7%

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

KIMEANDIKWA NA

SAYYID MUJTABAA MUUSAWIY LARI

KUHUSU MWANDISHI

Sayyid Mujtaba Mussawi Lari ni mtoto wa marehemu Ayatullah Sayyid Ali Asghar Lari mmojawapo wa wanachuoni na watu mashuhuri katika jamii ya Iran. Babu yake alikuwa marehemu Ayatullah Hajj Sayyid Abd ul- Husayn Lari ambaye alipigania uhuru wakati wa mapinduzi ya kikatiba. Wakati wa kipindi kirefu cha mapambano yake dhidi ya serikali dhalimu ya wakati huo, alijaribu kuanzisha serikali ya Kiislamu na alifaulu kufany hivyo kwa kipindi kifupi huko Larestan.

Sayyid Mujtaba Musawi Lari alizaliwa mwaka 13/4/1935 kwenye jiji la Lar ambako alihitimu elimu yake ya Msingi na masomo ya mwanzo ya Kiislamu. Mnamo mwaka wa 1332/1953, aliondoka Lar na akaenda Qum kuendelea na masomo yake ya elimu ya Kiislamu, akiwa anafundishwa na maprofesa na waalimu wa taasisi ya Kidini, pamoja na wanazuoni wakuu katika maarifa ya sheria (maraji).

Mnamo mwaka wa 1341/ 1962, akawa mshiriki katika Maktabil-Islam, gazeti la kidini na kisayansi lililokuwa lianaandika mfululizo wa makala kuhusu maadili ya Kiislamu. Makala hizi baadaye zilikusanywa na kuchapishwa kitabu kilichoitwa Ethical and psychological Problems. Matoleo tisa katika kitabu hiki kwa lugha ya kiajemi (Fursi) yamechapishwa, na pia kimetafsiriwa katika lugha ya Kiarabu na hivi karibuni kwa Kifaransa.

Mnamo mwaka 1342/1963. Alisafiri kwenda Ujerumani kutibiwa, na alirudi Iran baada ya miezi kadhaa, aliandika kitabu kiitwacho 'The face of Western Civilization'. Kitabu hiki kinajumuisha mazungumzo ya kulinganisha ustaarabu wa Kimagharibi na Kiisilamu, ndani ya kitabu hiki, mwandishi anataka kuthibitisha, kwa njia ya utambuzi, kifikira na ulinganisho kamili, ubora wa utambuzi na mambo mengi ya ustaarabu wa Uislamu kwa ule wa Magharibi. Kitabu hiki hivi karibuni tu kimechapishwa tena kwa mara ya saba. Mnamo 1349/1970, kitabu hiki kilitafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na mtaalam wa mambo ya nchi za Mashariki, F.G. Goulding, na kilichochea hisia za watu huko Ulaya. Makala kuhusu kitabu hiki zilionekana kwenye magazeti kadhaa ya kimagharibi na BBC ilifanya mpango wa mahojiano na mtarjumi huyo ambapo sababu za kutafsiri na jinsi kilivyopelekwa hapo Uingereza zilizungumziwa. Tafsiri ya Kiingereza ya kitabu hiki hadi sasa imechapishwa mara tatu huko Uingereza, mara tano Iran na mara mbili Marekani.

Mnamo takriban miaka mitatu baada ya kuchapishwa tafsiri ya Kiingereza, Rudolf Singler, profesa wa chuo Kikuu wa Kijerumani alikitafsiri katika lugha ya Kijerumani, na tafsiri hiyo ilithibitisha kuwa yenye kuvutia huko Ujerumani. Mmojawapo wa viongozi wa chama cha Social Democratic Party alimtaarifu Mtarjumi katika barua kwamba kitabu hicho kimeacha mvuto wa kina juu yake yeye, na kusababisha yeye kubadilisha maoni yake kuhusu Uislamu, na kwamba angelipendekeza Kitabu hicho kisomwe na marafiki zake. Tarjuma ya lugha ya Kijerumani imerudiwa kuchapishwa mara tatu hadi sasa.

Tafsiri za Kiingereza na Kijerumani za kitabu hiki zilichapishwa na Wizara ya Mwongozo wa Kiislamu kwa ajili kuisambaza zaidi nje ya Iran kupitia Wizara ya mambo ya Nje na taasisi ya mafunzo ya Kiislamic nchi za nje. Wakati huo huo ilipochapishwa tafsiri ya kwanza ya lugha ya Kijerumani, mwanachuo Muislamu wa asili ya kihindi aitwaye Maulana Raushan Ali alikitarjumi kitabu hiki katika lugha ya Urdu kwa lengo la kukisambaza India na Pakistani. Tarjumi hii ya Urdu imechapishwa mara tano hadi sasa. Sayyid Mujtaba Musawi Lari pia ameandika kijarida kuhusu Tawhid (upweke wa Mwenyezi Mungu), ambacho kilitafsiriwa Uingereza na kuchapishwa mara kadhaa Marekani.

Mnamo mwaka 1343/1964, aliasisi taasisi ya kutoa msaada huko Lar kwa madhumuni ya kueneza Uislamu, kutoa mafunzo ya Kiislamu kwa vijana walioko vijijini, na kuwasaidia wasiojiweza. Taasisi hii iliendelea kufanya kazi hadi 1346/1967. Taasisi hii ilitekeleza mambo makuu kama kuwapeleka wanafunzi wa sayansi za Kidini vijijini kufundisha Uislamu kwa watoto na vijana, kuwagawia maelfu ya watoto wa shule nguo, vitabu, vifaa vya kuandikia, kujenga idadi ya misikiti, mashule, zahanati mijini na vijijini, na huduma nyingine nyingi.

Sayyid Mujtaba Musawi Lari aliyaandama matakwa yake katika maadili ya Kiislamu, akiandika makala mpya kuhusu somo hilo. Mnamo mwaka wa 1353/1974, mkusanyiko wa makala hizi, zilizopitiwa upya na kuongezewa maneno, zilitoka katika muundo wa kitabu kilichoitwa 'The Function of Ethics in Human Development.' Kitabu hiki kimechapishwa mara sita hadi sasa.

Mnamo mwaka 1357/1978, alisafiri hadi Marekani kwa mwaliko wa Taasisi ya Kiislamu nchini humo. Halafu akaenda Uingereza, Ufaransa na baada ya kurudi Iran alianza kuandika mfululizo wa makala kuhusu itikadi za Uislamu kwa ajili ya gazeti la Sorouch. Makala hizi baadaye zilikusanywa na kutengenezwa kitabu chenye juzuu nne kuhusu imani za misingi za Uislamu (tauhid, uadilifu wa Mwenyezi Mungu, utume, uimamui, na ufufuo) kwa jina la 'The Foundations of Islamic Doctrine.' Kitabu hiki chenye juzuu nne kimetafsiriwa katika lugha ya Kiarabu, sehemu zake zingine zikiwa tayari zimekwisha chapishwa mara tatu. Tafsiri ya Kiingereza ya juzuu ya kwanza ya kazi hii ndio imetengeneza kitabu hiki cha sasa; juzuu zilizosalia pia zitatafsiriwa na kuchapishwa. Tafsiri za Urdu, Hindi na Kifaransa pia zimo katika mpango wa kutayarishwa; juzuu mbili za lugha ya Kifaransa zimekwishatokea.

Mnamo mwaka wa 1359/1980, Sayyid Mujtaba Musawi Lari aliasisi Taasisi huko Qum iitwayo 'Office for The Diffusion of Islamic Culture Abroad.' Husambaza bure nakala za vitabu vyake vilivyotafsiriwa kwa watu wapendao kuzisoma duniani pote. Taasisi hii pia imechukua shughuli ya kuchapisha Qur'ani kwa lengo la kuisambaza kwa Waislamu binafsi, Taasisi na shule za Kidini hapa Afrika.