7
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NANE
هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن تَأْتِيَهُمُ الْمَلَائِكَةُ أَوْ يَأْتِيَ رَبُّكَ أَوْ يَأْتِيَ بَعْضُ آيَاتِ رَبِّكَ ۗ يَوْمَ يَأْتِي بَعْضُ آيَاتِ رَبِّكَ لَا يَنفَعُ نَفْسًا إِيمَانُهَا لَمْ تَكُنْ آمَنَتْ مِن قَبْلُ أَوْ كَسَبَتْ فِي إِيمَانِهَا خَيْرًا ۗ قُلِ انتَظِرُوا إِنَّا مُنتَظِرُونَ ﴿١٥٨﴾
158.Je, wananogoja jingine ila wawafikie Malaika au afike Mola wako au ziwafikie baadhi ya ishara za Mola wako? Siku zitakapofika baadhi ya ishara za Mola wako, basi mtu haitamfaa imani yake ambaye hakuamini zamani, au hakuchuma kheri kwa imani yake.Sema: Ngojeni , sisi pia tunangoja.
إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا لَّسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ ۚ إِنَّمَا أَمْرُهُمْ إِلَى اللَّـهِ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ ﴿١٥٩﴾
159.Hakika wale walioigawa dini yao na wakawa makundi makundi, huna uhusiano nao wowote. Hakika shauri lao liko kwa Mwenyezi Mungu tu. Kisha atawaambia yale waliyokuwa wakiyafanya.
مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿١٦٠﴾
160.Mwenye kufanya vizuri atalipwa mfano wake mara kumi. Na mwenye kufanya vibaya hatalipwa ila sawa na hivyo tu, Nao hawatadhulumiwa.
Aya 158 – 160
Je, wananogoja jingine ila wawafikie Malaika au afike Mola wako au ziwafikie baadhi ya ishara za Mola wako?
Swali hapo si la kuuliza bali ni la kukanusha. Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja kwamba washirikina wamekana dalili za Qur’an, wakakataa kuzingatia maana yake, sasa anasema katika Aya hii kuwa wao hawataamini isipokuwa mambo matatu: Kuja Malaika, kuja Mola na kuja baadhi ya ishara. Hata hivyo Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakubainisha Malaika ambaye anapasa kuwajia ili waamini.
Je, ni Malaika wa mauti au mwingine? Wala pia hakubainisha makusudio ya kuja Mola, Je, ni kuja kwake kwa madai yao au ni kuja amri yake, kama ilivyotokea? Vilevile hakubainisha baadhi ya ishara, Je, ni ishara walizozitaka au ni alama za Kiyama?
Wafasiri wengi wamesema kuwa makusudio ya Malaika ni Malaika wa mauti. Na makusudio ya kuja Mola ni kuja adhabu na mateso yake. Na baadhi ya ishara, ni ishara za Kiyama.
Tafsir hii ndiyo iliyo karibu zaidi na maana. Kwa sababu, maneno yanayofuatia yanataja mambo haya matatu yakitambulisha kauli ya wafasiri na kuitilia nguvu; nayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
Siku zitakapofika baadhi ya ishara za Mola wako, basi mtu haitamfaa imani yake ambaye hakuamini zamani, au hakuchuma kheri kwa imani yake.
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba toba na imani wakati wa kuja mojawapo ya mambo haya matatu, haifai kitu; isipokuwa inayofaa ni imani na amali njema anayoichuma mumin kabla ya kutokea hayo. Kwani wakati wa kutolewa roho, au ishara za Kiyama au wakati wa kushuka adhabu huwa hakuna taklifa yoyote. Ikiwa hivyo, basi kuweko imani na kutokuweko ni sawa tu.
Kauli yake Mwenyezi Mungu: Au kuchuma kheri kwa imani yake, inaishiria kuwa kumwamini Mungu kunamwokoa mtu na kukaa milele tu motoni, lakini hakumwokoi na adhabu ya moto. Ama anayemwamini Mwenyezi Mungu na akafanya amali njema, basi hataguswa na moto.
Sema: Ngojeni haya mambo matatu,sisi pia tunangoja.
﴿ فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ مَن يَأْتِيهِ عَذَابٌ يُخْزِيهِ﴾
“Punde tu mtajua ni nani itakayemjia adhabu ya kufedhehesha” (11:39).
Hakika wale walioigawa dini yao na wakawa makundi makundi, huna uhusiano nao wowote.
Hapa anaambiwa Mtume(s.a.w.w)
Kama ambavyo walihitalifiana wale walioigawa dini yao na wakawa makundi makundi, vilevile wafasiri nao wamekuwa makundi makundi katika kufasiri makusudio ya ‘walioigawa dini yao.’ Baadhi wamesema kuwa hao ni washirikina kwa kuwa baadhi yao wanaabudu masanamu, wengine nyota na baadhi yao mwanga na giza. Wafasiri wengine wamesema kuwa ni watu wa Kitab.
Kwani Mayahudi waligawanyika makundi ya Masadukayo, Mafarisayo na Mahaasid[1] Ama Wakristo wao waligawanya kanisa la Mashariki na la Magharibi.
Pia imesemekana kuwa ni makundi ya Kiislamu. Na ikasemekana kuwa ni wote wenye mila na vikundi.
Maelezo bora niliyosoma kuhusu tafsir ya Aya hii ni yale aliyosema mwenye tafsir Al-Manar: “Makusudio ya wale walioigawa dini yao wakawa vikundi ni watu wa Kitab. Na makusudio ya kujitenga nao Mtume ni kuhadharishwa Waislamu wasigawanye dini yao wakawa na vikundi kama watu wa Kitab, ili wajue kwamba wao wakifanya vitendo vya watu wa Kitab, basi Muhammad(s.a.w.w) atakuwa mbali nao.”
Hakika shauri lao liko kwa Mwenyezi Mungu tu.
Yeye peke yake ndiye anayemiliki hisabu na adhabu ya mwenye kufarikisha waja wake na kuleta uadui na chuki katika dini na penginepo.
Kisha atawaambia yale waliyokuwa wakiyafanya. Kuanzia wale watakaokubali mpaka wale wanaochochea:
﴿وَقَالَتْ أُولَاهُمْ لِأُخْرَاهُمْ فَمَا كَانَ لَكُمْ عَلَيْنَا مِنْ فَضْلٍ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنْتُمْ تَكْسِبُونَ﴾
“Na wa mwanzo wao watawaambia wa mwisho wao; basi nyinyi pia hamkuwa na ubora kuliko sisi. Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyachuma.” (7:39)
Mwenye kufanya vizuri atalipwa mfano wake mara kumi. Na mwenye kufanya vibaya hatalipwa ila sawa na hivyo tu, Nao hawatadhulumiwa.
Kila lililo na radhi ya Mwenyezi Mungu na manufaa kwa watu basi ni zuri; na kila lenye machukivu ya Mwenyezi Mungu na ufisadi kwa watu basi ni baya.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni mwadilifu, mkarimu. Miongoni mwa uadilifu wake ni kumlipa mwenye kufanya uovu, adhabu inayolingana nao. Na miongoni mwa ukarimu wake ni kusamehe, na kumwongozea mtenda mema ziada inayofikia kumi, au mia saba, au isiyo na idadi kulingana na lengo la mtenda mema, sifa zake na hali yake. Angalia Juz 2. (2:261).
Kuna Hadith ya Mtume(s.a.w.w) isemayo: “Hakika Mwenyezi Mungu amesema: “Wema malipo yake ni kumi au zaidi, na uovu ni moja au kusamehewa. Basi ole wake yule ambaye kumi yake imeshindwa na moja yake”.
Anaendelea kusema Mtume: “Mwenyezi Mungu anasema: ‘Mja wangu akikusudia wema mwandikieni jema moja hata kama hatafanya; na akifanya basi mwandikieni kumi mfano wake, Kama atakusudia uovu, msimwandikie kitu; kama ataufanya basi mwandikieni moja.”
قُلْ إِنَّنِي هَدَانِي رَبِّي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ دِينًا قِيَمًا مِّلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۚ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١٦١﴾
161.Sema: Kwa hakika mimi Mola wangu ameniongoza katika njia iliyonyooka, dini yenye msimamo ndiyo mila ya Ibrahim mnyoofu, Wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾
162.Sema: Hakika Swala yangu na ibada zangu na uhai wangu na mauti yangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu.
لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ ﴿١٦٣﴾
163.Hana mshirika. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu.
قُلْ أَغَيْرَ اللَّـهِ أَبْغِي رَبًّا وَهُوَ رَبُّ كُلِّ شَيْءٍ ۚ وَلَا تَكْسِبُ كُلُّ نَفْسٍ إِلَّا عَلَيْهَا ۚ وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۚ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُم مَّرْجِعُكُمْ فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ ﴿١٦٤﴾
164.Sema: Je, nimtafute Mola mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu? Na hali yeye ni Mola wa kila kitu? Na kila nafsi haichumii ila (inajichumia) yenyewe. Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu, naye atawaambia yale mliyokuwa mkihitalifiana.
وَهُوَ الَّذِي جَعَلَكُمْ خَلَائِفَ الْأَرْضِ وَرَفَعَ بَعْضَكُمْ فَوْقَ بَعْضٍ دَرَجَاتٍ لِّيَبْلُوَكُمْ فِي مَا آتَاكُمْ ۗ إِنَّ رَبَّكَ سَرِيعُ الْعِقَابِ وَإِنَّهُ لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٦٥﴾
165.Naye ndiye aliyewafanya makhalifa wa ardhi na akawainua baadhi yenu juu ya wengine ili awajaribu katika aliyowapa. Hakika Mola wako ni mwepesi wa kuadhibu. Na hakika yeye ni mwingi wa maghufira, mwenye huruma.
Aya 161 – 165
Sema: Kwa hakika mimi Mola wangu ameniongoza katika njia iliyonyooka.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwataja wale walioigawanya dini yao wakawa vikundi, alimwamrisha Mtume wake kuwatangazia washirikina, watu wa Kitab na wengineo kuwa Mwenyezi Mungu amemwongoza Mtume kwa umbile safi, akili kamili na kwa wahyi utokao kwake, kwenye njia inayomweka mbali na batili na kumfikisha kwenyedini yenye msimamo ndiyo mila ya Ibrahim mnyoofu.
Yaani njia ambayo Mwenyezi Mungu amemuongoza nayo Mtume wake Muhammad ndiyo dini ya Nabii Ibrahim(a.s) kipenzi cha Mwenyezi Mungu ambayo wanaitukuza watu wa dini zote.
Wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
Bali ni katika maadui wakubwa wa ushirikina na watu wake. Hili ni jibu la Washirikina wa Kiquraish ambao wanadai kwamba wao wako kwenye dini ya Nabii Ibrahim(a.s) .
Sema: Hakika Swala yangu na ibada zangu na uhai wangu na mauti yangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu.
Maudhui ya Aya iliyotangulia ni misingi ya dini na itikadi kwa kulinganisha na neno: ‘Wala hakuwa miongoni mwa washirikina’ na maudhui ya Aya hii ni matawi ya dini na sharia, kwa kulinganisha Swala na ibada.
Kuunganisha ibada kwenye Swala ni katika hali ya kuunganisha ujumla kwenye mahsusi; kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿وَمَا أُوتِيَ مُوسَىٰ وَعِيسَىٰ وَالنَّبِيُّونَ مِنْ رَبِّهِمْ﴾
“Na waliyopewa Musa na Isa na Mitume kutoka kwa Mola wao” (3:84)
Uhai na mauti hapa ni fumbo la uthabiti na kuendelea. Maana ni kuwa ibada za Muhammad(s.a.w.w) na maisha yake yote ya kiitikadi, nia na amali, yanaekelea kwa Mwenyezi Mungu peke yake wala hakengeuki nayo mpaka kufa.
Hana mshirika, Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu.
Aya hii ni ufafanuzi na usisitizo wa yaliyo katika Aya iliyotangulia – Tawhid na ikhlasi. Na Muhaammad ni Mwislamu wa kwanza katika umma wake kwa sababu yeye ndiye mwenye wito huo.
Sema: Je, nimtafute Mola mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu?
﴿فَأَيْنَمَا تُوَلُّوا فَثَمَّ وَجْهُ اللَّهِ﴾
Atakayemtafuta Mola huyo atampata wapi, na hali: “Mahala popote mnakoelekea ndiko kwenye uelekeo wa Mwenyezi Mungu? ”Juz. 1 (2:115)
Na hali yeye ni Mola wa kila kitu?
Na Mola wa kila kitu ni mmoja tu, hana wa kinyume chake.
Na kila nafsi haichumii ila (inajichumia) yenyewe.
Kila alifanyalo mtu liwe kheri au shari basi ni mazao ya silika yake na hali yake kwa ujumla. Anayenasibisha matendo ya mtu kwa mwingine, ni sawa na anayemnasibisha mtoto kwa asiyekuwa mama yake, na matunda kwa usiokuwa mti wake.
Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine.
Makusudio ya mzigo hapa ni dhambi. Jumla hii inatilia mkazo jumla iliyo kabla yake, na maana yake ni kwamba:
﴿ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ ﴾
“Faida ya yale iliyoyachuma ni yake na hasara iliyochuma ni yake.” Juz. 2 (2:286).
Sio yaliyochumwa na nafsi nyingine.
Hii ndiyo asili ya kidini na kiakili; haiwezekani kuifuta au kuigeuza. Maulama wa lugha na fasaha wametoa masuala mengi na hukumu kwenye asili hii.
Utauliza : Aya hii inaonyesha kuwa kila mtu na lake tu, sasa uko wapi wajibu wa Jihadi, kutoa nasaha na kusaidiana katika wema na takua.
Jibu : Maadhui ya Aya hii yanahusiana na adhabu tu, na kwamba mtu hataadhibiwa kwa kosa la mwingine; wala haina uhusiano wowote na jihadi na nasaha na mengineyo, kwa umbali au karibu. Kwa sababu kuadhibiwa kwa kosa la mwingine ni jambo mbali na wajibu wa jihadi na kurekebisha ufisadi ni jambo jengine.
Swali la pili : watu wamezoea kutoa sadaka ya mali na chakula kwa ajili ya roho za maiti wao; wakasoma Qur’an na kuwapelekea thawabu; je, hii inajuzu kisharia? Na je, maiti wananufaika nayo, Kama ni hivyo, itakuwaje na ilivyo ni kuwa wafu hawaadhibiwi kwa maovu ya walio hai, basi iwe pia wasineemeke na mema yao?
Jibu : Tumesema kuwa akili na sharia inakataa kuadhibiwa mtu kwa kosa la mtu mwingine na kushirikishwa kwenye kosa hilo. Kuhusu thawabu, katika mtazamo wa akili, hakuna kizuizi kwa aliyefanya wema kumshirikisha asiyefanya wema ule katika thawabu anazostahiki kwa amali yake.
Na sharia imelieleza hilo, hivyo imepasa kulisadiki. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anasema: “Mwanadamu akifa, hukatika amali yake isipokuwa mambo matatu: Sadaka inayoendelea, au elimu inayopatiwa manufaa, au mtoto mwema atakayemwombea, dua?” Akaendelea kusema: “Atakayekufa na ana saumu anayodaiwa basi na amfungie walii wake”.
Akasema tena: “Mwenye kuingia makaburini akasoma Sura ya Yasin huwahafifishia waliozikwa hapo siku hiyo. Na anapata wema kwa idadi ya waliomo makaburi.” Imam Jafar As-sadiq(a.s) naye anasema: “Ni jambo gani linalomzuia mtu kuwafanyia wema wazazi wake mara kwa mara?”
Kwa hiyo Hadith hizi na nyinginezo zinafahamisha kwamba maiti ananufaika kwa kupelekewa thawabu kwa amali ya kheri. Na akili hailikatai hilo kabisa. Kwa sababu hilo linaafikiana na fadhila za Mwenyezi Mungu na ukarimu wake.
Lakini watu wamezidisha mno na kupetuka mipaka ya ilivyoelezwa. Na mafakihi wameafikiana kuwa kila mwenye kufanya ambalo halikuelezewa kwa makusudio ya kuwa linatiliwa mkazo na sharia basi amefanya uzushi (bid’a) katika dini na amemzulia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kwa hiyo ni bora ampelekee thawabu maiti kwa kutarajia anufaike nazo, bila ya kukusudia kuwa hilo llimependekezwa na dini na sharia.
Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu, naye atawaambia yale mliyokuwa mkihitalifiana.
Bila ya kutegemea akili au Wahyi; mkakubali yale mliyoyazoea na sio haki, na mkayakana yale yanayochukiwa na mapenzi yenu na matamanio yenu.
Naye ndiye aliyewafanya makhalifa wa ardhi na akawainua baadhi yenu juu ya wengine ili awajaribu katika aliyowapa.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameiumba ardhi hii akaifanya ni mahali pema panapofaa kwa maisha ya binadamu kutokana na mazingira yake, mpangilio wake, umbo lake na kuwa mbali kwake na jua na mwezi. Akaiandalia yote anayoyahitaji mtu mpaka nyenzo za kujipumbaza na kujistarehesha; sawa na nyumba iliyokamilika kila kitu. Kisha akamweka mtu, ndani ya hiyo ardhi baada ya kumwandalia nyenzo zote za kunufaika na kheri zake na baraka zake.
Na hekima yake ikataka watu watofautiane katika nyenzo hizo na kwamba baadhi yao wawe zaidi ya wengine katika akili, elimu na nguvu za mwili. Na akawawekea njia iliyo sawasawa ili awajaribu wenye nguvu kuwa je wataishukuru neema hii na kuzielekeza nguvu zao kwenye masilahi yao na maslahi ya ndugu zao wanaadamu; au watazifanya ni nyezo za kudhulumu, kunyang’anya, kujiadhimisha na kujifaharisha?
Aya hii imefahamisha kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemleta mtu katika ardhi hii kwa ajili ya elimu na matendo yenye kunufaisha.
Utauliza : Utaiunganishaje Aya hii na Aya isemayo:
﴿ وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنْسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ﴾
“Na sikuumba majini na watu ila waniabudu?.” (51:56)
Jibu : Hazipingani Aya hizi mbili. Kwa sababu elimu na kazi yenye kunufaisha ni ibada ya Mwenyezi Mungu, bali ni katika ibada bora, na twaa iliyo kamili.
Hakika Mola wako ni mwepesi wa kuadhibu.
Anawajaribu waja wake ili ampambanue mwovu na mwema, amwadhibu huyu na kumpa thawabu yule.
Na hakika yeye ni mwingi wa maghufira, mwenye huruma.
Huruma yake haina mpaka, wala msamaha wake hauna kifungu chochote, Ndio! Toba inajaalia msamaha ndio malipo yake yenye kulingana na unabaki msamaha wa ukarimu na kutoa kwa aombaye, hana wa kumlazimisha, isipokuwa yeye mwenyewe mtukufu. Hii ndiyo dalili ya kauli yake:
﴿ وَمَا أَصَابَكُمْ مِنْ مُصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَنْ كَثِيرٍ ﴾
“Na masaibu yanayowasibu ni kwa sababu ya yaliyochumwa na mikono yenu; na Mwenyezi Mungu husamehe mengi.” (42:30).
Yaani mengi yaliyochumwa na mikono yetu.
Mola! tuokoe na yanayotokana na sisi wenyewe na tunakuomba utusamehe mizigo yetu wenyewe!