20%

BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE

KIMEANDIKWA NA: MUHAMMAD IBRAHIM EL-QAZWINIY

Nafasi Ya Sinema Na Picha Za Video Katika Uharibifu Wa Jamii

Sinema na picha za video zinachangia kwa kiwango kikubwa katika kuharibu mwelekeo sahihi na wa kweli kwa vijana kutokana na kuonesha filamu zinazohusu mambo ambayo ni ya siri baina ya mke na mume. Isitoshe sinema hizi huonesha maumbile ya shemu hizi mbili za siri wazi wazi kiasi kwamba, hupanda mbegu mbaya kifikra kati ya wasichana na wavulana. Si hivyo tu bali sinema hizi zinawaondolea vijana wetu aibu machoni mwao na kuwapokonya imani, kisha kuwaingiza kwenye matendo maovu na machafu ambayo yanawafanya wasahau utamaduni wao wa Kiislamu na kuwafanya waige wanayoyaona humo.

Ni mara nyingi sinema na picha za video zimekuwa zikitumiwa kupotosha jamii zetu, kwa kuonesha miili iliyo uchi ya wanawake.

Wacheza sinema huthubutu kudhihiri mbele ya watazamaji kwa kitendo ambacho kwa kweli ni aibu na ni fedheha kwa mwanadamu kukitenda hadharani, na hiyo ni tabia ya kinyama kabisa. Kwa hali hiyo basi, sinema zinatangaza uchafu huu wazi wazi na kuupigia kampeni huu kama kwamba ni kitendo kizuri. Mwenyezi Mungu anajua sana idadi ya maovu haya na matukio yanayotokea kutokana na jamii zetu kuendelea kuoneshwa filamu hizi chafu. Katika kuonesha madhara ya filamu hizi, kuna kijana mmoja wa kiume alikwenda kuangalia filamu zinazohusu mapenzi kati ya mume na mke. Baada ya kuangalia onesho hilo ambalo liliyateka mawazo yake na alirudi nyumbani kwao haraka sana. Alipofika tu alimkamata dada yake aliyekuwa kalala na kumtenda kitendo kichafu huku akiigiza namna ya kitendo hicho kama alivyoona katika filamu. Kitendo hiki kilisababisha maumivu makali kwa nduguye huyu aliyekuwa mdogo kwa umri, maumivu ambayo baadaye yalisababisha kifo cha msichana huyu[17] .

Bila shaka ndugu msomaji kwa mfano huu mmoja tu, unaona ni jinsi gani sinema zimekuwa ni nyenzo kubwa ya kueneza uchafu ndani ya jamii zetu. Kwa hiyo basi, sinema hizi ni vituo vikubwa wanavyovitumia wakoloni wa magharibi katika kuwavua Hijabu mabinti zetu na hatimaye kuwasukumiza kwenye shimo la maovu. Vile vile vituo wanavyotumia kugeuza vijana wetu kuwa watumwa wa matamanio yanayohusu mambo ya jinsiya na kuwafanya kuwa wasomi wa maraha na upuuzi huo. Sasa hivi imefikia mahali ambapo vijana wetu hakuna wanachokiwaza isipokuwa starehe tu, hawafikirii tena suala la maendeleo au utalaamu wa aina mbali mbali.

Hizi ni siasa za mataifa hayo makubwa, na lengo lao ni kuona vijana wetu na mataifa yetu hayajikwamui kiuchumi wala kisiasa, ili maendeleo ya viwanda, uchumi na elimu viendelee kuwa chini ya milki yao. Kamwe hawataridhika mpaka watuone sisi Waislammu tunabakia katika unyonge na udhalili, tukiendelea kuwategemea wao kwa kila mambo makubwa na hata madogo, na wao waendelee kuwa watawala wetu. Kwa hakika wametunyooshea panga zao mbele ya nyuso zetu na wametufanya kuwa ni vinyago vyao na wanatuchezea na kututumia namna wapendavyo.

Mpaka hapa mimi nauona umuhimu wa kuelekeza tena usemi wangu kwa Waislamu wote wanaohisi wajibu na jukumu katika dini. Mimi nawaambia kwamba, "Zipigeni vita sana sana hizi sinema za X[18] na wawakemee watu wasiziangalie. Si hivyo tu bali wanapaswa kuwatahadharisha watu, kwani kujiingiza katika mambo hayo licha ya kuwa ni kumuasi Mwenyezi Mungu, bali hali hii inatumikia maslahi ya maadui wa Uislamu na kuharibu mwenendo wa vijana wa Kiislamu kwa kutumia kigezo cha utaalamu na maendeleo.

Madhara Ya Kuchanganyika Wanaume Na Wanawake

Mchanganyiko unaokusudiwa hapa ni ule wa kukaa pamoja wanaume na wanawake wakawa wanatazamana ana kwa ana bila kuwepo kizuizi baina yao kitakacho tenganisha pande mbili hizi.

Kutokana na maumbile ya wanaadamu yalivyo, sheria ya KiIslamu haikubaliani na kitendo hiki cha kuchanganyika wanawake na wanaume, na hapana shaka kwamba Mwenyezi Mungu anachukizwa na jambo hili. Kwa nini basi jambo hili liwe baya?

1. Ni kuvunja moja katika sheria za Kiislamu (Hijabu) na ni kukaribisha maovu katika jamii.

2. Jambo hili huandaa na kurahisisha njia za kupatikana mahusiano ya kijinsiya baina ya pande mbili hizi kinyume na utaratibu uliowekwa kisheria.

3. Jambo hili huwa ndiyo chanzo na sababu ya kuharibu familia na kuzitenganisha na ni kivutio kikubwa cha maovu ndani ya jamii.

4. Jambo hili linasababisha misiba na majonzi, pia linaleta uharibifu mkubwa kati ya pande mbili husika.

Kwa hiyo mchanganyiko kati ya wanaume na wanawake ni kirusi chenye maradhi hatari yanayotishia usalama na mwenendo wa familia, kiasi kwamba tunaweza kuyafananisha na maradhi ya kansa ambayo mgonjwa huwa hapati nafuu isipokuwa kwa kuikata shemu iliyopatwa na ugonjwa huo na kukiondoa kiini cha ugonjwa. Katika nchi au jamii zilizoruhusu mchanganyiko huu, hapana shaka kwamba zimechangia sehemu kubwa ya ongezeko la maovu na kufikia idadi inayotisha hasa katika mashule na vyuo vikuu ambako wasichana na wavulana wanachangaywa pamoja utadhani ni viumbe wenye jinsi ya moja. Matokeo ya mchanganyiko huu ni kugeuka kwa mashule haya na vyuo hivi kuwa vituo vya mafunzo ya uhuni na mambo machafu ambapo lengo lake lilikuwa ni kupafanya kuwa mahali pa kujifunza elimu. Yote haya yanakuja kwa sababu ya kukosekana kwa sitara au kizuwizi cha kuzitenganisha jinsiya hizi mbili.

Katika ripoti moja iliyotolewa na Jaji mmoja wa Kimarekani anasema: "Asilimia 45% ya wasichana wanaosoma katika shule za mchanganyiko hupoteza bikra zao kabla ya kutoka shuleni, na asilimia hii huzidi kadri wasichana wanavyoendelea katika masomo ya juu." Huko Uingereza wasichana wamekuwa wakiandaliwa kutembea na vidonge vya kuzuwiya mimba, na kwamba asilimia 80% ya wasichana hutembea na vidonge hivyo katika mikoba yao. Hii ni dalili ya wazi inayotuonesha kwamba, wasichana hao huwa wako tayari wakati wowote ule kutenda kitendo kichafu kwa kuwa kinga wanayo. Wasichana hawa wanayafanya haya kukwepa matokeo mazito yanayoweza kuwakuta ndani ya uchafu huo wanaoutenda[19] . Lakini je hivi kweli ni sahihi kumuacha msichana akawa katika mazingira kama haya ndani ya jamii hasa ya Kiislamu?

Baada ya maelezo haya bila shaka ina dhihiri wazi hekima kubwa iliyomo katika Uislamu katika kupiga marufuku michanganyiko baina ya wanaume na wanawake. Hapana shaka kabisa kwamba, Uislamu lengo lake ni kutaka kuiepusha jamii kutokana na hatari tulizozitaja hapo kabla. Ndiyo maana umeharamisha mchanganyiko kati ya wanaume na wanawake katika sehemu zote, kama vile mashuleni, vyuoni, katika sehemu za sherehe, na kwa ujumla popote katika jamii mchanganyiko kati ya wanaume na wanawake hauruhusiwi.

Yote haya makusudio ni kuihifadhi jamii kutokana na maovu yanayozaliwa na michanganyiko. Na ama hali ya mikusanyiko ya wanaume na wanawake tunayoiona katika msimu wa Hija na katika maeneo matakatifu na pia ndani ya kumbi za Huseiniyyah, mikusanyiko kama hiyo haikuharamishwa hasa kwa kuwa wanawake wanaohudhuria ndani ya maeneo hayo huwa wako katika hali ya kujisitri kama sheria inavyowataka wajisitri.

Uislamu Siyo Dini Ya Nadharia

Mara nyingi tunasoma katika baadhi ya magazeti kwamba, baadhi ya watu waliohadaika na wasiojuwa chochote kuhusu Uislamu, eti wanajaribu kutoa fikra zao katika kukosoa baadhi ya kanuni za sheria ya Kiislamu. Miongoni mwa kanuni ambazo wamekuwa wakijaribu kuzikosoa kwa kutumia kalamu zao ni hili vazi la Hijabu. Waandikapo husema: "Mimi sioni umuhimu wa Hijabu, kwani Hijabu katika maoni yangu sio lazima kwa kuwa inarudisha nyuma maendeleo." Au hupata wakasema kuwa: "Kuna ubaya gani wanaume na wanawake kuchanganyika pamoja?" Na mengine mengi wanasema lakini kifupi ni hayo. Sisi tunawajibika kuwaambia watu hawa na wengine mfano wa hao kwamba: "Ninyi ni kina nani? Ninyi ni kina nani hasa mpaka mnathubutu kutoa maoni yenu dhidi ya desturi na mila ya Mbinguni? Na mna utukufu gani mbele ya maamuzi ya MwenyeziMungu na sheria nzima ya Kiislamu? Na je Uislamu ni dini ya fikra za kinadharia mpaka mumediriki kuusemea kwamba mimi naona kadhaa, au mtazamo wangu katika sheria ya Kiislamu naona hivi au vile.? Kisha nawauliza hawa wanaosema maneno haya: "Je, ninyi kweli ni Waislamu? Ikiwa wao ni Waislamu wanawajibika kuwa watiifu katika maamrisho ya Mwenyezi Mungu na makatazo yake, pia washikamane na sheria za Kiislamu ambazo miongoni mwake ni Hijabu. Na kama ninyi siyo Waislamu basi, hamna haki ya kuingilia mambo ya Kiislamu, wala hamna haki ya kutoa maoni yenu potofu mbele ya Umma wa Kiislamu.

Mpaka hapa ndugu msomaji nashangazwa na ujeuri wa watu hawa dhidi ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na ni kwa misingi gani viumbe hawa dhaifu wamejasirika na kufikia kiasi cha kukosoa hukmu na kanuni za Mwenyezi Mungu? Je wanasahau kwamba Mwenyezi Mungu anasema katika Sura Al-Maidah katika

وَمَنْ لَمْ يَحْكُمْ بِمَا أَنْزَلَ اللَّهُ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ

Aya tatu mfululizo: "Na wale wasiyohukumu ( kwa sheria) aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu basi watu hao ni makafiri, madhalimu, mafasiki [20] .

Watu hawa mbele ya Mwenyezi Mungu watabeba mzigo mzito kwa makosa yao ya kuhamasisha watu kuvunja amri za Mwenyezi Mungu na kutenda machafu yaliyo katazwa. Malipo (adhabu) yao pia ni mazito kutokana na maneno yao hayo, kwa adhabu kali watakayoadhibiwa kutokana na wao kuunga mkono maasi na kuyatia nguvu yatendwe.

Mimi naamini kuwa, watu hawa hawasemi kutoka katika nafsi zao, bali wao wanatumwa na maadui wa Uislamu wanaoupiga vita Uislamu kupitia nyuma ya pazia. Lengo lao ni kuiangamiza maana nzima ya Uiislamu, na kisha kuwapotosha wasichana na wavulana wa Kiislamu. Jambo la kusikitisha na kuhuzunisha ni kwamba, kauli kama hizi zimekuwa zikirudiwa mara kwa mara na katika nyakati tofauti, ima ndani ya magazeti na majarida na au katika mikutano mbali mbali. Kuna lugha nyingi zinazotumika katika kampeni hii ikiwemo lugha ya Kiarabu ambayo inawaunganisha Waislamu wa dunia nzima kama lugha ya dini yao.

Yote haya ndugu Waislamu, ni majaribio ya makusudi kabisa yenye lengo la kuivuruga na kuipoteza jamii takatifu ya Kiislamu. Kinachotakiwa kwa Waislamu wenye uchungu na dini yao ni kunyanyuka na kuyapinga magazeti haya kwa kuwa yenyewe ndiyo sauti ya vita vya kuutokomeza Uislamu na Waislamu. Kwa hakika wajibu wa kisheria unamtaka kila Mwislamu kupambana na majaribio haya hatari kwa uwezo wake wote kinadharia na kivitendo, hadi lengo la maadui hawa lisitimizwe katika nchi zetu tukufu za Kiislamu na jamii za Kiislamu popote zilipo duniani.

Kadhalika kukabiliana na maadui hawa dhidi ya njama zao za kutaka kugeuza nchi zetu kuwa ni mapori ya wanyama kufuatia mila zao wanazokusudia kuturithisha.Watu hawa madhalimu, katika nchi zao wamebadilika kutoka katika mila ya wanaadamu na wamekuwa na tabia za wanyama, kiasi kwamba mwanamke na mwanaume wanakidhi matamanio yao mabarabarani kama wafanyavyo wanyama bila kuwa na hisiya zozote za kuona haya wala kuogopa kwamba wao ni viumbe teule na watakatifu kwa kuumbwa kwao kama wanaadamu.

Vipi Wamefaulu Kutupotosha ?

Sasa tuangalie namna gani watu hawa wamefanikiwa kutupotosha, kwa kuwavua binti zetu na wake zetu mavazi ya Kiislamu. Pia ni kwa vipi wamefaulu kututeka kwa kupitia anuani ya kutetea uhuru wa mwanamke. Ili kupata ufumbuzi wa suala hili hatuna budi kufanya ziyara ya uchunguzi katika nchi za magharibi na kuiangalia jamii yao, na ni vema pia kufuatilia magazeti yao na majarida ili tuyaone mazingira mabaya wanayoishi wanawake wasio na Hijabu huko kwao. Kwa watu wa magharibi mambo hayaishii kwenye kukosa Hijabu na kutembea kichwa wazi na miundi nje basi. Bali hali yao inakwenda mbele zaidi kiasi kwamba kifua nacho huwa wazi, na wanawake hao kadhalika huvaa nguo nyepesi inayodhihirisha rangi ya mwili hadi kufikia kufanana na mtu aliye uchi kabisa.

Matokeo ya mavazi haya ni umalaya au kutekwa nyara na baadaye kubebeshwa mimba za haramu kisha kuingia katika kufanya mauaji pindi wanapotaka kuzitoa mimba hizo. Linalojitokeza hapa ni kudhulumu kiumbe hicho kinachotolewa kwa nguvu au muhusika kukumbwa na kifo wakati wa zoezi hilo.

Hali hii ndiyo iliyoko kwenye nchi zinazoitwa zimeendelea. Nchi zetu za Kiislamu na Waislamu kwa jumla kwa sasa wanakabiliwa na tishio la hatari hii inayokuja kwa kasi ya ajabu kutoka kwenye hizo nchi za mashariki na magharibi. Kinachotakiwa kwa Waislamu ni kuwa na tahadhari kubwa na kuikabili kasi hii ya hatari inayokuja kutoka katika nchi hizo za mashariki na magharibi. Kwa hakika wameeneza uovu wao katika jamii yetu chini ya kivuli cha utaalamu na elimu.

Idadi kubwa ya makosa ya jinai yanayotokea katika nchi zinazodaiwa kuwa zimeendelea ni mengi mno, ukilinganisha na matukio kama hayo yanayotokea katika nchi zetu za Kiislamu. Tofauti hii ni kwa sababu Uislamu unahimiza na kutilia mkazo watu wawe na maadili mema, tabia nzuri na waepukane na kila tabia chafu. Pamoja na hali hii ambayo kwa kiasi fulani inaonesha tofauti baina ya nchi za Kiislamu na hizo za magharibi, Ni lazima kwa Waislamu kuchukua tahadhari, wasihadaike na hali waliyonayo, kwani hatari inakuja na shari zinaandaliwa dhidi yao, na ni wajibu wa kila Mwislamu kuwa na tahadhari. Yafuatayo ni baadhi ya mambo yanayotendeka katika nchi ambazo ndizo zinazoongoza katika kupiga vita utamaduni wa Kiislamu.

1. Nchini Uingereza peke yake karibu filamu 10 zinazohusu mambo machafu hukamilika kutengenezwa kila wiki na kutumwa nchi za nje. Kwa hali hii basi kila mwaka filamu zisizopungua 500 hutengenezwa nchini Uingereza na zote ni za kuonesha mambo ya aibu tupu na uchafu ambao jamii yetu inapotea na kuangamia kutokana na yaliyomo ndani ya filamu hizi.

2. Mwaka 1961 polisi wa Uingereza walijaribu kuwaangamiza wanawake wapatao laki moja, ambao kazi yao ilikuwa umalaya na machafu mengineyo, lakini baadaye walitangaza kushindwa kwa jaribio hilo[21] .

3. Mjini Rome kuna majumba yapatayo mia tano ya malaya, humo ndani mna maelfu ya wanawake ambao kazi yao ni kusubiri wanaume[22] .

Gazeti la " The Gurdian" liliandika kwamba takwimu za polisi zinaonesha kuwa, makosa ya jinai ya kubaka yanaongezeka mwaka hadi mwaka. Katika mji wa Washington peke yake kila baada ya dakika kumi na tano huwa kuna tukio la kubaka.

Na katika mji mkuu wa Ungereza (London) yalitokea matukio 2095 ya kubaka wanawake na wasichana mwaka 1970 peke yake. Haya ni machache katika mengi ambayo tungeweza kukuorodheshea.