WAJIBU WA VIJANA
MTUNGAJI: SHEYKH HASAN SAFFAR
MFASIRI: ABU AHMAD HUSSEIN
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
Jaribio la Kumfahamu Kabla ya kufikia umri wa miaka kumi na mitano kwa kipindi kidogo, mwanadamu hukabiliana na kipindi muhimu na cha hatari katika uhai wake, nacho ni kipindi cha ujana (ubarobaro) ambacho huendelea nacho hadi kufikia umri wa miaka ishirini au ishirini na tano hivi. Hiki ndicho kipindi cha ubarobaro (ushababi), nacho ni kipindi muhimu na cha hatari.
Hebu tujiulize kwa nini kuwa ni muhimu na hatari?
Ni muhimu kwa kuwa huihukumu hali ya baadaye ya umma na mwisho wake. Vijana hawa wanaokua hivi leo bila shaka wao ndio umma wa kesho. Umma huu ulioko hivi sasa utaondoka na pahali pao na vyeo vyao vitachukuliwa na hawa vijana. Naam, utawaachia pahali pake umma unaokuja, umma mpya. Nao huo umma mpya ni hawa vijana wa leo na mabarobaro wa sasa.
Kwa hakika ni kweli kabisa kwamba mwanachuoni wa leo wa kidini hatakuwa ndiye mwanachuoni wa kesho, bali hapana shaka yoyote kwamba pahali pake na cheo chake ataviacha kisha atakuja mtu mwingine miongoni mwa hawa vijana mabarobaro iIi achukue pahali pake. Mkuu wa mkoa au wilaya wa leo hatakuwa ndiye mkuu wa mkoa au wilaya wa siku zijazo, bali hapana budi nafasi yake itafikia kikomo, atakufa na pahali pake patachukuliwa na mtu mwingine.
Vivyo hivyo, rais wa nchi wa leo, hakimu, amiri, waziri, kiongozi, n.k. watakufa na pahali pao patachukuliwa na vilana wa leo. Hii ndiyo tabia ya uhai na tabia ya maumbile. Huu ndio mwenendo wake kwamba kizazi kimoja kinapoondoka badala yake huja kizazi kingine. Je, hao watu wengine watakaochukua nafasi ya jamii ya sasa katika siku zijazo ni akina nani? Hakika wao ni hawa vijana wa leo, kwani wao ndio watakaounda jamil ya kesho. Siku moja Imam Hasan bin Ali(a.s) aliwakusanya watoto wake na kuwaambia: "Nyinyi leo ni watu wadogo, mnatarajiwa kuwa watu wazima kwa wengine. "
Vijana wetu wa leo ikiwa watalelewa vyema hadi wawe wema na wanyofu, tunaweza kubashiri kuwa umma wetu na jamii zetu bali na vizazi vyetu vijavyo vitakuwa na mustakbali mwema; lakini wasipokuwa wema au wasipofuata njia nyofu basi itamaanisha kuwa huenda mustakbali wao ukawa mwovu, mweusi na wenye giza.
Kipindi cha ushababu ni muhimu sana kwa sababu ndicho upeo wa mustakbali wa umma na mustakbali wa wananchi, na kutokana na sababu hii ndio mafundisho bayana ya dini yanatilia mkazo sana kukizangatia kipindi hiki kutokana na umuhimu wake. Kwa mfano kauli ya Mtume Muhammad(s.a.w.w) aliposema: "Hakika nyayo za mja hazitaweza kunyanyuka katika siku ya Kiyama hadi aulizwe ameumaliza umri wake katika njia gani na ameutumia ujana wake katika nini. "
Wakati kama huu ni hatari kwa kijana kwa kuwa huishi katika hali maalum inayoathirika kimwili, kifikra na kijamii. Katika hali hii ya pekee anayoishi kijana katika kipindi cha ujana, inatakikana ama ajiimarishe katika mazingira yaliyo mema na maongozi yaliyo salama ili aweze kuvuka kipindi hiki akiwa ni kijana mwenye juhudi sana ambaye ataweza kuunufaisha umma kutokana na kuwepo kwake na harakati zake; au aondokee kuwa ni kijana aliyeharibika katika mazingira ya ufisadi na matokeo yake iwe ni kuibomoa nafsi yake na kuibomoa jamii yake.
Vipambanuzi vya Kipindi cha Ujana Kipindi cha ubarobaro kinajipambanua kwa wingi wa sifa na vipawa. Sifa hizi na vipawa hivi hupatikana kwa wingi katika shakhsia ya barobaro katika pande zote za maisha yake.
Upande wa Kimwili: Katika kipindi cha uvulana na ubarobaro, mwili wa mwanadamu hutangaza kuwasili kwake kwenye kilele cha kukomaa na kukamilika, kwani huchukua umbile lake halisi na nguvu zake hukamilika na kimo chake humuongezea urembo wa kitabia. Qur'ani Tukufu yaelezea kuwa wakati wa uvulana ndio wakati wa nguvu. Mwenyezi Mungu amesema:
اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن ضَعْفٍ ثُمَّ جَعَلَ مِن بَعْدِ ضَعْفٍ قُوَّةً ثُمَّ جَعَلَ مِن بَعْدِ قُوَّةٍ ضَعْفًا وَشَيْبَةً يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ وَهُوَ الْعَلِيمُ الْقَدِيرُ ﴿٥٤﴾
"Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na udhaifu kisha akajaalia nguvu baada ya unyonge, kisha akajaalia baada ya nguvu unyonge tena na ukongwe. Anaumba atakavyo. Naye ndiye Mjuzi, Mwenye uweza." (30:54).
Mwanadamu huja kwenye uhai akiwa yu mtoto mdogo dhaifu, hawezi hata kumwondoa nzi aliyetua usoni mwake, kisha hukipita kipindi hicho cha udhaifu (utoto) huenda katika kipindi cha uvulana, kipindi chenye nguvu na nishati; kisha unyonge humjia tena na kumtawala mara nyingine kwa jinsi ambayo huingia katika zama za uzee na ukongwe. Vilevile katika wakati wa ujana, hisia za mwanadamu hulipuka na hisia za jinsia hazimpi nafasi. Kijana huishi katika hali ya zahama, dhiki na vurugu za kijinsia (shahawa) na huendelea katika hali hii. Hisia hizi huwa zinahitaji kushibishwa na kuondoshewa kiu yake.
Upande wa Kijamii: Baada ya kukipita kipindi cha utoto alipokuwa mdogo akinyenyekea amri za wakubwa, akiwa hana rai wala hamiliki jambo lolote, sasa huona kuwa ni barobaro. Nafsini mwake anajihisi kuwa ana nguvu, na kifuani mwake amejawa na hisia ya kujamini dhati yake. Wakati huo hutafuta jukumu Ia kutekeleza katika jamii. Sasa yeye si mtoto tena, bali hujihisi kuwa ni mtu mzima (mme) aliyekamilika uume (utu), na ni wajibu wake kufanya yale yanayofanywa na wakubwa. Umekwisha ule wakati aliokuwa akitendewa kama mtoto mdogo, wakati alipokuwa akitii amri za wakubwa na kunyenyekea matakwa yao. Hivi sasa yeye amekuwa mkubwa si mdogo tena. Anayo rai anataka aitekeleze na anatafuta jukumu katika jamii alitekeleze ili aijaze hi faragha ya kinafsi aliyokuwa nayo muda mrefu.
Upande wa Kinafsi: Katika kipindi hiki cha ubarobaro, ndani mwa nafsi ya ubarobaro huwemo matakwa ya kutaka kukataa kila jambo na roho ya kutaka kuasi, kama kulipizia kisasi kwa aliyofanyiwa alipokuwa mdogo, wakati alipokuwa akitii matakwa ya wazazi wake na vilevile kuzinyenyekea ada za jamii yake bila ya kuweza kupinga au kuhalifu na kujitenga. Kijana anapokuwa mkubwa na mwenye nguvu hupendelea naye atekeleze haki yake katika kupinga au kukubali na kuwa na rai huru. Huu ndio wakati ambao hukua nafsini mwake roho ya kutaka kupinga na kuasi. Tena hapa kuna sifa nyingine anayosifiwa barobaro kuwa nayo katika wakati huu wa uvulana na ujana, nayo ni ule upendo wake wa kujitolea na kuwa tayari kwake kujitoa mhanga. Tabia ya binadamu na umbile lake kila anapoishi muda mrefu hapa duniani, tamaa na pupa lake Ia kutaka kubakia zaidi hapa duniani huzidi kuambatana naye.
Ama tunapomzingatia barobaro kwa kuwa ni chipukizi anayeanza kukua katika hii dunia, yeye hawi mwingi wa tamaa na pupa Ia kutaka kubakia hapa duniani kama anavyokuwa mzee mwenye umri mkubwa. Mwenye kuyachunguza kwa makini matendo ya barobaro atagundua kuwa ana tabia ya kujiingiza kwenye hatari au kushikilia lilelile analolitaka, kupambana bila ya kujali kufa hasa anapojawa na hamasa. Ama mtu mkubwa wa umri, yeye hujihifadhi, tena huwa mwenye utulivu na husara katika matendo yake na shughuli zake. Kule kuwa kwake na majaribio humpa aina fulani ya kuwa na mizani na kujihifadhi, tena pupa lake Ia kubakia duniani halimkubalii kuwa na upendo wa kujiigiza katika mambo bila ya kuzingatia.
Hapa kuna mfano mwepesi kuhusu hakika hii. Hebu mpeleleze barobaro anapoendesha gari, kisha mpeleleze mtu wa makamo uendeshaji wake uko namna gani. Imerekodiwa kwamba katika zama za khallfa wa Kiabbasi Harun Rashid, aliambiwa kuwa yuko mtu aliyeishi na Mtume Mtukufu na akasikia hadithi zake. Yeye ni sahaba aliyekuwa na umri mrefu ambaye aliishi tokea zama za Mtume Mtukufu hadi zama za Harun Rashid. Umri wake ulikaribia miaka mia moja na thelathini (130) Kwa vile sahaba huyu ana heshima kuu, Harun Rashid alipendelea kukutana naye. Harun Rashid akaamuru aletwe na akaletwa kwake huku amebebwa. Harun Rashid akamwuliza: "Je, wewe umekutana na Mtume wa Mwenyezi Mungu?"
Mzee akainamisha kichwa chake kama kuonyesha alama ya kujibu ndio.
"Je, umewahi kuyasikia mazungumzo (hadithi) ya Mtume wa Mwenyezi Mungu?"
"Ndio."
"Je, unakumbuka mazungumzo yoyote miongoni mwa mazungumzo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu?"
"Ndio"
"Hebu nizungumzie iIe hadithi unayoikumbuka uliyoipokea kwa Mtume Mtukufu." Mzee akasema kwa sauti dhaifu sana: "Nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu siku moja akisema: 'Mwanadamu huzeeka na hubakia ndani mwake sifa mbili -tamaa na matumaini." Mzee akayakata mazungumzo huku akiwa hana uwezo wa kuendelea nayo. Harun Rashid akaamuru apewe zawadi, nayo ilikuwa ni kiwango fulani cha mali, na iliwekwa juu ya kitanda chake. Kisha wakambeba ili kumrudisha nyumbani kwake.
Harun Rashid akahisi kwamba mdomo wa sahaba mzee ulikuwa ukichezacheza kana kwamba alikuwa akisema kitu. Akaamuru arejeshwe. Watumishi wakaja naye hadi ubavuni karibu na Harun Rashid. Akamwuliza: "Nimeuona mdomo wako ukichezacheza wakati ulipokuwa ukirudishwa kana kwamba ulikuwa ukisema kitu." Mzee akasema: "Ndio, nilikuwa nikiwauliza waliokuwa wakinibeba: 'Je, huyu Harun Rashid ataifanya zawadi hii iwe ni ya kila mwaka, awe akinipa mfano wake ili niweze kumzuru mwanzo wa kila mwaka?'" Harun Rashid akacheka, kisha akasema: "Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema kweli kabisa katika ile hadithi uliyoisema hivi sasa kwamba: 'Mwanadamu huzeeka na hubakia ndani mwake sifa mbili - tamaa na matumaini.'" Hivi ndivyo ilivyo.
Tamaa ya mwanadamu na matumaini yake ya kutaka kuishi duniani huzidi kukua nafsini mwake kila umri wake unapozidi. Hubakia ana busara na hujihifadhi katika matendo yake na mambo yake yote, ambapo barobaro huwa yuko tayari kujitoa sadaka na kujiingiza katika mambo ya hatari bila ya kujali hatari zilizoko mbele yake.
Upande wa Kinafsi: Aghlabu vijana na barobaro katika kipindi hiki cha ujana huwa na faragha na udhaifu wa kiakili katika kufungamana kwao na watu. Katika kipindi hiki cha ubarobaro akili ya binadamu hufumka na vipawa vyake hufunguka. Huanza kuyafikiria mambo kwa undani. Akilini mwake huchoreka maswali mengi kuhusu maisha yake na maisha ya jamii. Maswali ambayo hayana budi kujibiwa wazi. Vilevile hujiona kwamba halazimiki tena kuzikubali fikra za watu wake na mazingira yao, madamu ameamini nafsini mwake kuiamini dhati yake, na kupendelea kufuata mtindo wa kukataa na kupinga kila jambo na kupondokea zaldi upande wa kubeba majukumu mazito mazito na ya hatari. Kwa ajili hiyo, barobaro huwa yuko tayari kuipokea na kuifuata fikra yoyote mpya japo iwe ya hatari namna gani.
Ama mtu mkubwa yeye ana ukinaifu, imani na fikra anazoziamini na kuzitukuza miaka mingi. Yeye hana faragha ya kiakili wala hahisi kuwa na haja ya kuwa na itikadi nyingine mpya, bali yeye hayuko tayari kuiacha fikra aliyoiamini muda mrefu na kuitukuza miaka mingi. Kwa ajili hiyo utaona kwamba kila ujumbe na mafunzo kutoka mbinguni yalisimama na kupata nguvu kutokana na mabarobaro (vijana) wale ambao kwamba wao huwa wepesi kuziamini hizo fikra mpya na huwa tayari kujitoa mhanga kwa ajili ya kuzitetea. Tuchukue mfano mmoja:
Nabi Ibrahim(a.s) alipowapelekea watu wake ujumbe wa kumpwekesha na kutomshirikisha Mwenyezi Mungu, ni nani aliyemwamini na kuukubali wito wake? Watu wake hawakuukubali ujumbe wake, isitoshe wakamtuhumu kwa kuwa aliaminiwa na kikundi cha vijana maskini, kama Qur'ani Tukufu inavyosema:
وَمَا نَرَاكَ اتَّبَعَكَ إِلَّا الَّذِينَ هُمْ أَرَاذِلُنَا بَادِيَ الرَّأْيِ ﴿٢٧﴾
"Na hatukuoni wamekufuata isipokuwa wale wanyonge katika sisi wenye fikra ya mwanzo." (11:27).
Naye Nabii wetu Muhammad(s.a.w.w) pia. Wale waliofanya upesi kumwamini na kuufuata ujumbe wake walikuwa ni kikundi cha mabarobaro, wadogo kwa umri, kama Ali bin Abu Talib(a.s) , Bilal Mhabeshi na Ammar bin Yaasir, n.k.
Jambo hili liliwafanya wazee na viongozi wa Makureshi kumtuhumu Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba yeye amewaharibu vijana wao na wakayasema hayo hayo katika mashitaka yao waliyoyapeleka kwa ami yake Abu Talib. Wakasema: "Hakika mwana wa nduguyo amewatusi miungu wetu, na amezipuuza ndoto zetu na amewaharibu mabarobaro wetu ." lli kuitilia nguvu hakika hii, Mtume Mtukufu amesema: "Nawausia kuwafanyia wema mabarobaro, kwani wao wana mioyo laini zaidi. Hakika Mwenyezi Mungu amenituma mimi (niwe) mbashiri na mhofishaji, mabarobaro wakaapa kushikamana nami na wazee wakanihalifu... Na muda wao (wa kuishi duniani) ukawa mrefu na nyoyo zao zikasusuwaa (zikawa ngumu) ."
Amirul Mu'miniyn Ali bin Abu Talib amesema: "Hakika moyo wa kijana ni kama ardhi isiyokuwa na kitu (isiyolimwa) chochote kinachoingizwa (kinacholimwa) ndani yake hukikubali. "