9
MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE
SOMO LA TISA
QUR'ANII INAMUWASILISHAJE MWENYEZI MUNGU
Tunapotaka kutathmini tabia na ujuzi wa kisayansi wa msomi, tunapima kazi zake na kuzichunguza kwa karibu zaidi. Vivyo hivyo, ili tuweze kupima kipaji, ubunifu na uwezo wa msanii wa kuvumbua michoro bunifu, tunafanya uchunguzi wa bidhaa zake za kisanii.
Kwa njia hiyo hiyo, tunaweza pia kutambua sifa na tabia za nafsi halisi ya Muumba kutokana na sifa na mpangilio ulioenea katika maumbile yote, pamoja na ustadi na utaratibu wake. Hapo, ndani ya mipaka iliyowekwa na uwezo wetu wa kujua na kutambua, tunaweza kufahamu ujuzi wa Mwenyezi Mungu, hekima, uhai na uwezo.
Endapo likiwa ni suala la ujuzi kamili na mpana juu ya Mwenyezi Mungu basi, kwa kweli, lazima tukubali kwamba uwezo wa mwanadamu wa kujua haufikii kiwango hicho. Sifa za Mwenyezi Mungu haziwezi kuwekwa ndani ya mipaka yoyote inayofahamika, na ulinganisho wowote au mfanano tunaoutoa juu ya sifa hizo hauna budi uwe wa uwongo, kwani chochote kinachoweza kuchunguzwa na sayansi na fikira katika nyanja ya maumbile ni kazi ya Mwenyezi Mungu na matokeo ya utashi na amri yake, ambapo dhati yake sio sehemu ya maumbile na haitokani na aina ya vitu vilivyoumbwa. Hivyo, dhati ya Mwenyezi Mungu haiwezi kueleweka kwa mwanadamu kwa njia ya ulinganisho na analojia - mfanano na kilichotangulia kuwepo.
Kwa ufupi, Yeye ni nafsi Ambaye kwa elimu ya dhati Yake hakuna kipimo au kigezo chochote kilichopo na kwa ukadiriaji wa uwezo Wake, mamlaka na ujuzi Wake, hatunazo tarakimu wala takwimu zake. Hivi, mwanadamu ni duni sana na asiye na uwezo wa kutambua kitu chochote cha dhati na sifa za ukweli wenye kutokeza kiasi hiki? Kukubali udhaifu wa uwezo wetu na kutoweza kwetu kupata elimu kamili, ya kina na pana ya Mwenyezi Mungu haimaanishi kwamba tumenyimwa kila aina ya ujuzi, uwe mdogo kiasi gani.
Mpangilio wa utaratibu wa ulimwengu unatangaza kwa sauti kubwa sifa Zake kwetu, na tunaweza kuuelewa uwezo na ubunifu usio na mipaka wa Mola Mlezi kutoka kwenye uzuri na manufaa ya maumbile. Maajabu yanayoonekana, kwetu sisi ni dalili ya Dhati Yake ya kipekee.
Mazingatio ya utashi, utambuzi ujuzi na upatanifu wa asili katika mpangilio wa maumbile na mambo yote mbalimbali ya maisha, hufanya iwezekane kwetu kutambua kwamba sifa zote hizi - pamoja na vipengele vingine vyote vinavyozungumzia lengo, mwelekeo na madhumuni ni muhimu vitoke kwenye utashi wa Muumbaji Ambaye Yeye Mwenyewe anazo sifa hizi kabla hazijaakisiwa katika kioo cha maumbile.
Kile kinachokuja kumjua Mwenyezi Mungu na kugusa nafsi Yake ni uwezo usio kifani wa fikra - mwanga wa ghafla ambao kutokea kwenye kile chanzo cha kabla ya umilele ukamulika juu ya mata na kuipatia uwezo wa kupata ujuzi na kusonga mbele kuelekea kwenye ukweli. Ni kutoka ndani ya zawadi hii kuu ya ki-Mungu ambamo elimu ya Mwenyezi Mungu inadhihirishwa.
Uislamu hushughulika na elimu ya Mwenyezi Mungu kwa njia ya wazi na ya simulizi. Qur'ani, chanzo cha msingi wa kujifunzia falsafa ya maisha ya Kiislamu, inatumia mbinu ya kukana na kuthibitisha kwenye swali hili. Kwanza ilikana, kwa njia ya ushahidi wa kusadikika na dalili, kuwepo kwa miungu ya uwongo, kwa sababu katika kuyaendea mafundisho ya juu sana ya upweke, kwanza ni lazima kukana aina zote za miungu ya uwongo na ibada ya mwingine mbali na Allah. Hii ndio hatua ya kwanza muhimu katika njia ya kuuelekea upweke.
Qur'ani inasema:
أَمِ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ آلِهَةً قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ هَـٰذَا ذِكْرُ مَن مَّعِيَ وَذِكْرُ مَن قَبْلِي بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ الْحَقَّ فَهُم مُّعْرِضُونَ ﴿٢٤﴾
"Au wanawaabudu miungu mingine badala yake? Sema: Leteni ushahidi wenu! Huu ni ukumbusho wa hawa walio nami, na ukumbusho wa walio kabla yangu. Lakini wengi wao hawaijui kweli, na kwa hiyo wanapuuza." (Anbiya:21:24).
قُلْ أَتَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا نَفْعًا وَاللَّـهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٧٦﴾
"Sema: Je! Mnawaabudu, badala ya Mwenyezi Mungu, wale ambao hawawezi kukudhuruni wala kukufaeni? Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kujua." (Maida:5:76).
Yule ambaye amevunja uhusiano wake na upweke wa Mwenyezi Mungu husahau pia, nafasi yake halisi kuhusiana na dunia na uhai na nafasi hiyo inakuwa imetenganishwa na yeye mwenyewe. Kwani namna mbaya kabisa ya mfaraka binafsi ni kukata viunganisho vyake vyote na hali yake ya asili kama mwanadamu. Kinyume chake, pindi mtu anapotenganishwa na asili yake mwenyewe, kwa athari ya mambo ya ndani na ya nje, pia atatengwa na Mungu wake na kufanywa mtumwa na asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
Kujiweka chini ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu, ndipo basi huchukua nafasi ya fikira yote ya kimantiki. Hii inawakilisha kugeuka na kuanza kuabudu maada, kwani kuabudu sanamu na kuweka ubora kwenye maada, zote ni aina za muanguko ambao unamnyang'anya mwanadamu uwezo wake wa asili wa ukuaji.
Tauhiid (Upweke wa Mungu mmoja) tu, ndio nguvu inayomwezesha mwanadamu kukamata tena uumbwaji wa maadili ya binadamu. Kwa kuirudisha tena hadhi yake halisi, mtu huingia katika hali ya uelewano na asili yake mwenyewe ya kibinadamu na asili ya msingi ya viumbe wote, hivyo kufikia muundo kamilifu zaidi wa uhai ukiwa wazi kwa ajili yake. Katika historia yote, miito yote na vuguvugu za kidini zilianza kwa kutangaza upweke wa ki-ungu na utukufu pekee wa Mwenyezi Mungu.
Hakuna fikra ambayo imepata kutokea kwa mwanadamu ambayo ni yenye kuleta matunda zaidi ya utambuzi wa ubunifu na wenye kuhusika zaidi kwenye maeneo mbalimbali ya maisha ya binadamu, kizuizi chenye nguvu zaidi katika upotovu wa mwanadamu, kuliko dhana ya upweke wa Mwenyezi Mungu. Kwa kutumia ushahidi wa wazi kabisa, Qur'ani inamwonyesha mtu njia ya kupata elimu juu ya Mwenyezi Mungu kama ifuatavyo:
أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ ﴿٣٥﴾ أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بَل لَّا يُوقِنُونَ ﴿٣٦﴾
"Ama wao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji? Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini." (52:35-36).
Qur'ani inamwachia mwanadamu atumie fikira na akili yake ya kawaida ili atambue uwongo wa nadharia mbili hizi - kama mwanadamu ametokea kuwepo mwenyewe tu vivi hivyi, au kama alikuwa amejiumba yeye mwenyewe - kwa kuzifanyia majaribio na kuzichanganua kwenye maabara ya akili yake. Kwa kutafakari juu ya dalili na ishara za Mwenyezi Mungu, atatambua kwa uhakika uliowazi na dhahiri kabisa kile chanzo cha maumbile yote na kuelewa kwamba hakuna tathmini yoyote inayoweza kutolewa juu ya mtindo wowote wa ulimwengu isipokuwa pawepo na akili inayopanga na yenye uwezo inayofanya kazi nyuma yake.
Kwenye Aya zingine, mazingatio ya mwanadamu yameelekezwa kwenye jinsi alivyoumbwa na kutokeza kwake pole pole kutokea kwenye hali ya kutokuwepo kabla. Hivyo, anakuja kutambua kwamba uumbwaji wake wa kipekee, pamoja na maajabu yote uliyonayo, ni dalili na ishara za utashi wa ki-ungu usiyo na ukomo, miale inayopenyeza na kugusa viumbe vingine vyote. Qur'ani inasema:
وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن سُلَالَةٍ مِّن طِينٍ ﴿١٢﴾ ثُمَّ جَعَلْنَاهُ نُطْفَةً فِي قَرَارٍ مَّكِينٍ ﴿١٣﴾ ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَامًا فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْمًا ثُمَّ أَنشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ فَتَبَارَكَ اللَّـهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ ﴿١٤﴾
"Na kwa yakini tumemuumba mwanadamu kutokana na asili ya udongo. Kisha tukamjaalia awe tone ya mbegu ya uzazi katika kalio madhubuti. Kisha tukaliumba tone kuwa damu iliyoganda, na tukaiumba damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa na mifupa tukaifunika na nyama. Kisha tukamfanya kiumbe kamili. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu, Mbora wa waumbaji." (23:12-14).
Wakati ambapo kijusi (mimba) kinapokuwa tayari kuanza kupata mwili na umbo, chembehai zote za macho, masikio, ubongo na viungo vingine, huanza kufanya kazi na huanza utendaji wao usiyo na ukomo. Huu ndio ukweli ambao Qur'ani inaelekeza mazingatii ya mwanadamu. Halafu, Qur'ani inamuuliza mwanadamu swali la kwamba kama maajabu yote haya yanaendana na ile nadharia ya kwamba hakuna Mungu.
Wala sio suala la kwamba mambo kama haya yanathibitisha na kuonesha, kwa msisitizo mkubwa, kuwepo na haja ya mpango, usanifu, mkono unaoongoza ukisukumwa na utashi makini? Hivi inawezekana kwamba chembe hai za mwili ziweze kujifunza kazi zao, zifuatilie malengo yao kwa mtindo sahihi na mpangilio, na kujidhihirisha kimuujiza kiasi hicho katika ulimwengu wa viumbe, bila ya kuwepo nafsi yenye utambuzi na uwezo mkubwa na ambayo inatoa maelekezo?
Qur'ani inajibu swali hili ifuatavyo:
هُوَ اللَّـهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ يُسَبِّحُ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢٤﴾
"Yeye ndiye Muumbaji, Mtengenezaji, Mtiaji sura, Mwenye majina mazuri kabisa. Kila kilichoko katika mbingu na ardhi kinamtakasa, naye ni Mwenye kushinda, Mwenye hikima." (Hashir:59:24).
Qur'ani inaelezea kila jambo la hisia ambalo mtu analiona karibu yake kama ni kitu kinachohitaji kutafakari na kupata hitimisho lake:
وَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ ﴿١٦٣﴾ إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَالْفُلْكِ الَّتِي تَجْرِي فِي الْبَحْرِ بِمَا يَنفَعُ النَّاسَ وَمَا أَنزَلَ اللَّـهُ مِنَ السَّمَاءِ مِن مَّاءٍ فَأَحْيَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا وَبَثَّ فِيهَا مِن كُلِّ دَابَّةٍ وَتَصْرِيفِ الرِّيَاحِ وَالسَّحَابِ الْمُسَخَّرِ بَيْنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿١٦٤﴾
"Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapanaa Mungu ila Yeye. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kuhitilafiana usiku na mchana, na marikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayoyateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza kila aina ya wanyama; na katika mabadiliko ya pepo, na mawingu yanayoamrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka humo zimo Ishara kwa watu wanaozingatia" (Baqarah :2:163-164.
قُلِ انظُرُوا مَاذَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا تُغْنِي الْآيَاتُ وَالنُّذُرُ عَن قَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ ﴿١٠١﴾
"Sema: Angalieni kwa makini yaliyomo mbinguni na kwenye ardhi! Na Ishara zote na maonyo hayawafai kitu watu wasioamini". (Yunus: 10:101).
Qur'anii pia inataja uchunguzi wa historia ya mwanadamu na watu wa kale pamoja na mabadiliko yote ambayo yamefanyika kama chanzo maalum cha elimu. Qur'ani inamlingania binadamu kuzingatia, ili aweze kugundua ukweli, kwenye ushindi na kushindwa, utukufu na udhalili, bahati na misiba ya watu mbali mbali wa zama za kale, hivyo kwamba kwa kujifunza mpangilio na sheria sahihi za historia, ataweza kunufaika yeye na jamii yake kwa kulinganisha historia ya wakati wake mwenyewe na sheria hizo.
Kwa hiyo Qur'ani inatangaza:
وَكَمْ قَصَمْنَا مِن قَرْيَةٍ كَانَتْ ظَالِمَةً وَأَنشَأْنَا بَعْدَهَا قَوْمًا آخَرِينَ ﴿١١﴾
"Na mingapi katika miji iliyokuwa ikidhulumu tumeiteketeza na tukawasimamisha baada yake watu wengine." (21:11).
قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِكُمْ سُنَنٌ فَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ ﴿١٣٧﴾
"Kabla yenu zimepita nyendo nyingi; basi tembeeni katika ulimwengu muangalie vipi ulikuwa mwisho wa wanaokanusha" (Imran: 3:137).
Qur'ani pia inatambua dunia ya ndani ya mwanadamu, ambayo inaielezea kwa neno anfus (nafsi) kama chanzo cha tafakari yenye kutoa matunda mazuri na ugunduzi wa ukweli. Inaonyesha umuhimu wake kama ifuatavyo:
سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ أَوَلَمْ يَكْفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ ﴿٥٣﴾
Tutawaonyesha ishara zetu kwa dhahiri kabisa katika dunia na ndani ya nafsi zao, mpaka iwabainikie kwamba Mwenyezi Mungu ni Haki." (Fussilat: 41:53)
وَفِي الْأَرْضِ آيَاتٌ لِّلْمُوقِنِينَ ﴿٢٠﴾ وَفِي أَنفُسِكُمْ أَفَلَا تُبْصِرُونَ ﴿٢١﴾
"Na katika ardhi zipo Ishara kwa wenye yakini. Na pia katika nafsi zenu. Je! Hamwoni? ( Zariyat: 51:20-21).
Kwa maneno mengine ni kwamba kipo chanzo kikubwa cha elimu katika uzuri na mpachano wa mwili wa binadamu, pamoja na viungo vyake vyote na uwezo, matendo yake na athari zake, taratibu zake zilizo sahihi na stadi, nishati zake mbali mbali na silika zake, utambuzi wake, hisia na misisimko yake, yote, ya kinyama na kibinadamu, na hasa zaidi katika uwezo wa kushangaza wa akili na utambuzi ambao mtu amepewa - uwezo ambao bado unabakia kwa kiadi kikubwa haujajulikana, kwani mwanadamu amechukua hatua chache tu katika kuichunguza nguvu hii isiyoonekana na uhusiano wake na umbile la mwili wake.
Qur'ani inatangaza kwamba inatosha kutafakari na kuipima nafsi yako mwenyewe ili uweze kuongozwa kwenye chanzo cha milele na kisichokuwa na ukomo kisichohitajia kitu chochote, chenye ujuzi usio na mipaka, ustadi na uwezo, na ule mfano dhaifu ambao unaonekana katika utu wako. Hapo ndipo utakapojua kwamba ni huo ukweli usio na ukomo ambao umezikusanya mahali pamoja mchanganyiko wenye manufaa kiasi hicho wa vitu asili na kuutokeza kwenye uwanja wa uhai.
Kujulikan kwa dalili za wazi kama hizo na uthibitisho wenye maamuzi, ambao umewekwa wazi mikononi mwako na ndani ya mwili wako mwenyewe ili uweze kutafuta elimu ya Mwenyezi Mungu, hakuna kisingizio kitakachokubaliwa kutoka kwako kwa upotofu na ukanusho. Qur'ani pia inatumia mbinu ya ukanushaji na uthibitisho kwenye suala la sifa za Mwenyezi Mungu. Hivyo, inatoa maelezo ya sifa ambazo kwamba dhati ya Muumbaji inakuwa nazo kama 'sifa za kukubali.' Miongoni mwa hizo ni ujuzi, uwezo, utashi, ukweli kwamba kuwepo Kwake hakukutanguliwa na kutokuwepo na kwamba dhati Yake haina mwanzo, na ukweli kwamba misogeo yote ya dunia inapatikana kutokana na utashi Wake na uwezo Wake.
Qur'ani inasema:
هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ ﴿٢٢﴾ هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٢٣﴾
"Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, ambaye hapana Mungu isipokuwa Yeye tu. Mwenye kuyajua yaliyofichikana na yanayoonekana. Yeye ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana aabudiwaye isipokuwa Yeye tu. Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani, Mwenye nguvu, Anayefanya analolitaka, Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayomshirikisha nayo." (Hashir: 59:22-23).
'Sifa za ukanushaji' ni zile ambazo Mwenyezi Mungu yupo huru nazo. Ni pamoja na ukweli kwamba Mwenyezi Mungu hana mwili na hana mahali; dhati yake takatifu haina mshirika wala wakufanana nayo; Yeye si mfung- wa kwenye mipaka iliyowekwa na ukomo wa hisia; Hakuzaa wala hakuzaliwa; wala hakuna mabadiliko wala msogeo katika dhati Yake, kwani Yeye ni mkamilifu kabisa, na Yeye haikabidhi kazi ya uumbaji kwa yeyote.
Qur'ani inasema:
قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ ﴿١﴾ اللَّـهُ الصَّمَدُ ﴿٢﴾ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ ﴿٣﴾ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ ﴿٤﴾
"Sema; Yeye Mwenyezi Mungu ni Mmoja. Mwenyezi Mungu ndiye anayekusudiwa kwa haja. Hakuzaa wala hakuzaliwa. Wala hana anayefanana naye hata mmoja." (Iklas: 112:1-4).
سُبْحَانَ رَبِّكَ رَبِّ الْعِزَّةِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿١٨٠﴾
"Ameepukana Mola Wako, Mola Mwenye enzi na yale wanayomsifu nayo." (37: 180).
Mantiki ya kibinadamu, ambayo bila kupingwa hufikiria kwa namna yenye ukomo, hana uwezo wa kuketi katika kuhukumu utakatifu, kwa sababu lazima tukubali kwamba si rahisi kutambua msingi halisi wa nafsi hiyo ambayo juu yake hakuna kifanani au kilingano cha kuonekana au kufahamika kinachopatikana katika ulimwengu wa maumbile. Madhehebu kubwa sana na mbinu kubwa sana za tafakuri hapa zinaangukia kuwa mawindo ya utatanishi.
Kama vile ambavyo viumbe vyote hai lazima virudi nyuma kwenye asili ambayo kwayo uhai unafanana, kwa nafsi huru ambayo juu yake viumbe vyote vingine vinategemea, hivyo pia, lazima vitokane na chanzo cha uhai, uwezo na ujuzi, kutoka kwenye ile nafsi ambamo humo ndimo sifa hizi na ubora zinamochipukia.