18%

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

DIBAJI YA AL-MIZAN

Katika kazi nyingine alizozifanya mfasiri mkubwa allama tabatabai Al-Mizan inachukuwa nafasi ya kwanza katika kutambuliwa, kwa sababu ya sifa zake zisizokuwa na kifani. Jambo hili si katika vitabu vyake tu bali ni katika vitabu vyote vya Kiislamu vilivyo andikwa kuhusu Dini, Sayansi, Falsafa, na hasa kuhusu aina zote za tafsiri ya Qur'an mpya ama zamani zilizoandikwa na Sunni ama Shia. Maelezo haya hayawezi kueleza kwa urefu mambo yaliyomo lakini yanaweza kuwasaidia wasomaji kwa kuwapa fununu juu ya umaridadi wa Al Mizan. Ninaona kwamba sistahili kuifanya kazi kubwa kama hii kama watu wakubwa mfano Ayatullah Mutahhari ambaye yeye mwenyewe ni mtu mwenye fikra mpya, mjuzi wa Qur'an na mfasiri vile vile, aliposema: "Al- Mizan ni tafsiri kubwa zaidi ya Qur'an iliyowahi kuandikwa tangu kuanza Uislamu; na itachukua miaka sitini ama mia moja mpaka watu wetu kuutambua umuhimu wa Al-Mizan ya Allama Tabatabai. "Wanachuoni wengine, wajuzi na watu walio na busara walitoa maoni kama haya kuhusu kitabu hiki. Majaribio yoyote ya kuonyesha maana ndani ya Al- Mizan hata kama ni kwa njia ya juujuu, katika maelezo mafupi kama haya, ni kama kujaribu kuitia bahari ya Atlantiki katika chungu kidogo.

Hata hivyo ninatarajia kukusanya matone machache katika bahari hii ya elimu ya Kiislamu kulingana na uwezo wangu ili nitosheleze kiu yangu. Nataraji roho njema ya mwandishi mcha Mungu wa kitabu hiki cha milele, itaniwia radhi kwa kazi hii ndogo nitakayoitanguliza.

Historia Ya Al-Mizan Kabla ya kugusia zile alama zinazoipambanua tafsiri hii na nyinginezo, tutaandika historia fupi ya Al- Mizan. Allama Tabatabai, aliyekuja katika hawzah ya Qum mwaka wa 1325 A.H aliandika na akatoa hotuba kuhusu matawi mbali mbali ya elimu za Kiislamu. Tafsiri na maelezo ya Qur'an lilikuwa ni somo moja katika mazungumzo yake, aliyoyafanya na wanachuoni na wanafunzi na "Hawzeh Ilmiyyah" ya Qum. Kuhusu azimio lake la kuandika Al- Mizan, Allama Tabatabai alisema kwamba, alipokuja Qum kutoka Tabriz alijaribu sana kutathmini mahitaji ya jamii ya Kiislamu, na vile vile alzingatia hali iliyokuwapo katika Hawzah Ilmiyyah ya Qum. Baada ya kulizingatia jambo hili, suluhisho lilikuwa, shule ile ilihitaji maelezo ya Qur'an ili waweze kuielewa vyema na kuzifahamu sharia zake na vilevile kuyaelewa maana halisi ya vitabu vyote vya Kiislamu na maandishi yote yaliyo na vipaji vikubwa.

Kwa upande mwingine kwa vile nadharia za mada zilikuwa zikipata nguvu siku hadi siku, palikuwa na haja kubwa ya kupata hoja za kiakili na kifalsafa ili kuiwezesha Hawza kukabiliana na hali mpya na kuchambua misingi ya kifikra na imani ya Uislamu, pamoja na msaada wa hoja za kiakili ili kutetea maoni ya Uislamu. Basi aliona ni jukumu lake kufanya juhudi ili ayatimize mambo haya mawili muhimu kwa msaada wa Mwenyezi Mungu aliye Mtukufu zaidi. Alipanga masomo ya tafsiri ya Qur'an kwa mpango huu. Pengine Alama Tabatabai alitoa masomo ya Qu'ran nzima kwa wanafunzi kwa mara nyingi na huku akiandika yale aliyofundisha. Wakati wa darasa hizi zilizoandaliwa vizuri kwa undani wa fikra, pengine, alitoa vikao hivi vya masomo kwa ufasaha , na baadae yalichapishwa katika mijalada ya vitabu.

Uchapishaji wa kwanza wa Al - Mizan ambao ulikuwa katika lugha ya Kiarabu ulifanyika Iran na ilirudiwa kuchapishwa huko Beirut. Mpaka wakati huu, zaidi ya chapa tatu zimechapishwa huko Iran na Beirut kwa idadi nyingi zaidi. Ni Maktaba chache za watu binafsi na za serkali ambazo hazina seti kamili ya Al Mizan. Vile vile maktaba zote zinayo baadhi ya majalada ya tafsiri hii juu ya rafu zao. Kitabu cha asili cha Al Mizan ambacho kinakusanya majalada ishirini kiliandikwa katika lugha la Kiarabu. Kila mjalada una kurasa mia nne. Ilikusudiwa kwamba watu wote waliyopenda kusoma tafsiri ya Qur'an, wawe watapata faida ya kutosha kutokana na mafundisho ya Quran. Baadhi wa wanafunzi wa Allama Tabatabai walikifasiri kitabu hiki katika lugha ya Kifursi chini ya uongozi na usimamizi wake. Kila mjalada mmoja wa lugha ya Kiarabu ulifasiriwa katika mijalada miwili ya lugha ya Kifursi na idadi ya mijalada hii ikawa arobaini. Jukumu hili lilichukuliwa na Syed Muhamad Baqir Musawi Hamadani. Ili tafsiri ya Al Mizan iliyokuwa katika lugha ya kifursi isionekane tofauti, jambo ambalo lingeharibu usomaji wa kitabu hicho, Allama Tabatabai alimpa mijalada ya mwanzo ya Al Mizan kuifasiri tena.

Ni lengo letu kwamba tafsiri hii ya maneno matukufu ya Qur'an itafasiriwa katika lugha nyengine pia, ili iwe rahisi kwa wale wanaotaka kuondoa kiu ya elimu tukufu na kwa wale wanaotaka kuzijua sheria za Kiislamu zenye kuokoa maisha. Ingekuwa bora tafsiri hii kufanywa na watu na wanachuoni ambao wanaijua vyema lugha ya Qur'an. Ingekuwa ni kazi nzuri kama ujumbe wa Qur'an Tukufu ungetolewa katika njia hii ili uwafikie binadamu na kuwaokoa na mila za makafiri. Elimu ya kumwabudu Mwenyezi Mungu katika Qur'an humwepusha binadamu na aina zote za aibu na utumwa.

Alama Zinazoipambanua Tafsiri Ya Al Mizan: Al Mizan inakusanya aina mbali mbali za elimu: kama vile ya Sayansi, Ufundi, Usanifu na Uzuri. Vile vile Falsafa, Elimu ya Adabu (literature), Historia, Elimu ya Jamii na Elimu ya Hadithi (za Mtume(s.a.w.w) Mambo matatu kati ya haya hayako wazi wakati mengine yanahusiana nayo.

1. Tafsiri Ya Qur'an Kwa Qur'an: Allama Tabatabai katika maelezo yake juu ya Qur'an kwanza anonyesha asili ya kuingiliana kwa aya mbalimbali, na vile vile kusibitisha kwamba, kwa sababu hii ya kuingiliana kwa aya, aya hizi hufasiriana na kujieleza zenyewe. Kwa maneno mengine Allama Tabatabai anaonyesha kwamba baadhi ya sehemu ya Qur'an hufasiri sehemu nyingine.

Ili kuzielewa aya tukufu za Qur'an na Tafsiri zake ni lazima tutafute msaada kutoka katika Qur'an yenyewe. Alizungumzia tatizo la tafsiri ya Qur'an katika kitabu chake " Qur'an dar Islam" (Mahali pa Qur'an katika Uislamu). Baada ya kufafanua jambo hili; Allama Tabatabai alisema ' kwamba tafsiri sawa ya Qur'an inawezekana kupitia kufikiria kwa makini na kushauri aya nyingine kuutazama mwongozo wa aya za Qur'an. Kwa maneno mengine, zipo njia tatu ambapo njia yoyote kati yake iko wazi kwetu kuitumia katika tafsiri ya sawa ya aya.

1.Tafsiri ya aya zozote bila ya kuhusisha maana ya aya nyinginezo; na kwa msaada wa maelezo ya elimu maelezo za Sayanzi tuliyo nayo; au pasi na elimu hizo.

2. Tafsiri ya aya ikiwa na mwongozo na Hadith, ikichukuliwa kutoka kwa mmoja wa Ma'sumin(a.s) , inayofuatia aya.

2. Tafsiri ya aya kwa kufukiria kwa makini maneno na maana ya aya kwa kutumia msaada wa aya zinazohusika. Vile vile kutafuta ushauri katika Hadith mahali inapopasa. Njia ya tatu ndiyo iliyoelezewa katika sura iliyopita (nayo ni mahali pa Qur'an katika Uislamu). Hii ndiyo njia aliyoitumia Mtume(s.a.w.w) na Maimami(a.s) , kama tunavyosoma katika mafundisho yao. Mtume(s.a.w.w) alisema: "Aya nyengine huzungumzia baadhi ya aya nyengine na baadhi yake huzithibitisha nyengine."

Allama huyu mwisho anatukumbusha jambo muhimu; nalo ni kwamba, Qur'an hutafasiriwa kwa Qur'an. Siyo kwa maoni ya mfasiri - njia ambayo imekataliwa na Hadith mushuhuri ya Mtume(s.a.w.w) . Mwisho Allama Tabatabai anazifananisha na kuzieleza njia hizi tatu za tafsiri, kwa urefu. Kisha anasema, njia ya tatu ndiyo njia bora ya kuifahamu Qur'an kulingana na majadilano ya Qur'an na uthibitisho wa hadith. Mwisho wa sehemu hii ya mazungumzo anatuonyesha mfano na tafsiri ya Qur'an kwa Qur'an ambao hatuwezi kuonyesha hapa kwa ajili ya kufupisha. Al-Mizan inaonyesha jambo muhimu la kuzielewa sifa za miujiza ya Qur'an tukufu kufanana na kuingiliana kwa ya zake.

2. Upande Wa Kijamii:

Tafsiri zote za Qur'an kwa uchache ama kwa wingi zimejadili mambo muhimu kuhusu mazingira ya jamii, lakini Al-Mizan haina mfano ikifafanishwa na tafsiri myengine. Mijadala ya kuhusu jamii iliyomo katika Al-Mizan ina kina kikubwa sana cha thamani kwa wingi. Kwa namna alivyoitazama migawanyiko mingi na matatizo ya kijamii, Allama Tabatabai alifaulu kuyatatua kwa kutumia aya za Qur'an. Ametoa mwangaza mpya kuhusu baadhi ya matatizo hAya Na kijamii kwa maoni ya Qur'an, matatizo ambayo mpaka kufikia wakati huu yalikuwa yamepuuzwa. Allama Tabatabai amefungua ukumbi mpya kwa wasomaji walio na ari ya kuvumbua sehemu mpya katika maana ya Qur'an tukufu.

3. Upande Wa Falsafa:

Allama Tabatabai ambaye ni mwanafalsafa mwenye mwelekeo wa mustakbali na usanii nadra na wa asili, alifanya kazi kubwa katika elimu ya tafsiri, kufafanua ughaibu wa Qura'n, jambo ambalo linatupa uoni mkunjufu na wenye faida katika kufahamu bara bara maisha ya ughaibu Aliyakanusha makosa yote yasiyo na msingi yaliyotolewa katika Qur'an. Kwa maoni yake, ughaibu wa Uislamu una mizizi yake katika Qur'an, nayo ni ufafanuzi wa Qur'an kuhusu Mwenyezi Mungu, binadamu na ulimwengu. Allama Tabatabai vile vile anaonyesha kwamba ada ya kuogopa kuzungumzia mambo ya ughaibu (yasiyoonekana), inatokana na ukosefu wa kufahamu mambo hayo na kutokuwa na habari sahihi kuhusu mambo hayo.

Katika vitabu vyake kama vile Usul-e-Falsafa wa Rawish-e-Riyalism (Misingi ya falsafa na utaratibu wa madhehebu ya ukweli), maelezo juu ya kitabu kiitwacho Al-Asfar cha Mulla Sadra, katika makala mbili za (Bidayat, Al-Himah, na Nihayat, al-Hikmah), alieleza na kuyasawazisha makosa yote juu ya asili ya ughaibu. Katik Al-Mizan amezungumza masuala hAya Na a falsafa kadhaa za kifalsafa kutokana na aya hizo. Hili ni jambo ambalo halina mfano katika historia ya tafsiri ya Qur'an. Katika kutafsiri kwake aya za Qur'an na kuelezea uhusiano wake na fikra za ughaibu, alionyesha uthabiti wa Qur'an na vile vile kuonyesha upuuzi na ukosefu wa msingi wa falsafa ya mada. Sehemu hii ya tafsiri yake ni ya asili na vile vile ni mpya katika uwanja wa masomo ya falsafa. Mijadala yake hii ina undani wa maana ulio nadra, usahihi na ustadi ambao utaendelea kuwavutia wasomi katika siku za usoni.

Katika Juzuu Ama masomo mabili mbali ambayo yanazungumzwa kulingana na Sura ni

1. Mazungumzo kuhusu maumbile ya binadamu kutoka katika Qur'an.

2. Mazungumzo kuhusu viapo katika Qur'an orodha ya vitu ambavyo Mwenyezi Mungu anaapia katika kitabu kitukufu.

3. Mazungumzo kuhusu maana ya Roho (Ruh) katika Qur'an.

4. Mazungumzo kuhusu vipi malaika wanafanya kazi kama mawakili katika hali ya maisha.

Mwisho ni lazima nikiri kwamba maarifa yangu machache ambayo huenda yameathiri katika kufahamu undani wa na upana wa fikra za historia zilizomo katika Al-Mizan, yametia kasoro na dosari kubwa. Allah aiweke pema roho ya Allama Tabatabai kwa kazi yake kubwa aliyoifanya.

Abu-Al-Qasim Razzaqi

Kwa Wasomaji Sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa uwezo wa kutafsiri tafsiri hii ya Qur'an iliyoandikwa na mwanachuoni mkubwa Bwana Muhammad Hussein Tabatabai. Ni lazima ieleweke kwamba haikuniwiya rahisi kazi hiyo hasa kwa kuzingatia undani na upana wa fikra za mwanachuoni huyo. Ugumu zaidi ulikuwa pale niliposhindwa kupata maneno ya Kiswahili yatakayotoa maana halisi yaliyokusudiwa jambo ambalo limenilazimisha kuacha baadhi ya ibara hasa zile za kanuni za lugha ya Kiarabu (Nahwu). Hata hivyo nimejitahidi kugusia kila ambacho ni muhimu katika tafsiri hiyo. Kwa vile tafsiri hii imeelezewa kwa undani sana na kwa njia ya kifalsafa, jambo ambalo pengine halikuzoeleka kwa vitabu vya dini vilivyoandikwa kwa Kiswahili, basi ndugu msomaji nawe itakubidi uisome kwa undani na wala sio kuipitia juu juu. Pengine itakubidi urudierudie baadhi ya ibara.

Ndugu msomaji ikiwa macho yako utayafungua kwenye makosa tu, na kuyafumba kwenye usawa na faida, basi ninakwambia Mungu akusamehe na aniongoze mimi na wewe. Hata hivyo sina maana ya kukukataza kunikosoa, bali ninakuomba hasa ufanye hivyo na Inshallah Mwenyezi Mungu atakulipa kwa nia yako. Kwani walikwishasema wahenga : "Binadamu si kamili". Shukrani: Shukrani zangu za dhati ziwaendedd London Islamic Foundation kwa kujitolea kuisimamia na kuigharimia kazi ya kukichapisha kitabu hiki. Pia shukrani nyingi zimwendee Sheikh Islam Khiyar Islam kwa taabu kubwa aliyoichukuwa ya kusahihisha kitabu hiki. Na wengineo ambao kwa namna moja au nyingine wamechangia kukitayarisha kitabu hiki; Mungu awajaze heri ya dunia na akhera (Amin).

Desemba 1988 Hassan Ali Mwalupa