ASSALATU KHAIRUN MINAN NAUM
NENO LA MCHAPISHAJI
Kitabu kilichoko mikononi mwako, ni tarjuma ya kitabu cha Kiarabu kwa jina la: " As-Salaatu Khayrun Mina Nawm" kilichoandikwa na Sayyid Abdul Rahim al-Musawi, Sisi tumekiita: Kitabu hiki kinazungumzia kuhusu Asili ya Adhana na jinsi ilivyokuja kwa Mtukufu Mtume.
Kuna tofauti za kimapokezi kati ya madhehebu za Kiislamu, hususan Sunni na Shia. Na pia zipo hitilafu miongoni mwa wanachuo wenyewe kwa wenyewe ndani ya madhehebu za Kisunni kuhusu suala hili, kama utakavyoona katika kitabu hiki. Kitu ambacho wamehitalafiana ni maneno: as-Salaatu Khayrun Mina Nawm, kwamba ni maneno ya asili ya adhana au yaliongezwa na watu baada ya Mtukufu Mtume kuondoka? Hili ndio suala linalojadiliwa katika kitabu hiki.
Mwaandishi wa kitabu hiki amefanya utafiti wa hadithi na matukio ya kihistoria kuhusiana na suala hili, na kutokana na utafiti wake huo anaonesha kwa uwazi kabisa kwamba maneno: Assalaatu khayrun mina naumi, yamekuja baada ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) na kwamba hayana asili katika Adhana na kwamba maneno yenye asili katika Adhana ni: hayya alaa khayril-a.mal.
Madhumuni ya kitabu hiki sio kuleta ugomvi au malumbano na wale wanao yakubali maneno: Assalaatu khayrun mina.n-naumi, bali ni kuwafahamisha wale wanaoshangaa wanapowasikia Waislamu wengine hawayaleti maneno haya katika Adhana yao na badala yake wanaleta maneno: hayya alaa khayril-amal.
Taasisi yetu ya 'Al-Itrah Foundation' imeona ikitoe kitabu hiki ili wasomaji wetu Waislamu wa Kiswahili waifahamu tofauti hii na waelewe maana yake na waondokane na dhana ziszokuwa na maana.
Tunamshukuru ndugu yetu, Ust. Mohamed Abdallah kwa kukubali jukumu hili la kukifanyia tarjuma kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.
Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam, Tanzania.