9
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
SURA INSHIQAAQ (KUPASUKA)( NA: 84)
INA AYA 24
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
إِذَا السَّمَاءُ انشَقَّتْ ﴿١﴾
1. Mbingu zitakapopasuka.
وَأَذِنَتْ لِرَبِّهَا وَحُقَّتْ ﴿٢﴾
2. Zikamtii Mola wake na zikafanya ndivyo.
وَإِذَا الْأَرْضُ مُدَّتْ ﴿٣﴾
3. Na ardhi itakaponyooshwa.
وَأَلْقَتْ مَا فِيهَا وَتَخَلَّتْ ﴿٤﴾
4. Ikatupa vilivyomo na ikawa tupu;
وَأَذِنَتْ لِرَبِّهَا وَحُقَّتْ ﴿٥﴾
5. Ikamtwii Mola wake na ikafanya ndivyo.
يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ إِنَّكَ كَادِحٌ إِلَىٰ رَبِّكَ كَدْحًا فَمُلَاقِيهِ ﴿٦﴾
6. Ewe mwanadamu: Hakika wewe ni mwenye kufanya juhudi mpaka (kufikilia) kwa Mola wako; basi ni mwenye kukutana naye.
فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ ﴿٧﴾
7. Ama atakayepewa kitabu chake kwa kuumeni kwake.
فَسَوْفَ يُحَاسَبُ حِسَابًا يَسِيرًا ﴿٨﴾
8. Atahisabiwa hisabu nyepesi.
وَيَنقَلِبُ إِلَىٰ أَهْلِهِ مَسْرُورًا ﴿٩﴾
9. Awarejee (atarudi kwa) watu wake huku akiwa na furaha.
وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ وَرَاءَ ظَهْرِهِ ﴿١٠﴾
10. Ama atakayepewa kitabu chake nyuma ya mgongo wake.
فَسَوْفَ يَدْعُو ثُبُورًا ﴿١١﴾
11. Yeye atauita ole wake.
وَيَصْلَىٰ سَعِيرًا ﴿١٢﴾
12. Aingie na motoni.
إِنَّهُ كَانَ فِي أَهْلِهِ مَسْرُورًا ﴿١٣﴾
13. Maana yeye alikuwa kati ya watu wake (ulimwenguni) ni mwenye furaha.
إِنَّهُ ظَنَّ أَن لَّن يَحُورَ ﴿١٤﴾
14. Kwa kudhaani kwamba hatarejea (kwa Mola wake).
بَلَىٰ إِنَّ رَبَّهُ كَانَ بِهِ بَصِيرًا ﴿١٥﴾
15. Kwani? Hakika Mola wake alikuwa akimjua.
فَلَا أُقْسِمُ بِالشَّفَقِ ﴿١٦﴾
16. Naapa kwa mawingu mekundu.
وَاللَّيْلِ وَمَا وَسَقَ ﴿١٧﴾
17. Na usiku na ulichokikusanya.
وَالْقَمَرِ إِذَا اتَّسَقَ ﴿١٨﴾
18. Na mwezi unapotimia.
لَتَرْكَبُنَّ طَبَقًا عَن طَبَقٍ ﴿١٩﴾
19. Mtakutana na hali baada ya hali.
فَمَا لَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٢٠﴾
20. Basi wananini hao hawaamini.
وَإِذَا قُرِئَ عَلَيْهِمُ الْقُرْآنُ لَا يَسْجُدُونَ ﴿٢١﴾
21. Na wanaposomewa Qur'an hawanyenyekei.
بَلِ الَّذِينَ كَفَرُوا يُكَذِّبُونَ ﴿٢٢﴾
22. Bali wale ambao wamekufuru hukadhibishwa.
وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا يُوعُونَ ﴿٢٣﴾
23. Na Allah ni mjuzi wa waliyoyakusanya.
فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٢٤﴾
24. Basi wape habari ya adhabu yenye uchungu.
إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ أَجْرٌ غَيْرُ مَمْنُونٍ ﴿٢٥﴾
25. Ila wale ambao wameamini wakatenda amali njema (wao) watapata malipo mema yasiyokoma.
Sura inaishiria kusimama Kiyama na inakumbusha kwamba mtu ni mwenye kwenda kwa Mola wake mpaka akutane naye atamuhisabu kwa mujibu wa kitabu chake. Sura hii inatilia mkazo jambo hilo na pia imesisitiza zaidi upande wa maonyo kuliko ule na biashara. Mpangilio wa aya ni wa Makka.
Ni sharti ambalo jawabu lake limeondolewa kukadiria kwake ni: Mbingu zitakapopasuka, mtu atakutana na Mola wake atahisabiwa na kulipwa yale aliyoyatenda. Kupasuka kwa mbingu ni katika alama za Kiyama kama kukunjwa jua, kukutana jua na mwezi, kupuputika nyota, n.k.
Kusikiliza ni fumbo, maana yake ni kutii na kufuata. Kufanya ndivyo: ni kufanya ndivyo huko kumtii na kufuata; yaani zikamtii Mola wake na zikafanya ndivyo kumtii na kumfuata.
Kwa dhahiri makusudio ni kufanywa pana ardhi; Mwenyezi Mungu anasema: "Siku ambayo ardhi hii itabadililishwa kuwa ardhi nyengine ." (14:48).
Yaani itatupa vilivyomo ndani yake katika wafu na kuwa tupu. Imesemwa kuwa makusudio ni kutupa wafu na hazina; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na ikatoa ardhi mizigo yake " (99:2) Imesemwa maana ni kutupa vilivyo ndani yake nakuwa tupu na vitu vilivyo juu yake miongoni mwa majabali na bahari. Huenda maelezo ya kwanza ndiyo yaliyo karibu zaidi na maana.
Dhamiri hapa ni ya ardhi na maana ni kama yaliyotangulia katika mbingu.
Anasema Raghib maana ya neno Kad-h ni kwenda na kufanya juhudi. Na imesemwa maana yake ni juhudi ya nafsi katika amali. Kwa hivyo maana itakuwa ni kwenda, kwa dalili ya herufi ila yenye maana ya mpaka. Kauli ya: "basi ni mwenye kukutana naye" (kuwa katika hukumu yake) inaungana na neno kad-h. Mwenyezi Mungu amebainisha kwa neno hii (Kad-h) kwamba ukomo na mwenendo huu na mahangaiko haya ni kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t), kwa kuwa yeye ndiye Mola Mlezi. Yaani, kwa kuwa mtu ni kiumbe mwenye kulelewa, kumiliki na mwenye akili, daima ni mwenye kuelekea kwa Mwenyezi Mungu kawa sababu yeye ndiye Mola wake mwenye kupanga mambo yake. Mja hajiamulii mwenyewe alitakalo au alifanyalo. Yeye anao uwezo wa kutaka, lakini anafanya tu lile alilolitaka Mwenyezi Mungu na kumwamuru alifanye, sababu yeye ndiye bwana wake. Hivyo mja anachukua jukumu la aliyoyapenda na kuyatenda.
Kwa hivyo hapa yanadhihiri mambo haya:
Kwanza : "Hakika wewe ni mwenye kufanya juhudi mpaka (kufikilia) kwa Mola wako" ni hoja huu ya marejeo ya Kiyama kwa vile ulivyo kuwa ubwana hautimii ila pamoja na jukumu na utumwa, wala hautimii utumwa ila pamoja na jukumu na halimtii jukumu ila kwa kurejea na kuhisabiwa na hakutimu kuhisabiwa ila kwa malipo.
Pili : Kwamba makusudio ya kukutana naye ni kuishia kwake, ambako hakuna hukumu isipokuwa hukumu yake bila ya kuweko kuziwizi chochote.
Tatu : Mwenye kuambiwa ni jinsi ya mtu yeyote, hivyo ulezi wa Mungu ni wenye kuenea kwa kila mtu.
Ni ufafanuzi wa mpangilio juu ya yale yalioelezewa na aya iliyotangulia, kwamba kuna marejeo na maswali juu ya amali na hesabu, na makusudio ya kitabu ni karatasi ya matendo (amali).
Hisabu nyepesi ni ile iliyosahilishwa na ikawa haina malumbano yoyote.
Makusudio ya watu wake hapa ni wale aliomwanadalia Mwenyezi Mungu katika pepo miongoni mwa Hurulaini, watumishi, n.k. Haya ndiyo yanayofahamika kutokana na mpangilio wa aya. Imesemwa kuwa makusudio ni jamaa zake waumini atakaoingia nao peponi, Imesemwa kuwa waumini hata kama sio jamaa zake; kwa sababu waumini wote ni ndugu. Njia zote mbili haziepukani kuwa ziko mbali zaidi na maana.
Huenda ikawa kupewa vitabu vyao nyuma ya migongo yao ni kwa sababu ya kugeuzwa nyuso zao visogoni mwao kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "..kabla hatujazigeuza nyuso tukazipeleka kisogoni. ." (4:47).
Hapana mgongano kati ya kupewa vitabu vyao nyuma ya migongo yao na kupewa kushotoni mwao; kama ilivyo katika kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Ama atakayepewa kitabu chake katika mkono wake wa kushoto. Basi atasema Oo! Laiti nisingelipewa daftari langu ."(69:25).
Yatakuja maelezo zaidi kuhusu maana ya kupewa kitabu nyuma ya migongo katika utafiti wa hadith (Inshallah).
Yaani atakaposema kitabu chake ataita "Oo kuangamia.
Yaani moto wenye joto kali ambao hauna mfano kwa adhabu yake wala hauna kiasi kwa joto lake.
Yalimfurahisha yale aliyokuwa akiyapata katika starehe za dunia na kuvutika na anasa za dunia. Hilo lilimsahaulisha mambo ya akhera. Mwenyezi Mungu anaishutumu furaha ya mtu kutokana na kheri za dunia anazozipata na ameiita furaha pasi na haki. Anasema Mwenyezi Mungu baada ya kuutaja moto na adhabu yake: "Haya (yaliyowapata) ni kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyafurahia duniani pasi na haki na yale mliyokuwa mkijivunia ." (40:75)
Makusudio ni kurejea kwa ajili ya hisabu na malipo. Hakuna kinachomsababisha kudhania hivyo isipokuwa kujiingiza katika dhambi kunakopelekea kuona kufufuliwa ni jambo lisilo wezekana.
Ni jibu la dhana yake; kwamba sio hivyo anavyodhania, kwani hakika Mwenyezi Mungu(s.w.t) ndiye Mola wake na mfalme wake mwenye kuzingatia jambo lake. Anamjua na kuona yote aliyokuwa akiyafanya katika matendo yake. Na matendo yake yana malipo mema au mabaya. Kwa hiyo hapana budi kurudi kwake na amlipe yale yanayostahiki matendo yake. Kwa hali hiyo inadhihiri kuwa kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Hakika mola wake alikuwa akimwona" ni katika kutoa hoja juu ya kupasa marejeo; aya hii ni kama ile iliyotangulia katika kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Hakika wewe ni mwenye kufanya juhudi mpaka (kufikilia) kwa Mola wako."
Vile vile inadhihiri kutokana na mkusanyiko wa aya hizi tisa, kwamba utoaji wa vitabu ni kabla ya hisabu kama kunavyofahamisha kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Na kila mtu tumemfungia vitendo vyake shingoni mwake; na tutamtolea siku ya Kiyama daftari atakayoikuta imekunjuliwa. (Ataambiwa), Soma daftari yako, hii leo nafsi yako inatosha kukuhisabu ." (17;13).
Ni wekundu unaofuatiwa na manjano kisha weupe ambao unatokea magharibi mwanzo wa usiku
Yaani kukusanya vile vilivyotawanyika wakati wa mchana miongoni wa watu na wanyama kwani wao hytawanyika mchana na kurudi katika makazi yao usiku na kutulia. Baadhi wamefasiri neno Wasaq kwa maana ya kufukuza yaani usiku unazifukuza nyota kutoka katika kujificha kwenda kwenye kudhihiri.
Yaani kukusanyika nuru yake na kuwa mwezi mtimilifu.
Ni jawabu la kiapo. Makusudio yake ni mtakutana na hali baada ya hali kwa namna yoyote yatakavyokuwa masafa anayoyakata mtu katika kufikia kwa Mola wake, kutoka katika maisha ya dunia, kisha mauti kisha maisha ya Barzakh, kisha kwenda akhera kisha maisha ya akhera kisha hesabu na malipo. Kiapo - kama unavyoona - ni kutilia mkazo yale yalio katika aya ya 6 na yaliyo baada yake katika hanari za ufufuo Aya hii pia inaonyesha kuwa vipindi anavyopitia mtu ni vyenye kupangwa katika kumfikia Mola wake.
Ni swali la kustaajabu na kutayarisha, kwa hiyo limeoana na mgeuko huu wa ghafla kutoka kwenye mazungumzo ya ana kwa ana na kuwa anamzungumzia mtu mwingine asiyekuwepo; kana kwamba yeye alipowaona kuwa hawaidhiki kwa waadhi wake, aliachana nao na kumwelekea Mtume kwa kumwambia: "wana nini hao hawaamini"
Yaani hawakuacha imani kwa sababu ya upungufu wa ubainifu, au kwisha dalili, bali wao wamefuata majadi wao na viongozi wao, wakazama katika kufuru na wakaendelea na kukadhibisha. Mwenyezi Mungu anayajua waliyoyakusanya katika nyoyo na waliyoyaficha katika nyoyo zao, miongoni mwa ukafiri na ushirikina. Imesemwa kuwa makusudio yake ni kuwa wana kitu walichoficha katika nyoyo zao ambacho hakiwezi kuelezwa kwa ibara yoyote: Hakijui isipokuwa Mwenyezi Mungu tu! Lakini maelezo hayo yako mbali na mpangilio wa aya. Kuita maonyo ya adhabu kuwa ni biashara hii ni namna Fulani ya mabezo. Jumla hii ni fungu la (malipo ya) kukadhibisa.
Hapo wanavuliwa na hayo walio amini.
Utafiti Wa Hadithi Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu "mbingu zitakapopasuka" amesema ni siku ya Kiyama. Katika Durril-Manthur ametoa Ibn Abu Hatim kutoka kwa Ali amesema : Itapasuka mbingu hii yenye nyota. Katika Tafsiri ya Qummi: Na ardhi itakaponyooshwa, ikatupa vilivyomo, na ikawa tupu, amesema itanyooshwa ardhi itapasuka wa watatoka watu. Katika Durril Manthur ametoa Hakim kwa isnadi nzuri kutoka kwa Jabir naye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) amesema: itanyooshwa ardhi siku ya Kiyama kama inavyonyooshwa ngozi kisha mwanadamu hatakuwa na mahali isipokuwa mahali pa nyayo zake.
Katika Ihtijaj kutoka kwa Ali(a.s) katika hadith amesema: watu siku hiyo watakuwa na sifa na daraja mbali mbali. Kuna katika wao atakayehisabiwa hisabu nyepesi na kurudi kwa watu wake huku akiwa na furaha, na katika wao kuna ambao wataingia peponi bila ya hisabu kwa sababu hawakuvaana na jambo lolote la dunia. Hii ni kwa sababu kisabu huko ni kwa wale waliovaana na dunia. Na muka katika wao watakaohisabiwa hisabu isiyopungua hata chembe na kuwa katika adhabu ya moto mkali.
Katika Maani kwa isnadi yake kutoka kwa Ibn Abu Jaffar(a.s) amesema: Amesema Mtume(s.a.w.w) kila mwenye kuhisabiwa ni mwenye kuadhibiwa akaambiwa: "Basi nini maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) "Atahisabiwa hisabu nyepesi?" Akasema: Hilo ni kwa kusamehe. Imepokewa hadith mfano wa hiyo katika Durril Manthur kutoka kwa Bukhari, Muslim, Tirmidhi na wengineo kutoka kwa Aisha.
Katika Tafsir ya Qummi katika riwaya ya Abul-Jarud kutoka kwa Abu Jaffar(a.s) kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu: "Ama atakayepewa kitabu chake kwa kuumeni kwake" yeye ni Abu Salama Abdulla bin Abdul-Aswad bin Hilal Al-Makhzumi. "Ama mwenye kupewa kitabu chake nyuma ya mgongo wake" ni ndugu yake ambaye ni Al-Aswad bin Abdul-Aswad Al-Makhzumiy aliyeuliwa na Hamza bin Abdul-Muttalib siku ya vita vya BAdr.
Katika Majmau kauli yake Mwenyezi Mungu: "Mtakutana na hali baada ya hali". Amesema: Maana yake ni shida baada ya shida ya uhai kisha mauti, kisha kufufuliwa, kisha malipo. Hadithi hiyo imepokewa marfui. Katika Jawaamiul-Jami kuhusu aya hiyo hiyo, kutoka kwa Abu Abayadah: Mtakutana na desturi ya waliokuwa kabla yenu na hali zao. Na yamepokewa hayo kutoka kwa Imam Sadiq(a.s) .