6%

10

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MAISHA YA MOTONI

Moto umetumiwa katika Qur'an na Hadithi kuonyesha makazi mabaya watakaposhukia waovu, walioamua kumpinga Allah (s.w.) na kuendesha maisha yao ya hapa duniani kinyume na kanuni na taratibu alizoziweka Allah (s.w.). Maisha ya motoni ni kinyume na maisha ya peponi ambayo picha yake tumeshaiona. Hebu tuelekeze kamera yetu motoni na kupiga picha ya maisha ya huko. Kwanza kabisa tunafahamishwa na Qur'an kuwa motoni kuna daraja au milango saba.

﴿ وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمَوْعِدُهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٤٣﴾ لَهَا سَبْعَةُ أَبْوَابٍ لِّكُلِّ بَابٍ مِّنْهُمْ جُزْءٌ مَّقْسُومٌ ﴾

"Na bila shaka Jahannam ndipo mahali pao walipoahidiwa Ina milango saba, na kwa kila mlango iko sehemu yao iliyogawanywa" [15:43-44]

Daraja hizi za moto zimepewa majina kama tusomavyo katika Qur'an: Jahannam: Jina hili limetumiwa katika aya nyingi za Qur'an kama jina la ujumla la maisha ya motoni. Hutwamah:

﴿كَلَّا لَيُنبَذَنَّ فِي الْحُطَمَةِ ﴾

"Moto wa kuvunja vunja - moto uliowashwa kwa ukali barabara". [104:4]

Moto mkali wa kuunguza [4:55]

Moto unaobabua. [74:26]

Moto mkali. Qur'an (26:9 na 102:6]

Moto uwakao kwa ukali. Qur'an (101:9]

Mioto hii itawaunguza wakosaji kulingana na makosa yao.

Kwa ujumla aina yoyote ya moto ulioandaliwa makafiri hata ukiwa na daraja ya chini namna gani, utakuwa ni mkali usiokifani na usiovumilika hata kwa muda mfupi sana kama Allah anavyotufahamisha:

﴿إِنَّهَا سَاءَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا ﴾

"Hakika hiyo (Jahannam) ni kituo kibaya na mahali (pabaya kabisa) pa kukaa (hata kwa muda mfupi) " [25:66]

Hebu tuone pia anavyotufahamisha Mtume(s.a.w.w) juu ya kiwango cha ukali wa adhabu ya motoni: Nuuman bin Bashir amesimulia kuwa, Mtume(s.a.w.w) amesema:Hakika atakayekuwa na adhabu nyepesi kabisa katika wakazi wa motoni atakuwa yule atakayekuwa na viatu vya moto. Kwa moto huu (wa nyayoni) utachemsha ubongo wake kama maji yachemkayo kwenye birika. Haitaonekana kuna mwenye adhabu kali kuliko hii, lakini hiki ndio kiwango cha chini kabisa cha adhabu .[Bukhari na Muslim]

Kwa ujumla moto wa adhabu aliouandaa Allah (s.w.) kwa watu waovu ni mkali sana wenye miale yenye kupanda juu kwa hasira. Moto huu umeunguzwa kwa ukali kwa muda wa miaka elfu moja mpaka ukabadilika kuwa mwekundu. Uliunguzwa tena kwa muda wa miaka mingine elfu moja mpaka ukabadilika kuwa mweupe. Kisha uliunguzwa tena kwa miaka mingine elfu moja mpaka ukabadilika kuwa mweusi. Hivi ndivyo tunavyofahamishwa katika Hadithi ifuatayo:Abu Hurairah amesimulia kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ambaye amesema: Moto uliunguzwa kwa muda wa miaka elfu moja mpaka ukawa mwekundu. Kisha uliunguzwa kwa muda mwingine wa miaka elfu moja mpaka ukawa mweupe. Tena uliunguzwa kwa mara nyingine kwa muda wa miaka elfu moja mpaka ukawa mweusi. Sasa ni mweusi tii. [Tirmidh]

Pia tunafahamishwa kuwa Jahannam kutakuwa shimoni kama tunavyofahamishwa katika Hadith ifuatayo: Uthman bin Ghazwaan amesimulia: Imesimuliwa kwetu na Mtume(s.a.w.w) kuwa jiwe litatupwa kutoka ukingoni mwa moto. Litaendelea kuanguka kwa miaka sabini bila kufika chini. Naapa kwa jina la Allah kuwa itajazwa. Na tulifamishwa kuwa umbali katika kati ya milango miwili ya moto na mwendo wa siku arubaini na patakuja siku ambapo itajaa watu. [Muslim]

Humo ndani ya shimo la moto wa Jahannam patakuwa na mashimo (mabonde) na shimo baya kabisa kuliko yote ni "Jabal- Huzn", ambapo Jahannam yenyewe inaomba kukingwa na moto huo wa "Jabal-Huzn" mara sabiini kwa siku. Ndani ya mazingira ya motoni pia patakuwa na miti michungu, na miti maarufu kwa uchungu wake hujulikana kwa jina la "Zaquum". Tumefahamishwa katika Hadith kuwa: Ibn Abbas amesimulia kuwa Mtume (s.a.w.w) alisoma aya hii:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴾

"Enyi mlioamini muogopeni Allah kama ipasavyo kumuogopa,wala msife isipokuwa mmeshakuwa Waislamu kamili". (3:102).

Mtume(s.a.w.w) alisema:Kama tone la Zaquum lingeanguka kwenye nyumba ya dunia hii, lingelitosha kuharibu vitu vyote wanavyovitumia wakazi wa dunia. Sasa itakuwaje kwa yule ambaye hicho kitakuwa ndio chakula chake? [Tirmidh]

Tunapata maelezo kamili ya mti wa Zaquum. Ambao umemea katikati ya Jahannam na watakaostahiki kuula katika aya zifuatazo:

﴿ أَذَٰلِكَ خَيْرٌ نُّزُلًا أَمْ شَجَرَةُ الزَّقُّومِ ﴿٦٢﴾ إِنَّا جَعَلْنَاهَا فِتْنَةً لِّلظَّالِمِينَ ﴿٦٣﴾ إِنَّهَا شَجَرَةٌ تَخْرُجُ فِي أَصْلِ الْجَحِيمِ ﴿٦٤﴾ طَلْعُهَا كَأَنَّهُ رُءُوسُ الشَّيَاطِينِ ﴿٦٥﴾ فَإِنَّهُمْ لَآكِلُونَ مِنْهَا فَمَالِئُونَ مِنْهَا الْبُطُونَ ﴿٦٦﴾ ثُمَّ إِنَّ لَهُمْ عَلَيْهَا لَشَوْبًا مِّنْ حَمِيمٍ ﴾

"Je, karibisho la namna hii silo bora au kupata mti wa Zuqquum? (Mti mchungu kabisa watakaolishwa watu wa motoni). Kwa yakini sisi tumeufanya ni adhabu ya (hao) madhalimu (wa nafsi zao). Hakika huo ni mti unaotoka (unaoota) katikati ya Jahannam. (Panda za) matunda yake (zinatisha) kama kwamba ni vichwa vya mashetani. Bila shaka wao watakula katika (mti) huo, na kwa huo wajaze matumbo (yao). Kisha bila shaka utawathubutikia, juu ya uchungu wa mti huo, mchanganyiko wa maji ya moto". [37:62-67]

Pia katika mazingira ya motoni patakuwa na nyoka na nge wakubwa wenye sumu kali ambao watakuwa wanauma wakazi wa humo kama sehemu ya adhabu yao kama tunavyofahamishwa katika Hadith ifuatayo:

Abdullah bin Harith bin Jazin amesimulia kuwa Mtume(s.a.w.w) amesema:"Kuna nyoka huko motoni wakubwa kama ngamia. Mmoja wao akikuuma mara moja, uchungu wake hubaki kwa miaka arobaini. Kuna nge huko motoni wakubwa kama nyumba. Mmoja wao atamuuma mtu na uchungu wake utabakia kwa muda wa miaka arobaini . [Ahmad]

Kwa vyovyote itakavyokuwa maisha ya motoni yatakuwa magumu sana kwa wakazi wake. Chakula chao kitakuwa cha moto wa kuunguza kila kitu tumboni, mavazi yao yatakuwa ya moto, kinywaji chao cha moto kitakachochemsha matumbo yao. Picha halisi ya mazingira ya motoni, maisha ya wakazi wake na sifa zitakazowafanya wastahiki kuingia humo, aya zifuatazo zinafafanua zaidi:

﴿وَقَالُوا أَإِذَا ضَلَلْنَا فِي الْأَرْضِ أَإِنَّا لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ بَلْ هُم بِلِقَاءِ رَبِّهِمْ كَافِرُونَ ﴿١٠﴾ قُلْ يَتَوَفَّاكُم مَّلَكُ الْمَوْتِ الَّذِي وُكِّلَ بِكُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ ﴿١١﴾وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الْمُجْرِمُونَ نَاكِسُو رُءُوسِهِمْ عِندَ رَبِّهِمْ رَبَّنَا أَبْصَرْنَا وَسَمِعْنَا فَارْجِعْنَا نَعْمَلْ صَالِحًا إِنَّا مُوقِنُونَ ﴿١٢﴾ وَلَوْ شِئْنَا لَآتَيْنَا كُلَّ نَفْسٍ هُدَاهَا وَلَـٰكِنْ حَقَّ الْقَوْلُ مِنِّي لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ ﴿١٣﴾ فَذُوقُوا بِمَا نَسِيتُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَـٰذَا إِنَّا نَسِينَاكُمْ وَذُوقُوا عَذَابَ الْخُلْدِ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴾

"Nao husema (kwa maskhara): "Je, tutakapopotea katika ardhi, (tukageuka mchanga) ndio tutarudishwa katika umbo jipya?" (Ndio) Bali wao hawakiri kwamba watakutana na Mola wao. Sema: "Atakufisheni malaika wa mauti aliyewakilishwa kwenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu".Na ungaliwaona waovu wakiinamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao, (na kusema): "Mola wetu! Tumekwishakuona na tumekwisha kusikia, basi turudishe tutafanya vitendo vizuri, hakika (sasa) tumeyakinisha.Na tungalitaka tungempa kila mtu uwongofu wake (kwa lazima kama tulivyowapa malaika, lakini binadamu amepewa nguvu ya kufanya alitakalo lililo jema na baya), lakini imehakikika kauli iliyotoka Kwangu: Kwa yakini nitaijaza Jahannam kwa wote hawa; majini na watu (ambao ni wabaya). "Basi ionjeni (adhabu) kwa sababu ya kusahau makutano ya siku yenu hii, na sisi tutakusahauni (humo motoni) na onjeni adhabu idumuyo kwa yale mliyokuwa mkiyatenda". [32:10-14]

﴿ إِنَّ جَهَنَّمَ كَانَتْ مِرْصَادًا ﴿٢١﴾ لِّلطَّاغِينَ مَآبًا ﴿٢٢﴾ لَّابِثِينَ فِيهَا أَحْقَابًا ﴿٢٣﴾ لَّا يَذُوقُونَ فِيهَا بَرْدًا وَلَا شَرَابًا ﴿٢٤﴾ إِلَّا حَمِيمًا وَغَسَّاقًا ﴿٢٥﴾ جَزَاءً وِفَاقًا ﴿٢٦﴾ إِنَّهُمْ كَانُوا لَا يَرْجُونَ حِسَابًا ﴿٢٧﴾ وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا كِذَّابًا ﴿٢٨﴾ وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ كِتَابًا ﴿٢٩﴾ فَذُوقُوا فَلَن نَّزِيدَكُمْ إِلَّا عَذَابًا ﴾

"Kwa hakika Jahannam inawangoja wabaya.Ni makazi ya maasi.Wakae humo dahari nyingi (karne baada ya karne) Hawataonja humo baridi (wala usingizi) wala kinywaji.Ila maji yachemkayo sana na usaha (wanalipwa) malipo yaliyo sawa (na amali zao).Hakika wao hawakuwa wakiogopa hisabu (ya Mwenyezi Mungu).Na wakikadhibisha aya zetu kukadhibisha (kukubwa kabisa). Na (hali ya kuwa) kila kitu tumekidhibiti kwa kukiandika. Basi onjeni (leo adhabu yangu). Nasi Hatutakuzidishieni (kitu) ila adhabu (juu ya adhabu) ". [78:21-30]

﴿وَجِيءَ يَوْمَئِذٍ بِجَهَنَّمَ يَوْمَئِذٍ يَتَذَكَّرُ الْإِنسَانُ وَأَنَّىٰ لَهُ الذِّكْرَىٰ ﴿٢٣﴾يَقُولُ يَا لَيْتَنِي قَدَّمْتُ لِحَيَاتِي ﴿٢٤﴾ فَيَوْمَئِذٍ لَّا يُعَذِّبُ عَذَابَهُ أَحَدٌ ﴿٢٥﴾ وَلَا يُوثِقُ وَثَاقَهُ أَحَدٌ ﴾

"Basi siku hiyo italetwa Jahannam.Siku hiyo mwanadamu atakumbuka,lakini kukumbuka huko kutamfaa nini? Atasema:"Laiti ningalitanguliza (wema) kwa ajili ya uhai wangu (huu wa leo)".Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu Kwake (Mwenyezi Mungu). Wala hatafunga yeyote jinsi ya kufunga Kwake (Mwenyezi Mungu) " [89:23-26]

Aya hizi kwa ujumla zimesisitiza kuwa, watakaostahiki adhabu ya motoni ni wanadamu na majini waovu ambao waliendesha maisha yao ya hapa duniani kwa kibri na kinyume na utaratibu aliouweka na kuuridhia Allah (s.w.). Kuhusu adhabu yenyewe itakavyokuwa tunafahamishwa katika aya zifuatazo:

﴿إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِنَا سَوْفَ نُصْلِيهِمْ نَارًا كُلَّمَا نَضِجَتْ جُلُودُهُم بَدَّلْنَاهُمْ جُلُودًا غَيْرَهَا لِيَذُوقُوا الْعَذَابَ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَزِيزًا حَكِيمًا ﴾

"Hakika wale waliozikataa Aya zetu, tutawaingiza katika moto. Kila ngozi zao itakapowiva, tutawabadilishia ngozi nyingine badala ya zile, ili wawe wanaonja (uchungu wa) adhabu (maisha). Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu (na Mwenye Hikima) " [4:56]

Hawa mahasimu wawili waliohasimiana kwa ajili ya Mola wao. Basi wale waliokufuru watakatiwa nguo za moto na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yachemkayo.

﴿هَـٰذَانِ خَصْمَانِ اخْتَصَمُوا فِي رَبِّهِمْ فَالَّذِينَ كَفَرُوا قُطِّعَتْ لَهُمْ ثِيَابٌ مِّن نَّارٍ يُصَبُّ مِن فَوْقِ رُءُوسِهِمُ الْحَمِيمُ ﴿١٩﴾ يُصْهَرُ بِهِ مَا فِي بُطُونِهِمْ وَالْجُلُودُ ﴿٢٠﴾ وَلَهُم مَّقَامِعُ مِنْ حَدِيدٍ ﴿٢١﴾ كُلَّمَا أَرَادُوا أَن يَخْرُجُوا مِنْهَا مِنْ غَمٍّ أُعِيدُوا فِيهَا وَذُوقُوا عَذَابَ الْحَرِيقِ ﴾

"Kwa (maji) hayo vitayayushwa vilivyomo matumboni mwao na ngozi zao (pia). Na kwa ajili yao (yatakuwapo) marungu ya chuma. Kila mara watakapotaka kutoka humo (adhabuni) kwa sababu ya uchungu watarudishwa humo na (kuambiwa): "Ionjeni adhabu ya kuungua".[22:19-22]

﴿وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فِي جَهَنَّمَ خَالِدُونَ ﴿١٠٣﴾ تَلْفَحُ وُجُوهَهُمُ النَّارُ وَهُمْ فِيهَا كَالِحُونَ ﴿١٠٤﴾أَلَمْ تَكُنْ آيَاتِي تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَكُنتُم بِهَا تُكَذِّبُونَ ﴿١٠٥﴾ قَالُوا رَبَّنَا غَلَبَتْ عَلَيْنَا شِقْوَتُنَا وَكُنَّا قَوْمًا ضَالِّينَ ﴿١٠٦﴾ رَبَّنَا أَخْرِجْنَا مِنْهَا فَإِنْ عُدْنَا فَإِنَّا ظَالِمُونَ ﴿١٠٧﴾ قَالَ اخْسَئُوا فِيهَا وَلَا تُكَلِّمُونِ ﴾

"Na wale ambao mizani yao itakuwa nyepesi, hao ndio waliozitia hasarani nafsi zao, na katika Jahannam watakaa muda mrefu. Moto utababua (utaziunguza) nyuzo zao, nao watakuwa humo wenye kukenya (meno yao kwa adhabu).(Waambie): Je! Hazikuwa aya zangu mkisomewa na nyinyi mkizikadhibisha? Watasema:"Mola wetu: Tulizidiwa na ubaya wetu na tukawa watu wenye kutopea. Mola wetu! Tutoe humu (motoni, uturejeshe ulimwenguni, tukafanye amali nzuri), na tufanyapo tena bila shaka tutakuwa madhalimu (wa nafsi zetu kweli kweli). Atasema (Mwenyezi Mungu):"Hizikeni humo wala msinisemeshe (msiseme nami) ". [23:103-108]

﴿إِنَّ شَجَرَتَ الزَّقُّومِ ﴿٤٣﴾ طَعَامُ الْأَثِيمِ ﴿٤٤﴾ كَالْمُهْلِ يَغْلِي فِي الْبُطُونِ ﴿٤٥﴾ كَغَلْيِ الْحَمِيمِ ﴿٤٦﴾ خُذُوهُ فَاعْتِلُوهُ إِلَىٰ سَوَاءِ الْجَحِيمِ ﴿٤٧﴾ ثُمَّ صُبُّوا فَوْقَ رَأْسِهِ مِنْ عَذَابِ الْحَمِيمِ ﴿٤٨﴾ ذُقْ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْكَرِيمُ ﴿٤٩﴾ إِنَّ هَـٰذَا مَا كُنتُم بِهِ تَمْتَرُونَ ﴾

"Bila shaka mti wa Zaqquum, ni chakula cha (kuliwa na) maasi,(kwa umoto wake ni) kama shaba iliyoyayushwa; huchemka matumboni kama chemko la maji ya moto kabisa. (Kuambiwe):"Mkamateni (huyo asi) na mumtupie katikati ya Jahannam.Kisha mwagieni juu ya kichwa chake (aonje) adhabu ya maji ya moto. (Aambiwe): Onja! Ulikuwa (ukijidai kuwa) wewe ni mwenye nguvu, mhishimiwa, (onyesha leo nguvu zako).Hakika hii ndiyo ile (adhabu) mliyokuwa mkibishana (mkiitilia shaka) ". [44:43-50]

﴿ثُمَّ إِنَّكُمْ أَيُّهَا الضَّالُّونَ الْمُكَذِّبُونَ ﴿٥١﴾ لَآكِلُونَ مِن شَجَرٍ مِّن زَقُّومٍ ﴿٥٢﴾ فَمَالِئُونَ مِنْهَا الْبُطُونَ ﴿٥٣﴾ فَشَارِبُونَ عَلَيْهِ مِنَ الْحَمِيمِ ﴿٥٤﴾ فَشَارِبُونَ شُرْبَ الْهِيمِ ﴿٥٥﴾ هَـٰذَا نُزُلُهُمْ يَوْمَ الدِّينِ ﴾

"Kisha nyinyi, mliopotea (na kukadhibisha) kwa yakini mtakula mti wa Mzaqquum, na kwa huo mtajaza matumbo (yenu).Na juu yake mtakunywa maji ya moto yanayochemka. Tena mtakunywa kama wanywavyo ngamia wenye kiu sana.(Na kila wakinywa kiu haiweshi). Hiyo ni karamu yao siku ya malipo". [56:51-56]

﴿هَـٰذَا وَإِنَّ لِلطَّاغِينَ لَشَرَّ مَآبٍ ﴿٥٥﴾ جَهَنَّمَ يَصْلَوْنَهَا فَبِئْسَ الْمِهَادُ ﴿٥٦﴾ هَـٰذَا فَلْيَذُوقُوهُ حَمِيمٌ وَغَسَّاقٌ ﴿٥٧﴾ وَآخَرُ مِن شَكْلِهِ أَزْوَاجٌ ﴾

"Hivyo (ndivyo itakakavyokuwa).Na kwa hakika wale warukao mipaka, pa kurudia pao patakuwa pabaya: Jahannam - wataingia. Nayo ni matengenezeo mabaya kabisa.(Ndivyo hivyo itakavyokuwa). Basi waonje (wanywe) maji ya moto na usaha. Na (adhabu) nyingine za namna hii nyingi.(Kila likitiwa jeshi jingine huko motoni waambiwe wale waliotangulia". [38:55-58]

﴿وَلِلَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ عَذَابُ جَهَنَّمَ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿٦﴾ إِذَا أُلْقُوا فِيهَا سَمِعُوا لَهَا شَهِيقًا وَهِيَ تَفُورُ ﴿٧﴾ تَكَادُ تَمَيَّزُ مِنَ الْغَيْظِ كُلَّمَا أُلْقِيَ فِيهَا فَوْجٌ سَأَلَهُمْ خَزَنَتُهَا أَلَمْ يَأْتِكُمْ نَذِيرٌ ﴿٨﴾ قَالُوا بَلَىٰ قَدْ جَاءَنَا نَذِيرٌ فَكَذَّبْنَا وَقُلْنَا مَا نَزَّلَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا فِي ضَلَالٍ كَبِيرٍ ﴿٩﴾ وَقَالُوا لَوْ كُنَّا نَسْمَعُ أَوْ نَعْقِلُ مَا كُنَّا فِي أَصْحَابِ السَّعِيرِ ﴿١٠﴾ فَاعْتَرَفُوا بِذَنبِهِمْ فَسُحْقًا لِّأَصْحَابِ السَّعِيرِ ﴾

"Na kwa waliomkufuru Mola wao iko adhabu ya Jahannam (inawaongojea). Na ni marejeo mabaya yaliyoje: Watakapotupwa humo watasikia rindimo (mngurumo) lake, na hali ya kuwa inafoka. Unakaribia kupasuka kwa hasira (yake juu ya wabaya).Kila mara litakapotupwa humo kundi (la wabaya) walinzi wake watawauliza: Je! Hakukufikieni mwonyaji? Watasema: Kwanini? Alitujia muonyaji, lakini tulikadhibisha na tulisema: Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote, nyinyi hamumo ila katika upotofu (upotevu) mkubwa. Na watasema: Kama tungalikuwa tunasikia au tungalikuwa na akili tusingalikuwa katika watu wa motoni (leo). Watakiri dhambi zao; (lakini hapana faida).Basi kuangamia kumewastahikia watu wa motoni". [67:6-11]

﴿إِنَّهُ مَن يَأْتِ رَبَّهُ مُجْرِمًا فَإِنَّ لَهُ جَهَنَّمَ لَا يَمُوتُ فِيهَا وَلَا يَحْيَىٰ﴾

Hakika atakayekuja kwa Mola wake, hali ya kuwa mkosa, basi kwa yakini atapata moto wa Jahannam, hatakufa humo wala hataishi (maisha mazuri). [20:74]

﴿فَيَوْمَئِذٍ لَّا يُعَذِّبُ عَذَابَهُ أَحَدٌ﴾

Basi siku hiyo hataadhibu yoyote namna ya kuadhibu Kwake(Mwenyezi Mungu). [89:25]

Aya hizi chache zimetupa picha ya kutisha ya maisha ya Motoni ambapo wakazi wake hawatakuwa na hata chembe ya furaha na hawatakufa japo watatamani wafe. Na hasara kubwa zaidi watakayoipata ni kutomuona Allah (s.w.). Kwani kumuona Allah (s.w.) ni kilele cha furaha na ilihali watu wa motoni wameharamishwa hata chembe ya furaha. Kwa ujumla marejeo ya motoni ni marejeo mabaya kabisa na kila mja mwema hana budi daima aombe:

﴿وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا اصْرِفْ عَنَّا عَذَابَ جَهَنَّمَ إِنَّ عَذَابَهَا كَانَ غَرَامًا ﴿٦٥﴾ إِنَّهَا سَاءَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا﴾

"Mola wetu: Tuondolee adhabu ya Jahannam, bila shaka adhabu yake ni yenye kuendelea. Hakika hiyo (Jahannam) ni kituo kibaya na mahali (pabaya kabisa) pa kukaa (muda mfupi au mrefu). [25:65-66]