6%

19

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURA INSHIRAAH (UKUNJUFU) (NA. 94)

INA AYA 8

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenya kurehemu

أَلَمْ نَشْرَحْ لَكَ صَدْرَكَ ﴿١﴾

1. Je, hatukukunjulia moyo wako?

وَوَضَعْنَا عَنكَ وِزْرَكَ ﴿٢﴾

2. Tukakuondolea uzito wako.

الَّذِي أَنقَضَ ظَهْرَكَ ﴿٣﴾

3. Ambao uliuelemea mgongo wako?

وَرَفَعْنَا لَكَ ذِكْرَكَ ﴿٤﴾

4. Tukakutukuzia utajo wako?

فَإِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا ﴿٥﴾

5. Hakika pamoja na uzito kuna wepesi.

إِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا ﴿٦﴾

6. Hakika pamoja na uzito kuna wepesi.

فَإِذَا فَرَغْتَ فَانصَبْ ﴿٧﴾

7. Basi ukishamaliza (amali yako) jitaabishe kwa ibada.

وَإِلَىٰ رَبِّكَ فَارْغَب ﴿٨﴾

8. Na Mola wako (peke yake) mtake haja.

UBAINIFU

Ni amri ya kujitaabisha kwa ibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kujipendekeza kwa kumtaka haja. Sura hii inawezekana kuwa imeshuka Makka au Madina, na mpangilio wa aya zake unawafikiana zaidi na Madina. Katika baadhi ya riwaya za Maimamu wa Ahlul Bait(a.s) zinasema kuwa Sura ya Adh-dhuha na Al-Inshiraah ni Sura moja. Na yamepokewa hayo vile vile kutoka kwa Twaaus na Umar bin Abdul-Aziz.

Amesema Arrazi katika Tafsiri Kabir baada ya kuwanakili hao wawili: Jambo lililofanya Twaaus na Umar kusema kuwa hizo ni Sura moja ni kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t): "Je hatukukukunjulia moyo wako ?" Nikama linaungana na neno; "Je hakukukuta ni yatima akakuhifadhi?" Lakini sababu hiyo siyo, kwani neno la kwanza kushuka kwake, lilikuwa ni katika hali ya kuwa Mtume(s.a.w.w) yuko kwenye ghamu kutokana na maudhi ya makafiri, akawa katika hali ya misukosuko na dhiki ya moyo. Na neno la pili linahukumilia kuwa liliposhuka, Mtume alikuwa katika hali ya kukunjuka na kutulia moyo, basi yataungana vipi haya?

Katika hiyo hiyo Tafsiri Kabir imesemwa makusudio ya kuukunjua moyo wake Mtume(s.a.w.w) ni kufanywa Mtume anakunjukiwa na hakika zote anazopewa wala hapati dhiki yoyote kutokana na maarifa yanayomshukia na wala hapati dhiki kutokana na adha ya watu katika kuyafikisha hAya Na nayomshukia. Na wala sio kutulia moyo na furaha, kama yatakavyokuja maelezo zaidi (Inshallah). Yanafahamisha hayo yale yaliyopokewa na Ibn Abu Hatim kutoka kwa Said bin Jubayr naye kutoka kwa Ibn Abbas amesema: Amesema Mtume(s.a.w.w) : "Nilimuuliza Mola wangu masuala ambayo nilitamani nisingemuuliza. Nilimwambia "Ewe Mola wangu Mitume waliokuwa kabla yangu kuna katika wao waliofanyiwa upepo uwatii na waliokuwa wakiwafufua wafu. Ndio akasema Mwenyezi Mungu: "Je sikukuta ni yatima nikakuhifadhi?" Nikasema: "Kwa nini?" Akasema: "Je sikukuta umedangana nikakuongoza?" Nikasema: "Bila shaka ewe Mola wangu." Akasema: "Je sikukukunjulia Moyo wako na nikakuondolea uzito wako?" Nikasema "Bila shaka ewe Mola wangu." Maelezo zaidi yako katika Tafsiri ya Sura Quraish (Liiylafi Quraish).

Aya Na 1

Asili ya neno Nashrah ni kuichangua nyama na mfano wake, na miongoni mwa maana yake ni kukunjua moyo yaani kuukunjua kwa nuru ya Mungu na utuvu unaotokana upande wa Mwenyezi Mungu na Roho inayotoka kwake. Qur'an inasema: "Ewe Allah nikunjulie moyo wangu ." (20:25).

"Je hatukukunjulia moyo wako?" "Je ambaye amekunjuliwa moyo wake na Allah " (39:22).

Kuzifuatisha aya tatu za mwanzo katika madhumuni yake kisha kuzibainisha kwa kauli "Hakika pamoja na uzito kuna wepesi", kwa dhahiri inaonyesha kufungika hali yake Mtume katika mwanzo wa mlingano wake, katikati yake na mwisho wake. Kisha kukaririka kuthibitisha ila na kuzifanya aya mbili za mwisho kuwa ni sehemu yake. Yote hayo yanashuhudia kuwa makusudio ya kukunjua moyo wake Mtume(s.a.w.w) ni kuukunjua kiasi ambacho yatakunjuka yale yanayomfikia miongoni mwa wahyi, yale anayoamrishwa kuyafikisha na yale yanayompata katika maudhi na adha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Kwa maneno mengine tunaweza kusema ni kuifanya nafsi yake tukufu ni yenye kujiandaa kwa ukamilifu kwa kukubali yale yanayoifikia hiyo nafsi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Aya Na 2-3

Makusudio ya kuondoa uzito wake kutokana na unavyofahamisha mpangilio wa maneno ni kutekeleza mlingano wake na kupitisha juhudi zake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa kuwafiki sababu. Kwani hakika ujumbe (Utume), na mlingano ndio uzito aliochukua mara tu! Baada ya kukunjuliwa moyo wake. Inasemekana kuwa kuondoa uzito kunaonyesha kunaelekeana na yale yaliyopokewa kwamba Malaika wawili walimshukia Mtume wakakipasua kifua chake na wakautoa moyo wake wakautoharisha, kisha wakaurudisha mahali pake. Maelezo zaidi yatakuja baadae.

Inasemekana makusudio ya uzito ni yale yaliyomtokea kabla ya kupewa utume, pia imesemwa ni kupatwa kwake na mshangao katika baadhi ya mambo kama kutekeleza haki ya ujumbe na imesemwa kuwa ni uadui wa watu wake na maudhi yao mengi. Pia imesemwa ni huzuni yake kwa kufiwa na ami yake Abu Twalib na mkewe Khadija. Na ikasemwa uzito ni maasi na kuondolewa uzito ni isma (kuhifadhiwa na dhambi) yake na imesemwa kuwa uzito ni dhambi za uma wake na kuondolewa uzito huo ni kusamehewa. Njia hizi baadhi yake ni za kipuuzi na baadhi yake ni dhaifu zisizoafikiana na mpangilio wa maneno. Nazo ziko kati ya imesemekana na inawezekana tu! Hazina uhakika wowote.

Aya Na 4

Kuutukuza utajo maana yake ni kutajwa sana jina lake kuliko mtu mwengine. Miongoni mwa kuutukuza utajo wake ni kukutanisha Mwenyezi Mungu jina lake pamoja na jina la Mtume. Kwani jina la Mtume liko pamoja na la Mola wake katika shahada mbili ambazo ndizo msingi wa dini na ni wajibu kwa kila muislamu kumtaja Mtume pamoja na Mola wake katika swala tano za wajibu kila siku. Ni katika wema kutokea kutukuzwa utajo baada ya kuondolewa uzito.

Aya Na 5

Siyo mbali kuwa ni sababu ya yale yaliyotangulia (kuondoa uzito na kulitukuza jina). Yale aliyobebeshwa na Mwenyezi Mungu na akaamrishwa kuyalingania - ambayo ni mazito kwa mtu kuyachukua - yalikuwa yamezidi. Vile vile watu wake walizidi kumfanya mwongo kwa mwito wake, kumdharau na kujitahidi kuuzima utajo wake (jina lake). Kwa hivyo Mwenyezi Mungu akamwondolea uzito wake ambao ameuchukua kwa kuwafanya watu kumwitikia mwito wake na akautukuza utajo wake ambao walikuwa wanataka kuuzima.

Hayo yanayotokana na desturi yake Mwenyezi Mungu katika ulimwengu kuleta wepesi baada ya uzito, kwa hiyo huenda kumwondolea shida kulikotajwa ni katika desturi yake. Basi kwa hali hii herufi lam katika neno Usri ni ya Jinsiya yaani jinsi ya uzito baadhi yake na wala sio kila uzito. Na huenda desturi na desturi ya kubadilisha matukio na hali isibakie milele.

Amesema Zamakh-Shari katika Kash-Shaff: Washirikishaji Mwenyezi Mungu walikuwa wakimkashifu Mtume(s.a.w.w) kwa ufukara na dhiki mpaka akatambua Mtume kuwa wao wanajiepusha na uislamu kwa sababu ya ufakiri wa watu wake. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu anamkumbusha yale aliyomneemesha miongoni mwa neema nyingi kisha akasema: "Hakika pamoja na uzito kuna wepesi". Kana kwamba amesema: "Tumekufadhili yale tuliyokufadhili basi usikate tamaa na fadhila za Mwenyezi Mungu, kwani uzito ulio nao uko pamoja na wepesi." Kwa dhahiri herufi lam ni ya Ahdiyya na wala sio Jinsiyya yaani uzito maalum uliokusudiwa na kwamba makusudio ya wepesi ni ghanima nyingi walizoruzukiwa waumini na Mwenyezi Mungu.

Lakini hayo ni yenye kupingika kwani utambuzi wake Mtume (SAWW) ni mkubwa zaidi kuliko kuogopea hali zao. Kuwa wanajiepusha na usilamu kwa sababu ya ufakiri wa watu wake. Isipokuwa wao walikuwa wakiukataa mwito wake kwa kiburi tu! Na Mwenyezi Mungu alikwishamkatisha tamaa Mtume wake kuwa wengi wao hawataamini aliposema: "Hakika imehakikika kauli juu ya wengi katika wao; kwa hivyo hawaatamini " (36: 7-10).

Na aya hizo zilishuka Makka. Na aya nyengine iliyoshuka Madina inayosema: "Hakika wale ambao wamekufuru ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye hawataamini ". (1:6).

Lau inachukuliwa kuwa wepesi baada ya uzito ni nguvu ya kiislamu na kuinuka kwake baada ya kuwa chini pamoja na kuchukulia kuwa Sura imeshuka Makka, basi kusingekuwa na ubaya sana.

Aya Na 6

Ni kutilia mkazo na kusisitiza. Imesemekana kuwa ni kuanza upya na wametaja kwamba katika aya mbili hizo (5 na 6) kuna ufahamisho kuwa pamoja na hali nzito moja pana nyepesi mbili. Kwa kawaida jina lenye herufi lam likirudishwa mara ya pili katika maneno, linakuwa kama lile la kwanza kinyume cha jina lisilokuwa na lam. Lakini kawaida hii sio ya lazima, huwa ikabadilika.

Aya Na 7-8

Inatokana na yote yaliyobainishwa mwanzo, miongoni mwa kuchukua ujumbe na kumneemesha kwake Mwenyezi Mungu kwa kuukunjuwa moyo na kuondoa uzito na kuunyanyua utajo na yote hayo ni wepesi baada ya uzito. Kwa hiyo maana inakuwa, ikiwa uzito unafuatiwa na wepesi na mambo yote yanatokana na Mwenyezi Mungu tu! Basi ukimaliza yale uliyofaradhiwa, itaabishe nafsi yako kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa ibada zake na dua zake na umtake kukuneemesha raha baada ya taabu hii na wepese baada ya uzito huu.

Imesemwa makusudio yake ni ukiishamaliza faradhi, jitaabishe katika suna na pia imesemwa ukishaswali jitaabishe na dua. Na madhumuni ya kauli mbili hizi ni baadhi ya yanayokubalika. Imesemwa maana yake ni ukishamaliza vita, jitahidi katika ibada. Na pia imesemwa makusudio yake, ukisha maliza yale ya duniani jitaabishe katika akhera yako. Na yemesemwa zaidi na hayo, lakini zote hizo ni njia dhaifu.

Utafiti Wa Hadith Katika Durril Manthur ametoa Abdalla bin Ahmad katika Rawaid ez-zuhd kutoka kwa Ubayya bin Kaab kuwa Abu Hurayra alisema kumuuliza Mtume(s.a.w.w) : "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ni jambo gani uliloona kwanza kuhusu utume?" Mtume(s.a.w.w) akakaa vizuri akasema: "Umeuliza swali ewe Abu Huraira. Mimi nilipokuwa na umri wa miaka ishirini na miezi kadhaa siku moja nilisikia maneno juu ya kichwa changu mara tu mmoja akawa anamwambia mwenzake ndiye huyu? Wakanikabili na sura ambazo sijaziona kwa kiumbe yoyote na roho ambao sijazipata kwa mtu yoyote na nguo sijaziona kwa mtu yoyote kabisa. Wakaja kila mmoja akanishika mkono.

Mmoja wao akamwambia mwenzake mlaze, akanilaza bila kuchelewa, mmoja akasema mpasue kifua chake, akashika kifua changu na kukipasua katika hali ambayo sikuona damu wala maumivu. Akamwambia mwenzake na mfundo wa hasadi, akatoa kitu mfano wa pande la damu kisha akikitupilia mbali akamwambia tia upole na huruma. Mara akatia kitu mfano wa kile kilichotolewa, lakini kikiwa mfano wa fedha, kisha akatingisha kidole gumba cha mguu wangu wa kulia na akasema: "Ondoka uko salama". Basi nikarudi nikawa nina mfanyia upole mdogo na kumuhurumia mkubwa."

Baadhi yao kama katika Rauhilmaani wamesema kwamba alikuwa na umri wa miaka kumi. Na katika baadhi ya riwaya kimenukuliwa kisa wakati wa kushuka Sura ya Alaq (96).

Na wengine kama katika Sahih ya Bukhari, Muslim, Tirmidhi na Nasai, kimenukuliwa kisa wakati wa Israi wa Mtume. Kisa hiki kwa hali yoyote ni cha kufananisha tu! Sio tukio la kweli na wamefanya upekuzi mrefu kwa madhumuni ya kuonyesha kuwa tukio la kweli wakautia nguvu hup upekuzi wao kwa njia ambazo hazina faida kujishughulisha nazo.

Katika hiyo Durril Manthur ametoa Abu Yaala, Jariyr, Ibn Mundhir, Ibn Hatim, Ibn Habban, Ibn Murdawayh na Abu Naim katika Dalail wamepokea kutoka kwa Abu Said El-Khudri naye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) amesema: "Alinijia Jibril akasema: Hakika Mola wako akasema: "Je, unajua vipi alivyotukuza utajo wako?" Nikasema, "Mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi ". Akasema: "Nikitajwa, unatajwa pamoja nami." Katika hiyo hiyo Durril Manthur ametoa Abdurrazzaq, Ibn Jariyr, Hakim na Bayhaqi, kutoka kwa Hassan amesema: Siku moja alitoka Mtume(s.a.w.w) akiwa na furaha na kucheka huku akisema: "Nzito moja haiwezi kushinda nyepesi mbili".

"Hakika pamoja na uzito kuna wepesi, hakika pamoja na uzito kuna wepesi." Katika Majmau kuhusu Aya Na 7 na 8 maana yake ukimaliza kuswali swala ya faradhi jitaabishe kwa Mola wako kwa dua na umtake haja. Na hayo pia yamepokewa kutoka kwa Abu Jaffar na Abu Abdiallah(a.s) .