23
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
SURA SILZAAL ( TETEMEKO)(NA. 99)
INA AYA 8
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema , Mwenye kurehemu
إِذَا زُلْزِلَتِ الْأَرْضُ زِلْزَالَهَا ﴿١﴾
1. Itakapotetemeshwa ardhi huo mtetemeko wake.
وَأَخْرَجَتِ الْأَرْضُ أَثْقَالَهَا ﴿٢﴾
2. Na ikatoa ardhi mizigo yake.
وَقَالَ الْإِنسَانُ مَا لَهَا ﴿٣﴾
3. Na akasema mwanadamu ina nini?
يَوْمَئِذٍ تُحَدِّثُ أَخْبَارَهَا ﴿٤﴾
4. Siku hiyo itatoa habari zake.
بِأَنَّ رَبَّكَ أَوْحَىٰ لَهَا ﴿٥﴾
5. Kwa kuwa Mola wako ameiamrisha.
يَوْمَئِذٍ يَصْدُرُ النَّاسُ أَشْتَاتًا لِّيُرَوْا أَعْمَالَهُمْ ﴿٦﴾
6. Siku hiyo wataondoka watu wametawanyika tawanyika ili kuonyeshwa amali zao.
فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ ﴿٧﴾
7. Basi atakayefanya wema (hata) uzani wa sisimizi atauona.
وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ ﴿٨﴾
8. Na atakayefanya uovu (hata) uzani wa sisimizi atauona.
Sura hii inaelezea Kiyama, kutolewa watu kwa ajili ya malipo ya sharti za kiyama ambazo ni tetemeko la ardhi na kuzungumza habari zake. Sura hii inawezekana kuwa imeshuka Makka au Madina.
Mwenyezi Mungu anasema "Itakapotetemeshwa ardhi huo mtetemeko wake" kwa maana ya kuwa tetemeko hilo ni la aina yake, kutokana na ukubwa wake.
Neno athqal lina manna ya mizigo. Kwa vyovyote vile iwavyo makusudio ya aya ni kuwa ardhi itatoa mizigo yake iliyoichukua ambayo ni wafu kama ilivyosemwa au hazina za madini au vyote hivyo. Kauli ya kwanza (wafu) ndyo iliyokaribu zaidi na maana.
Yaani mtu atapigwa na mshangao wa ajabu kutokana na tetememko hilo kiasi cha kujiuliza: Ina nini ardhi? Mbona inatetemeka hivi? Imesemwa kuwa makusudio ya mtu hapa ni kafiri asiyeamini ufufuo, na yamesemwa zaidi ya hayo kama yatakavyokuja maelezo (Inshallah).
Ardhi itakuwa shahidi wa vitendo vya mwanadamu, kama vile vitavyokuwa shahidi viungo vya binadamu na maandishi ya Malaika. Hiyo ni kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu. Na hii inafahamisha kuwa vitu vina uhsai na hisia, ijapokuwa sisi hatujui hilo, kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na hakuna chochote ila kinamsabihi (Mwenyezi Mungu) kwa sifa zake njema lakini nyinyi hamfahamu kusabihi (kutukuza) kwake.." (17:44).
Akasema tena: "Hata watakapoujia (huo moto), hapo ndipo masikio yao, na macho yao na ngozi zao zitakapotoa ushahidi juu yao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.. Na wao waziambie ngozi zao; "Mbona mnatushuhudilia? "Nazo ziwaambie: "Allah aliyekitamkisha kila kitu ndiye aliyetutamkisha, naye ndiye aliyekuumbeni mara ya kwanza. Na kwake hivi sasa) mnarudishwa (41:20-21).
Kumekuwa na hiitilafu kubwa juu ya maana ya kuzungumza ardhi; kuwa itapewa uhai na hisia au itaumbwa sauti tu! Lakini hatuna haja na hitilafu hizo, kwa sababu vyovyote iwavyo ni kwamba ardhi itatoa ushahidi.
Makusudio ya kuondoka kutawanyika tawanyika, ni kuenda zao kwenye makazi yao katika pepo na katika moto. Na kuona matendo yao ni kuona malipo ya matendo ya au kuona umbo halisi la hayo matendo. Imesemwa kuwa makusudio yake ni kutoka makaburini mwao kuelekea kwenye mkusanyiko wakitofautina kwa nyuso nyeusi na nyeupe,na kwa fazaa na amani, ili yafahamike malipo yao kwa kuangalia tu!, kama alivyosema Mwenyezi Mungu; "Siku ambayo kila nafsi itakuta mema iliyoyafanya yamehudhurishwa, na pia ubaya iliofanya .(3:30).
Kauli ya kwanza ndiyo iliyo karibu zaidi na maana.
Dharra ni chembe ndogo za vumbi zinaonekana katika mwanga wa jua au sisimizi wadogo. Aya hiyo inatilia mkazo yaliyotangulia kuwa amali yoyote hata iwe ndogo kiasi gani, itaonekana. Lakini aya hizo hazikanushi kuharibika kwa amali, au kugura amali kwenda kwenye nafsi nyingine; kama kugura mema ya mwuuaji kwenda kwa mwenye kuuwa, au kubadilika maovu kuwa mema kwa baadhi ya wenye kutubia, nk; kama ilivyoelezwa katika Sura zilizotangulia kama aya inayosema: "Ili Allah apate kuwapambanua walio wabaya na walio wazuri ." (8:37).
Kwa hiyo aya hizo zinahukumia aya hizi mbili, kwani mwenye kuharibikiwa na amali yake ya heri, ni kuwa hana amali ya heri atakayoiona. Na juu ya mfano huu unaweza kukisia na kufahamu..
Utafiti Wa Hadith Katika Durril Manthur, ametoa Ibn Murdawayh na Bayhaqi kutoka jwa Anas bin Malik, kwamba Mtume(s.a.w.w) amesema: "Hakika Ardhi itatoa habari siku ya Kiyama kila lililofanywa juu ya mgongo wake, na akasoma Mtume(s.a.w.w) : "Itakapotetemeshwa ardhi huo mtetemeko wake" mapaka alipofikia: "Siku hiyo itatoa habari zake" akasema " Je, mnajua habari yake? Jibril amenijia akaniambia kuwa; kitakapokuwa Kiyama ardhi itatoa habari ya kila yaliyofanywa juu ya mgongo wake". Na imepokewa hadith ya mfano huo kwa Abu Huraira.
Ametoa Hussein bin Sufiani na Abu Naim kutoka kwa Shaddad bin Aus; amesema: Nimemsikia Mtume(s.a.w.w) akisema: "Enyi watu, hakika dunia ni maonyesho ya sasa hivi anakula mwema na muovo. Na hakika Akhera ni kiaga cha kweli, atahukumu huko Mfalme muweza, itathibiti haki na itabatilika batili, Enyi watu kuweni watoto wa akhera wala msiwe watoto wa dunia, kwani kila mtoto humfuata mama yake. Fanyeni amali kwa tahadhari. Jueni kwamba mtaonyeshwa amali zenu na mtakutana na Mwenyezi Mungu. Basi mwenye kufanya wema (hata) uzani wa sisimizi atauona na mwenye kufanya uovu (hata) uzani wa sisimizi atauona! Katika Tafsiri ya Qummi, kuhusu Aya Na 2, amesema: Mizigo ni watu. Na kuhusu aya 4-6 amesema: Yatakuja makundi ya waumin, makafiri na ya wanafiki ili waone matendo yao. Katika riwAya Na Abu Jarudi kutoka kwa Ab Jaffar(a.s) kuhusu Aya Na 7-8 anasema: Ikiwa mtu ni katika watu wa motoni na amefanya amali ya heri ya uzani wa sisimizi itakuwa ni majuto ikiwa ameifanya siyo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na akiwa ni mtu wa peponi na amefanya amali ya shari ya uzani wa sisimizi, ataonyeshwa shari hiyo, kisha atasamehewa.
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema , Mwenye kurehemu.
وَالْعَادِيَاتِ ضَبْحًا ﴿١﴾
1. Naapa kwa farasi wanaokwenda mbio wakihema.
فَالْمُورِيَاتِ قَدْحًا ﴿٢﴾
2. Wanaotoa moto, kwa kupiga kwata.
فَالْمُغِيرَاتِ صُبْحًا ﴿٣﴾
3. Wanaowashambulia maadui ghafla wakati wa asubuhi.
فَأَثَرْنَ بِهِ نَقْعًا ﴿٤﴾
4. Wakatifua vumbi wakati huo.
فَوَسَطْنَ بِهِ جَمْعًا ﴿٥﴾
5. Wakaliingilia kati wakati huo kundi (la maadui).
إِنَّ الْإِنسَانَ لِرَبِّهِ لَكَنُودٌ ﴿٦﴾
6. Hakika mwanadamu ni mwenye utovu wa shukrani sana kwa Mola wake.
وَإِنَّهُ عَلَىٰ ذَٰلِكَ لَشَهِيدٌ ﴿٧﴾
7. Na yeye ni shahidi wa hilo.
وَإِنَّهُ لِحُبِّ الْخَيْرِ لَشَدِيدٌ ﴿٨﴾
8. Na hakika yeye kwa sababu ya kupenda mali ni bakhili.
أَفَلَا يَعْلَمُ إِذَا بُعْثِرَ مَا فِي الْقُبُورِ ﴿٩﴾
9. Je, hajuwi watakapofufuliwa waliomo makaburini.
وَحُصِّلَ مَا فِي الصُّدُورِ ﴿١٠﴾
10. Yakadhihirishwa yalipo nyoyoni.
إِنَّ رَبَّهُم بِهِمْ يَوْمَئِذٍ لَّخَبِيرٌ ﴿١١﴾
11.Hakika Mola wao siku hiyo ni mjuzi mno wa hali zao.
Sura inataja ukanushaji wa mtu kwa neema ya Mola wake na kupenda kwake sana heri. Na yeye atahisabiwa juu ya hayo. Sura hii imeshuka Madina kwa ushahidi wa habari ya vita inayoelezwa katika Sura hiyo kwa mfano: "Naapa kwa farasi wa wapigania Jihadi"; kama yatakavyokuja maelezo yake. Na vita vya jihadi vilianza baada ya Hijra. (kuhama wa Mtume(s.a.w.w) . Hayo yanatiliwa nguvu na hadith zilizopokewa na Shia kutoka Maimamu wa Ahlul Bait kuwa, Sura hiyo ilishuka kwa ajili ya Ali(a.s) katika vita vya Salasil (Minyororo). Yatakuja maelezo yake katika utafiti wa hadith (Inshallah) kwa kufuatana na mapokezi ya Ahli Sunnah.
Mwenyezi Mungu anaapa kwa farasi wanaokwenda mbio wakihema; yaani wakitoa sauti ya pumzi mbele ya maadui na hali hiyo ni maarufu kwa farasi, ingawaje inadaiwa kuwa wanyama wengine wanayo. Maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu anaapa kwa jeshi lililo na farasi wa namna hiyo. Imesemwa kuwa makusudio yake ni ngamia wa mahujaji wanapokuwa Mina siku wa Nahr (ya kuchinja). Na pia imesemwa kuwa ni ngamia wa vita. Lakini aya zinazofuata hazionyeshi kuwa makusudio yake ni ngamia !
Yaani farasi wanaotoa moto kwa kupiga kwato katika mawe au ardhi ngumu. Imesemwa kuwa makusudio ya kuwasha moto hapa ni hila za wanaume katika vita. Na imesemwa kuwa ni kuwasha moto tu! Na pia imesemwa kuwa makusudio ni ndimi za wanaume zinazowasha moto kutokana na uzito wa yale wanayoyasema. Lakini njia zote hizo ni dhaifu kwa dhahiri kabisa.
Wanatajwa farasi kuwa ndiyo wenye kushambulia maadui kwa njia ya fumbo kwa maana ya wenye farasi hao.
Watawatimulia vumbi maadui kutokana na mashambulizi.
Yaani kuliingilia kati kundi la maadui. Imesemwa kuwa maana yake ni kuingia kati ngamia katika Mina siku ya Hijja. Lakini kuzifikiria aya zote tano kuwa na maana ya ngamia wa mahujaji wanaomiminika kwenda Mina, ni kinyume kabisa. Ilivyo hasa makusudio yake ni farasi wa vitani. Na mpangilio wa aya inayosema: (Wanaoshambulia maadui ghafla wakati wa asubuhi:) na (wakaingia katikati ya kundi), unafahamishwa kuwa Mwenyezi Mungu anaapa kwa farasi wa vita. Ne herufi fa katika aya nne, inafahamisha mpangilio wa kufuatana kila moja baada ya nyingine.
Ni jawabu ya Qasam (kiapo) inayotolea habari yale yaliyo katika tabia ya mtu, kama kufuata matamanio, kuyavamia na mambo ya dunia yanayokwisha na kuacha kumshukuru Mola wake juu ya alivyomneemesha. Inaonyesha aina ya watu wanaoshambuliwa. Inaonyesha kuwa makusudio ya kukanusha kwao, ni kukanusha neema ya uislamu aliyowaneemesha Mwenyezi Mungu juu yao. Nayo ni neema kubwa waliyopewa na kutengeneza vizuri maisha yao ya dunia na wema wa maisha yao mengine ya milele.
Dhamira katika neno "na yeye" inamrudia mtu, kwa hiyo makusudio yanakuwa: mtu yeye mwenyewe anashuhudia juu ya kukanusha na kukufuru kwake. Kwa hiyo aya iko katika maana ya aya nyengine inayosema: "Bali mtu juu ya nafsi yake ni mwenye kushuhudia ". (75:14).
Na imesemwa kuwa dhamira inamrudia Mwenyezi Mungu, kwa maana kuwa yeye Mwenyezi Mungu ni shahidi. Lakini mpangilio wa dhamira hauliwafiki hilo.
Neno Khayr hapa limekuja kwa maana ya mali, yaani mtu kwa ajili ya kupenda sana mali anakuwa bakhili. Imesemwa kuwa makusudio yake ni hakika mtu ni mwingi wa kupenda mali na hilo linampelekea kujuzuwiya na kutoa haki ya Mwenyezi Mungu na kutoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Namna hii wamefasiri. Lakini hayo hayaweki mbali kuwa makusudio ya Khayr ni kheri ya aina yoyote. Na kwamba kupenda kheri ni maumbile ya kiutu, ndipo mtu anaona anasa za dunia ndio kheri, kwa hiyo zinamuingia na zinamsahauliza kumshukuru Mola wake.
Yaliyo katika nyoyo ni sifa ya imani au ukafiri, kama alivyosema Mwenyezi Mungu "Siku itakayofuniliwa siri ". (87:9).
Na maana kwa ujumla - na Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi - ni kuwa; hivi hajui mtu kuwa kwa sababu ya kukanusha kwake na kumkufuru kwake Mola wake atalipwa? Wakati watakapotolewa waliomo makaburini na kudhihirishwa siri za nafsi, miongoni mwa imani na kufuru na utii na uasi. Hakika Mola wao, siku hiyo ni mjuzi mno wa hali zao, kwa hiyo atawalipa.
Utafiti Wa Hadith Katika Majmau imesemwa kuwa; Mtume(s.a.w.w) alipeleka kikosi katika makao ya ukoo wa Kinana kikiongozwa na El-Mundir bin Amri El-Ansari mmoja wa Makamanda. Walipochelewa kurudi, Mwenyezi Mungu akampa khabari Mtume(s.a.w.w) kwa kusema: "Naapa kwa farasi wenye kwenda mbio wenye kuhema." Imesemwa kuwa Sura hii ilishuka wakati Mtume(s.a.w.w) alipompeleka Ali(a.s) kwa Dhatus-Salasil (Wenye Minyororo) na akawashinda. Na hilo ni baada ya kuwapeleka masahaba wengine mara nyingi. Wote wakarudi kwa Mtume bila ya kufaulu. Hadith hii imepokewa kutoka kwa Abu Abdillah(a.s) katika hadith ndefu. Na vita hivyo viliitwa vya minyororo kwa sababu baadhi yao walitekwa, wakauawa na wakafungwa mateka kwa kamba za mikoni kama vile wamefungwa na nyororo.
Utafiti Wa Hadith Iliposhuka Sura hii Mtume(s.a.w.w) alitoka akawaswalisha watu swala ya asubuhi na akasoma katika swala Sura hiyo. Alipomaliza kuswali masahaba zake wakasema: "Sura hii haituijui", Mtume(s.a.w.w) akasema: "Ndio hakika Ali amewashinda maadui wa Mwenyezi Mungu na Jibrail amenifahamisha hilo usiku huu. Baada ya siku kidogo Ali akafika pamoja na ngawira na mateka kadhaa ."