NAHJUL BALAGHA
JUZUU YA PILI
MTARJUMI: HARUNA PINGILI
Kitabu kilichoko mkononi mwako ni tarjumi kutoka lugha ya Kiarabu ya kitabu maarufu katika ulimwengu wa Kiislamu, Nahju 'l-Balaghah. Kitabu hiki kitachapishwa katika juzuu mbili, na hii uliyo nayo mkononi ni juzuu ya pili.
Nahju 'l-Balaghah ni mkusanyiko wa khutba, barua na maelekezo ya Imam Ali (a.s) Mengi yamesemwa kuhusu ubora na ufasaha wa maneno yaliyomo katika khutba na harua hizo. Kwa ufupi, Nahju 'l-Balaghah ni kilele cha ufasaha.
Mbali na mawaidha yaliyomo humo, msomaji atafaidika na lugha iliyomo katika khutba na barua hizo, hususan kwa wasomaji wa Kiarabu. Inasemekana kwamba baada ya Qur'ani Tukufu na maneno ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) , Nahju 'l-Balaghah ndiyo inayofuatia kwa ufasaha na ubora wa maneno.
Si rahisi kwa msomaji wa Kiswahili kupata ladha ileile aipatayo msomaji wa Kiarabu kutokana na ukweli kwamba lugha ya Kiarabu ni pana mno na msamiati wake ni mkubwa. Pamoja na hayo, mtarjumi wetu amejitahidi sana kuleta mafhumu ya Kiarabu kwenye lugha ya Kiswahili bila kupoteza maana.
Kwa vile kitabu hiki ni muhimu sana, tumeona ni bora tukichapishe katika lugha ya Kiswahili ili Waislamu na wasomaji wetu wazungumzao Kiswahili wapate kunufaika na yaliyomo humo. Hivyo, ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki kitakkuwa ni chenye manufaa sana kwao na katika jamii yetu.
Tunamshukuru ndugu yetu, Sheikh Haruna Pingili kwa kukubali jukumu hili kukitarjumi kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiri- ki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.