15%

20

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

SABABU ZA KUSHINDWA KWA MFUMO WA MKE KUWA NA WAUME WENGI

Sababu kubwa ya kushindwa kwa mfumo huu ni kuwa ulikuwa haufai kwa maumbile ya mwanaume wala ya mwanamke. Haufai kwa maumbile ya mwanaume, kwa sababu, kwanza hauafikiani na asili yake ya kupenda umiliki pekee (yaani awe wake peke yake) na pili kwa sababu haukubaliani na kanuni ya kwamba baba aweze kujiamini juu ya ubaba wake. Ni maumbile ya mwanadamu kuwa na mafungamano maalumu na wanawe. Kila mwanadamu kwa asili anatamani kuzaa watoto na anataka uhusiano na kizazi chake kilichopita na kijacho uwe unaeleweka na wa uhakika. Anataka kujua yeye ni mtoto wa nani na ni baba wa nani. Mfumo wa mke kuwa na waume wengi haukubaliani na silika hii ya mwanadamu. Kwa upande mwingine mfumo wa mume kuwa na wake wengi (mitala) hausababishi matatizo haya, si kwa mwanaume, wala mwanamke.

Imeelezwa kuwa wakati fulani wanawake wapatao arobaini walimwendea Imam Ali(a.s.) na kumuuliza kwa nini Uislamu umewaruhusu wanaume kuoa wake wengi lakini haujaruhusu wanawake kuwa na waume wengi. Wakamuuliza kama huu sio ubaguzi wa wazi. Imam Ali(a.s.) aliagiza viletwe vikombe vya maji na akampa kila mwanamke kikombe kimoja cha maji. Kisha akawaamuru wamwagie maji yote yale katika chombo kimoja kikubwa kilichokuwa katikati yao. Baada ya kutekeleza agizo hilo, Imam Ali(a.s.) aliwaamuru kila mmoja wao achukue maji yale tu yaliyokuwa kwenye kikombe chake. Wanawake wote walisema kuwa hilo lilikuwa haliwezekani kutokana na ukweli kwamba maji yote yalikuwa yamechanganyika.

Imam Ali(a.s.) alisema kuwa:kama mwanamke mmoja angeolewa na wanaume wengi, ni wazi kuwa angeingiliana nao. Akipata mimba na kuzaa, haitafahamika mtoto yule ni wa baba yupi. Kwa upande wa mwanamke, mfumo huu pia hauafikiani na maumbile yake. Mwanamke hamhitaji mume kwa ajili ya kukidhi silika yake ya ngono tu. Ingekuwa hivyo tungesema kuwa 'Wanaume wengi zaidi, raha zaidi'.

Mwanamke anataka mwanamume ambaye yeye mwanamke ataudhibiti moyo wake, atakayekuwa mlinzi na mwangalizi wake, atakayejitoa mhanga kwa ajili ya mkewe na atakayefanya kazi kwa bidii na kumletea fedha. Fedha anazojitafutia mwanamke huwa hazitoshi kukidhi mahitaji yake wala huwa hazina thamani sawa na zile alizopewa na mwanaume anayempenda. Mume hukidhi mahitaji ya kifedha ya mke wake kwa moyo wa kujitolea. Mke na watoto ni hamasa kubwa na bora kabisa kumhamasisha mwanaume kufanya kazi.

Katika mfumo wa mke kuwa na waume wengi mwanamke hawezi akadai na kupata mapenzi ya kweli na kujitolea kutoka kwa yeyote kati ya wanaume hawa. Hii ndiyo sababu, kama ilivyo tu kwa umalaya, huu umekuwa ni mfumo unaochukiza kwa mwanamke. Hivyo mfumo huu wa mke kuwa na waume wengi haukidhi wala kukubaliana na asili na mahitaji ya mwanaume wala mwanamke.

KUSHINDWA KWA UKOMONISTI WA NGONO

Katika mfumo huu si mwanaume wala mwanamke anayeweza kudai au kujinasibisha na mke au mume maalumu kuwa ni wake na hii ndiyo sababu mfumo huu kamwe haukupata kuwa maarufu sehemu yoyote ile. Ilipendekezwa na Plato ambaye aliliruhusu jambo hili kwa tabaka la watawala au 'wanafalsafa watawala.' Lakini pendekezo lake halikuwa kama la wengine na yeye mwenyewe baadaye ilibidi abadilishe maoni yake. Katika karne iliyopita, Frederick Engels, baba wa pili wa ukomunisti alitoa wazo hili na akalitetea kwa nguvu. Lakini halikukubaliwa hata katika ulimwengu wa kikomunisti.

Inasemekana kuwa Urusi ilijaribu kutekeleza nadharia ya familia ya Engels, lakini kufuatia machungu waliyayopata yaliyotokana na mfumo huu walilazimika kuutambua mfumo wa mume mmoja mke mmoja kuwa ndio sera rasmi. Mitala inaweza kuonekana kuwa ni jambo la fahari kwa mwanaume lakini kamwe suala la mke kuwa na waume wengi halijawahi na halitapata kuwa ni jambo la fahari kwa mwanamke. Sababu ni kuwa mwanaume anataka mwili wa mwanamke na mwanamke anataka moyo wa mwanaume. Mwanaume anachojali ni kuumiliki mwili wa mwanamke, haijalishi hata kama haumiliki moyo wake.

Hii ndio sababu mwanaume huwa hajali hata kama mmoja wa wake zake atapunguza upendo kwake, lakini kwa mwanamke, kitu muhimu kabisa ni moyo wa mwanaume na hisia zake za moyoni. Akivipoteza hivyo, huwa amepoteza kila kitu. Kwa maneno mengine, kuna vitu viwili katika maisha ya unyumba, mwili na hisia za moyoni. Mwili unahusiana na ngono, ambayo hamu yake huwa kileleni katika kipindi cha ujana na baadaye hupungua polepole. Hisia za moyoni huhusiana na hisia za upendo, upole na kujitoa. Hisia hizi hukua na kukomaa kwa kadri muda unavyokwenda.

Kwa vile maumbile ya mwanamke ni tofauti na ya mwanaume, mwanamke hujali zaidi hisia za moyoni katika maisha yake ya ndoa. Lakini kwa mwanaume, ama mwili ndio muhimu zaidi au vyote viwili, mwili na hisia za moyoni vina umuhimu sawa. Huko nyuma, tulimnukuu mwanasaikolojia wa kike ambaye ana maoni kuwa mwanamke ana tabia za kipekee za akili. Mtoto hukua katika tumbo lake na kunyonyeshwa na kulelewa katika mapaja yake. Anahitaji sana kujitolea na upendo wa dhati wa mumewe kama baba wa mtoto. Hata kiasi cha upendo kwa wanawe kinategemeana na kiasi cha upendo anachokipata kutoka kwa baba yao.

Ni ndoa ya mume mmoja tu ndiyo inaweza kukidhi mahitaji haya. Ni kosa kubwa sana kulinganisha ndoa ya mke mmoja kuwa na waume wengi na ndoa ya mume mmoja kuwa na wake wengi na kudai kuwa hakuna tofauti yoyote kati ya aina hizi mbili za ndoa. Pia ni makosa kusema kuwa ndoa za mitala zilikuwa mashuhuri katika baadhi ya sehemu za dunia kwa sababu mwanaume ana nguvu zaidi, na kwamba ndoa za mke kuwa na waume wengi zilishindwa kutokana na mke kuwa ni jinsia dhaifu.

Mwandishi wa zama hizi, ambaye ni mwanamke anasema: "Tunaweza kusema kuwa kwa vile mwanaume anaweza kuwa na wake wanne, basi mke pia anapaswa kuwa na haki hiyo kwani wote ni binadamu. Hitimisho hili la kimantiki ni la kuudhi, zaidi kwa wanaume. Wanakasirishwa kusikia hoja hii na wanapiga kelele: 'Inawezekanaje mwanamke akawa na waume zaidi ya mmoja?' Kujibu hilo sisi kwa sauti ndogo tunasema: Inawezakanaje mwanaume akawa na mke zaidi ya mmoja?" Pia anasema: "Hatukusudii kupalilia ufisadi au kupuuzia umuhimu wa maisha ya usafi wa kimaadili. Tunataka tu wanaume waelewe kuwa maoni yao juu ya wanawake hayakujengwa juu ya hoja za maana.

Mwanaume na mwanamke ni sawa kama wanaadamu. Kama mwanaume ana haki ya kuwa na wake wanne, basi mwanamke pia lazima awe na haki kama hiyo. Hata kama tukichukulia kwamba mwanamke kiakili sio bora kuliko mwanaume, lakini ni hakika kwamba kiroho mwanamke sio dhaifu kuliko mwanaume." Kama ambavyo utakuwa umebaini kauli hiyo haioneshi tofauti yeyote kati ya mitala na ndoa za mke kuwa na waume wengi, isipokuwa kwamba kwa kuwa mwanaume ni wa jinsia yenye nguvu zaidi basi amechukuwa mfumo wa mitala kwa manufaa yake, na mwanamke kwa kuwa ni wa jinsia dhaifu hakuweza kuutumia utaratibu huo.

Mwandishi huyo pia anasema kuwa mwanaume anamuona mwanamke kuwa ni mali yake, na ndio maana anataka kuwa na wake wengi. Kwa maneno mengine ni kuwa mwanaume anataka kujikusanyia mali nyingi kwa kadri inavyowezekana. Kwa vile mwanamke yupo katika nafasi ya mtumwa, hawezi kuwa anamilikiwa na bwana zaidi ya mmoja.

Kinyume na maoni ya mwandishi huyu, ukweli kwamba mfumo wa mke kuwa na waume wengi haujawahi kukubaliwa na idadi yoyote kubwa ya watu popote pale duniani unathibitisha kuwa mwanaume hamchukulii mke wake kuwa ni mali yake, kwani katika mali, ni mashuhuri duniani kote kuwa mali humilikiwa kwa ubia na wamiliki wote hunufaika na mali hiyo kwa ubia. Kama mwanaume angekuwa anamchukulia mwanamke kuwa ni mali, ni wazi kuwa asingekuwa na pingamiza katika kuichangia na wengine.

Hakuna sheria duniani inayolazimisha kuwa mali imilikiwe na mtu mmoja tu. Inasemwa kwamba mume ni mtu mmoja na mke ni mtu mmoja. Wanapaswa kuwa na haki sawa. Kwa nini mume awe na haki ya kufurahia mitala na mke anyimwe haki hiyo ya kuwa na waume wengi? Tunasema kuwa hapa ndio kuna makosa. Unadhania kwamba mitala ni sehemu ya haki za mume, na mke kuwa na waume wengi ni sehemu ya haki za mke. Ukweli ni kwamba mitala ni sehemu ya haki za mwanamke, na ndoa ya mke kuwa na waume wengi sio sehemu ya haki za mwanaume wala mwanamke. Ni mfumo usio na faida kwa wote wawili, mwanamke na mwanaume.

Tutathibitisha baadaye kuwa mfumo wa mitala umewekwa na Uislamu kwa nia ya kulinda maslahi ya mwanamke. Kama nia ingekuwa kumpendelea mwanaume, Uislamu ungemruhusu mwanaume kufanya mapenzi na mwanamke mwingine mbali na mke wake na usingeweka uwajibikaji juu yake kuhusiana na mke wake wa halali na watoto wake wa halali. Mfumo wa mke kuwa na waume wengi kamwe haujapata kuwa na maslahi yoyote kwa mwanamke. Sio haki aliyonyimwa.

Mwandishi ambaye tumenukuu maoni yake anasema: "Tunataka wanaume waelewe kuwa maoni yao juu ya wanawake hayajajengwa juu ya hoja ya maana." Kwa bahati sisi pia hicho ndicho tunachokusudia kukifanya. Katika sura zinazofuata tutaeleza msingi wa mtazamo wa Uislamu juu ya mitala. Tunawaalika watu wote wanaofikiri kuutazama na kuona kama mtazamo wa Uislamu umejengwa au haukujengwa juu ya hoja zozote za maana. Tunaahidi kuwa tutayabatilisha yale yote, tuliyoyasema ikiwa mtu yeyote atathibitisha kuwa msingi wa mtazamo wa Uislamu ni mbovu.