MAISHA YA IMAM HASANI
AL ASKARI (A.S)
Uislamu haukuwa mkusanyo wa mafundisho ya kanuni tu. Uliletwa ili uwe kitu cha kutumika kutatulia matatizo ambayo yanawatokea watu katika maisha yao ya kila siku. Uislamu hauweki mawazo ya kielimu tu ambayo hayana kiini cha maisha halisi, bali hutoa mifano bora ya maisha ya Uchamungu na maisha maizuri.
Ni kweli kwamba maisha ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) hayangeweza kuchukua hali zote zitokanazo na maisha ya binadamu. Kwa hilo baada ya yeye, walifuata makhalifa wake kumi na wawili ambao walikuwa mfano mzuri wa maisha ya Uchamungu, na kwa vile iliwabidi waishi katika hali za namna mbalimbali, walionyesha namna ya mtu awezavyo kuishi katika nyakati za amani au vita. Hapa tunaona kwa kifupi maelezo ya maisha ya Imamu Hasan Askari,(a.s) Khalifa wa kumi na moja wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) .
Jina lake ni Hasan. 'Kunyat' (Jina la heshima) ni Abu Muhammad.
Na kwa kuwa aliishi katika sehemu ya jiji la Samarrah iliyoitwa Askari, jina lake lililojulikana zaidi ni lile la Askari.
Baba yake alikuwa Imamu Ali Naqi(a.s) . Na mama yake ni Bibi Salil Khatun ambaye alikuwa mfano wa utawa wa hali ya juu, Uchamungu, Utakatifu na Ukarimu.
Alizaliwa tarehe 10 ya Rabi-ul-Thani (Mfunguo Saba) mnamo mwaka 232 Hijiriya huko Madina.
Alikaa na baba yake kwa muda usio pungua miaka kumi na moja katika sehemu ya kwao. Muda huu unaweza kuitwa muda wa amani. Baada ya hapo ilimbidi Ali Naqi(a.s) aende Iraq na Imamu Hasan Askari(a.s) alifika Samarrah na baba yake baada ya taabu zote za safari ndefu. Huko aliishi na baba yake jela chini ya uchunguzi na wakati mwingine aliishi katika uhuru kidogo. Lakini kila wakati aliishi na baba yake akijifunza kwa makini tabia yake katika hali za kila aina ambayo, pamoja na Mwanga alioupewa na Mwenyezi Mungu, alikuwa kamili kabisa kwa kazi ambazo alitazamiwa kuzishika.
Mnamo mwaka wa 254 Hijiriya, Imamu Ali Naqi(a.s) alifariki wakati Imamu Hasan(a.s) akiwa na umri wa miaka 22. Miezi minne kabla hajafa, Imamu Ali Naqi(a.s) aliutangaza Uimamu wa mwanawe na aliwaita wafuasi wake waje kushuhudia.
Mu'tazz Billah Abbasi alikuwa Mfalme wakati Imamu Hasan Askari(a.s) alipopata Uimamu. Baada ya Mu'tazz kupinduliwa, Muhtadi alitawala kwa muda wa miezi kumi na moja na siku chache naye alirithiwa na Mu'tamad. Hakuna hata mmoja wa hao Wafalme aliyemwacha Imamu(a.s) akae kwa amani. lngawaje Serikali ya ukoo wa Bani Abbas ilikuwa katika machafuko, licha ya matatizo hayo yote wote waliona afadhali kumwacha Imamu(a.s) abaki humo jela. Sababu muhimu ilikuwa ni ile hadithi ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) ibashiriyo kuwa atafuatiwa na Maimamu kumi na wawili, wa mwisho wao akiwa ni Mahdi Akhirul Zaman (Imamu wa Zama hizi) na Qaimu Ali Muhammad (endelezo la Ukoo wa Mtukufu Mtumes.a.w.w ). Hadithi hii ilienea kote katika ulimwengu wa Kiislamu.
Watawala wa ukoo wa Bani Abbas walijua sana kuwa hao ndiyo makhalifa halali wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) na katika hao Imamu Hasan Askari(a.s) alikuwa wa kumi na moja, kwa hiyo mwanawe atakuwa ni kutimia kwa ubashiri wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) . Kwa hiyo kila wakati walikuwa wakizuia kuwepo kwa Khalifa wake. Ndiyo maana hawakuacha kumchunguza Imamu Hasan Askari(a.s) kama ilivyokuwa kwa baba yake, hivyo waliona kuwa ni lazima kumfungia katika jela ya peke yake. Lilikuwa jambo tofauti kabisa wakati mapinduzi ya kisiasa yameacha pengo katika nyakati za ufungwa wake, Iakini kila Mtawala aliyetawala alifuata shauri la watawala wa kabla yake la kumfunga Imamu tena. Hivyo karibuni muda wake mfupi wote wa Uimamu aliumalizia jela. Kuchungwa kwake kulifikia kilele wakati wa utawala wa Mu'tamad, ingawaje naye, kama wale wengine wa nyuma wote, alikijua vizuri cheo cha Imamu(a.s) . Kwani, wakati mmoja njaa iliingia nchini na mtawa mmoja wa Kikristo alidai kuwa anaweza kufanya mvua inyeshe na alifaulu kufanya hivyo. Hivyo kulikuwepo mlegolego katika imani ya Waislamu. Mu'tamad alihofia kuwa serikali yake itaangushwa hivyo aIimwita Imamu Hasan Askari(a.s) kutoka jela. Imamu(a.s) alimwomba mfalme amruhusu mtawa huyo kuja hadharani na kufanya muujiza wake mbele ya Imamu mwenyewe na alimtuma mtu fulani amwendee haraka yule mtawa wakati alipoinua mikono yake kuomba mvua na kuchukua cho chote kile alichokuwa nacho mikononi mwake. Wakati mambo haya yanafanika yule mtawa alionekana akionyesha mfupa kwenye jua na mvua zilianza kunyesha. Imamu alimwambia kuwa mfupa ule ulitoka katika mwili wa Mtume fulani na kwamba ilikuwa ni tabia ya mifupa va Mitume kuwa kama inaonyeshwa kwenye jua, mawingu yatatanda. Kisha Imamu aliufunika ule mfupa na yeye mwenyewe aliomba mvua inyeshe na ikanyesha kwa wingi sana.
Maimamu wa Ukoo wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) wakati wote walifanya kazi zao wakiwa Maimamu katika hali zote. Imamu Hasan Askari(a.s) alikuwa akiishi katika vizuizi vya namna nyingi sana kwamba ilikuwa vigumu kwa wenye kupenda kujifunza kutoka kwa Imamu kuweza kuonana naye. Hivyo Imamu aliwateua watu wenye kuaminika kutokana na uaminifu wao kuelewa kwao na elimu yao. Wajumbe hawa waliwaongoza watu kwa kadiri ya uwezo wao na kama palitokea tatizo lililokuwa zaidi ya uwezo wao basi walingojea mpaka wapate nafasi ya kumuona Imamu ili awape majibu na wao wawape watu. Mpango huu haukukataliwa sana na serikali kwa sababu ulihitaji mtu mmoja mmoja kwenda kumwona.
Wajumbe hawa walifanya kazi nyingine zaidi. Khums (moja ifananayo na Zaka) ilikuwa inatolewa na wale waliokiri kuwa Imamu alikuwa mwakilishi wa serikali ya Mwenyezi Mungu na kupewa hao wajumbe ambao waliitumia kama alivyoagiza Imamu. Watu hawa walipata jaribio gumu kweli, kwani wapelelezi wa serikali ya ukoo wa Bani Abbas walikuwa wakipeleleza shughuli zao. Hivyo Bwana Uthman bin Sa'id na mwanawe Abu Ja'afar Muhammad bin Uthman ambao walikuwa wajumbe mashuhuri wa Imamu walifungua duka kubwa la mafuta na manukato mjini Baghdad walikokuwa wakikaa ili kuepukana na kutiliwa wasiwasi na watu waliokwenda kumwona Imamu(a.s) . Kwa hiyo licha ya shari ya serikali, kazi ya Uislamu ilikuwa inaendelea.
Maisha yake yalikuwa ni yale ya wenzake wa Ukoo wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) . Alikuwa wa pekee katika upole ustahimilivu, ukarimu, uvumilivu, huruma na Kumuabudu Mungu kwake kulifanyika kiasi ambacho, hata wakati alipokuwa kafungwa katika kizuizi kikali sana kila Mu'tamad alipoulizia habari zake, aliambiwa kuwa Imamu alikuwa aki funga mchana na usiku kucha akisali na alikuwa hasemi neno ila maneno ya ibada tu.
Ingawaje Imamu(a.s) alikuwa na uhuru mdogo sana hata hivyo ilipowezekana watu walikwenda kumwona na kutoa hamu yao ya kujifunza na walirudi wakiwa wametosheka kabisa.
Maadili yake na tabia zake viliwavutia watu wote. Bwana Ahmad bin Khazan aliyekuwa mwangalizi mkuu wa zaka, khums, sadaka, n.k., katika Mji wa Qum (nchini Iran), kila walipotajwa mbele yake Masayyid wa Alawi (wa ukoo wa Alia.s ), alisema kuwa alikuwa hajapata kuona mtu mwingine mwenye tabia nzuri kama za Imamu Hasan Askari(a.s) au Mchamungu na mwenye kumwabudu Mungu, mpole, anayeheshimiwa,mwenye kustahili heshima au anayefikiriwa kuwa yu astahili kuheshimiwa sana.
Alipofariki Imamu Ali Naqi na watu wote walipokuwa wakishughulika na mipango ya maziko yake, baadhi ya watumishi wa nyumbani waliiba vitu kadhaa. Walikuwa hawakufikiria kuwa labda Imamu angejua yote hayo.Shughuli za maziko zilipomalizika aliwaita wote wale waliohusika na kuwaambia kuwa kama wakimwambia ukweli atawasamehe kwa yale yote waliyoyatenda, la sivyo watavirudisha vile vitu walivyoviiba na atawaadhibu. Kisha akavitaja vile vitu vyote kila mmoja wao alivyoiba na walipokubali aliwasamehe.