akisema:

أنت سيِّد ابن سيِّد، أنت إمام ابن إمام أبو الأئمة، أنت حجة ابن حجة أبو حُجَج تسعة من صلبك، تاسعهم قائمهم)

"Wewe ni bwana mtoto wa bwana, wewe ni Imamu mtoto wa Imamu na baba wa maimamu, wewe ni hojjah mtoto wa hojjah na baba wa mahojjah tisa watokanao na kizazi chako, watisa wao ndie Qaaimu wao"[92] .

Pia Kulayni katika kitabu Alkafi, amepokea hadithi sahihi, kutoka kwa Ali Ibni Ibrahimu, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Abu Umairi, kutoka kwa Saidi Ibni Ghazawani, kutoka kwa Abu Baswiri, kutoka kwa Abu Jaafari(a.s) kuwa alisema:

(يكون تسعة أئمة بعد الحسين بن علي، تاسعهم قائمهم)

"Baada ya Huseini Ibni Ali(a.s) , wata kuwa maimamu ( viongozi) tisa, watisa wao ni Al-imamu al-mahdi".

Shekhe Swaduq kati Akhiswali, amepokea hadithi yenye sanadi na matini kama hiyo hiyo, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Ali ibni Ibrahimu[93] .

NATIJA: Nikwamba Sanadi za hadithi hizi ni sahihi, nazo zinathibisha kwa uwazi kabisa kuwa; Almahdi ni mtoto wa tisa wa Imamu Huseini(a.s) , na Imamu Huseini hana mtoto wa tisa anaefaa kuwa Imamu, zaidi ya Imamu Almahdi, Muhammadi Ibni Hasani Al-askari(a.s) .

KUNDI LA PILI: hadithi zinazo thibisha kuzaliwa kwa Imamu Almahdi, Muhamadi Ibni Hsani Al-askari(a.s) .

Amepokea Kulaini, katika Alkafi, kutoka kwa Huseini Ibni Muhammadi Al-ash’ari, kutoka kwa Muala Ibni Muhammadi, kutoka kwa Ahmadi Ibni Abdallah kuwa; Alisema: alitoka kwa Abu Muhamadi(a.s) , pindi alipo uliwa Zubair ( laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake) huku akisema; haya ndio malipo ya aliemfanyia ujasiri Mwenyezi Mungu kwa mawalii wake, aliekuwa akidai kuwa ataniua, na kwamba sina mtoto, Mwenyezi Mungu kamuonyesha uwezo wake. Akapata mtoto mwaka wa mia mbili khamsini na sita, aka mwita Muhammadi[94] .

Pia Kulaini alipokea katika Alkafi, kutoka kwa Ali Ibni Muhammadi, kutoka kwa Muhammadi Ibni Ali Ibni Bilali, kuwa Alisema: siku moja Abu Muhammadi alinijulisha kuhusu atakae kuwa baada yake, kabla ya kumalizika miaka miwili. Kisha kabla ya kupita siku tatu, akanijulisha pia atakae kuwa baada yake.

(و روى أيضاً في الكافي بسند صحيح، عن محمد بن يحيى، عن أحمد بن إسحاق، عن أبي هاشم الجعفري قال: قلت لأبي محمد×: جلالتك تمنعني من مسألتك، أتأذن لي أن أسألك؟ فقال: سل. قلت: يا سيّدي هل لك ولد؟ فقال: نعم. فقلت: فإن حدَثَ بِكَ حدَثٌ فأين أسأل عنه؟ فقال: بالمدينة).

" Pia Kulaini (Mungu amrehemu) katika kitabu chake cha Alkaafi, Alipokea kwa Sanadi sahihi, kutoka kwa Muhammadi ibni Yahya, kutoka kwa Ahmadi Ibni Is’haqa, kutoka kwa Abi Hashimu Aljaafari kuwa alisema: nili mwambia Abu Muhammadi(a.s) : utukufu wako unanifanya nishindwe kukuuliza, je unaniruhusu ni kuulize? Akasema: uliza. Nika muuliza: bwana wangu, je unamtoto? Akanijibu: ndio. Nikamuuliza: je kama litakukuta la kukuta, nitamtafutia wapi? Akajibu: mtafute mjini" [95] .

KUNDI LA TATU: hadithi zinazo thibisha kuwa baadhi ya watu walimuona:

Hadithi hizo ni nyingi mno, na sanadi zake ni sahihi. Miongoni mwa hadithi hizo, ni ile iliyo pokewa na Kulaini katika Alkaafi, kutoka kwa Muhammadi Ibni Abdallah na Muhammadi Ibni Yahya, kutoka kwa Abdallah Ibni Jaafar Alhimyari, kuwa alisema:

"Siku moja, nilikuwa na Alshekh Abu Amru (Mungu amrehemu) kwa Ahmadi Ibni Is’haqa, akaniashiria kuwa; ni muulize Abu Amru kunako Almahdi, nami nikamuuliza: ewe Abu Amru, hakika mimi nina taka nikuulize kitu, ambacho sina mashaka nacho, kwani imani yangu ni kuwa; Ardhi haikosi Hojja, mpaka zibakie siku arobaini kabla ya kiyama, hapo ndipo Mwenyezi Mungu ata muondosha na kufunga mlango wa toba, hivyo haito faa imani ya mtu, ambaye hakuwa ame amini kabla ya hapo. Hao ndio viumbe washari zaidi, na hao ndio watakao pata adhabu kali mno. Lakini mimi nilipenda nizidi imani, kwani hata Ibrahimu, alimuomba Mwenyezi Mungu mtukufu, Amuonyeshe vipi anavyo wa fufua wafu. Mwenyezi Mungu aksema: kwani huamini? Akasema: Hasha, lakini ili moyo wangu utue. Hakika aliniambia Abu Ali Ahamadi Ibni Is’haq, kutoka kwa Abu Alhasani(a.s) kuwa alimuuliza: kwa nani nichukue hadithi, na nani ni amiliane nae, na kukubali maneno yake? Akamjibu: Al-amri, ni mkweli kwetu, hivyo atakacho kwambieni kutoka kwangu, basi kimetoka kwangu, msikilize na umtii, kwa hakika yeye ni mkweli muaminifu. Pia aliniambia Abu Ali kuwa; alimuuliza Abu Muhammadi(a.s) swali kama hilo, akamjibu: Al-amru na mwanae ni wakweli, hivyo watakacho kufikishia kimetoka kwangu, na watakacho kwambia, kimetoka kwangu, wasikilize na uwatii, kwa hakika wao ni wakweli waaminifu. Haya ni maneno ya maimamu wa wili. Muulizaji akasema: Abu Amru baada ya kusikia maneno hayo, alisujudu na kulia, kisha akasema: uliza. Nikamuuliza: Je uliwahi kumuona Imamu Almahdi, kiongozi baada ya Abu Muhammadi(a.s) ? akajibu: ndio. Nikamwambia: limebaki swali moja. Akaniambia: uliza. Nikamuuliza: ni lipi jina lake? Akaniambi: mmekatazwa kuuliza jina lake, haya siyasemi kutoka kwangu, kwani mimi sina haki ya kuharamisha au kuhalalisha, bali nayasema haya kutoka kwake(a.s) , kwa sababu mfalme anadai kuwa Abu muhammadi Alifariki bila mtoto... hivyo kama jina lake litatajwa, wataanza kumtafuta, hivyo muogopeni Mwenyezi Mungu, na acheni kuuliza juu hya hilo" [96] .

Vile vile amepokea kuleyni katika Alkaafi, kwa Sanadi sahihi kutoka kwa Ali Ibni Muhammadi, kutoka kwa Muhammadi Ibni Ali Ibni Ibrahimu, kutoka kwa Abu Adallah Ibni Swaaleh kuwa: hakika yeye alimuona Almahdi(a.s) Mkkah, watu wakitufu katika hali ya kusukumana, nae asema: hivyo sivyo walivyo amrishwa[97] .

KUNDI LA NNE: hadithi zisemazo kuwa atatoweka, hivyo watu kushakia kuzaliwa kwake:

Amepokea kulayni katika Usulu Alkaafi, kwa Sanadi sahihi, kutoka kwa Ali Ibni Ibrahimu, kutoka kwa Alhasani Ibni Musa Alkhasshaab, kutoka kwa Abdallah Ibni Musa, kutoka kwa Abdallah Ibni Bukayri, kutoka kwa Zurara kuwa alisema: nili msikia Abu Abdallah akisema: hakika Almahdi atatoweka kabla ya kudhihiri. Akasema: nikamuuliza: kwa nini? Akanijibu: kwahofia kuuliwa. Kisha akasema: ewe zurara, huyo ndie Almuntadhwar, ambaye yatashukiwa mazazi yake. Kuna ambao watasema: baba yake alifariki bila kuacha mtoto. Na kuna wengine watasema: baba yake alifariki kabla ya kuzaliwa. Na miongoni mwao kuna ambao watasema: alizaliwa miaka miwili kabla ya kufariki baba yake. Yeye ndie Almuntadhwar, isipo kuwa Mwenyezi Mungu atawatahini Mashia, hapo ndipo watajulikana wakweli...[98] .

Pia katika Usulu Alkaafi, kwa sanadi sahihi, kutoka kwa Ibni Yahya, kuto kwa Muhammadi Ibni Huseini, kutoka kwa Ibni Mahbub, kuto kwa Is’haaq Ibni Ammar, alisema kuwa: alisema Abu Abdallah(a.s) : Alqaaimu atatoweka mara mbili: mara ya kwanza; atachukua muda mfupi, na mara nyingine; atachukua muda mrefu. Kutoweka kwa kwanza, hawata fahamu isipo kuwa Mshia wake maalumu. Na kutoweka kwa pili, hawata fahamu sehemu yake isipo kuwa wafuasi wake maalumu[99] .

Kundi la sita: hadithi zinazo thibitisha kuwa; Almahdi ndiye Alhujjah Ibni Alhasani Al-askari.

Amepokea Swaduuq katika (Kamaalu Alddini), kwa Sanadi Sahihi, kutoka kwa Ibni Alhasani (Mungu amrehem), kuwa alisema: alituambia Saadi Ibni Abdallah, alisema kuwa: alituambia Abu Jaafar Ibni Ahmadi A-alwi, kutoka kwa Abu Hashimu Daudi Ibni Alqaasimu Aljaafar, Alisema kuwa: Nilimsikia Abu Alhasani Swahibu Al-askari(a.s) akisema:

"kiongozi baada yangu ni mwanangu Alhasani... hamta muona, na hamruhusiwi kumuita kwa jina lake. Nika muuliza: tumwite je? Akanijubu: mwiteni: Alhujjah min Aali Muhammadi (s.a.w.w) " [100] .

Kutokana na yote yaliyo tangulia, tunaona kuwa: hakuna njia zaidi ya kuhukumu kuwa; Al-imamu Muhammadi Ibni Alhasani Al-askari, alisha zaliwa. Hayo ni kwa mujibu wa hadithi Sahihi tulizo zitaja baadhi yake. Ambazo zime pokewa katika vitabu vya hadithi, ambavyo ni maarufu kwa mashia, kama vile Alkafi, Alttahadhibu, Al-istibswari, na Man La Yahbwuruhu Alfaqihi.

Hayo yote ni kwa mwenye kuzi amini hadithi za Ahlul Bayti(a.s) . Lakini pia akatumia njia sahihi katika kusahihisha hadithi, kama alivyo dai Ahmadi Alkatibu. Na kuzikanusha hadithi hizo, ni ubishi wa bili ushahidi.