SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S)

FATIMA (A.S) KWA MUHTASARI.

Hakika Mwenyeezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba (ya Mtume), na anataka kukutakaseni sana sana.{33:33)

Mwenyeezi Mungu (s.w) amewataja Ahlul-bayt (a.s) kwa kuwakirimu na kuwanyanyua hadi katika daraja ya juu kabisa,kisha Mtume (s.a.w) akamchukua Fatima,kisha Ali,kisha Hassan,kisha Husein (a.s) akasema:

"Hawa ni Ahlul-bayt wangu". Fatima (a.s) alikuwa ni bint mdogo sana kati ya mabinti wa Mtume (s.a.w) na anayependwa zaidi na Mtume (s.a.w) kuliko yeyote yule kati yao.Na alikuwa ni mbora wa wanawake wote wa ulimwenguni,na Mtume (s.a.w) amezungumza kuhusiana na Fatima (a.s) kwa kusema:

{{Hakika Fatima ni sehemu ya nyama yangu, kinanitia wasi wasi (shaka) kinachomtia wasi wasi (au shaka), na kinaniudhi kinachomuudhi}} Na hili ni moja kati ya yale mambo yanayoonyesha utukufu wa Sayyidat Fatima (a.s) na daraja yake ya juu kabisa.Ama wema wake,ubora wake,mazuri yake na Fadhila zake ni nyingi sana na kubwa,na Baba yake s.a.w) amemwambia kwa kusema: "Hakika ya Mwenyeezi Mungu huridhia unaporidhia,na hughadhibika unapoghadhibika".