6%

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KWANZA

AL - FATIHA

BISMILLAH (UFUNGUZI)

SURA YA KWANZA KUSHUKA

Wametofautiana kuhusu mahali iliposhuka, imesemwa kuwa ni Makkah wengine wakasema ni Madina bali kuna kundi jengine linasema kuwa imeshuka mara mbili Makkah na Madina.Hata hivyo wafasiri wengi wamesema imeshuka Makkah.

Tofauti hii, kwa hakika, haina faida kwani surah hii tukufu haina Aya zozote zinazotofautiana kimaana kwa kutofautiana kushuka. Majina yake Wametaja majina mengi; yaliyo maarufu ni haya yafuatayo:-

Faatiha (ufunguzi) : Kwa sababu ndiyo sura ya kwanza katika msahafu, na ni wajibu kuisoma mwanzo wa swala. Pia mafundisho, kwa ujumla, yalikuwa yakianzwa kwa sura hiyo.

Al-Hamdu : kwa sababu ndilo tamko la mwanzo katika sura hiyo.

Ummul-Kitab na Ummul-Quran (mama wa Quran) : kwa sababu imetangulia sura nyingine, ijapokuwa ni kwa kimandishi tu.Kwani mama huwatangulia wanawe. Na kwa vile imekusanya misingi miwili; kutaja utawala wa Mungu na utumwa wa mja, na mambo mawili hayo ndiyo nguzo ya mafundisho ya Quran.

Sabu’ul-Mathani (Saba mbili) : kwa sababu ina aya saba, au ina Aya saba zinazorudiwa mara mbili katika swala, au ni kwa sababu inataja maambo mawili: Mola na mja wake.

Vyovyote iwavyo majina haya yana mwelekeo kidogo.

Ayah 1-7

﴿بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴾

1.Kwa jina la Mwenyezi Mungu,Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

﴿الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴾

2.Sifa njema (zote) ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe (vyote).

﴿لرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴾

3.Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu.

﴿ مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ﴾

4.Mwenye kumiliki Siku ya Malipo.

﴿يَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ﴾

5.Wewe tu tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada.

﴿اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ﴾

6.Tuongoze njia iliyonyooka.

﴿صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ ﴾

7.Njia ya (wale) uliowaneemesha; Sio ya (wale) waliokasirikiwa wala ya (wale) waliopotea.

SIFA NJEMA (ZOTE) NI ZA MWENYEZI MUNGU

Sifa njema (zote) ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe (vyote).

Jumla hii ni habari, kwa maana ya insha; Kwa sababu msomaji anakusudia kuleta sifa njema za Mwenyezi Mungu, wala sio kutoa habari za kuthibitisha sifa Zake njema.

Jumla hiyo ina maana ya mafunzo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa waja wake, jinsi watakavyomsifu Mwenyezi Mungu. Yaani:Semeni enyi Waja wangu! Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu.

Maana ya sifa njema (zote) ni za Mwenyezi Mungu, ni kumsifu kwa kukusudia kumwadhimisha katika hali zote, hata katika madhara. Amirul Muminin(a.s) anasema katika moja ya khutba zake za Nahjul-Balagha:

Tunamsifu Mwenyezi Mungu kwa neema zake, kama tunavyomsifu kwa balaa.

Muhammad, Ahmad, Mahmuud na Hamdaan, ni majina yaliyochukuliwa kutoka katika neno Al-Hamdu. Neno Hamd linakuja kwa kukisifu kitu unachokiridhia. Mwenyezi Mungu (s.w.t) hapa anataja Mahmuud (chenye kusifika) akisema:

﴿عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا﴾

Huenda Mola wako akakuinua cheo chenye kusifika (17:79)

Neno: Rabb linaweza kutumiwa kwa maana ya Bwana na Mwenye kumiliki.Maana zote mbili zinasihi hapa, lakini maana ya Mola Muumbaji ndiyo inayoelekea zaidi katika aya hii tukufu.

MAKUSUDIO YA ALALAMIN (VIUMBE)

Makusudio ya Alalamin (viumbe) hapa ni; kila kisichokuwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo linaenea kwa viumbe vyote.

MAANA YA RABBIL-AALAMIN (MOLA WA VIUMBE VYOTE)

Maana ya Rabbil-Aalamin (Mola wa viumbe vyote) ni Muumbaji wa kila kitu, na mwenye kupangilia vizuri.

NENO MOLA

Neon: Mola linafahamisha utukufu; yaani:Hakika mimi ninamsifu Mwenyezi Mungu kwa sababu Yeye ni Mola wa viumbe vyote.

MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

Mwingi wa rehema mwenye kurehemu: Maelezo yake yameshapita katika maelezo ya Bismillah Miongoni mwa maneno ya Amirul Muminin katika kumsifu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:Ghadhabu haimshughulishi (asiwe) na rehema wala rehema haimshughulishi (asiwe) na mateso.

Nilivyofahamu jumla mbili hizi ni kwamba ghadhabu ya Mwenyezi Mungu kwa waasi, na adhabu yao kesho, haimzuii Yeye kuwarehemu katika maisha haya wanayostarehe kwa neema yake na kwamba rehema Yake kesho haiwaondolei waumini balaa na maovu katika maisha haya. Mwenye kumiliki siku ya malipo Neno Din lina maana nyingi; miongoni mwayo ni malipo. Na maana haya ndiyo yanayonasibiana na hapa, ambapo siku hiyo italipwa kila nafsi yale iliyoyachuma.

NENO MAALIKI

Neno: Maaliki husomwa kwa alifu, kwa maana ya kuhusisha (umilikaji); kama inavyosemwa: Fulani ndiye mwenye kumiliki bustani hii (mwenye kuhusika nayo). Pia husomwa Maliki bila ya Alifu (kwa kutovuta) kwa maana ya mfalme, kama inavyosemwa: Mfalme wa Ugiriki, kwa maana ya Mtawala.

Visomo vyote viwili vinatumika, ingawaje cha kwanza ndicho kinachotumika zaidi.Maana inayokuja haraka akilini, kwa kusoma namna zote mbili ni moja: Kuwa kila kitu kiko mikononi mwa Mwenyezi Mungu peke yake, leo na kesho. Yeye ni Mola wa viumbe vyote, na Mola wa Siku ya malipo. Lengo ni kukemea watu na maasia na kuwavutia katika twaa. Katika Nahjul Balagha Imam Ali(a.s) amesema:

Hakika sisi hatumiliki chochote kwa Mwenyezi Mungu, wala hatumiliki isipokuwa kile alichotumilikisha. Alipotumilikisha kile ambacho Yeye amekimiliki huwa ametukalifisha nacho, na anapotuondolea huwa ametuondolea taklifa yake.

Wewe tu tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada. Mja kumzungumzia Mola wake kwa dhamiri ya Mmoja (Wewe tu) ni kwa ajili ya kumtakasa katika Umoja wake, na pia kumtakasa na shirk. Kwa ajili hii, halinganiwi Mwenyezi Mungu kwa tamko la wingi. Ama dhamiri ya wingi (sisi) katika neno tunakuabudu na tunakuomba msaada ni ya mwenye kusema (mja) pamoja na mwingine, wala sio ya kutukuza.

Ibada inathibitika kwa Saumu, Swala, Hijja na Zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu. Vile vile inathibitika kwa huduma yoyote ya kibinadamu ya kutekeleza haja za watu. Kuna Hadith inayosema:Watu wa mema duniani ni wa mema Akhera. Bora wa watu ni yule mwenye kuwafaa zaidi watu.

MAANA YA WEWE TU TUNAKUABUDU NA WEWE TU TUNAKUOMBA MSAADA

Sio kwamba Mungu ni wa kuabudiwa tu basi iwe imetosha. Bali vile vile Aya inafahamisha kuwa mtu ni kiumbe kitakatifu aliyekombolewa (aliyehuru) kutokana na utumwa na unyonge isipokuwa kwa haki tu, ambayo iko juu ya kila kitu na wala haikaliwi juu. Kimsingi ni kwamba uhuru usiowekewa mpaka na haki, hubadilika na kuwa machafuko. Katika maneno yenye faida niliyoyasoma, yanayohusiana na mlango huu, ni maneno ya Jean Paul Sartre, aliposema, Hakika uhuru hasa ni akujilaz- imisha mtu kujitolea nafsi yake na uhuru wake katika kuwatumikia wengine.

KISA

Kulikuwa na watu wawili wakitembea katika bustani. Mmoja alikuwa na fimbo akicheza nayo.Mara ikagusa ncha ya pua ya mwenzake. Alipomlaumu kwa kitendo hicho, yule mwenye fimbo akajigamba: Nina uhuru bwana! Mwenzake akamwambia, Uhuru wako una mpaka; mwisho wake ni pua yangu!

Mimi siupingi uhuru ikiwa mpaka wake ni kumwamini Mwenyezi Mungu na kumwabudu Yeye peke yake. Kwa sababu mwenye kuabudu haki tu atakuwa amejikomboa na batili; na mwenye kujikomboa na kuabudu haki, bila ya shaka atakuwa mtumwa wa batili. Haiwezekani kutofautisha katika mawili hayo isipokuwa kwa yule ambaye hana mpangilio; asiyeamini halali wala haramu, wala kuamini kitu chochote kingine isipokuwa nafsi yake peke yake.

*1 Sartre mwanzo alikuwa na nadharia ya Existentialism (kuwako) akidai kwamba kila mtu na lake, na hanasibiani na chochote isipokuwa kuwako kwake peke yake. Huko kuwako kwake hakuwezi kuthibiti isipokuwa kwa kuwa huru bila ya kuwa na kikwazo chochote au sharti lolote. Ama dini, misingi, na kuweka mambo katika vipimo, ni upuuzi. Hakuna heri isipokuwa heri ya mtu mwenyewe wala hakuna shari isipokuwa shari yake mwenyewe.

Kwa nadharia hii Satre anatoa dalili kuwa mtu amekuja kutoka katika ulimwengu usiojulikana,na anaelekea ulimwengu usiojulikana na kwamba yeye alikuwako kabla ya kanuni za kiakili na za kidini. Kwa hiyo, yeyote atakayejitia katika dini au katika msingi wowote, atakuwa amejifunga na kuuacha uhuru wake na kwa hivyo amejikanushia kuwako kwake.

Kisha akabadilisha falsafa yake hii akaingia katika falsafa ya Uhuru mkubwa, nao ni uhuru kwa ajili ya mamilioni; kwamba mtu anaichumia, nafsi yake, ikiwa atajiweka katika kuwahudumia wengine; kwambamtu hasa ni yule anayelazimiana na misingi hii. Badala ya kuwa anazungumzia juu ya hali ya mtu mmoja peke yake, akawa Satre anazungumzia juu ya haki za watu wengi na kulitetea hilo!

MAKUSUDIO YA NJIA ILIYONYOOKA

Tuongoze njia iliyonyooka : Makusudio ya njia iliyonyooka si elimu tu, bali ni elimu pamoja na tawfiki katika vitendo (amali). Mwenye kukutakia uongofu amekutakia heri yote, na mwenye kukutakia elimu amekutakia baadhi ya heri.

Maajabu ni kuwa watu wengi wanakuwa wazito kuomba uongofu, hasa wanavyuoni na watu wakubwa, pamoja na kujua kuwa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) alikuwa akikariri kuomba uongofu usiku na mchana katika swala zake na sehemu nyinginezo.

Sijui kama kuna uongofu na tawfiki bora na kubwa zaidi kuliko ile ya mtu kugundua aibu zake mwenyewe na kujilaumu, na kumchoma sana.Kwa kutambua hayo inawezekana mtu kuokoka. Mwenyezi Mungu atukinge na ghururi na maovu yake!

MAKUSUDIO YA WALIOKASIRIKIWA NA WALIOPOTEA

Njia ya (wale) uliowaneemesha; sio ya (wale) waliokasirikiwa wala ya (wale) waliopotea . Imepokewa Hadith kwamba:makusudio ya waliokasirikiwa ni Wayahudi, na waliopotea ni Wakristo . Lakini tamko la Aya ni la jumla, wala sio mahsusi au kuvua wengine (kubagua).

Kila mtiifu anaingia katika neema na rehema ya Mwenyezi Mungu, na kila mwenye kuasi ni mwenye kupotea na kughadhibikiwa.

LENGO LA SURA NZIMA YA FATIHA

Vyovyote iwavyo, lengo la Aya hii na sura nzima ya Fatiha, ni kuwa mja asimame mbele za Bwana wake akiwa ni Muumini mwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, mwenye kushukuru, mwenye kumsifu, mwenye ikhlasi, na mwenye kuomba tawfiki kwa elimu na kwa vitendo.

Na kila mtu ataikuta amali aliyoitanguliza kwa Muumba wake. Ama maneno tu, hayana athari isipokuwa kujikurubisha na twaa, au kujiweka mbali na maasia.