11
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
SURA TARIQ (CHENYE KUJA USIKU) (NA. 86)
INA AYA 17
Kwa Jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
وَالسَّمَاءِ وَالطَّارِقِ ﴿١﴾
1. Naapa kwa mbingu na chenye kuja usiku.
وَمَا أَدْرَاكَ مَا الطَّارِقُ ﴿٢﴾
2. Na lipi la kukujulisha ni nini chenye kuja siku.
النَّجْمُ الثَّاقِبُ ﴿٣﴾
3. Ni nyota inayong'ara usiku.
إِن كُلُّ نَفْسٍ لَّمَّا عَلَيْهَا حَافِظٌ ﴿٤﴾
4. Hakuna nafsi isipokuwa kuna mwenye kuitunza.
فَلْيَنظُرِ الْإِنسَانُ مِمَّ خُلِقَ ﴿٥﴾
5. Basi mtu na ajitazame ameumbwa kwa kitu gani..
خُلِقَ مِن مَّاءٍ دَافِقٍ ﴿٦﴾
6. Ameumbwa kwa maji yanayotoka kwa nguvu.
يَخْرُجُ مِن بَيْنِ الصُّلْبِ وَالتَّرَائِبِ ﴿٧﴾
7. Yanayotoka baina ya uti wa mgongo na mifupa ya kifua.
إِنَّهُ عَلَىٰ رَجْعِهِ لَقَادِرٌ ﴿٨﴾
8. Hakika yeye ni mweza wa kumrejeza.
يَوْمَ تُبْلَى السَّرَائِرُ ﴿٩﴾
9. Siku zaitakapofunuliwa siri.
فَمَا لَهُ مِن قُوَّةٍ وَلَا نَاصِرٍ ﴿١٠﴾
10. Basi hatakuwa na nguvu wala wa kumnusuru.
وَالسَّمَاءِ ذَاتِ الرَّجْعِ ﴿١١﴾
11. Naapa kwa mbingu yenye kurudi.
وَالْأَرْضِ ذَاتِ الصَّدْعِ ﴿١٢﴾
12. Na ardhi yenye mipasuko.
إِنَّهُ لَقَوْلٌ فَصْلٌ ﴿١٣﴾
13. Hakika hii (Qur'an) ni kauli yenye kupambanua.
وَمَا هُوَ بِالْهَزْلِ ﴿١٤﴾
14. Wala si upuuzi.
إِنَّهُمْ يَكِيدُونَ كَيْدًا ﴿١٥﴾
15. Hakika wao wanakuchimbia vitimbi.
وَأَكِيدُ كَيْدًا ﴿١٦﴾
16. Nami (pia) ninawachimbia vitimbi.
فَمَهِّلِ الْكَافِرِينَ أَمْهِلْهُمْ رُوَيْدًا ﴿١٧﴾
17. Basi wape muhula makafiri wape muhula kidogo.
Katika Sura hii kuna maonyo kwa marejeo ya akhera na kufufuliwa. Na hayo yanafamisha uwezo wake Mwenyezi Mungu. Na inamalizia Sura kwa kueleza kiaga cha makafiri. Sura hii imeshuka Makka bila ya ubishi.
Neno Twariq asili yake- kama ilivyosemwa- ni kugonga kiasi cha kutoa sauti, miongoni mwao, ni nyundo na lina maana njia. Njia imeitwa hivyo kwa vile mpita njia anaigonga kwa nyayo zake. Kywa hivyo likaenea neno hilo kutumiwa kwa njia, kisha likahusishwa na kuja usiku, kwa sababu mwenye kuja usiku aghlabu hukuta milango imefungwa, kwa hiyo hugonga, kisha likaenea hilo neno kwa kila chenye kuhidhiri usiku. Makusudio ya neno hilo katika aya ni nyota yenye kutokeza usiku. Neno Thaqb asili yake ni kupasua; kisha likawa ni nuru yenye kuangaza, kwa sababu inapasua giza, na linakuja kwa maana ya kuwa juu kama kusema: imepaa juu ndege, nikama vile inapasua anga kwa kuruka kwake. Kwa hivyo makusudio ya Aya Na kwanza ni kuapa kwa mbingu na nyota inayotokeza usiku. Na Aya Na pili ni kwa ajili ya kulikuza jambo la chenye kuapiwa ambacho ni hicho chenye kutokeza usiku. Aya Na tatu ni ubainifu wa hicho chenye kutokeza usiku. Jumla hiyo ni jawabu ya swali.
Ni jawabu la kiapo. Herufi Lamma ni kwa maana ya illa (isipokuwa). Makusidio ya kutunza hapa ni kuandika matendo yake mema na maovu, ili yaweze kuhisabiwa siku ya Kiyama na kulipwa. Kwa hivyo mtunzaji ni malaika na chenye kutunzwa ni matendo, kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na hakika mna wenye kuwatunza watukufu wenye kuandika ." (82:10-11).
Sio mbali kuwa makusudio ni kutunza nafsi dhati yake na vitendo vyake, kwa hiyo inafahamisha kuwa nafsi ni zenye kutunzwa hazimaliziki kwa mauti wala haziharibiki mpaka Mwenyezi Mungu atakapovifufua viwiliviwili, atavirudisha nafsi na atakuwa mtu kama alivyokuwa mtu wa duniani kwa dhati yake; kisha alipwe kwa mujibu wa vitendo vyake vyenye kuchungwa, vikiwa ni kheri au shari. Hilo linatiliwa nguvu na aya nyingi zinazofahamisha juu ya kutunzwa vitu, kama vile kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Sema atawaua Malaika wa mauti aliye wakilishwa kwenu kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu. " (32:11).
"Allah huzichukua roha wakati wa mauti yake na zile zisizokufa katika usingizi wao. Basi huzizuwiya zile alizozihukumia mauti. ." (39:42).
Hayo hayakanushi dhahiri ya Aya Na Sura ya (82:10).
kuwa kutunza kwa Malaika ni kuandika, kwa sababu kuitunza nafsi pia kutokana na kuandika kama anavyofahamisha Mwenyezi Mungu kwa kusema: "Hakika sisi tulikuwa tukiandika yale aliyokuwa mkiyatenda ." (45:29).
Kwa njia hii kunabatilika kutia makosa juu ya yale yanayofahamisha juu ya marejeo ya Kiyama katika kuenea Kudura, kwamba kumrusisha mtu kwa dhati yake ni muhali kwa sababu mtu ataumbwa tena mara ya pili mfano wa yule mtu wa duniani aliyeumbwa kwanza, lakini si yule yule na mfano wa kitu sio kitu chenyewe. Njia ya kubatilisha hoja hiyo ni kwamba: utu wa mtu unatokana na mtu kwa nafsi yake sio kwa kiwilikiwili chake na nafsi ni yenye kihifadhiwa kwa hivyo akiumba kiwilikiwili na kukifungamanisha na nafsi atakuwa ndiya yule yule mtu wa duniani kwa utu wake, ijapokuwa sio dhati yake.
Yaani aangalie nini mwanzo wa umbile lake? Na ni kitu gani ambacho Mwenyezi Mungu amekifanya kuwa mtu? Jumla hii ni mtiririko wa aya iliyotangulia. Maana yanavyofahamisha kutokana na mpangilio wake, ni kwamba, ikiwa kila nafsi ni yenye kuhifadhiwa kwa dhati yake na vitendo vyake, bila ya kwisha hiyo nafsi na kusahauliwa vitendo vyake basi akubali mtu ukweli kwamba yeye atarudi kwa Mola wake na kulipwa aliyoyatenda, wala hilo asilihisabu kuwa ni mbali. Naangalie ukweli huu kwenye asili ya umbile lake na akumbuke kwamba yeye ameumbwa kwa maji yanayoka kwa nguvu yanayotoka baina ya uti wa mgongo na mifupa ya kifua. Basi yule aliyeanza kumuumba kutokana na maji haya anaweza kumrudisha na kumuhuisha baada ya mauti.
Maji yenye kutoka kwa kuruka ni manii. Jumla hiyo iko katika jawabu la swali.
Neno Sulb lina maana ya mgongo na Taraib ni mifupa wa kifua. Wamehitalifiana kiajabu kwenye matamko yao katika aya hii na iliyo kabla yake. Kwa dhahiri makusudio yake ni sehemu iliyokatikati ya uti wa mgongo na mifupa ya kifua.
Yaani ambaye amemuumba mtu kutokana na maji, sifa yake ni hiyo hiyo, ni mwenye kuweza kumrudisha na kumuhuisha baada ya mauti.
Aya Na 9: Ni siku yatakayofichuka yale alioyoyaficha mtu na kuyafanya siri katika itikadi na matendo ya kheri au ya shari. Aya hii iko katika maana ya aya inayosema "Na mkidhihirisha yaliyomo katika nyoyo zenu au mkiyafichua, Allah atawataka hisabu ya (yote) hayo ." (2:284)
Hana uwezo katika nafsi yake utakaomzuia na adhabu ya Mwenyezi Mungu wala hana wa kumnusuru atakayemkinga na adhabu yaani hakutakuwa na uwezo wowote utakaomkinga na shari kutoka kwake au kwa mtu mwengine.
Kiapo baadha ya kiapo, ni kwa ajili ya kutilia mkazo jambo la Kiyama na kurejea kwa Mungu. Makusudio ya kurudi ni kuhisi kwenda kwake kwa kuchimbuka nyota na kutua. Imesemwa kuwa makusudio yake ni mvua. Makusudio ya kupasuka ni kupasuka kwa ajili ya mimea.
Maana ya neno Fasl ni kupambanua kati ya vitu viwili. Aya hizi mbili ni jawabu la kiapo kwa maana; ninaapa kwa hivyo nilivyoviapia hakika Qur'an ni neno lenye kupambanua kati ya haki na batili na sio maneno yasiyokuwa na maana. Yale inayoyahakikisha ni haki isiyokuwa na shaka na yale inayoya batilisha ni batili isiyokuwa na shaka. Kwa hiyo yale iliyoyatolea habari katika ufufuo na marejeo ni haki isiyokuwa na shaka ndani yake. Imesemekana kuwa dhamiri katika neno Innahu ni ya hayo yaliyotangulia kuelezwa katika habari ya marejeo lakini tuliyoyaeleza mwanzo ndiyo yanayoelekea zaidi.
Yaani makafiri wanaichimba vitimbi wakikusudia kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu na kubatilisha mlingano wako.
Ikiwa wao wanavyo vitimbi na mimi ninavyo vitimbi. Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kushinda juu ya jambo lake, kwa hivyo wangojee tu; wala usifanye haraka, ngoja kidogo tu! Yatawajia yale waliyoahidiwa, na kila linalokuja liko karibu.
Utafiti Wa Hadithi Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu kusema kwake Mwenyezi Mungu "Hakika kila nafsi ina mwenye kuichunga" amesema ni Malaika. Na kuhusu "Ameumbwa kwa maji yanayotoka kwa nguvu" amesema ni manii ambayo hutoka kwa nguvu". Kuhusu "yanayotoka kati ya uti wa mgongo na mifupa ya kifua" amesema uti wa mgongo ni mwanaume na mifupa ya kifua ni mwanamke. Katika Majmau imepokewa hadith marfuu kutoka kwa Abu Dardai amesema: "Amesema Mtume(s.a.w.w) :Amedhamini Mwenyezi Mungu kuumba kwake vitu vine: Swala, Zaka, Kufunga Ramdhan na kuoga janaba na hizo ndizo siri alizozisema Mwenyezi Mungu "Siku itakayofunuliwa siri ."
Huenda ikawa maana ya hadithi hiyo ni kutaja baadhi ya mambo ya ukweli, kama inavyotilia nguvu hilo hadithi inayofuata. Katika hiyo hiyo Majmau kutoka kwa Muadh bin Jabal amesema: "Nilimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu: ni siri zipi ambazo Mwenyezi Mungu atawafunuliwa waja katika akhera? Akasema siri zenu ni matendo yeno ya swala, kufunga, zaka, udhu, kuoga janaba na kila lenye kufaradhiwa, kwa sababu matendo yote ni siri yenye kufichamana, mtu akitaka anaweza kusema ameswali na asiwe ameswali au aseme ametawadha kumbe hakutawadha. Basi ndiyo kusema kwake Mwenyezi Mungu "siku itakayofunuliwa siri."
Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu: "Basi hatakuwa na nguvu wala wa kumnusuru." Amesema: hatakuwa na nguvu yoyote kwa muumba wake wala wa kumnusuru kama Mwenyezi Mungu akimtakia uovu. Katika hiyo Tafsiri ya Qummi amesema kuhusu neno Raj'n amesema ni mvua na ardhi yenye mipasuko ni ardhi yenye mimea. Katika Majmau kuhusu : "hakika hii Qur'an ni kauli ya haki" amesema "Hakika Qur'an inapambanua kati ya haki na batili kwa kuibainisha kila moja. Hayo yamepokewa kutoka kwa Imam Assadiq(a.s) .
Katika Durril Manthur ametoa Ibn Abi Shayba, Addarami, Tirmdhi, Muhammad bin nasr na Ibn el- Ambari katika Masahif kutoka kwa Harith el-Aa'war amesema: Niliingia msikitini mara watu wakaingia katika mazungumzo. Nikamwendea Ali nikampa habari; akasema: "Je wamekwishafanya? Mimemsikia Mtume(s.a.w.w) akisema: "Kutatokea fitna. Nikasema: Ni kitu gani cha kutokea katika fitna hiyo Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Je ni sawa hapa? Akasema:kitabu cha Mwenyezi Mungu kina habari za kabla yenu baada yenu na kimekwisha wahukumia, ni upambanuzi na sio upuuzi, mwenye kukiacha Mwenyezi Mungu kumuangamiza, mwenye kukusudia pengine Mwenyezi Mungu humpoteza .
Ni kamba madhubuti, mauidha yenye hekima na njia yenye kunyooka. Ni ambachi hakipotezi wala hawashibi nacho wanavyuoni, hazitatiziki nacho ndimi wala haiishi ajabu yake. Ndicha ambacho majini waliposikia walisema: " Hakika tumesikia Qur'an ya ajabu inaongoza kwenye uongofu." Mwenye kusema kwacho huwa mkweli, mwenye kuhukumu kwacho amefanya uadilifu na mwenye kuganya amali kwacho amepata thawabu, na mwenye kulingania kwenye kitabu hicho ameongoka katika njia iliyonyooka. Amepokea karibu na maana hayo Muadh bin Jabal kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) .