11%

10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NANE

وَإِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً قَالُوا وَجَدْنَا عَلَيْهَا آبَاءَنَا وَاللَّـهُ أَمَرَنَا بِهَا قُلْ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَأْمُرُ بِالْفَحْشَاءِ أَتَقُولُونَ عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢٨﴾

28. Na wanapofanya machafu husema: Tumewakuta nayo baba zetu na Mwenyezi Mungu ametuamrisha hayo. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi machafu Je, mnasema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua?

قُلْ أَمَرَ رَبِّي بِالْقِسْطِ وَأَقِيمُوا وُجُوهَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ وَادْعُوهُ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ كَمَا بَدَأَكُمْ تَعُودُونَ ﴿٢٩﴾

29. Sema: Mola wangu ameamrisha uadilifu. Na elekezeni nyuso zenu katika kila msikiti, na muombeni yeye tu kwa ikhlas kama alivyowaumba kwanza ndivyo mtarudi.

فَرِيقًا هَدَىٰ وَفَرِيقًا حَقَّ عَلَيْهِمُ الضَّلَالَةُ إِنَّهُمُ اتَّخَذُوا الشَّيَاطِينَ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَيَحْسَبُونَ أَنَّهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٣٠﴾

30. Kundi moja ameliongoa. Na kundi jingine limethibitikiwa na upotofu, Hakika wao wamefanya mashetani kuwa watawala wao badala ya Mwenyezi Mungu, Na wanadhani kwamba wao wameongoka.

WANAPOFANYA UCHAFU

Aya 28-30

MAANA

Na wanapofanya machafu.

Dhamir inawarudia wale ambao hawaamini, waliotajwa mwisho wa Aya iliyotangulia. Kundi la wafasiri wamesema kuwa makusudio ya uchafu ni walivyokuwa wakifanya Waarabu wakati wa ujahilia kutufu Al-Kaaba wakiwa uchi, wake kwa waume. Lakini ilivyo hasa ni kuwa neno hilo linaenea yote ya haramu waliyokuwa wakifanya.

Wanapokatazwa husema:

Tumewakuta nayo baba zetu na Mwenyezi Mungu ametuamrisha hayo.

Kitendo cha mababa kimekuwa ni hoja ya washirikina na wengineo; hata kwa maulamaa wengi wa kidini, lakini hawatambui. Ama madai ya washirikina kuwa Mwenyezi Mungu amewaamrisha machafu yameetole- wa dalili na Aya isemayo:

“Watasema walioshirikisha: Lau angelitaka Mwenyezi Mungu tusingelimshirikisha sisi wala baba zetu;” Mwenyezi Mungu akawarudi kwa kuwaaambia:

قُلْ هَلْ عِندَكُم مِّنْ عِلْمٍ فَتُخْرِجُوهُ لَنَا إِن تَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ أَنتُمْ إِلَّا تَخْرُصُونَ ﴿١٤٨﴾

“Je, mnayo elimu mtutolee? Nyinyi hamfuati ila dhana tu, na hamsemi ila uwongo tu.” (6:148).

Na hapa Mwenyezi Mungu akawarudi kwa kusema: Sema:

Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi machafu.

Bali “Shetani anawatisha na ufukara na anawaamrisha ubakhili”Juz.3 (2:257)

Je, mnasema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua?

Na kila anayesema, bila ya ujuzi wowote, basi ni mzushi mwongo, na ameruka patupu.

Sema: Mola wangu ameamrisha uadilifu.

Nao ni usawa na msimamo. Amesema Tabrasi: “Uadilifu ni neno linaloku- sanya kheri zote.” Maana yoyote yatakayokuwa ni kuwa kuamrisha uadilifu ni kupinga madai yao kuwa Mwenyezi Mungu amewaamrisha uovu.

Na elekezeni nyuso zenu katika kila msikiti, na muombeni yeye tu kwa ikhlas.

Makusudio ya elekezeni nyuso zenu ni kumwabudu Mwenyezi Mungu. Neno ‘Masjid’ ni mahali pa kusujudia na pia wakati wa kusujudu.

Lakini limetumika sana kwa maana ya jengo maalum la ibada (msikiti) mpaka likawa ni jina lake mahsusi. Makusudio ya kila msikiti sio misikiti yote bali ni msikiti wowote.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu anawaamrisha kufanya ibada kwenye msikiti, kwa kumwabudu yeye tu kwa ikhlas katika dini yenu na ibada yenu.

Kama alivyowaumba kwanza ndivyo mtarudi kwake siku ya Kiyama kwa ajili ya hisabu na malipo. Hili ni kemeo na onyo kwa yule anayekhalifu aliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa uadilifu, kufanya ibada na ikhlasi.

Kundi moja ameliongoa nao ni wale waliomfanya Mwenyezi Mungu ndiye mtawala wao na wakafuata amri yake na kujizuia makatazo yake, na wala wasihadaike na mambo ya shetani na ubatilifu wake.

Na kundi jingine limethibitukiwa na upotofu .

Nao katika akhera wana adhabu kubwa, Hilo ni kuwa Hakika wao wamefanya mashetani kuwa watawala wao badala ya Mwenyezi Mungu, Na anayemfanya shetani kuwa msimamizi badala ya Mwenyezi Mungu basi amepata hasara kubwa.

Na wanadhani kwamba wao wameongoka katika kufanya machafu, kuwafuata mababa na kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo. Mwenyezi Mungu anasema:

قُلْ هَلْ نُنَبِّئُكُم بِالْأَخْسَرِينَ أَعْمَالًا ﴿١٠٣﴾ الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا ﴿١٠٤﴾

Sema: Je, tuwaambie wenye hasara zaidi kwa vitendo, ni ambao bidii yao imepotea katika maisha ya dunia, nao wanafikiri kuwa wanafanya vyema.” (18: 103-104).

يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ ﴿٣١﴾

31. Enyi Wanadamu! Chukueni mapambo yenu katika kila msikiti, na kuleni na kunyweni wala msifanye ufujaji (israf), hakika Yeye hawapendi wafanyao ufujaji (israf).

قُلْ مَنْ حَرَّمَ زِينَةَ اللَّـهِ الَّتِي أَخْرَجَ لِعِبَادِهِ وَالطَّيِّبَاتِ مِنَ الرِّزْقِ قُلْ هِيَ لِلَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا خَالِصَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿٣٢﴾

32. Sema: Ni nani aliyeharamisha pambo la Mwenyezi Mungu ambalo amewatolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki? Sema: Hivyo ni kwa wale walioamini katika maisha ya dunia, ni vyao tu siku ya Kiyama. Namna hii tunazieleza ishara kwa watu wajuao.

قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالْإِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَأَن تُشْرِكُوا بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٣٣﴾

33. Hakika Mola wangu ameharamisha mambo machafu yaliyodhihirika na yaliyofichika. Na dhambi,na dhulma bila ya haki. Na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na ambacho hakukiteremshia dalili, Na kusema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua.

لِكُلِّ أُمَّةٍ أَجَلٌ فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ لَا يَسْتَأْخِرُونَ سَاعَةً وَلَا يَسْتَقْدِمُونَ ﴿٣٤﴾

34. Kila umma una muda, utakapofika muda wao hawatakawia (hata) saa moja wala hawatatangulia.

CHUKUENI MAPAMBO YENU

Aya 31-34

MAANA

Enyi Wanadamu! Chukueni mapambo yenu katika kila msikiti

Wafasiri wanasema watu wa wakati wa ujahiliya walikuwa wakitufu Al- Kaaba wakiwa uchi, wake kwa waume: Na walikuwa hawali mafuta wakati wa Hijja; wala hawali chakula ila kiasi tu cha kuzuia tumbo, kwa ajili ya kuadhimisha Hijja, ndipo ikashuka Aya hii.

Na kwamba Mtume(s.a.w.w) alisema: “Baada ya mwaka huu pasihijiwe na mshirikina yeyote wala Al-kaaba haitazungukwa uchi”, basi kauli yake hiyo ikatangazwa kwenye msimu. Miongoni mwa visa vinavavyoingia katika maudhui haya ni kile cha mwanamke mmoja mzuri wa Kiarabu aliyevua nguo na kuweka mkono kwenye tupu yake na akatufu. Macho ya watu yalipompata sana alitunga shairi hili:

Kuona yote au sehemu sihalali kitachoonekana

Kivuli kikubwa adhimu hata akali hamtavuna

Hata mwenye fahamu naye pia hudangana

Akimaanisha kuwa tupu yake ni adhimu pale ilipo, ina haiba na hifadhi, wala hakuna yeyote anayeweza kuifikia; na kwamba yeye anamkemea na kumchukiua anayemwangalia.

Kwa vyovyote itakayokuwa sababu ya kushuka Aya ni kwamba Mwenyezi Mungu ameharamisha kwa mtu kando kuangalia uchi wa mwingine awe mwanamume au mwanamke.

Na amewajibisha kusitiri tupu mbili katika Swala na tawafu.

Makusudio ya kila msikiti ni kama yale tuliyoyaeleza katika Aya iliyotangulia. Maana ni kuhimiza usafi na utwahara kutokana na uchafu na hadath na vilevile kujipamba nguo nzuri katika Swala ya Ijumaa, ya Jamaa, ya Idd au kutufu, ambapo sehemu hizo wanakusanyika watu, ili watu wasimkimbie kwa harufu yake mbaya na mandhari yake. Kujipamba ni vizuri, hata kwa fukara pia ajipambe kwa kiasi cha hali yake. Kuna Hadith isemayo: “Hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri na hupenda uzuri.”

Na kuleni na kunyweni.

Hii ni kupinga mwenye kuharamisha baadhi ya vyakula na vinywaji.

Wala msifanye ufujaji (israf) katika kula na kunywa na katika kujipamba kwa mavazi.

Hakika yeye hawapendi wafanyao ufujaji (israf)

Katika Aya nyingine anasema Mwenyezi Mungu:

﴿ إِنَّ الْمُبَذِّرِينَ كَانُوا إِخْوَانَ الشَّيَاطِينِ ﴾

“Hakika wabadhirifu ni ndugu wa mashetani” (17:27)

Na kuna Hadith isemayo: “Tumbo ni nyumba ya kila ugonjwa, na kula kwa makadirio ni msingi wa kila dawa, na uzoesheni kila mwili vile ulivyozoea.” Na Ali Al-Murtadha(a.s) anasema: “Ni mara ngapi tonge moja imezuia matonge mengi?”

Sema: Ni nani aliyeharamisha pambo la Mwenyezi Mungu ambalo amewatolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki?

Dhahiri ya maneno ni swali na maana yake ni kukana sana uharamu wa kujipamba na vilivyo vizuri katika riziki. Na kwamba ni katika wasiwasi wa Shetani na si katika Wahyi wa Mwenyezi Mungu.

Kutegemeza neno mapambo kwa Mwenyezi Mungu kunafahamisha uhalali, na neno vitu vizuri linajifahamisha hilo lenyewe. Kwa sababu kila lililo haramu ni baya na wala si zuri.

Neno pambo linakusanya aina zake zote, ikiwa na pamoja na nyumba, na neno vitu vizuri linakusanya vyakula, vinywaji, kustarehe kwa mambo mazuri na wanawake, sauti nzuri, mandhari nzuri na kila starehe iliyo nzuri ambayo, sharia haikukataza.

Maulamaa wa Kiislam wameafikiana kwa kauli moja kwamba kila kitu ni halali mpaka uje ukatazo. Wakatoa dalili kwa hukumu ya akili, kwamba hakuna adhabu bila ya ubainifu, na kwa kauli ya Mtume Mtukufu(s.a.w.w) :

“Watu wako katika wasaa wa wasiyoyajua.” na kauli yake: “Yale ambayo Mwenyezi Mungu amewafunikia waja kuyajua basi yameondolewa kwao.” Amesema tena: “Kila kitu kimeachiwa mpaka uje ukatazo kwenye kitu hicho.”

Sema: Hivyo ni kwa wale walioamini katika maisha ya dunia, ni vyao tu siku ya Kiyama.

Yaani katika maisha haya ya dunia wataneemeka wote waumini na makafiri, lakini kesho watakaoneemeka kwa mapambo ya Mwenyezi Mungu na vitu vizuri katika riziki, ni wale walioamini tu, peke yao bila ya kushirikiana na wale waliokufuru na kumshirikisha Mwenyezi Mungu.

Namna hii tunazieleza ishara kwa watu wajuao.

Mwenye kuifuatilia Qur’an ataona kuwa Mwenyezi Mungu anatumia neno Wajuzi (Ulama) kwa yule anayejua hukumu za Mwenyezi Mungu na akazitumia. Vilevile hulitumia kwa yule anayetarajiwa kuzijua na kuzitumia akifafanuliwa.

Kwa hiyo, makusudio ya watu wanaojua hapa ni aina ya pili ambao wanan- ufaika na ubainifu wa hukumu ya mapambo na vitu vizuri na vinginevyo na wanaowarejea maulama wa dini katika kujua hukumu za Mwenyezi Mungu (s.w.t) na kutoa dalili kwa Aya za Mwenyezi Mungu kwa halali yake na haramu yake.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumkana anayeharamisha mapambo na vitu vizuri, sasa anabainisha misingi ya vilivyo haramu kama ifuatavyo:

Sema: Hakika Mola wangu ameharamisha mambo machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika.

Umetangulia ubainifu wake katika kufasiri Sura 6:151 kifungu cha wasia.

Na dhambi ni kila jambo ambalo anaasiwa kwalo Mwenyezi Mungu, iwe kauli au kitendo. Kuunganisha machafu kwenye dhambi ni katika hali ya kuunganisha mahsus kwenye ujumla; kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ ﴾

“Kama tulivyompa Wahyi Nuh (a.s) na Mitume…” (4:163).

Na dhulma bila ya haki.

Kuna hadith inayosema “Lau jabali lingedhulu- mu jabali jingine, basi Mwenyezi Mungu angelifanya lile lililodhulumu lipondekepondeke” Na Amirul-Muminin anasema: “Mwenye kuchomoa upanga wa dhuluma atauwawa nao.”

Na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na ambacho hakukiteremshia dalili.

Hakuna dhambi nyingine baada ya ukafiri na shirk. Shirk ni kinyume cha Tawhid ambayo muhtasari wake ni:

﴿ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ﴾

“Hakuna chochote kama mfano wake” (42:11).

Umetangulia ufafanuzi katika kufasiri Sura 6:153, kifungu cha ‘Wasia kumi.’

Na kusema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua.

Miongoni mwa hayo ni yale yaliyoashiriwa katika Aya 28 ya Sura hii:“Na wanapofanya machafu husema tumewakuta nayo baba zetu na Mwenyezi Mungu ametuamrisha .” Hakuna uchafu mbaya kama kusema bila ya kujua; na hakuna tofauti katika hukumu baina ya kumzulia Mungu na kumshirikisha. Imam Ali amesema: “Mwenye kuliacha neno ‘sijui’ atakuwa hana salama.”

Kila umma una muda makusudio ya umma hapa ni kundi, kama lilivyotumika neno hilo katika Aya isemayo:

﴿ وَلَمَّا وَرَدَ مَاءَ مَدْيَنَ وَجَدَ عَلَيْهِ أُمَّةً مِنَ النَّاسِ يَسْقُونَ ﴾

“Alipofikia maji ya Madian alikuta umma wa watu wakinywesha.” (28:23)

Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja uovu wa washirikina katika Aya 28; na yale aliyohalalisha katika Aya 31: na aliyoyaharamisha katika Aya 33. Baada ya haya yote anasema kila kundi, ikiwa ni pamoja na washirikina waliomzulia Mwenyezi Mungu, lina muda maalum katika maisha haya; kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu waambiwe yale waliyokuwa wakiyafanya.

Katika haya mna makemeo na kiaga kwa washirikina na wenye kufanya uovu na watu wa dhulma na kila anayesema juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ujuzi.

Utakapofika muda wao, hawatakawia (hata) saa moja wala hawatatangulia.

Imepita tafsir yake katika kufasiri Juz. 4 (3:145).

﴿ يَا بَنِي آدَمَ إِمَّا يَأْتِيَنَّكُمْ رُسُلٌ مِنْكُمْ يَقُصُّونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِي فَمَنِ اتَّقَىٰ وَأَصْلَحَ فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴾

Enyi: Wanadamu! Watakapowafikia Mitume kutoka miongoni mwenu, wakawaeleza ishara zangu, basi watakaoogopa na kufanya mema, haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.

﴿ وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَاسْتَكْبَرُوا عَنْهَا أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴾

Na wale watakaokadhibisha ishara zetu na kuzifanyia kiburi, hao ndio watu wa motoni, watadumu humo.