ASHURA
SHAHADA YA IMAM HUSAYN
MTAZAMO WA KIHISTORIA
KISA CHA SIKU YA ASHURA NA KUULIWA KWA IMAM HUSAYN
Hii ni kumbukumbu ya kujitolea mhanga na kuuliwa kwa Imam Husayn na takriban Familia yote ya Mtume Muhammad(s.a.w.w) katika kuinusuru dini na kuitetea haki dhidi ya hao walowezi na wapinzani wa dini, na kuregesha mwito ule ule wa "hakuna Mungu apasae kuabudiwa ila Allah".
Imam Husayn(a.s) ambaye ni mjukuu wa Mtume Muhammad(s.a.w.w) aliuwawa kwa ajili ya kuutetea Uislamu. Sababu kuu ya kuuwawa Imam Husayn ni kwamba yeye alikataa dhulma na uwongo. Alikataa kula kiapo cha utii (baiyat) kwa Yazid. Imam Husayn alitaka kuisimamisha haki na ukweli kama aliokuwanao babu yake Mtume Muhammad(s.a.w.w) .
Sifa njema zote ni zake Mwenyezi Mungu Bwana wa viumbe vyote aliyeniwezesha kufasiri mfululizo wa 'tukio la Siku ya Ashura na kuuwawa (Shahidi) kwa Imam Husayn'(a.s) kama ulivyochapishwa kwa lugha ya kiingereza katika gazeti la 'Daily Nation' tarehe 19th hadi 28th Mei 1996 kwa hisani ya 'Tawhid Distribution Service'. Inapata zaidi ya miaka 1360 tangu kuuwawa (shahidi) kwa Imam Husayn(a.s) na wafuasi wake katika uwanja wa karbala na majeshi katili ya Yazid ibne Muawiya ibne Abu Sufiyan. Tukio hili halikuwa la kawaida kwani alishalibashiri mtume Muhammad(s.a.w.w) aliposema:
''Kwa hakika kifo (shahada) cha (Imam) Husayn kitaamsha mori katika nyoyo za waumini ambao hautapoa milele' '[1] . Hakuna shahidi aliyeheshimika na kukumbukwa kila mara, na kwa wakati mrefu zaidi kama Imam Husayn(a.s) kujitoa kwake muhanga kupigania haki na kumuamini Mwenyezi Mungu hata katika majaribio mengi ni hakikisho wazi la ukweli wa Uislamu. Mfululizo huu una azma ya kutilia nguvu Aya inayosema:
وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتًا بَلْ أَحْيَاءٌ عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ ﴿١٦٩﴾
Wala kabisa usiwadhanie walio uliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni maiti. Bali hao ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi. (Qur'an 3:169).
Nakukumbusha hekima na mafundisho ya Imam Husayn. Ni tumaini letu k wamba mawazo ya Imam Husayn yatakuwezesha kuwa na mtazamo usio wa anasa za dunia, bali wa kutafuta malengo makuu zaidi unaporudi kwa muumba wako.
Wasomaji wanaulizwa kutuandikia maoni yao na maswali kuhusu tukio hili au jambo lolote kuhusu Uislamu. Tunawatunukia kitabu hiki mashujaa shahidi wa Karbala akiwemo kiongozi thabiti Sayyidu Shuhada Aba Abdillah Husayn bin Ali bin Abi Talib na mashujaa wote waliojitolea mhanga kuitetea dini tukufu ya Uislamu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu S.W.T. atukubalie juhudi zetu za kuchapisha kitabu hiki.
Bilal Muslim Mission of Kenya
P. O. Box 82508, Mombasa - Kenya.