50%

MOTO NA PEPO

PEPONI NA MOTONI

KITABU HIKI KIMEKUSANYWA NA KUTARJUMIWA NA: AMIRALY M. H. DATOO

1. PEPONI

UTANGULIZI

Ingawaje Qur'an Tukufu inatujulisha vya kutosha kuhusu Pepo (Pepo) na Jahannam (Motoni), vile vile tunapata habari zaidi kutoka Ahadith Qudsi zilizoletwa na Malaika Jibraili(a.s) kwa Mtume Muhammad(s.a.w.w) ambaye ananakiliwa na Imam Ali(a.s) na Maimamu Kumi na moja(a.s) waliobakia. Mtume(s.a.w.w) wakati wa Me'raj aliweza kuona na kutembea Peponi, kula matunda ndani mwake na kuangalia yale yaliyokuwamo. Vile vile alitembelea jahannam au Motoni ambamo aliweza kujionea vile wahalifu walivyokuwa wakiadhibiwa kwa madhambi yao.

Al Tirmidhi na Abu Daud wananakili Ahadith Qudsi ifuatayo kutokea Mtume Muhammad(s.a.w.w) :

Allah swt alipoumba Pepo na Jahannam, alimtuma Malaika Jibraili(a.s) kwenda Pepo, akisema, "Angalia ndani mwake kile nilichokiwatengenezea wakazi wa humo." Malaika Jibraili(a.s) alikwenda akaangalia vizuri na kwa makini, na aliporudi kwa Allah swt alisema, "Kwa utukufu wako naapa kuwa hakuna atakayeisikia illa atatamani kuingia humo." Kwa hayo Allah swt alizungushia vizuizi na magumu mbalimbali, na alimwamrisha Malaika Jibraili akaangalie vizuizi na magumu yaliyozungushiwa. Malaika Jibraili(a.s) aliporudi baada ya kuyaangalia kwa makini, alimwambia Allah swt, "Kwa Utukufu wako, Naapa na kuhofu kuwa hakuna hata mtu mmoja ambaye ataweza kuingia ndani mwake." Allah swt alimwambia, "Sasa nenda kaangalie Jahannam na yale niliyowaandalia wakazi wake." Malaika Jibraili(a.s) alikwenda na kuona tabaka moja baada ya nyingine. Aliporejea akasema,"Kwa utukufu wako, hakuna hata mtu mmoja atakayetamani kuingia ndani humo atakapoisikia." Hapo Allah swt aliamrisha kuzungushiwa vivutio na vipotoshavyo, na kumwamuru Jibraili(a.s) kurudi kuangalia tena. Aliporudi Jibraili(a.s) alisema, "Kwa kiapo cha Utukufu Wako! Hakika ninahofu kuwa hakuna mtu atakayeweza kujiepusha kuingia ndani humo."

Sasa tujaribu kuchunguza na kuelewa zaidi kuhusu sehemu hizi mbili: Pepo na Jahannam.