13
MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE
SOMO LA KUMI NA TATU
ELIMU YA MWENYEZI MUNGU ISIYO NA MIPAKA
Muumbaji ambaye hawezi kuzingirwa na mahali, Ambaye Dhati yake haiwezi kuwekewa ukomo, Ambaye uhai wake umeenea kila sehemu ya mbingu na dunia - Muumbaji kama huyu kwa kawaida anatambua vitu vyote, hapana kitu kilichomo katika mpangilio wote wa maumbile ambamo miale yenye nuru kali ya elimu yake haikiangazii.
Matukio yanayotokea sehemu za mbali sana za ulimwengu, matukio yaliyotokea mabilioni ya miaka iliyopita au ambayo yatatokea mabilioni ya miaka ya wakati ujao baadaye - yote yamo ndani katika ujuzi wake, na majaribio makubwa, mapana sana katika kuitafsiri elimu yake, hayana budi kwa hiyo kutofanikiwa.
Ili kuweza kuuelewa upeo mkubwa wa elimu Yake, tunapanua wigo wa fikra zetu, tunatumia akili zetu kutafakari na kutafiti, na kujaribu kusonga mbele kuelekea lengo letu tukiwa na akili nzuri. Mambo mengine yote yakishindikana, hata hivyo, chombo chetu cha kiakili hupungukiwa ustadi unaohitajika kufikia lengo hilo. Kama tungekuwa tuwepo kila mahali kwa namna ile ile ambayo tunaishi mahali maalum kwa muda uliopangwa, ili kwamba hakungekuwa na mahali ambapo panakoseshwa kuwepo kwetu sisi, hakuna kitu kingefichikana kwetu na tungetambua kila kitu.
Kwetu sisi, dunia ya maumbile imegawanywa katika sehemu mbili: sehemu tunayoiona dhahiri na ile tusiyoiona. Vitu "vimefichikana" kwa maana kwamba, ukweli fulani, ambao hauna ukomo na usio na umbile, hauwezi kutambuliwa na milango ya fahamu za nje. Ni muhimu kukumbuka kwamba mfumo wote wa uhai hauwi na mambo yaliyomo kwenye upeo wa sayansi za kutegemea majaribio. Ili kuzielewa siri na miujiza ya maumbile, tunahijati, kama ilivyo kuwa, jukwaa la kujiinulia (kielimu). Muinuko tunaoweza kufika unategemea nguvu ya akili yetu tuliyonayo na kiwango cha uelewa wetu unaosukuma mbele mwinuko wetu. Pindi tunapokuwa na jukwaa linalofaa, ukweli mwingi utakuwa ni wenye kujulikana kwetu.
Kwa kupitia matumizi ya neno ghaibu (fichwa) Qur'ani Tukufu inamfunulia mwanadamu mwonekano mpana wa ukweli halisi. Mitumbe wa Mwenyezi Mungu pia wamejitahidi kuunyanyua utambuzi wa mwanadamu juu ya ulimwengu ulioumbwa hadi kwenye kiwango kinachojumuisha visivyo na ukomo na vyenye ukomo na mipaka ya visivyoonekana na vipimo vya vinavyoonekana. Kwa upande wa Mwenyezi Mungu, hayo "yaliyofichika" hayapatikani kamwe; kwake Yeye, ulimwengu wote 'unaonekana.'.Qur'ani inasema:
هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ ﴿٢٢﴾
" ..Mwenye kuyajua yaliyo fichikana na yanayoonekana. Yeye ni Mwingi wa rehema, Mwingi wa kurehemu." (59:22).
Chochote kilichotengenezwa na binadamu kinatokana na ustadi, akili na ujuzi wa mtu aliyekitengeneza. Jinsi kitu hicho kitakavyokuwa kigumu kiufundi na kisafi zaidi, ndivyo kitakavyoonyesha wazi wazi ukubwa na upana wa elimu ya mtengenezaji wake, na ndivyo kwa ukamilifu zaidi kitakavyozidi kuthibitisha uwezo wake wa kubuni na kuunda. Kazi za mikono za mwanadamu haziwezi kulinganishwa kwa hali yoyote na ule mwujiza na utukufu ya maumbile. Hata hivyo, kwa upande wetu inatuashiria kwamba ule utaratibu wa ulinganifu na mpangilio wa ulimwengu, na kuonekana kwa akili nyingi kwenye mtindo huu ulio mpana, mzuri na wa kustaajabisha mno wa maumbile, lazima uwe unaonyesha kwa umuhimu kwamba mtayarishaji mwenye kuupanga lazima awe na elimu kubwa isiyo na mipaka. Mpangilio wa ulimwengu ndio uthibitisho wenye nguvu zaidi juu ya kuwepo kwa dhati ambayo inafurika kwa elimu, utashi, utambuzi na hekima na imebuni maajabu ya maumbile kwa mujibu wa mpango uliokadiriwa kwa ufasaha na usahihi. Dalili za ujuzi Wake usio na ukomo unaonekana wazi kwenye kila sehemu ya kila kiumbe.
Majaribio na nadharia za wanasayansi yanatoa uthibitisho kwa yeyote anayeutaka kuhusu ujuzi wa Mwenyezi Mungu usio na mipaka na kujidhihirisha kwake kwenye wadudu, wanyama na katika nyanja ya mimea. Mwenyezi Mungu ana utambuzi wa njia zipitamo nyota angani, dunia ya nyota nyingi za mbali sana iliyojaa ghasia na mzunguko wa makundi makubwa ya nyota; wa vitu vyote vya kabla ya umilele na baada ya umilele; wa jumla ya idadi yote ya chembechembe ndani ya maumbile yote ya mbinguni; wa miondoko ya mabilioni ya viumbe, vikubwa na vidogo, vile vinavyotembea kwenye mgongo wa dunia na ndani ya vina vya bahari; wa desturi na kanuni zinazodhibiti maumbile bila ya kukosea; wa vipengele vya mambo yote, vilivyofichika na vya dhahiri. Yeye anaijua pia ile mikanganyiko yenye kufadhaisha, vizuri zaidi kuliko wanavyoijua wao wenyewe.
Sikiliza tena Qur'ani inasema nini:
أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ ﴿١٤﴾
"Je! Hivi asijue Yeye aliyeumba? Naye ndiye mjuzi wa ya siri Mwenye habari? (67:14).
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَخْفَىٰ عَلَيْهِ شَيْءٌ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ ﴿٥﴾
"Hakika hakifichiki Kwake Mwenyezi Mungu kitu chochote kilichomo ardhini au mbinguni."(3:5).
Wataalam wa sayansi ya viumbe wanafahamu vema zaidi kuliko wengine kuhusu miujiza yenye kutatiza na ya sahihi ambayo imepandikizwa kwenye kila chembe ya maumbile; wanatambua kutokana na uchunguzi na utafiti wao wa mahesabu mbalimbali ambayo yamewekwa ndani ya viumbe vyote, vile vyenye uhai na visivyo na uhai, kwenye seli na matone; wa aina mbali mbali ya matendo na matokeo, ya nje na ya ndani, yale yanayofanyika ndani mwao, na athari za vitu na maudhui zao.
Hivyo, wanashuhudia ishara za hekima ya kushangaza ya Mwenyezi Mungu na ujuzi usio na ukomo katika maumbile au kama Qur'ani inavyoliweka, " ..katika upeo wa mbali." (41:53).
Zaidi ya wengine, wanasayansi hao wamepata fununu ya sifa za Mwenyezi Mungu na ukamilifu Wake, ikiwa ni pamoja na ujuzi Wake usio na mipaka, na endapo hawakatai wito wa dhamira zao, pia watatambua kuwepo kwa Muumbaji kwa uwazi zaidi. Mwanafikra fulani alisema; "Dunia yetu inafanana na dhana kubwa kuliko inavyofanana na mashine kubwa. Kama nadharia au ufasiri wa kisayansi, inaweza kusemekana kwamba dunia ni matokeo ya dhana kubwa, udhihiri wa fikira na dhana iliyo kubwa kuliko yetu. Fikra ya kisayansi inaelekea kusonga kuelekea upande wa nadharia hii."
Ujuzi wa Mwenyezi Mungu haukomeshei kwenye mambo yalivyopita au matukio na mambo ya sasa; ujuzi Wake wa wakati ujao ni sawa kabisa na ule ujuzi wa wakati huu. Ujuzi wa Mwenyezi Mungu, ni kusema kwamba ni wa "papo hapo" katika maana kamili ya neno lenyewe. Sio muhimu kwanza kabisa kwamba pawepo na kitu cha kielimu ambamo ujuzi Wake upasike kujiambatanisha nacho. Vitu vyote vinabakia wazi mbele Yake, kwani kwa wakati huo huo dhati Yake tukufu ingawa ni nyingine tofauti kabisa na viumbe na vitu vyote, pia haikutengana mbali navyo; vitu vyote, vilivyopita na vya wakati ujao; vyote viko kwenye hadhira Yake ya moja kwa moja bila kuingiliwa.
Ali(a.s) Amirul-Mu'minin, anasema:"Yeye Anajua vitu vyote, lakini si kwa kutumia njia au vifaa; ambavyo kutokuwepo kwao kungeweka ukomo wa elimu Yake. Hakuna kitu kilichoongezwa kiitwacho elimu kilichoingilia kati baina Yake na vitu vya ujuzi Wake; hakuna kitu chochote isipokuwa dhati Yake pekee." [39] Hapa, Ali(a.s) anazungumzia kanuni ya kiteolojia kwamba utambuzi wa mambo wa Mwenyezi Mungu ni wa moja kwa moja na wa papo hapo. Katika ujuzi wake wa vitu, Mwenyezi Mungu hana haja ya mifumo ya kiakili ambayo ndio msingi wa elimu inayopatikana. Angekuwa apate ujuzi Wake kwa kutumia mifumo hiyo, hali ya kuhitaji ingejitokeza ndani Yake, ambapo Yeye ameepukana na kuhitaji kabisa.
Yule ambaye kutoka Kwake dunia na vilivyomo humo vimepatikana, ambaye anaweza kutimiza kila mahitaji yanayofikirika, ambaye hutoa kila ukamilifu na neema - hivi inaweza kufikirika kwamba yeye mwenyewe awe wa kufungwa na kuhitaji? Mifumo ya kiakili inabakia akili mwetu tu almradi tunataka idumu humo; inatoweka pindi tu tunapoindolea nadhari zetu kwa sababu zinabuniwa na kutengenezwa na sisi wenyewe. Namna hii ya elimu sio ya moja kwa moja na isiyoingiliwa kati, na kwa hiyo inaitwa "ujuzi wa kupatikana," kwa kutofautisha na "ujuzi wa papo hapo", ambao hauna haja ya njia. Tofauti baina yetu, sisi ambao tunatengeneza mifumo yetu wenyewe ya akili na Muumba aliyeanzisha maumbile yote ipo hapa, kwamba sisi kuwepo kwetu kwenyewe hasa kunatokana na Yeye, na kwa hiyo sisi tunakuwa ni wenye kumhitaji Yeye, ambapo yeye ndiye Muumba wa kweli na mhuishaji wa vitu vyote, si muhitaji, na hana haja ya zoezi la kutazama ili apate ujuzi.
Ufafanuzi wa matukio yaliyopita na yajayo ambayo hutokea katika upeo nafsi na fikra zetu ni lazima una ukomo, kwani tunatumia muda na nafasi maalum ambao nje ya hapo sisi hatuna kuwepo tena. Sisi ni viumbe vya maada tu; na dutu, kwa mujibu wa kanuni za fizikia na nadharia ya uwiano, inahitaji muda na mahali katika maendeleo ya polepole endelevu ya kukua na kubadilika. Yaliyopita na yajayo hayana maana kwa nafsi ambayo imekuwepo kabla na baada ya umilele, kila mahali na wakati wote na iliyoepukana ufungiwaji wa maada na athari zake.
Kwa kuwa kila kiumbe kinategemea juu ya uwepo wa milele wa Muumba kwa ya asili yake na uhai wake, hakuna pazia au kizuizi ambacho kinaweza kuwepo kati ya Mwenyezi Mungu na kiumbe hicho; Mwenyezi Mungu anazienea sehemu zake za ndani na nje na anao uwezo mkubwa kabisa juu ya kiumbe hicho. Mtu mmoja alimuuliza Amirul-Mu'minin Ali(a.s) , "Hivi! Mwenyezi Mungu yupo wapi?" Ali alimjibu: "Sio sahihi kuuliza Mwenyezi Mungu yuko wapi kwa sababu ni Mwenyezi Mungu ndiye Aliyeumba nafasi. Wala si sahihi kuuliza Mwenyezi Mungu alivyo, na ni wa asili gani, kwani ni Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba kila asili. Zaidi ya hayo, si sahihi kuuliza Mwenyezi Mungu ni nini kwa sababu ni Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba vyanzo (vinavyofanya kitu kiwe kitu - quiddity) vya vitu vyote.
"Atukuzwe Mwenyezi Mungu Mweza wa yote ambaye kwenye mawimbi ya utukufu Wake wenye hekima hushindwa kuogelea, ukumbukaji wa umilele Wake husimamisha fikra zote katika mkondo wake, na Ambaye katika mbingu yake pana ya utakatifu akili hupotea njia!"[40] .
Qur'ani inasema:
وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٥٩﴾
"Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye anajua kilichoko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinachobainisha." (6:59)
Hebu tufikirie kwamba tumo katika chumba kinachoelekea mtaani na tunatazama kupitia dirisha dogo msururu mkubwa wa magari ambayo yanapita kwa kasi mtaani hapo. Ni wazi kwamba hatuwezi kuyaona magari yote kwa wakati mmoja; bali tunayaona moja moja yanapopita mbele ya dirisha hilo, halafu yanatoweka machoni. Kama tungekuwa hatujui lolote kuhusu magari, tungeweza kudhani kwamba yanakuja kuwepo pole pole upande moja wa dirisha halafu yanakoma kuwepo ule upande mwingine wa dirisha.
Sasa dirisha hili dogo linashabihiana kabisa na nyanja yetu ya kuona, linathibitisha wakati uliopita na unaokuja wa magari hayo. Wale walioko nje ya chumba hicho wakiwa wamesimama kando kwenye nia ya migu wanayaona magari yote yakipita kwa pamoja. Hali yetu kuhusiana na muda uliuopita na ujao wa dunia hii ni kama ile ya mtu yule anayetazama magari kupitia kwenye dirisha dogo. Pindi tutakapotambua kwamba Mwenyezi Mungu yuko juu ya muda na nafasi, tunaelewa kwamba matukio yote yaliyopita na yajayo wakati wote huwa yanakuwepo na yanaendelea kuwepo mbele Yake, kama mchoro.
Kwa hiyo, tunatakiwa kuwa na hisia ya wajibu kwa Mumba Ambaye anatambua hata chembe ndogo sana ya shughuli na kitendo cha maumbile - kama isemavyo Qur'ani:"..Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yale mnayoyatenda." (2:283) - na tuepuke dhambi au kosa lolote ambalo linaweza kusababisha sisi k uwa mbali na Yeye. Tunapaswa kumuabudu Mwenyezi Mungu, Mmiliki wa elimu yote Ambaye ametufanya sisi kupita kwenye hatua zote hizi mbali mbali na kupata uwezo tulio nao sasa. Hatupaswi kutozitii amri Zake ambazo hutufungulia njia yetu kuelekea kwenye furaha ya kweli na shabaha ya mwisho ya mwanadamu na tusikubali lengo jingine mbali na Yeye.
Ili tuweze kumfikia Mwenyezi Mungu lazima tujipambe sifa takatifu na tujiandae, katika muda wetu mfupi hapa duniani, kwa ajili ya kukutana Naye. Halafu tuweze kurejea Kwake, ambaye ni chanzo, chimbuko na mwanzo wa kuwepo kwetu. Jambo hili linahitaji bidii ya utendaji yenye kulenga katika utakasaji wa nafsi, kwani wajibu wa kutekeleza busara hii umewekwa juu ya mwanadamu kama dhamana tukufu.