6
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA PILI
﴿الشَّهْرُ الْحَرَامُ بِالشَّهْرِ الْحَرَامِ وَالْحُرُمَاتُ قِصَاصٌ فَمَنِ اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ فَاعْتَدُوا عَلَيْهِ بِمِثْلِ مَا اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ ﴾
194.Mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu; na vitu vitakatifu vina kisasi. Basi wanaowachokoza, pia nanyi wachokozeni kwa kadiri walivyowachokoza. Na mcheni Mwenyezi Mungu na jueni kwamba Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaomcha.
﴿وَأَنفِقُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَلَا تُلْقُوا بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ وَأَحْسِنُوا إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ﴾
195.Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamivu, na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.
Aya 194 - 195
Mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu.
Miezi mitakatifu ni minne; mitatu inafuatana, nayo ni Dhul-Qaada, Dhul Hijja na Muharram (mfunguo pili, mfunguo tatu na mfunguo nne). Na mwezi mmoja uko pekee na ni (Rajab). Miezi hii imeitwa mitakatifu kwa sababu ya kuharamishwa kuuana ndani ya miezi hiyo. Katika wakati wa ujahiliya na wa Uislamu, ilikuwa mtu anaweza kukutana na mtu aliyemuua baba yake katika miezi hiyo na asimfanye chochote. Yameshatangulia maelezo kwamba Mtume na sahaba zake walitaka kufanya umra katika mwezi wa dhul-Qaada (mfunguo pili) mwaka wa sita (6 Hijriya), wakazuiwa na washirikina na wakatupiwa mishale na mawe; kisha waka-fanyiana suluhu kuwa Waislamu warudi mwaka utakaofutia. Lakini Waislamu wakaogopa washirikina wasije wakaanza kupigana katika mwezi mtakatifu; ndipo Mwenyezi Mungu akawapa idhini ya kupigana na washirikina na akabainisha kuwa lenye kukatazwa ni kuanza uadui wa kupigana na sio kujikinga. Kwa hivyo maana ya mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu ni kwamba mwenye kuihalalisha damu yenu enyi Waislamu katika mwezi huu, basi nanyi ihalalisheni damu yake katika mwezi huo huo.
Na vitu vitakatifu vina kisasi. Yaani mwenye kuvunja heshima ya Mwenyezi Mungu atalipizwa kisasi na atafanywa kama alivyofanya. Hiyo ndiyo asili kwa ujumla inayoondoa kila udhuru wa mwenye kuvunja heshima. Mwenye kuhalalilisha damu za watu, mali zao na heshima zao, naye atahalalishwa kwa kiasi kile alichowafanyia. Heshima kwa mtu mwingine inatokana na heshima ya Mwenyezi Mungu isipokuwa kama akivunja heshima ya mwingine. Hapo itakuja haki ambayo daima inakuwa juu na wala haikaliwi. Hapa ndipo tunapata tafsiri ya:
Anayechokoza pia nanyi mchokozeni kwa kadiri alivyo wachokoza. Sharti la kulipiza ni kuwa sawa na kosa la aliyeanza bila ya kuzidisha au kupunguza. Hicho ndio kisasi hasa kilivyo. Unaweza kuuliza: Mwenye kuchokoza , yeye ni mchokozi bila ya wasiwasi wowote, lakini mwenye kulipiza kisasi bila shaka siye mchokozi. Kwa hiyo kuna wajihi gani kwa Mwenyezi Mungu kusema:Mchokozeni
Jibu : Makusudio ya kuwafanyia uchokozi, sio uchokozi hasa kwa maana yake, isipokuwa makusudio ni malipo ya uchokozi uliofanywa kwa kipimo chake bila ya kudhulumu. Hayo ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu(s.w.t.):
"Na malipo ya ubaya ni ubaya ulio sawa na (ubaya) huo..." (42:40)
Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kutoa katika njia yake Mwenyezi Mungu kunakuwa ni kwa masilahi ya umma; kama vile shule, hospitali na nyumba za kulea mayatima. Vile vile jihadi, sadaka kwa mafukara na masikini na kuwalisha watu wa nyumbani. Bora zaidi ya kutoa ni kule kunakohusika na kutia nguvu na kuieneza dini, kuthibitisha haki na kuibatilisha batili.
Wala msijitie, kwa mikono yenu, katika maangamivu
Mwenyezi Mungu ametumia neno mikono kwa maana ya mtu kujiingiza mwenyewe. Kama tukiangalia jumla hii peke yake tu bila ya kuangalia mfumo mzima wa maneno, ingelikuwa maana yake ni kuwa haijuzu kwa mtu kufanya lolote ambalo lina madhara na bila ya kuwako manufaa kwa ujumla. Lakini tukichunga mfumo wa maneno na kuja kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.):"wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamivu" baada ya kusema:"Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu", basi maana yanakuwa, toeni katika mali zenu sio kwa ubahili wala ubadhirifu, kwa sababu yote hayo mawili yanaleta uangamivu. Kwa hivyo Aya kwa maana haya inakuwa kama ile Aya isemayo:
﴿ وَالَّذِينَ إِذَا أَنفَقُوا لَمْ يُسْرِفُوا وَلَمْ يَقْتُرُوا وَكَانَ بَيْنَ ذَٰلِكَ قَوَامًا ﴾
"Na wale ambao wanapotoa hawafanyi ubadhirifu wala ubahili, bali wanakuwa katikati ya hayo."( 25:67)
Inasemekana pia kwamba maana yake ni: Msijitie kwa mikono yenu kwenye maangamivu kwa kuacha kupigana jihadi na maadui wa dini na kutoa mali kwa ajili ya kuwaandaa wapigania jihadi, kwa sababu hilo litawaogopesha na atawaweza adui; muangamie na mdhalilike. Haya ndiyo yaliyothibitishwa na majaribio waliyoyapitia Waislamu. Wamekosa uhuru wao na heshima yao tangu walipoacha jihadi na kutoa mali kwa ajili ya kuinusuru haki na uadilifu. Hivyo akapata tamaa kila mnyang'anyaji na mnyakuzi; hata Wazayuni, vibaraka wa ukoloni, nao waliivamia Palestina mnamo 1948. Baada ya Waarabu kunyamaza na wasifanye jihadi. Baada ya miaka ishirini wakateka Sinai na ukanda wa Gaza Magharibi mwa mto Jordan; wakazikalia sehemu hizo kwa msaada wa Amerika, Uingereza na Ujerumani Magharibi. Wakawaua wanaume na kuwafukuza wanawake na watoto. Lau Waislamu wangefanya jihadi kabla yake, wangeliokoka na maangamizo haya na udhalili huu, na wala dola ya Israel isingekuwepo kabisa.Na fanyeni wema Kwa jihadi na kujitolea mali katika njia ya Mwenyezi Mungu na katika kila njia inayomridhisha Mungu na yenye sifa nzuri.
﴿ وَأَتِمُّوا الْحَجَّ وَالْعُمْرَةَ لِلَّـهِ فَإِنْ أُحْصِرْتُمْ فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ وَلَا تَحْلِقُوا رُءُوسَكُمْ حَتَّىٰ يَبْلُغَ الْهَدْيُ مَحِلَّهُ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ بِهِ أَذًى مِّن رَّأْسِهِ فَفِدْيَةٌ مِّن صِيَامٍ أَوْ صَدَقَةٍ أَوْ نُسُكٍ فَإِذَا أَمِنتُمْ فَمَن تَمَتَّعَ بِالْعُمْرَةِ إِلَى الْحَجِّ فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ فِي الْحَجِّ وَسَبْعَةٍ إِذَا رَجَعْتُمْ تِلْكَ عَشَرَةٌ كَامِلَةٌ ذَٰلِكَ لِمَن لَّمْ يَكُنْ أَهْلُهُ حَاضِرِي الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴾
196.Na timizeni Hijja na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na kama mkizuiliwa, basi (chinjeni) wanyama walio wepesi kupatikana. Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike machinjioni mwao. Na ataka-yekuwa mgonjwa katika nyinyi au ana adha kichwani mwake, basi atoe fidia kwa kufunga au sadaka au kuchinja mnyama. Na mtakapokuwa salama, basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra, kisha akahiji, achinje mnyama aliye mwepesi kumpata. Na asiyepata, ni kufunga siku tatu katika Hijja na siku saba mtakaporudi; hizo ni siku kumi kamili. Hayo ni kwa yule ambaye watu wake hawako karibu na Msikiti Mtakatifu. Na mcheni Mungu na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
﴿ الْحَجُّ أَشْهُرٌ مَّعْلُومَاتٌ فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلَا رَفَثَ وَلَا فُسُوقَ وَلَا جِدَالَ فِي الْحَجِّ وَمَا تَفْعَلُوا مِنْ خَيْرٍ يَعْلَمْهُ اللَّـهُ وَتَزَوَّدُوا فَإِنَّ خَيْرَ الزَّادِ التَّقْوَىٰ وَاتَّقُونِ يَا أُولِي الْأَلْبَابِ﴾
197.Hijja ni miezi maalumu. Na anayejilazimisha kufanya Hijja katika miezi hiyo, basi hakuna kuchafua wala ufuska wala mabishano katika Hijja. Na heri yoyote mnayoifanya Mwenyezi Mungu anaijua. Na chukueni masurufu, na hakika masurufu bora ni takua; na nicheni Mimi, enyi wenye akili.
﴿ لَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَبْتَغُوا فَضْلًا مِّن رَّبِّكُمْ فَإِذَا أَفَضْتُم مِّنْ عَرَفَاتٍ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ عِندَ الْمَشْعَرِ الْحَرَامِ وَاذْكُرُوهُ كَمَا هَدَاكُمْ وَإِن كُنتُم مِّن قَبْلِهِ لَمِنَ الضَّالِّينَ ﴾
198.Si vibaya kwenu kutafuta riziki ya Mola wenu. Na mtakapomiminika kutoka Arafa, mtajeni Mwenyezi Mungu katika Mash'aril- Haram: Na mkumbukeni kama alivyowaongoza, ijapokuwa zamani mlikuwa miongoni mwa waliopotea.
﴿ ثُمَّ أَفِيضُوا مِنْ حَيْثُ أَفَاضَ النَّاسُ وَاسْتَغْفِرُوا اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴾
199.Kisha miminikeni kutoka mahali wanapomiminika watu (wote), na mumwombe Mwenyezi Mungu maghufira; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kughufiria Mwenye kurehemu.
﴿ فَإِذَا قَضَيْتُم مَّنَاسِكَكُمْ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَذِكْرِكُمْ آبَاءَكُمْ أَوْ أَشَدَّ ذِكْرًا فَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا وَمَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ ﴾
200.Na mmalizapo kuzitimiza ibada zenu, basi mtajeni Mwenyezi Mungu kama mlivyokuwa mkiwataja baba zenu; bali mtajeni zaidi. Na kuna baadhi ya watu wasemao: Mola wetu! Tupe duniani; nao katika Akhera, hawana lolote.
﴿ وَمِنْهُم مَّن يَقُولُ رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴾
201.Na miongoni mwao kuna asemaye; Mola wetu! Tupe mema duniani na (tupe) mema Akhera, na utulinde na adhabu ya Moto.
﴿ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ نَصِيبٌ مِّمَّا كَسَبُوا وَاللَّـهُ سَرِيعُ الْحِسَابِ ﴾
202.Hao ndio wenye fungu katika waliyoyachuma, na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
﴿ وَاذْكُرُوا اللَّـهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ فَمَن تَعَجَّلَ فِي يَوْمَيْنِ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ وَمَن تَأَخَّرَ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ لِمَنِ اتَّقَىٰ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّكُمْ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ﴾
203.Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika siku zinazohisabiwa. Na mwenye kufanya haraka katika siku mbili, basi si dhambi juu yake; na mwenye kukawia pia si dhambi juu yake, kwa mwenye takua. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba nyinyi mtakusanywa Kwake.
Aya 196 - 203
Aya hizi zimeonyesha baadhi ya hukumu za Hijja, Mafaqihi wameweka vitabu maalumu vinavyohusu Hijja, nami nimetunga kitabu kwa jina Al- Hajj ala Madhahabil-Khamsa; kisha nikakiunganisha katika kitabu Al- Fiqh ala Madhahabil Khamsa wakati kiliporudiwa kuchapishwa kwa mara ya tatu. Vile vile nimeizungumza kwa urefu katika Juzuu ya pili ya kitabu Fiqh ul-Imam Jaffar Sadiq(a.s) Hijja imekuwa maarufu tangu zama za Nabii Ibrahim na Ismail(a.s) na iliendelea katika zama za ujahiliya; na Uislamu ukaithibitisha baada ya kuisafisha na mambo machafu, na kuongeza baadhi ya ibada.
Na timizeni Hijja na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Maana ya Hijja kilugha, ni kukusudia, na kisharia ni ibada maalum katika mahali na wakati maalum. Umra kilugha ni ziara yoyote; na kisheria ni ziara katika Al-Kaaba kwa namna maalum, Hijja ni wajibu katika Quran, Hadith na Ijami. Bali wajibu wake umethubutu kwa dhahiri ya dini. Na mwenye kuikanusha sio Mwislamu, sawa sawa na aliyekanusha wajibu wa Saumu na Swala. Shia Imamiyya na Shafii wamesema Umra ni wajibu, Hanafi na Malik wamesema ni Sunna. Kusema kwake Mwenyezi Mungu Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Yaani Hijini na fanyeni Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke yake na sio kwa makusudio ya kidunia. Kwani Waarabu walikuwa wakikusudia kuhiji kwa ajili ya kukutana, kujifaharisha, kutafuta mahitaji na kuhudhuria soko. Ndipo Mwenyezi Mungu akaamrisha Hijja iwe ni kwa makusudio yake Yeye kwa ibada safi yenye kutakasika na makusudio yoyote mengine.
Na kama mkizuiliwa, basi (chinjeni) wanyama walio wepesi kupatikana.
Yaani ikiwa mmeherimia Hijja, kisha mkazuilika kukamilisha ibada kwa njia yake ya kisheria kutokana na maradhi au adui na mengineyo, basi ni juu yenu kuchinja mnyama atakayepatikana kwa urahisi; kwa uchache awe ni mbuzi, wastani ni ng’ombe na wa juu zaidi ni ngamia.
Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike machinjioni mwao.
Msemo unaelekezwa kwa wale waliozuilika ambao hawakuweza kutimiza Hijja au Umra. Wao hawatakuwa wametoka katika ihram yao (miko ya Hijja) mpaka wajue kwamba mnyama amefika mahali pake pa kuchinjwa. Na mahali pa kuchinja ni Mina ikiwa ni Hijja; na kama ni Umra basi ni Makka. Hayo ni itakapokuwa kizuizi ni maradhi. Ama ikiwa kizuizi ni adui, basi mahali pa kuchinja ni pale mahali palipotokea kizuizi. Kwa sababu Mtume(s.a.w.w) alichinja mnyama katika Hudaybiya, alipozuiliwa na washirikina kuzuru nyumba ya Mwenyezi Mungu tukufu (Al Kaaba).
Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi au ana adha kichwani mwake, basi atoe fidia kwa kufunga au sadaka au kuchinja mnyama.
Yaani ikiwa mwenye kuhirimia atanyoa kichwa chake kwa dharura, basi ni juu yake kutoa kafara, atakuwa na hiyari baina ya kufunga siku tatu, kuwalisha masikini sitini au kuchinja mnyama; kwa uchache awe ni mbuzi.
Na mtakapokuwa salama, basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha akahiji, achinje mnyama aliyemwepesi kupatikana.
Yaani mtu asiyekuwa na kizuizi, akafanya Umra kisha akahiji baadae katika mwaka huo huo, basi ni juu yake kuchinja mnyama. Hii ndiyo aina ya Hijja inayojulikana kwa jina la Haj Tamattui (Hijja ya starehe) ambayo ni wajibu kwa wasiokuwa watu wa Makka.
Imeitwa Hijja ya starehe, kwa sababu mwenye kuhiji baada ya kumaliza amali za Umra anatoka kwenye miko ya Umra mpaka aje ahirimie Hijja.
Na asiyepata, ni kufunga siku tatu katika Hijja na siku saba mtakaporudi; hizo ni siku kumi kamili.
Imam Jaffar Sadiq(a.s) amesema;Mwenye kufanya Hajj Tamattu, asipopata mnyama atafunga siku tatu katika Hijja; siku ya saba, ya nane na ya tisa katika Dhul-Hijja (mfungu tatu) wala hakuna sharti la Iqama na siku saba atafunga atakaporudi kwa watu wake. Hizo ni siku kumi kamili za kutosheleza mnyama.
Hayo ni kwa yule ambaye watu wake hawako karibu na msikiti mtakatifu.
Mwenye Majmaul Bayan amesema kuwa hayo yaliyotangulia kutajwa katika Tamattui ya Umra kisha Hijja, sio kwa watu wa Makka na walio karibu yake. Isipokuwa ni kwa ambaye hayuko Makka, yule ambaye yuko mbali na Makka kwa zaidi ya maili kumi na mbili (12) kwa kila upande. Mafaqihi wa Kishia Imamiya wamesema Hajj Tamattui ni wajibu kwa walio mbali na Makka, wala haijuzu kwa aliyembali na Makka kuhiji Hijja Qiran na Ifrad, kwani hizo ni wajibu kwa watu wa Makka na wa kando kando yake; na wao haijuzu kwao kuhiji Hajj Tamattui. Kwa ufafanuzi zaidi angalia vitabu vya Fiqh.
Hijja ni miezi maalumu.
Nayo ni kuanzia Shawwal, Dhul-qaad na kumi la mwanzo la Dhul-Hijja. (mfunguo mosi, mfunguo pili na mfunguo tatu) Mwenye kuhirimia kabla yake Hijja yake haitaswihi na mwenye kuhirimia ndani ya miezi hiyo itaswihi na ataleta amali zilizobakia.
Na anayejilazimisha Hija katika miezi hiyo, basi hakuna kuchafua wala ufuska wala mabishano katika Hijja.
Makusudio ya uchafuzi hapa ni kujamii. Mtu akimjamii mkewe na huku amehirimia Hijja, basi Hijja yake imeharibika, sawa sawa na aliyejamii au kula huku akiwa amefunga. Kwa hiyo atakamilisha Hijja yake, kisha aje alipe mwaka ujao; kama ilivyo kwa mwenye kuiharibu Saumu. Makusudio ya ufuska, ni uongo na kutukana. Ama kuhusu kubishana riwaya za Ahlul Bait zinasema, hilo ni kusema mtu; Hapana wallahi au Kwa nini, wallahi n.k.
Si vibaya kwenu kutafuta riziki ya Mola wenu.
Kwa vile wakati wa ujahilia watu walikuwa wakifanya biashara na kuchuma siku za Hijja, kukadhaniwa kuwa ni haramu, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.), akaondoa tuhuma hii na akabainisha kwamba kuchuma hakupingani na ikhlasi katika amali za Hijja.
Na mtakapomiminika kutoka Arafa, mtajeni Mwenyezi Mungu katika Masharil Haram.
Arafa ni mahali maalum. Kumiminika kutoka Arafa ni kuondoka, Masharil-Haram ndipo pale panajulikana kama Muzdalifa na kutua hapo ni wajibu; kama ilivyo kwa Arafa.
Kisha miminikeni kutoka mahali wamiminikapo watu (wote). Inasemekana kuwa Maquraish walikuwa hawatui Arafa pamoja na watu wengine kwa kiburi tu, ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha Mtume wake kutua hapo na kutoka pamoja na watu ili abatilishe waliyokuwa wakiyafanya Maquraish.
Na mmalizapo kuzitimiza ibada zenu, basi mtajeni Mwenyezi Mungu zaidi.
Imepokuwa kutoka kwa Imam Baqir baba wa Imam Sadiq(a.s) kwamba watu walikuwa wanapomaliza Hijja wanakusanyika huko na kuwataja wazazi wao kwa fahari, ndipo Mwenyezi Mungu akawaamrisha kuliacha hilo na badala yake wamtaje Mwenyezi Mungu na jinsi alivyowaneemesha. Kwa sababu Yeye ndiye mwenye kuwaneemesha wao na mababa zao.
Na baadhi ya watu kuna asemaye: Mola wetu! Tupe duniani; nao katika akhera hawana lolote. Na miongoni mwao kuna asemaye: Mola wetu! Tupe mema duniani na (tupe) mema akhera, na utulinde na adhabu ya moto. Hao ndio wenye fungu katika waliyoyachuma, na Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu.
Watu katika Hijja zao wako aina mbili. Aina ya kwanza ni yule asiyetaka lolote isipokuwa starehe ya dunia na hana makusudio yoyote isipokuwa dunia tu, na anapomwabudu Mwenyezi Mungu humwabudu kwa ajili ya dunia. Hawa ndio wenye kunyimwa neema ya Akhera. Ama aina ya pili ni yule anayetaka heri ya dunia na akhera na anafanya amali kwa ajili ya dunia yake na akhera yake. Huyu ndiye mwenye radhi mbele ya Mwenyezi Mungu kesho kwa kulipwa amali yake njema. Mwenye Tafsiri Rawhul Bayan amenukuu kutoka kwa Imam Ali bin Abi Twalib(a.s) kwamba wema katika dunia ni mwanamke mwema na katika akhera ni Hurulain. Ama adhabu ya moto makusudio yake ni mwanamke muovu.
Iwe ni sahih Hadith hiyo au la, lakini mimi najua kuna watu wanaohisi kwamba lau wao wangekuwa katika Jahanam kisha wakahiyarishwa kutoka katika Jahanam na warudi kwa wake zao waliokuwa nao duniani au wabaki Jahannam, basi wangelichagua kubaki katika Jahannam kuliko kuishi tena na wake zao hao.
Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika siku zinazohisabiwa.
Makusudio yake ni siku tatu za Tashriq nazo ni; Tarehe kumi na moja, kumi na mbili na kumi na tatu katika mwezi wa Dhul-Hijja (mfungo tatu). Si wajibu kwa mwenye kuhiji kulala Mina usiku wa kumi na tatu, lakini kwa sharti ya kuwa atoke Mina siku ya kumi na mbili baada ya kupinduka jua na kabla ya Maghrib na awe hakuvunja mwiko wa kuwinda au kujamii. Kwa hali hiyo ndipo tunapopata tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
Na mwenye kufanya haraka katika siku mbili, basi si dhambi juu yake; na mwenye kukawia pia si dhambi juu yake kwa mwenye takua.
Yaani mwenye kuacha kuwinda na wanawake katika ihram yake. Ikiwa amevunja mwiko wa kulala na mke au kuwinda au alichelewa na jua siku ya kumi na mbili akiwa yuko Mina, basi itakuwa wajibu kwake kulala usiku wa kumi na tatu na kutupia mawe vikuta vitatu (shetani).