21
MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE
SOMO LA ISHIRINI NA MOJA
TAFSIRI ISIOFAA YA MAJAALIWA NA HATIMA
Baadhi ya wasomi bandia wanazo fikra potofu kuhusu majaaliwa na hatima na hudhani kwamba msingi huu husababisha kuvia na kutojishughulisha, humzuia binadamu na juhudi za aina yoyote za kuboresha maisha yake. Chanzo cha fikra hii katika nchi za Magharibi ni kutokuelewa vya kutosha kuhusu dhana hii, hususan kama inavyofafanuliwa katika mafundisho ya Kiislamu. Huko nchi za Mashariki fikra hii imepata athari kwa sababu ya kufifia na kurudi nyuma kimaendeleo.
Inajulikana vya kutosha kwamba wakati wowote watu au jamii za kihistoria zinaposhindwa kufikia malengo na mawazo yao, kwa sababu yoyote ile, hujifariji kwa maneno kama vvile 'bahati' 'ajali', 'hatima', 'majaaliwa'. Mtume mtukufu kabisa(s.a.w.w) alijieleza kwa ufasaha sana kuhusu jambo hili: "Wakati utakuja kwa watu wa umma wangu ambapo watafanya dhambi na dhuluma, na ili waweze kuhalalisha uovu na uchafu wao, watasema: 'majaaliwa na hatima yametuamulia kwamba tufanye hivi.' Ukikutana na watu kama hao, waambie mimi siwatambui, ninawakana hao."
Kuamini majaaliwa na hatima haimzuii mtu kufanya jitihada kufikia malengo yake katika maisha yake. Kama wale wenye ujuzi muhimuwa kidini wanavyotambua, Uislamu unawataka wanadamu kujitahidi sana katika kuboresha maisha yao, kimaadili na kimali. Peke yake hiki ni kipengele madhubuti katika kuongeza juhudi anayofanya mwanadamu. Mmoja wa mabingwa wa nchi za Magharibi ambaye anao uelewa mfinyu wa majaaliwa na hatima ni Jean- Paul Sartre. Anadhani haiwezekani kwa wakati moja kuamini majaaliwa na hatima chini ya uamuzi wa Mwenyezi Mungu na katika uhuru wa binadamu, na kwa hiyo, ni muhimu ama kuchagua kumwanini Mwenyezi Mungu au hiari ya mwanadamu: "Kwa sababu mimi ninaamini katika uhuru, siwezi kumwamini Mwenyezi Mungu, kwa sababu endapo ninamwamini Mwenyezi Mungu, lazima nikubali dhana ya majaaliwa, na kama nikikubali majaaliwa, nitalazimika kukana uhuru.
Kwa kuwa mimi ninaambatana na uhuru, simwamini Mwenyezi Mungu." Hata hivyo, hakuna ukinzani kati ya kuamini majaaliwa kwa upande moja, na uhuru wa mtu, kwa upande mwingine. Wakati inapochukulia utashi wa Mwenyezi Mungu kuwa wa kila mahali kiuwezo, Qur'ani Tukufu pia inahusisha wajibu huru na hai kwa binadamu, ikimwelezea kama mwenye uwezo kutengeneza hatima yake mwenyewe akiwa na utambuzi wa wema na uovu, ubaya na uzuri, na uwezo wa kuchagua kati ya hayo:
إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا ﴿٣﴾
"Hakika sisi tumemuongoza njia, imma awe ni mwenye kushukuru au mwenye kukufuru." (76:3),
وَمَنْ أَرَادَ الْآخِرَةَ وَسَعَىٰ لَهَا سَعْيَهَا وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَـٰئِكَ كَانَ سَعْيُهُم مَّشْكُورًا ﴿١٩﴾
"Na aliyeitaka Akhera na akaifanyia juhudi, ile inayopasa, naye ni mwenye kuamini, basi hao ndio juhudi zao zitakubaliwa." (17:19).
Wale ambao mnamo siku hiyo ya Hukumu wataitafuta hifadhi kwenye uamini majaaliwa na kusema:
لَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا عَبَدْنَا مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ ﴿٣٥﴾
"Mwenyezi Mungu angetaka tusingeliabudu chochote badala yake....." (16:35).
Wanashutumiwa kwa kuhusisha utendaji dhambi wao na upotovu kwenye utashi wa Mwenyezi Mungu na majaaliwa.
Hakuna hata ndani ya Aya moja kwenye Qur'ani ambamo ufisadi na matendo maovu ya mtu au jamii yamehusishwa kwenye majaaliwa na hatima. Hivyo, majaaliwa na hatima ni mambo ambayo hayakuonyeshwa kama vikwazo kwa jamiii fisadi na ya kiuovu inayojirekebisha. Hakuna hata Aya moja inayoweza kupatikana ambayo kwamba utashi wa Mwenyezi Mungu umeshika nafasi ya hiari ya binadamu au ambamo inasemekana kwamba mtu alianza kuteseka kwa sababu ya majaaliwa na hatima.
Qur'ani imetamka kwa kurudia rudia ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ambayo itawakumba madikteta na mafisadi, kwa kuleta adhabu kali baada yake. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye mapenzi na huruma sana kwa waja wake, akiwa ametoa neema zisizohesabika juu yao na wakati huo huo ni mpole na yu tayari kukubali toba, wakati wote Ameacha wazi njia kwa mwenye dhambi anayetaka kurudi kwenye utakaso na unyofu. Kukubali toba kwa Mwenyezi Mungu, kwenyewe peke yake ni mfano mkubwa sana wa huruma Yake.
Ingawa upeo wa hiari ya binadamu ni mkubwa na mpana zaidi kuliko ule wa viumbe hai vingine vijulikanavyo na huchukua nafasi kubwa sana ya ubunifu zaidi, hiari yake ina athari kwenye maeneo yale tu ambayo yamewekewa mipaka na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya shughuli na matendo yake. Kwa hiyo, binadamu hawezi kutimiza kila kitu anachotaka katika maisha yake. Mara nyingi hutokea kwamba mtu huamua kufanya jambo lakini kila atakavyojitahidi, anakuwa hawezi kulitimiza. Sababu yake hili sio kwamba utashi wa Mwenyezi Mungu unajipinga wenyewe kuhusu hiari ya mwanadamu na kumzuia kufanya atakavyo. Ni kwamba hasa katika masuala kama hayo, vipengele vya nje visivyojulikana vilivyopo nje ya upeo wa ujuzi na udhibiti wa binadamu huzusha vikwazo kwenye njia yake na kumzuia kufanikisha malengo yake.
Watu binafsi na jamii wakati wote hukabiliana na vikwazo vya aina hii. Kuzingatia ukweli kwamba katika uwanja wa maumbile hakuna chanzo bila athari na hakuna athari bila chanzo, na kwamba uwezo wetu wa kutambua umewekewa mipaka katika dunia hii na kwenye milki ya binadamu, isiwe vigumu sisi kukubali kwamba matumaini yetu yanaweza yasitimie kama tunavyotaka.
Mwenyezi Mungu ameweka mabilioni ya vipengele katika utaratibu wa uhai. Wakati mwingine vipengele hivyo vipo dhahiri kwa mwanadamu, wakati mwingine havijulikani kwa binadamu na haviwezi kushirikishwa katika kufikiri kwake. Hali hii pia ina uhusiano na majaaliwa na hatima lakini sio tu kwamba haishii katika kumnyima mwanadamu hiari au kumzuia kujaribu kupata hali ya kujitosheleza katika maisha; pia humwongoza kifikra na kishughuli na humjaza ndani kabisa ya nafsi yake na matumaini makubwa. Binadamu hutafuta kuongeza ujuzi wake na utambulisho wake, kwa usahihi kadiri iwezekanavyo, mambo ambayo humnyooshea njia ya kupata mafanikio makubwa zaidi katika maisha. Imani ya majaaliwa na hatima kwa hiyo ni mambo yenye nguvu katika kumwendeleza binadamu kuelekea kwenye malengo yake na ubora wake.
Suala la ukombozi au kulaaniwa kwa mwanadamu limetafutiwa ufumbuzi kwenye mazungumzo yaliyotangulia, kwani ukombozi na kulaaniwa hutokana na matendo ya mwanadamu si kutoka kwenye mambo ambayo yapo nje ya upeo wa hiari zao au kutoka kwenye matukio ya asili ambayo yamepandikizwa na Muumbaji kwenye uhai wa mwanadamu. Wala sio mambo ya kimazingira na urithi ama uwezo wa kimaumbile uliopo ndani ya mwanadamu ambavyo vina athari zozote kuhusu ukombozi wa mtu au laana yake; hayawezi kutengeneza hatima yake. Kile kinachokadiria mambo ya binadamu ya siku za usoni, ni ule mhimili ambamo ukombozi au kulaaniwa kwake huzunguuka na chanzo cha kupanda au kushuka kwake, ni kiwango ambacho mwanadamu kama kiumbe ambacho kimepewa hiari ya kuchaga, hutengeneza matumizi yanayofaa ya akili yake na ujuzi na uwezo mwingine.
Furaha na ukombozi havitegemei wingi wa uwezo wa kimaumbile. Hata hivyo, ni kweli kwamba mtu ambaye ana uwezo mkubwa zaidi kuliko wengine pia huwa na wajibu mkubwa zaidi. Kosa dogo kwa upande wake ni la wazi zaidi kuliko kosa hilo hilo ambalo limefanywa na mtu dhaifu na asiye na uwezo. Kila mtu ataitwa kuwasilisha mahesabu yake kwa mujibu wa vipaji na uwezo aliokuwa nao.
Inawezekana kabisa kwamba mtu ambaye uwezo wake wa asili na maarifa ni madogo anatakiwa kuendesha maisha yake kwa mujibu wa kazi zake na wajibu wake, alizopewa na kufikia hiyo furaha ya kweli ambayo hiyo peke yake inastahili ya kituo cha juu sana cha mwanadamu. Kitakachomwezesha kupata matokeo hayo ni ukubwa wa juhudi zake anazotumia ili kufanya matumizi sahihi ya uwezo mdogo aliopewa.
Kinyume chake, mtu ambaye amepewa maarifa ya ndani mwengi sana na uwezo mkubwa, sio tu anaweza kutozitumia kwa kujinufaisha mwenyewe, anaweza kutumia vibaya na kufedhehesha hadhi yake ya ubinadamu; na kujitumbukiza kwenye dimbwi la uovu na dhambi. Mtu kama huyu, bila shaka ni mwovu anayetegemewa kulaaniwa na kamwe hatapata hata sekunde moja ya kuona ukombozi. Qur'ani inasema:
"Kila nafsi itafungika (motoni) kwa (maovu) iliyoyachuma." (74:38).
Kwa hiyo, ukombozi au laana ya mtu hutegemeana na matendo yake ya hiari, sio katika hali yake ya kimaumbile au kisaikolojia. Huu ni udhihirisho wa wazi mno wa uadilifu wa Mwenyezi Mungu.
Moja ya kanuni bainifu za madhehebu ya Shia ni badaa, neno lenye maana kwamba hatima za wanadamu hubadilika pale ambapo mambo na vyanzo vinavyoyarekebisha hubadilika; kile kinachoonekana kama cha milele na kisichobadilika, hubadilika kwa mujibu wa mabadiliko ya tabia ya mtu na matendo yake. Kama ambavyo vipengle vya kimaada vinavyoweza kubadili hatima ya mtu, vipengele visivyo vya kimaada pia vinaweza kuchochea matukio mapya.
Inawezekana kwamba vipengele visivyo vya kimaada kama hivi vinaweza kudhihirisha wazi yale yaliyofichika na kinyume na mkondo uliowazi wa matukio. Kwa kweli, kupitia kwenye mabadiliko ya sababu na mazingira, Mwenyezi Mungu ataamua kwamba tukio jipya litatokea, lenye manufaa zaidi ya lile lililobadilishwa. Hii inalingana na ile kanuni ya kutangua sheria iliyofunuliwa. Kama sheria ya mwanzo inatanguliwa kwa ajili ya nyingine, hii haionyeshi ujinga au kujuta kwa upande wa mtungaji-sheria za ki-mungu ila tu ni kwamba uhalali wa ile sheria iliyofutwa umefikia mwisho wake.
Hatuwezi kutafsiri dhana ya badaa kwa maana kwamba Mwenyezi Mungu anabadili mawazo Yake baada ya ukweli wa kitu ambacho mwanzoni hakukijua na akaja kukijua baadae. Hii itakuwa inapingana na kanuni ya ujuzi wa Mwenyezi Mungu unaojumuisha ulimwengu wote na kwa hiyo haiwezi kukubaliwa na Muislamu yeyote.
Maombi ya dua ni kipengele kingine, ambacho kwamba athari yake isidhalilishwe. Ni dhahiri kwamba Mwenyezi Mungu anatambua siri za ndani kabisa za kila mwanadamu, lakini katika uhusiano wa mtu na Mwenyezi Mungu, maombi ya dua huchukua nafasi kama ile ya juhudi na matendo katika uhusiano wake na maumbile. Mbali kabisa na athari zake za kisaikolojia, dua husababisha athari inayojitegemea.
Kila sekunde matukio mapya hutokea katika maumbile katika kutokea ambako sababu zinazotangulia hutoa mchango. Vivyo hivyo, katika fani moja mashuhuri sana ya maisha maombi ya dua yana athari kubwa sana katika kumwendeleza mtu kuelekea kwenye malengo yake. Kwa namna ileile tu ambayo Mwenyezi Mungu ameweka wajibu kwenye mfumo wa usababisho kwa kila kitu cha asili, vivyo pia, Ameweka wajibu kwenye maombi ya dua.
Mtu anapozungukwa na matatizo, asije akaangukia kwenye fikra za kukosa matumaini na kukataa tamaa. Milango ya huruma za Mwenyezi Mungu kamwe haikufungwa kwa yeyote yule. Inawezekana kwamba kesho hali mpya inatokea ambayo haiendani na vile alivyotegemea. Kwani, kama isemavyo Qur'ani:
".....Kila siku Yeye yumo katika mambo tofauti tofauti." (55:29).
Kwa hiyo, mtu anatakiwa asiache juhudi zake kamwe. Maombi ya dua ambayo hayaunganishwi na jitihada zinazofaa, kama Ali (a.s) Mkuu wa Wamwogopao Mwenyezi Mungu alivyosema, "Kama mtu anayetaka kuachia mshale kutoka kwenye upinde usiokuwa na kamba." Wakati anapofanya juhudi mfululizo, mtu anatakiwa kuweka matakwa yake mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kutumaini na kuamini, na kuomba msaada kwa moyo wote kutoka kwenye kile chanzo cha uwezo wa milele. Mwenyezi Mungu, kwa hakika atamshika mkono mhusika na kumsaidia.
Qur'ani inasema:
وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾
"Na waja wangu watakapokuuliza juu yangu basi hakika mimi nipo karibu, nayaitikia maombi ya muombaji anapoomba. Basi waniitikie na waniamini, ili wapate kuongoka." (2:186).
Roho ya binadamu itapaa juu kuelekea kwa Mwenyezi Mungu na kumtosa kwenye furaha ya kweli ikiwa atakwepa lindi la kuhitaji kwa kuvunja uhu- siano na vyanzo vyote na kumgeukia Mwenyezi Mungu. Hapo atajiona ameungana moja kwa moja na dhati ya Mwenyezi Mungu na kuhisi kuguswa na neema na baraka Zake zisizo na ukomo. Imamu Sajjad(a.s) anamuomba Mwenyezi Mungu ifuatavyo katika dua yake ijulikanayo kama Dua ya Abu Hamza:
"Ee Muumba! Naona njia za kuombea na kulalamikia zinazoelekea Kwako zikiwa wazi na zilizosawazishwa, na sababu za matumaini Kwako zikiwa nyingi sana. Naona inaruhusiwa kuomba msaaada kutoka kwenye neema Yako na huruma Yako, na ninaiona milango ya dua ipo wazi kwa wote wanaokujia Wewe na kuomba msaada Wako. Ninao uhakika kwamba Wewe upo tayari kujibu maombi ya wale wanaokuomba Wewe na kutoa hifadhi kwa wale wanaoitafuta kutoka Kwako."[46]
Pia ipo hadithi kuhusu athari za dhambi na matendo mema: "Wale wanaokufa kwa sababu ya dhambi ni wengi zaidi kuzidi wale wanaokufa kwa sababu za kawaida, na wale wanaoishi kwa sababu ya kutenda matendo mema ni wengi zaidi kuliko wale wanaoishi kwa sababu ya umri wao wa kawaida."[47]
Ilikuwa ni athari za dua zilizomwezesha Zakariya, Mtume wa kweli ambaye alikuwa amekata tamaa ya kupata mtoto, kufanikiwa matakwa yake; ilikuwa athari ya toba iliyomwokoa Mtume Yunus na watu wake kutokana na janga na kuangamia. Sheria ambazo Mwumbaji Mkuu amezipandikiza kwenye mfumo wa ulimwengu, kwa namna yoyote ile haziwezi kuwa mipaka ya uwezo Wake usio na ukomo au kupunguza upeo wake. Anao uamuzi ule ule wa uhakika katika kubadilisha sheria hizo, katika kuthibitisha au kutangua athari
zao, kama Alivyofanya katika kuziasisi. Hiyo dhati ya Pekee, Ambayo usimamizi wake wenye uangalifu na mpana unajumuisha mfumo wote wa uhai, haiwezi kutiishwa kabisa na sheria na viumbe ambavyo Ameviumba Mwenyewe, au Apoteze madaraka na uwezo wa kufanya Atakavyo. Tunaposema kwamba Mwenyezi Mungu anao uwezo wakati wowote kubadili jambo ambalo Ameliumba katika dunia, hatuna maana kwamba Huharibu utaratibu wa dunia na kanuni zake zilizowekwa au anabadilisha sheria na kanuni za maumbile. Kutendeka hasa kwa mabadiliko hutokea kwa kulingana na kanuni fulani zisizojulikana na vigezo ambavyo vinaupita uelewa na utambuzi wetu mfinyu. Endapo mtu analitazama kwa uangalifu na umakini jambo lenyewe na akaufikiria wigo mpana wa uwezekano ambao unamkabili, utamzuia kufanya majaribio makubwa kwa shauku kabisa, ya kutabiri vitu vyote kwa msingi wa kanuni zile chache ambazo ameweza kuzichunguza katika nyanja ya maumbile.