23
Tumeshaelezea sababu za kushindwa kwa ndoa za mke mmoja kuwa na waume wengi na kufanikiwa kwa mitala na tumeelezea sababu mbalimbali zilizosababisha kuibuka kwa mitala. Baadhi ya sababu zilitokana na moyo wa ukandamizaji na ubabe wa mwanaume na nyingine zilitokana na kutofautiana kwa mwanamke na mwanaume kuhusiana na kudumu kwa uwezo wao wa kuzaa na idadi ya watoto ambayo kila mmoja wao anaweza kuzaa. Hizi sababu za pili zinaweza kuchukuliwa kuwa ni sababu thabiti za mitala. Lakini sababu yake kuu katika kipindi chote cha historia imekuwa ni idadi ya wanawake inayozidi ya wanaume wanaofaa kuolewa na kuoa sawia.
Sababu hii husababisha kuzaliwa kwa haki ya mwanamke na jukumu la mwanaume. Ili kuepuka mjadala mrefu, tunaziruka sababu hizi ambazo zinaweza kuchukuliwa kuwa ni uhalalishaji tu wa mitala, na kushughulikia tu sababu yake kubwa, ambayo kama ikiwepo hubadilika kuwa haki ya jinsia dhaifu. Ili kuthibitisha hili, nukta mbili za utangulizi zinapaswa kuwekwa sawa. Kwanza ni kuthibitisha kuwa kwa mujibu wa takwimu za kuaminika, idadi ya wanawake wanaopwaswa kuolewa ni kubwa kuliko idadi ya wanaume wanaofaa kuoa. Nukta ya pili tunayotaka kuithibitisha ni kuwepo kwa mazingira halisi yanayounda wajibu kwa wanaume waliooa na wanawake walioolewa juu ya wanawake walionyimwa haki ya kuwa na ndoa.
Kuhusiana na nukta ya kwanza, kwa bahati nzuri takwimu zote thabiti zipo duniani. Sensa huchukuliwa katika kila nchi katika kila baada ya muda fulani. Katika nchi zilizoendelea, sio tu kwamba idadi wa wanaume na wanawake hukusanywa bali pia idadi ya wanaume na wanawake katika umri mbalimbali huonyeshwa. Takwimu hizi huchapishwa na Umoja wa Mataifa katika ripoti zake za kila mwaka juu ya idadi ya watu.* Inaweza kuonyeshwa kwamba kwa madhumuni yetu, haitoshelezi kujua idadi ya wanaume na wanawake katika kila nchi, tunahitaji pia kujua uwiano wa idadi ya wanaume na wanawake wanaofaa kuoa na kuolewa sawia.
Mara nyingi uwiano huu unatofautiana na uwiano wa jumla wa wanaume na wanawake. Kuna sababu mbili za tofauti hii. Moja ni kuwa wanawake hupevuka mapema zaidi. Hii ndio sababu katika nchi zilizo nyingi umri unaoruhusiwa wasichana kuolewa upo chini kuliko umri wa wavulana wanaoruhusiwa kuoa. Kwa wastani, umri wa mume huwa ni miaka mitano zaidi kuliko mkewe.
Sababu nyingine na muhimu zaidi ni kuwa idadi ya vifo vya wavulana ni kubwa kuliko wasichana, na matokeo yake ni kuwa katika umri wao wa ndoa, wasichana huwa ni wengi kuliko wavulana. Wakati fulani tofauti huwa kubwa. Inaweza kutokea kuwa idadi ya wanaume na wanawake katika nchi inalingana au hata wanaume wakawa wengi kuliko wanawake, lakini bado idadi ya wasichana wanaofaa kuolewa ikawa kubwa kuliko idadi ya wavulana wanaoweza kuoa, tena kwa idadi kubwa.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Uwingi wa watu kwa mwaka 1964, inashuhudia ukweli huu. Kwa mfano, kwa mujibu wa ripoti hii, jumla ya watu katika Jamhuri ya Korea ni 26,277,635. Kati ya hawa wanaume ni 13,145,289 na 13,132,326 ni wanawake. Hivyo idadi ya wanaume ni zaidi ya wanawake kwa 12,943. Uwiano huu unabaki hivi katika umri wa miaka 1-4, 5-9, 12-14 na 15-19.
* Tunayo mbele yetu ripoti ya 1964, iliyochapishwa tena 1965. Takwimu zinaonyesha kuwa katika makundi yote haya ya umri idadi ya wanaume ni kubwa kuliko ya wanawake. Lakini katika kundi la umri la miaka,20-24, uwiano unabadilika. Katika kundi hili la umri idadi ya wanaume ni 1,083,364, na idadi ya wanawake ni 1,110,051. Katika makundi yote ya umri wa juu, ambayo ni makundi ya wanayoweza kuoa na kuolewa idadi ya wanawake ni kubwa zaidi. Hata hivyo, Jamhuri ya Korea ni mfano wa pekee ambapo idadi ya wanaume ni kubwa kuliko idadi ya wanawake. Takribani, katika nchi nyingine zote, sio tu kwamba idadi ya wanawake wanaofaa kuolewa ni kubwa kuliko ya wanaume, bali hata katika idadi ya jumla, wanawake ni wengi kuliiko wanaume.
Kwa mfano idadi ya watu nchini Urusi ni 216,101,000 na wanawake ni 118,261,000, na tofauti hii inaendelea katika makundi yote ya umri, yale ambayo hayajafikia umri wa kuingia katika ndoa na yale yaliyofikia umri huo, hii ni kuanzia 20-24, 25-29, 30-34 na hata 80-84. Hali iko hivi hivi katika nchi nyingine pia kama vile Uingereza, Ufaransa, Ujerumani ya Magharibi, Ujerumani wa Mashariki, Czechoslavakia, Poland, Romania, Hungary, Marekani, Japan n.k. Katika baadhi ya sehemu kama vile Berlin Magharibi na Berlin Mashariki, tofauti ya idadi kati ya wanaume na wanawake ni kubwa mno. Nchini India, katika makundi ya umri ambapo watu wanaweza kuingia katika ndoa, idadi ya wanaume ni kubwa kuliko ya wanawake. Idadi ya wanawake ni kubwa tu kuanzia katika umri wa miaka 50 na kuendelea. Inavyoonekana uchache wa wanawake unatokana na ukweli kwamba watu wengi nchini India hawapendi kutaja majina ya wake zao vijana au binti zao wadogo, wakati wa sensa. Kwa mujibu wa takwimu za sensa iliyopita, Iran ni moja ya nchi ya pekee ambapo, idadi ya wanawake inaizidi ile ya wanaume.
Inashangaza kwamba baadhi ya wakosoaji wanasisitiza kuwa sheria inayoruhusu mitala ipigwe marufuku angalau katika nchi ambazo idadi ya wanaume ni kubwa kuliko ya wanawake. Katika hatua ya kwanza, sheria hii ni ya wote, sio ya nchi maalumu. Pili, haitoshi kujua uwiano wa wanaume na wanawake peke yake. Tumeona kuwa katika Jamhuri ya Korea, idadi ya wanaume ni kubwa kuliko ya wanawake, lakini idadi ya wanawake wanaofaa kuolewa ikawa kubwa kuliko idadi ya wanaume wanofaa kuoa. Aidha, takwimu za sensa, sio za kuaminika sana katika nchi zilizo nyingi.
Kwa mfano, tunajua kuwa ingawa mitala ni mila iliyozoeleka nchini Iran, mijini na vijijini, lakini haijawahi kutokea upungufu wa mabibi harusi watarajiwa. Ukweli huu peke yake unaongea vizuri zaidi kuliko takwimu za sensa. Ashley Montaque, katika kitabu chake, "Woman - The Superior Sex", anakiri kwamba duniani kote, idadi ya wanawake wanaofaa kuolewa ni kubwa kuliko ile ya wanaume wanaofaa kuoa.
Takwimu za mwaka 1950, zinaonyesha kuwa idadi ya wanawake waliofikia umri wa kuolewa nchini Marekani inaizidi ile ya wanume takriban kwa 1,430,000. Bertrand Russel katika kitabu chake, "Marriage and Morality", anasema kwamba katika Uingereza ya leo, wanawake wanazidi idadi ya wanaume kwa zaidi ya milioni mbili. Kwa mujibu wa mila yao, wanapaswa wabakie bila kupata watoto, jambo ambalo ni dhulma kubwa kwa upande wao.
Miaka kadhaa iliyopita, ilitangazwa kwenye vyombo vya habari kwamba, kufuatia shinikizo kubwa la wanawake wa Kijerumani ambao hawakuweza kupata waume na maisha ya kifamilia, kufuatia vifo vingi vya wanaume katika vita vya Pili vya Dunia, serikali ya Ujerumani imekiomba chuo kikuu cha Al-Azhar kiipatie mwongozo wa mitala. Baadaye ilifahamika kuwa kufuatia upinzani mkali wa kanisa, pendekezo hilo ilibidi liachwe. Kanisa liliona bora wanawake wakae bila kuolewa wala kuzaa wala kuishi maisha ya kifamilia, na ni bora uzinifu na ufuska kuliko kuukubali mfumo wa wanaume kuoa mke zaidi ya mmoja. Kwa vile tu mfumo huu ni wa Mashariki na wa Kiislamu.