UKWELI WA SHIA ITHNA ASHARIYA
KIMEANDIKWA NA: DR. ‘ASAD WAHID AL-QAASIM.
KIMEATAFSIRIWA NA: ABDUL KARIM J. NKUSUI
Kitabu kilichoko mikononi mwako, ni tarjuma ya kitabu cha Kiarabu, kwa jina la: Haqiqat Shi’a Ithna-Asahariyyah kilichoandikwa na, Dr. ‘Asad Wahid Al-Qaasim.
Kitabu hiki ni utafiti wa kina uliofanywa na mwanachuoni huyu mahiri, kuhusu mitafaruku iliyotokea katika Uislamu na baina ya Waislamu, kuanzia wakati wa Mtukufu Mtume(s . a . w . w) , na mara tu baada ya kufariki kwake hadi sasa. Katika utafiti wake huu, ameiangalia sana historia ya Kiislamu kama ilivyohifadhiwa katika vitabu vya historia vilivyo andikwa na wanachuoni wa Kiislamu wa kuaminika wa madhehebu zote za Kiislamu zijulikanazo. Katika kujadili masuala mbali mbali yenye utata, huwa ametumia dalili, hoja, akili na elimu.
KUHUSU MTUNGAJI
Mtungaji ni mtafiti katika misingi ya ukweli, mwenye kujitahidi jitihada kubwa kabisa katika njia ya kuufikia, hadi Allah (s.w.t.) akamwongoa katika njia ya sawa, “Na wale ambao wamejitahidi katika njia yetu. tutawaongoa katika njia zetu.”
Amezaliwa katika kijiji cha Dairul-Ghusun katika ukingo wa Magharibi, katika nchi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Amehitimu masomo yake ya Sekondari, kisha akaenda Jordan Na akapata Diploma ya Uhandisi, kisha akaenda Ufilipino na akapata Shahada ya kwanza ya Uhandisi kisha akapata Shahada ya pili katika Idara ya ujenzi. Na hivi sasa amepata shahada ya Udaktari katika Idara ya utawala wa serikali baada ya kumaliza utafiti wake (wa “Islamic public Administration” “Mfumo wa utawala wa Kiislam”).