Sura Ya Sita: Al-An'am
Imeteremshwa Makka isipokuwa baadhi ya Aya.
Ina Aya 165.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu
﴿الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَجَعَلَ الظُّلُمَاتِ وَالنُّورَ ثُمَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ يَعْدِلُونَ﴾
1.Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi na akafanya giza na mwangaza. Tena wale waliokufuru wanamlinganisha Mola wao (na wengine).
﴿هُوَ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن طِينٍ ثُمَّ قَضَىٰ أَجَلًا وَأَجَلٌ مُّسَمًّى عِندَهُ ثُمَّ أَنتُمْ تَمْتَرُونَ﴾
2.Yeye ndiye aliyewaumba kwa udongo. Kisha akapitisha muda; na muda maalum uko kwake, Tena nyinyi mnatia shaka.
﴿وَهُوَ اللَّـهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَفِي الْأَرْضِ يَعْلَمُ سِرَّكُمْ وَجَهْرَكُمْ وَيَعْلَمُ مَا تَكْسِبُونَ﴾
3.Na yeye ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini; anaijua siri yenu na dhahiri yenu na anayajua mnayoyachuma.
Aya 1 - 3
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi na akafanya giza na mwangaza.
Aya zote hizi tatu ni Aya za kilimwengu zinazofahamisha umoja wake na ukuu wake Mwenyezi Mungu.
Aya ya kwanza inaashiria kuumbwa mbingu na ardhi na giza na mwangaza.
Aya Ya pili, inaashiria kuumbwa mtu na kufufuliwa kwake baada ya kufa.
Na ya tatu, kuenea ujuzi wake kwa kila kitu.
Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:"Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu," anakusudia kufundisha; yaani semeni sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu (Alhamdulillah).
Kumsifu Mwenyezi Mungu ni kuzuri katika hali zote; hata wakati wa madhara. Kwa sababu yeye ndiye afaaye kutukuzwa na kuadhimisha. Ukipatwa na msiba na ukasema Alhamdulillah basi hapo unazingatiwa kuwa mvumilivu (mwenye subira) juu ya shida, na imani yako ni yenye nguvu iliyokita ambayo haiyumbishwi na chochote.
Uzuri wa Alhamdulillah unatiliwa mkazo wakati wa furaha na kuondolewa balaa. Kwa sababu ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa aliyoneemesha.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amejitaja kuwa ndiye Muumbaji wa mbingu na ardhi na giza na mwangaza ili azizindue akili kwamba Yeye hana mshirika katika uumbaji na Uungu. Kwa hiyo anakuwa Yeye peke yake ndiye mwenye kustahiki kusifiwa na kufanyiwa ikhlasi katika kuabudiwa.
Tena wale waliokufuru wanamlinganisha Mola wao (na wengine). Ajabu ya maajabu ni kwamba ulimwengu huu pamoja na ardhi yake na mbingu yake, na ubainifu huu ulio wazi na dalili mkato, bado hazikuliondoa giza zito kwenye akili ya mshirikina na kwenye moyo wake mpofu wa haki, na akaleta picha kuwa kuna mwingine mwenye kulingana sawa na Mwenyezi Mungu katika kustahiki kusifiwa na kuabudiwa.
Yeye ndiye aliyewaumba kwa udongo.
Yaani ameumba asili yenu, Adam kutokana na mchanga na maji. Au ameumba mada ya kila mtu kwa udongo, kwa sababu mtu anatokana na nyama na damu; na hivyo viwili vimetokana na mmea na nyama ya mnyama aliyetokana na mmea; na mmea nao umetokana na udongo.
Kisha akapitisha muda; na muda maalum uko kwake.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemwekea kila mtu muda (ajali) mara mbili: Wa kwanza, unaisha kwa kufa kwake, hapo hujulikana ameishi muda gani. Pili, ni kurudishwa na kufufuliwa kwake baada ya kufa. Ujuzi wa muda huu uko kwa Mwenyezi Mungu peke yake wala haujui yeyote katika viumbe vyake; kama lilivyofahamisha neno 'uko kwake'
Tena nyinyi mnatia shaka.
Yaani, baada ya kuweko dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu katika kuumba kukubwa, ambako ni ulimwengu, na katika kuumba kudogo ambako ni kuumba mtu na kufa kwake na kufufuliwa kwake. Baada ya haya yote mnatia shaka katika kuweko Mwenyezi Mungu, umoja wake na utukufu wake!
Tafsir bora ya jumla hii ni kauli ya Amirul-muminin Ali(a.s) :"Namwonea ajabu anayemtilia shaka Mwenyezi Mungu naye anaona kuumba kwa Mwenyezi Mungu; ninamwonea ajabu anayesahau mauti naye anayaona mauti; na ninamstaajabia anayepinga kufufuliwa kwa mwisho naye anaona kufufuliwa kwa kwanza."
Na yeye ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini; anaijua siri yenu na dhahiri yenu na anayajua mnayoyachuma.
Katika Aya ya kwanza Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja kwamba yeye ni Muumbaji wa mbingu na ardhi. Natija ya hayo ni kuwa yeye yuko mbinguni na ardhini; na maana ya kuweko humo ni kuweko athari zake. Katika Aya ya pili ametaja kuwa yeye ndiye Muumba wa binadamu, na atakayemfisha na atakayemfufua. Linalolazimiana na hilo ni kwamba Yeye ni Mjuzi wa anayoyaficha binadamu na anayoyadhihirisha na anayoyachuma katika imani na ukafiri, ikhlasi na unafiki na vilevile vitendo vinavyomrudia yeye vya kheri au shari.
﴿وَمَا تَأْتِيهِم مِّنْ آيَةٍ مِّنْ آيَاتِ رَبِّهِمْ إِلَّا كَانُوا عَنْهَا مُعْرِضِينَ﴾
4.Na haiwafikii ishara yoyote katika ishara za Mola wao ila wanaipinga.
﴿فَقَدْ كَذَّبُوا بِالْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُمْ فَسَوْفَ يَأْتِيهِمْ أَنبَاءُ مَا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ﴾
5.Wameikadhibisha haki ilipowafikia; kwa hiyo zitawafikia habari za yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.
﴿أَلَمْ يَرَوْا كَمْ أَهْلَكْنَا مِن قَبْلِهِم مِّن قَرْنٍ مَّكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ مَا لَمْ نُمَكِّن لَّكُمْ وَأَرْسَلْنَا السَّمَاءَ عَلَيْهِم مِّدْرَارًا وَجَعَلْنَا الْأَنْهَارَ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمْ فَأَهْلَكْنَاهُم بِذُنُوبِهِمْ وَأَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قَرْنًا آخَرِينَ﴾
6.Je hawaoni vizazi vingapi tulivyoviangamiza kabla yao? Tuliwamakinisha katika nchi tusivyowamakinisha nyinyi, Tukawapelekea mvua nyingi, Na tukaifanya mito inapita chini yao. Kisha tukawaangamiza kwa dhambi zao. Na tukaanzisha baada yao karne nyingine.
Aya 4-6
Imeelezwa katika Tafsiri Razi: Wamesema baadhi: Karne ni miaka sitini. Wengine wakasema ni sabini. Wengine wakasema ni thamanini. Lililo karibu zaidi na ufahamu ni kwamba si yenye kukadiriwa kwa muda fulani kwa zaidi au kupungua, bali makusudio ni watu wa kila zama. Wakimaliza muda mwingi husemwa: Imekwisha karne. Dalili ya hilo ni kauli yake Mtume mtukufu(s.a.w.w) :"karne bora ni karne yangu"
Misingi ya itikadi ni mitatu, Tawhid, Utume na Ufufuo. Aya tatu zilizotangulia zimeelezea Tawhid na dalili zake, na Aya hii inaelezea Utume na hali ya wanaoukanusha.
Na haiwafikii ishara yoyote katika ishara za Mola wao ila wanaipinga.
Makusudio ya ishara hapa ni hoja mkato ya kuweko Mwenyezi Mungu na umoja wake, ufufuo na Utume wa Muhammad. Maana ni kuwa makafiri wanakataa dalili ya haki na wanaipinga bila ya kuichunguza. Lau wangelikuwa ni watafutaji ukweli wangeliangalia dalili na kuzingatia maana yake. Ama kukataa na kuipinga kabla ya kuichunguza ni inadi na ujuba.
Wametofautiana wafasiri katika kuainisha makusudio ya hoja waliyoipinga na kuidharau. Je, ni Qur'an au muujiza mwingineo katika miujiza ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) ? Au ni miujiza ya Mitume wote? Nimegundua wakati nikifuatilia tofauti hizi kuwa Aya hii tunayoifasiri na mfano wake katika Qur'an zimekusanya maana ambayo wafasiri wamejihimu kuisherehesha (kuifafanua).
Aya imekusanya dalili kwamba Uislamu unasimamia uhuru wa akili na kutoa maoni na kwamba si haki kwa yeyote, vyovyote awavyo kumtaka mwingine akubali maneno yake hivi hivi tu kwa upofu na bila ya dalili. Hata Muumba wa ulimwengu, ambaye neno lake ni tukufu, hawalazimishi waja wake kumwamini yeye na vitabu vyake, bila ya dalili.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasimamisha hoja kwa kila anayoyasema na kuyatolea mwito na kumtaka kila mwenye akili kuichunguza na kuangalia vizuri maana yake. Mwenyezi Mungu katika hilo ametukuka kabisa - ni kama kila mjuzi anayechunga haki; hata kama ukiwa mbali mshabaha wa Muumba na kiumbe.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
﴿أَوَلَمْ يَتَفَكَّرُوا فِي أَنفُسِهِم مَّا خَلَقَ اللَّـهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ﴾
"Je, hawafikiri katika nafsi zao. Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa haki" (30:8)
Na akasema:
﴿أَفَلَمْ يَنظُرُوا إِلَى السَّمَاءِ فَوْقَهُمْ كَيْفَ بَنَيْنَاهَا وَزَيَّنَّاهَا وَمَا لَهَا مِن فُرُوجٍ﴾
"Je, hawaangalii mbingu zilizo juu yao, vipi tulivyozijenga na tukazipamba wala hazina nyufa" (50:6)
Na akasema tena:
﴿كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ﴾
"Namna hii tunazipambanua ishara kwa watu wanaofikiri" (10:24)
Aya hizi na nyinginezo, zinafahamisha kwa dalili mkato kuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu huleta dalili na hoja kwenye mwito wa haki na kutoa mwito wa kuzifikiria vizuri na kuzichunguza.
Akipinga yule asiyeamini ila yale anayoyataka yeye, basi yeye peke yake ndiye mwenye jukumu la kukanusha kwake na kupinga kwake.
Wameikadhibisha haki ilipowafikia; kwa hiyo zitawafikia habari za yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.
Mtu anaweza kujitia kutoijua haki bila ya kuitilia umuhimu, na kutoiamini, lakini akawa haiungi mkono wala kuipiga vita; kama ilivyo kwa mtu asiyejali mambo. Au anaweza kuwa katika msimamo wa mwenye kuikadhibisha.
Huyu ni mwenye kiburi, ikiwa atakadhibisha na huku anajijua. Ama akiikadhibisha na kuidharau, basi huyo ni mwenye kuipiga vita. Wa kwanza kosa lake ni hafifu kuliko wa pili kwa sababu yeye anafanana na mtu asiyepiga kura.Wa pili naye dhambi yake ni hafifu kuliko watatu kwa sababu yeye ameitia kura yake kwa waongo. Ama wa tatu amekadhibisha na akadhihirisha harakati dhidi ya haki, naye ndiye aliyekusudiwa kukemewa na kupewa kiaga, na kwamba yeye atakutana na malipo ya inadi yake na istihzai yake.
Je hawaoni vizazi vingapi tulivyoviangamiza kabla yao? Tuliwamakinisha katika nchi tusivyowamakinisha nyinyi.
Waarabu wa kijahiliya walikuwa wakijua mengi kuhusu watu wa Ad, Thamud, Lut na wengineo, na katika misafara yao walikuwa wakiona athari zao wakizishuhudia na kuzizungumzia. Walikuwa wakijua kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaangamiza kwa sababu wao walikadhibisha haki waliyokuja nayo Mitume yao kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Aya hii inawahusu wale waliomkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) kuwa wazingatie kuangamia kwa vizazi vilivyo pita. Nao walikuwa na milki na nguvu wasizokuwa nazo hao wanaoambiwa - Waarabu wa kijahiliya, Tukawapelekea mvua nyingi.
Yaani mvua inayoleta mavuno na kuwamiminia riziki. Na tukaifanya mito inapita chini yao. Ni fumbo la rutuba na mavuno mengi. Kisha tukawaangamiza kwa dhambi zao Mali na nguvu hazikuwafaa kitu. Na tukaanzisha baada yao karne nyingine. Mwenye akili ni yule mwenye kupata funzo kutokana na wengine kabla ya mwengine kupata funzo kutoka kwake.