11%

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

وَقَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِ فِرْعَوْنَ أَتَذَرُ مُوسَىٰ وَقَوْمَهُ لِيُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَيَذَرَكَ وَآلِهَتَكَ قَالَ سَنُقَتِّلُ أَبْنَاءَهُمْ وَنَسْتَحْيِي نِسَاءَهُمْ وَإِنَّا فَوْقَهُمْ قَاهِرُونَ ﴿١٢٧﴾

127. Na wakasema wakuu wa kaumu ya Firauni: Je, utamwacha Musa na watu wake walete uharibifu katika nchi na kukuacha wewe na waungu wako. Akasema: Tutawauwa watoto wao wa kiume na tutawaacha hai wanawake wao. Na hakika sisi ni wenye nguvu juu yao.

قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ اسْتَعِينُوا بِاللَّـهِ وَاصْبِرُوا إِنَّ الْأَرْضَ لِلَّـهِ يُورِثُهَا مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَالْعَاقِبَةُ لِلْمُتَّقِينَ ﴿١٢٨﴾

128. Musa akawaambia watu wake: Ombeni msaada kwa Mwenyezi Mungu na subirini. Ardhi ni ya Mwenyezi Mungu atamrithisha amtakaye katika waja wake na mwisho ni wa wenye takuwa.

قَالُوا أُوذِينَا مِن قَبْلِ أَن تَأْتِيَنَا وَمِن بَعْدِ مَا جِئْتَنَا قَالَ عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يُهْلِكَ عَدُوَّكُمْ وَيَسْتَخْلِفَكُمْ فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرَ كَيْفَ تَعْمَلُونَ ﴿١٢٩﴾

129. Wakasema: Tumeudhiwa kabla hujatufikia na baada ya kutujia. Akasema: Huenda Mola wenu atamwangamiza adui yenu na kuwafanya makhalifa katika ardhi aone jinsi mtakavyokuja fanya.

UTAMWACHA MUSA?

Aya 127 – 129

MAANA

Na wakasema wakuu wa kaumu ya Fir’aun: Je, utamwacha Musa na watu wake walete uharibifu katika nchi.”

Baada ya kwisha tukio hilo la kutisha ambalo Nabii Musa alipata ushindi na kufedheheka Firauni. Nabii Musa aliendelea kuwalingania kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake, na dalili yake ni yaliyotukia jana tu kati yake na wachawi, Watu wengi wakamkusanyikia.

Wakuu wa Firauni wakahofia hali isibadilike na mambo yakawageukia wao na bwana wao, hapo wakamchochea Firauni na kumwambia: “Mpaka lini utamnyamazia Musa na kumwacha akiharibu nchi?” Kuharibu nchi, wanamaanisha watu kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake.

Na wakuache wewe na waungu wako.

Kauli hii ya wakuu wa Firauni inafahamisha kuwa alikuwa nao waungu anaowaabudu; nayo inapingana, kwa dhahiri yake, na kauli ya Firauni kuwa Mimi ndiye mola wenu mkubwa na simjui kwa ajili yenu Mungu asiyekuwa mimi.

Wafasiri wamelijibu hilo kwa majibu kadhaa. Lenye nguvu zaidi ni kuwa Firauni alikuwa na miungu akidai kuwa yeye ni mwana kipenzi wa hiyo miungu na kwamba yeye anaitegemeza hukumu yake na utawala wake kwenye hiyo miungu. Kwa hiyo kauli yake simjui kwa ajili yenu Mungu na Mola isipokuwa yeye peke yake inamaanisha kuwa hakuna yeyote mwenye kuhukumu kwa jina la mungu isipokuwa yeye. Maana haya yanatiliwa nguvu na kauli yake:

أَلَيْسَ لِي مُلْكُ مِصْرَ وَهَـٰذِهِ الْأَنْهَارُ تَجْرِي مِن تَحْتِي ﴿٥١﴾

“Kwani ufalme wa Misri si wangu na hii mito inapita chini yangu?” (43:51).

Akasema: Tutawaua watoto wao wakiume na tutawaacha hai wanawake wao.

Kabla ya kuzaliwa Nabii Musa, Fir’aun alikua akwaiua watoto wa kiume wa Bani Israel waliposisitizia wakuu katika watu wake apambane na Nabii Musa, aliwajibu atarudisha mpango huo wa mwanzo.

Na hakika sisi ni wenye nguvu juu yao.

Yaani tuna nguvu juu yao kama ilivyokuwa kabla ya Musa.

Musa akawaambia watu wake: Ombeni msaada kwa Mwenyezi Mungu na subirini. Ardhi ni ya Mwenyezi Mungu atamrithisha amtakaye katika waja wake na mwisho ni wa wenye takuwa.”

Waisrael waliposikia vitisho vya Firauni na kiaga chake waliogopa. Nabii Musa(a.s) akawatuliza na kuwaamrisha kuwa na subira (uvumilivu) na kumtegemea Mwenyezi Mungu; na akawapa tumaini la ushindi ikiwa wao watasubiri na kumwogopa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu ardhi ni ya Mwenyezi Mungu si ya Firauni, na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye kumcha.

Wakasema: Tumeudhiwa kabla hujatufikia na baada ya kutujia!

Firauni alikuwa akiwakandamiza waisrael kabla ya kuja Nabii Musa na akawashtua kuwakandamiza zaidi baada ya kuja kwake. Walipomwambia Nabii Musa hivyo akasema:

Huenda Mola wenu akamwangamiza adui yenu na kuwafanya makhalifa katika nchi aone jinsi mtakavyokujafanya.

Nabii Musa(a.s) alikuwa anajua wazi kuwa Firauni ataangamia na kwamba Mungu atawaokoa wana wa Israil na kuwamakinisha katika ardhi, lakini alitoa ibara ya huenda ili wasibweteke na ahadi yake.

Kisha akaishiria Nabii Musa kwamba, si muhimu kuwa adui ataangamia na wao kuwa makhalifa katika ardhi, lakini muhimu zaidi ni kumcha Mungu na kuutumia vizuri huo ukhalifa katika ardhi yake; na kwamba Mungu atawaangalia je, watatengeza au wataharibu?

Na wamefanya mengi sana katika ardhi; hapo mwanzo waliwaua mitume na viongozi wema, baadae wakaunda dola isiyokuwa na sharia isipokuwa matamanio ya kuua na kufukuza watu makwao.

Mwaka huu wa 1968, kimetoka kitabu huko Israil kinaitwa Siyakh lokhamim yaani simulizi za wanajeshi. Gazeti la Al-ahram la Misr toleo la tarehe 23-8-1968, limefasiri baadhi ya yaliyomo katika kitabu hicho:

“Ambaye hawezi kuvunja nyumba na kuwafurusha waliomo katika nyumba hiyo, basi bora akae nyumbani kwake tu. Sisi tulipokuja kwenye nchi ya Palestina kulikuwa na watu wengine wanaoishi humo; hatukuwa na matumaini kuwa wataweza kukubali kutuachia mashamba yao na majumba yao. Kwa hiyo ikawa hakuna budi tuwaue au kuwatishia kuwaua ili wakimbie watuachie majumba na mashamba”

Hii ndiyo sharia na lengo la Israil: kuua na kufukuza. Hii sio dola kama dola nyinginezo; isipokuwa ni kikosi cha kizayuni cha mauaji chenye lengo la kuwafukuza wenyeji na kukalia nchi zao kuanzia mto Nail hadi Furat.

Je Waarabu wamejiandaa na nini? Hakuna njia wala mbinu yoyote isipokuwa misimamo ya kivietnam inayosema: ‘Kufa na kupona’ ama kusiweko na Israil au kusiweko na Mwarabu.

وَلَقَدْ أَخَذْنَا آلَ فِرْعَوْنَ بِالسِّنِينَ وَنَقْصٍ مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ ﴿١٣٠﴾

130. Na hakika tuliwaadhibu watu wa Firauni kwa ukame na kwa kupungukiwa na mazao, ili wapate kukumbuka.

فَإِذَا جَاءَتْهُمُ الْحَسَنَةُ قَالُوا لَنَا هَـٰذِهِ وَإِن تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ يَطَّيَّرُوا بِمُوسَىٰ وَمَن مَّعَهُ أَلَا إِنَّمَا طَائِرُهُمْ عِندَ اللَّـهِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٣١﴾

131. Ulipowafikia wema, walisema: Huu ni kwa ajili yetu na ulipowafikia ubaya walimnasibishia mkosi Musa na walio pamoja naye. Sikilizeni! Hakika mkosi wao unatoka kwa Mwenyezi Mungu lakini wengi wao hawajui.

وَقَالُوا مَهْمَا تَأْتِنَا بِهِ مِنْ آيَةٍ لِّتَسْحَرَنَا بِهَا فَمَا نَحْنُ لَكَ بِمُؤْمِنِينَ ﴿١٣٢﴾

132. Na wakasema: Hata ukituletea ishara yoyote kutur- oga hatutakuamini.

فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمُ الطُّوفَانَ وَالْجَرَادَ وَالْقُمَّلَ وَالضَّفَادِعَ وَالدَّمَ آيَاتٍ مُّفَصَّلَاتٍ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا مُّجْرِمِينَ ﴿١٣٣﴾

133. Basi tukawapelekea tufani na nzige na chawa na vyura na damu kuwa ishara mbalimbali, lakini wakatakabari na wakawa watu wakosefu.

TULIWAADHIBU WATU WA FIRAUNI

Aya 130-133

MAANA

Na hakika tuliwaadhibu watu wa Firauni kwa ukame na kwa kupungukiwa na mazao, ili wapate kukumbuka.

Misri ilikuwa ikibubujika rutuba na mazao. Firauni akajifaharusha kwa rutuba hii na kusema:

وَهَـٰذِهِ الْأَنْهَارُ تَجْرِي مِن تَحْتِي ﴿٥١﴾

"Na pia mito hii ipitayo chini yangu" (43:51)

Mwenyezi Mungu alitia balaa ya kahati na dhiki ya maisha wakati wa Firauni wa Musa ili ajutie upotevu wake na aitikie mwito wa haki. Kuna Hadith isemayo: "Wakiwa waovu watawala hufungwa mvua."

Ni sawa iwe kulikuwako na uhusiano baina ya dhuluma ya mtawala na kahati kwa njia ya ujumla au isiweko, lakini Mwenyezi Mungu aliwaadhibu watu wa Firauni kwa dhulma yao ili wao wakumbuke kabla ya kuwaingiza ndani kwenye uchungu.

Ulipowafikia wema, walisema: Huu ni kwa ajili yetu na ulipowafikia ubaya walimnasibishia mkosi Musa na walio pamoja naye.

Wanafasiri matukio kwa mantiki haya, Kila heri inayowapata basi wanaistahiki wao. Kwa sababu wao wanatawala watu, na kila ubaya unaowapa- ta, basi sababu yake ni yule anayewalingania kwenye haki. Ama rutuba na ukame wanautenga na Mwenyezi Mungu na maumbile aliyo yaumba.

Ndipo Mwenyezi Mungu akawajibu kwa kusema: Sikilizeni! Hakika mkosi wao unatoka kwa Mwenyezi Mungu lakini wengi wao hawajui. Mkosi wao ni fumbo la ukame uliowapata na huo ni kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu ambayo sababu zote huishia kwake, na kumnasibishia Musa na ujinga na upumbavu tu.

Utauliza : Kwa nini Mwenyezi Mungu ametumia neno wema kwa ibara yenye al (Al-Hasana) ambayo katika sarufi ya Kiarabu inaitwa ma'rifa, na neno ubaya aktumia bila ya al ambyo ni nakira?

Jibu : Sio mbali kuwa ni ishara ya kwamba maumbile ya heri, kama vile rutuba n.k, ni mengi, na kwamba ubaya, kama vile matetemeko na tufani na ukame ni machache.

Na wakasema: Hata ukituletea ishara yoyote kuturoga hatutakuamini

Huku ni kukiri wazi, kwamba wao wanaikataa haki, wakati huo huo wanakiri kushindwa kwao kwa hoja na dalili. Yakawa malipo ya inadi yao hii ni kuwapata balaa ya aina tano za adhabu:

1.Tukawapelekea tufani ya mvua ikaharibu mimea na mifugo.

2.Na nzige waliokuja baada ya tufani,kama kawaida, wakala mimea yao iliyobakia.

3.Na chawa.

4.Na vyura waliowaghasi maisha yao.

5.Na damu. Inasemekana maji yao yaligeuka kuwa damu na wasi weze kupata maji matamu. Na inasemekana walipatwa na maradhi ya kutokwa na damu za pua.

وَلَمَّا وَقَعَ عَلَيْهِمُ الرِّجْزُ قَالُوا يَا مُوسَى ادْعُ لَنَا رَبَّكَ بِمَا عَهِدَ عِندَكَ لَئِن كَشَفْتَ عَنَّا الرِّجْزَ لَنُؤْمِنَنَّ لَكَ وَلَنُرْسِلَنَّ مَعَكَ بَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿١٣٤﴾

134. Na ilipowaangukia adhabu wakasema: Ewe Musa Tuombee kwa Mola wako kwa yale aliyokuahidi. Kama ukituondolea adhabu bilashaka tutakuamini na hakika tutawaacha wana wa Israil waende nawe.

فَلَمَّا كَشَفْنَا عَنْهُمُ الرِّجْزَ إِلَىٰ أَجَلٍ هُم بَالِغُوهُ إِذَا هُمْ يَنكُثُونَ ﴿١٣٥﴾

135. Lakini tulipowaondolea adhabu kwa muda watakaoufikia, mara wakavunja ahadi.

فَانتَقَمْنَا مِنْهُمْ فَأَغْرَقْنَاهُمْ فِي الْيَمِّ بِأَنَّهُمْ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا عَنْهَا غَافِلِينَ ﴿١٣٦﴾

136. Basi tuliwapatiliza na tukawazamisha baharini kwa sababu walizikadhibisha ishara zetu na wakaghafilika nazo

وَأَوْرَثْنَا الْقَوْمَ الَّذِينَ كَانُوا يُسْتَضْعَفُونَ مَشَارِقَ الْأَرْضِ وَمَغَارِبَهَا الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا وَتَمَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ الْحُسْنَىٰ عَلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ بِمَا صَبَرُوا وَدَمَّرْنَا مَا كَانَ يَصْنَعُ فِرْعَوْنُ وَقَوْمُهُ وَمَا كَانُوا يَعْرِشُونَ ﴿١٣٧﴾

137. Tukawarithisha watu walionekana wadhaifu mashariki na magharibi ya ardhi tuliyoibariki. Na likatimia neno jema la Mola wako kwa wana wa Israil, kwa sababu walikuwa na subira; na tukayaangamiza yale aliyokuwa akiyafanya Firauni na kaumu yake na yale waliyokuwa wakiyajenga.

ILIPOWAANGUKIA ADHABU

Aya 134-137

MAANA

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja aina tano za adhabu alizowaadhibu watu wa Firauni. Na walikuwa kila inapowapata adhabu hutawasali kwa Musa kutaka kuondolewa adhabu hiyo kwa karamu yake mbele ya Mwenyezi Mungu.

Walikuwa wakijiwekea ahadi wao wenyewe kwa Musa kuwa akifanya, basi wataitikia mwito wa haki. Mwenyezi Mungu naye alikuwa akiwaondolea adhabu kwa muda fulani ili wajiandae na toba na kuwasimamishia hoja, Lakini walikuwa wakivunja ahadi, hawakutekeleza wanayoyasema.

Hapo Mwenyezi Mungu huwateremshia mara ya pili, Tena wanarudia kunyenyekea na kutawasali, na Mwenyezi Mungu huwaondolea. Ikawa namna hii mpaka adhabu ya tano, au jaribio la tano, ndipo akawatesa na kuwatupa ndani ya bahari.

Baada ya muda mrefu kupita tangu kufamaji Firauni na kufariki Musa na Harun, alitokea katika waisrail, Daudi na Suleiman wakafanya dola yenye mipaka mashariki na magharibi.

Lakini haraka sana dola iliyeyuka na Waisrail wakatawaliwa na Ebuchadnezer, wafursi na makhalifa wa Alexandria kisha wa Roma.

وَجَاوَزْنَا بِبَنِي إِسْرَائِيلَ الْبَحْرَ فَأَتَوْا عَلَىٰ قَوْمٍ يَعْكُفُونَ عَلَىٰ أَصْنَامٍ لَّهُمْ قَالُوا يَا مُوسَى اجْعَل لَّنَا إِلَـٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ قَالَ إِنَّكُمْ قَوْمٌ تَجْهَلُونَ ﴿١٣٨﴾

138. Na tukawavusha bahari wana wa Israil na wakawafikia waliokuwa wakiyaabudu masanamu yao; wakaema: Ewe Musa! Hebu nasi tufanyie waungu kama hawa walivyo na waungu. Akasema Hakika nyinyi ni watu wafanyao ujinga.

إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ مُتَبَّرٌ مَّا هُمْ فِيهِ وَبَاطِلٌ مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٣٩﴾

139. Hakika waliyona hawa yatawangamiza na ni bure waliyokuwa wakiyafanya.

قَالَ أَغَيْرَ اللَّـهِ أَبْغِيكُمْ إِلَـٰهًا وَهُوَ فَضَّلَكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ ﴿١٤٠﴾

140. Akasema je, niwatafutie mungu badala ya Mwenyezi Mungu, hali yeye ameweafadhilisha juu ya walimwengu?

وَإِذْ أَنجَيْنَاكُم مِّنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَسُومُونَكُمْ سُوءَ الْعَذَابِ يُقَتِّلُونَ أَبْنَاءَكُمْ وَيَسْتَحْيُونَ نِسَاءَكُمْ وَفِي ذَٰلِكُم بَلَاءٌ مِّن رَّبِّكُمْ عَظِيمٌ ﴿١٤١﴾

141. Na Tulipowaokoa kwa kaumu ya Firaun waliowapa adhabu mbaya wakiwaua watoto wenu wa kiume na kuwaacha hai wanawake wenu. Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa uliotokea kwa Mola wenu.

TULIWAVUSHA WANA WA ISRAIL

Aya 138-141

MAANA

Na tukawavusha bahari wana wa Israil na wakawafikia waliokuwa wakiyaabudu masanamu yao; wakaema: Ewe Musa! Hebu nasi tufanyie waungu kama hawa walivyo na waungu. Akasema: Hakika nyinyi ni watu wafanyao ujinga.

Baadhi ya riwaya zinaeleza kuwa Musa aliendelea miaka ishirini na tatu akipigana jihadi na Firauni kwa ajili ya Tawhid na kuwakomboa wana wa Israil kutokana ukandamizaji, Wakashuhudia miujiza ya kushangaza iliyodhihiri mikononi mwa Musa.

Mwisho wakaona kupasuka bahari kwa fimbo ya Musa, na jinsi zilivyotokea njia kavu kumi na mbili. Kila ukoo ukawa na njia yake. Vile vile waliona jinsi bahari ilivyofungika kwa Firauni na askari wake.

Yote hayo waliyashuhudia, lakini kabla ya kupita muda walisahau miujiza waliyoiona na macho yao yakawa kwa watu wanaoabudu masanamu, wakamtaka Musa awafanyie sanamu la kuabudu. Walitaka haya wakiwa wanajua kwamba Musa ni mtu wa Mwenyezi Mungu na kwamba umuhimu wake wa kwanza ni mwito wa Tawhid na kupiga vita ushirikina. Vile vile walikuwa wakijua kuwa Mwenyezi Mungu alimwangamiza Firauni na jeshi lake, kwa sababu ya ushirikina wake. Baadhi ya wafisri wanasema; "Lau wao wenyewe wangejifanyia mungu, mshangao ungelikuwa mdogo kuliko kumtaka Mtume wa Mola wa walimwengu wote kuwafanyia mungu. Lakini hao ndio Waisrail!

Hakika yaliyo na hawa yatawangamiza na ni bure waliyokuwa wakiyafanya.

Musa(a.s) alianza kuwajibu watu wake kuwa wao ni wajinga na wapumbavu; kisha akawapa habari kwamba mwisho wa washirikina na waabudu masanamu ni hasara na maangamizi.

Akasema je, niwatafutie mungu badala ya Mwenyezi Mungu, hali yeye ameweafadhilisha juu ya walimwengu?

Imepita tafsiri yake katika Juz.1 (2:47)

Kwa vyovyote kufadhilishwa kwao juu ya Firauni na watu wake hakuhisabiwi kuwa ni fadhila kubwa.

Na Tulipowaokoa kwa kaumu ya Firaun waliowapa adhabu mbaya wakiwaua watoto wenu wa kiume na kuwaacha hai wanawake wenu. Na kati- ka hayo ulikuwa mtihani mkubwa uliotokea kwa Mola wenu.

Umepita mfano wake katika Juz.1(2:49)